Nimekuwa nafuatilia kwa ukaribu kampeni za urais zinazoendelea nchini ambapo Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Chato Mkoani Geita imekuwa ni moja ya agenda KUU za mgombea urais wa CHADEMA TUNDU LISSU.
Kabla ya Kuanza kujadili kwa kina kuhusu umuhimu wa kiwanja hicho kwa sasa, ni AIBU kwa mgombea wa nafasi ya urais kutumia ujenzi wa kiwanja hicho kuwa miongoni mwa ajenda kuu ya kukuingiza Ikulu kwa hali ya kawaida ilitarajiwa mgombea wa nafasi ya urais wa upinzani kuja na Sera mbadala za kiuchumi, kisiasa na kijamii ili kuvuta hisia za wapiga kura.
Turejee kwenye mjadala wetu mama wa ujenzi wa ujenzi wa kiwanja cha Ndege Chato, nilichobaini katika mijadala mingi inayoendelea kuhusu jambo hilo ni wachangiaji wengi wanaoongozwa na mihemko na itikadi za kisiasa bila kuwa na tafakuri ya kina ili kubaini uhalisia wa jambo hilo.
Ili kupata uelewa mpana wa kwani ujenzi huo ulifanyika Chato ni muhimu sana walau kwa uchache tukafahamu mambo yafuatayo:
** kijiografia mji wa Chato ndio upo karibu zaidi na hifadhi za taifa za Burigi, Ibanda, Kimisi, Rumanyika na Biharamulo ambazo zote zinapatikana mkoa wa Kagera. Vilevile upo karibu sana na hifadhi ya Rubondo yenye wanyama mbalimbali kama Twiga, Tembo, Swala, Viboko, Pongo na Sokwe mtu.
** Wilaya ya Chato inapatikana katika mkoa wa Geita ambao una Mgodi mkubwa wa Geita Gold Mine uliochini ya wawekezaji na umekuwa ukitajwa kama miongoni mwa migodi ambayo inzauzalishaji mkubwa wa dhahabu barani Afrika. Kadhalika ndani ya chato kuna shughuli za uchimbaji madini zinazofanywa na wachimbaji wadogo katika maeneo ya Msasa, Matabe, Imwelu, Makurugusi, Bwanga, Iparamasa, Buseresere na Nyarutembo
** Wilaya ya Chato inapatikana karibu na Ziwa Victoria lenye samaki wa aina mbalimbali ikiwemo Sato, Sangara, Mumi, Dagaa, Gogogo, Kamongo n.k likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 100 na mialo 34.
Baada ya kupata wasifu ya Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita kwa ujumla na maeneo jirani, kwa mtazamo wa jicho la kiuchumi hasa uuchumi wa kati tulioufikia ujenzi wa uwanja wa ndege wa Chato umejengwa kwa kimkakati na utakuwa na manufaa yafuatatyo;-
i) Kuongeza idadi ya watalii katika hifadhi ya taifa ya Lubondo mkoani Geita na hifadhi zilizopo mkoani Kagera kwa kuwa kiungo muhimu kati ya Tanzania na Nchi jirani za DRC Congo, Burundi, Rwanda na Uganda ambazo ni jirani kabisa na vivutio hivyo. Hivyo kuiongezea Serikali mapato.
ii) Utasaidia kuongeza na kuimarisha usafirishaji wa abiria kwenda nchi jirani, mizigo, mazao na bidhaa mbalimbali kama vile asali, minofu ya samaki kutoka Tanzania kwenda nje ya Nchi.
iii) Utachangia katika kutoa ajira kwa vijana wa kitanzania, kukuza biashara katika wilaya ya Chato na Mkoa wa Geita kwa ujumla hivyo kuondokana na umasikini.
iv) Utasaidia kuongeza ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya Tanzania na mataifa jirani ya Uganda, DRC Congo, Rwanda, Burundi n.k
Kwa ujumla kiwanja hicho kitakuwa na tija katika maeneo ya Utalii, biashara na katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji. Pia utasaidia kuibua vivutio vingi mbalimbali vitavyovuta watalii wengi zaidi kuja kuitembelea Tanzania.
Licha ya sababu na manufaa lukuki ambayo yanatarajiwa kupatikan Chato, Geita na Tanzania kwa ujumla bado unakutana na mtu anajenga hoja dhaifu kama anapendelea Chato kwa kuwa ndio nyumbani, nimekuwa najiuliza hivi kumbe kata, wilaya, Mkoa au kanda ikitoa kiongozi wananchi wa eneo hilo HAWANA HAKI ya kuletewa maendeleo hadi kiongozi huyo atoke madarakani?? hebu tubadilike kwa kuachana na fikira hizo mgando, wakazi wa Geita kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wana haki ya kuletewa maendeleo kama wananchi wa maeneo mengine Kama Kilimanjaro, Arusha, Dar n.K