Sisi wengine siyo watu tunaopenda kuzunguzunguka, bali hupenda mambo yaliyonyoka.
Ni ukweli kuwa kumekuwa na tetesi kuwa Makamu wa Rais anaumwa sana, na wengine kusema ameenda nje ya nchi kutibiwa. Lakini baadaye Waziri Mkuu akasema kuwa Makamu wa Rais yupo Marekani kwa shughuli za kikazi. Taarifa ambayo ilitiliwa mashaka na wengi.
Na sisi wengine tulihoji, kama kweli Makamu wa Rais anaumwa kwa nini umma usiambiwe? Maana kuugua kwa mwanadamu ni jambo la kawaida, na hakuna mtu hata mmoja ambaye anaweza kusema kuwa yeye hawezi kuugua au hataugua. Ni sawa tu na kifo. Kama mtu anaumwa, kwa nini usisemwe ukweli? Hivi unajisikiaje mtu akikuficha kukudanganya juu ya habari ya kuugua kwa ndugu au rafiki yako? Kiongpzi wa nchi, katika ngazi ya Taifa ni kama kiongozi wa familia, katika ngazi ya familia. Kama kweli kiongozi wa familia anaumwa, kwa nini wanafamilia wasiambiwe ukweli? Waliokuwa wanahoji ili kuupata ukweli wana kosa gani?
Kuna watu, ambao mimi nawaita ni wajinga, wakageuza habari na kusema kuwa wanauuliza kupata uhakika juu ya taarifa za kuwa Makamu wa Rais anaumwa, eti wanamwombea mabaya Makamu wa Rais!
Huu ni uwongo mkubwa. Ni kutaka kupeleka ujumbe wa uwongo hata kwa Makamu wa Rais mwenyewe kuonesha kuwa kuna watu wanamchukia kiasi cha kumwombea mabaya. Jambo ambalo siyo kweli hata kidogo.
Mimi binafsi naamini kuwa Makamu wa Rais Dr. Mpango ni kati ya watu wanaoweza kuwa na maadui wachache sana, kama wapo. Dr. Mpango, hata ukiacha masuala ya uongozi, kwa hulka yake binafsi, ni mtu asiye na makuu, tena anayeamini, mtu kuwa kiongozi hakujabadilisha ubinadamu wake. Mtu wa namna hii, watu wamwombee mabaya kwa sababu gani?
Tumesikia Makamu wa Rais, Dr. Mpango atakuwa mgeni Rasmi leo kwenye tukio moja huko Arusha. Kama alikuwa anaumwa na sasa amepona, au amepata nafuu, au hakuwa anaumwa, naamini ni habari njema kwetu sote.
Tunajua Dr. Mpango alipitia changamoto kubwa ya kiafya wakati wa covid 19, tena wakati wa kipindi kigumu, tulichoshuhudia kuondoka kwa viongozi wengi wakubwa na baadhi ya jamaa zetu, lakini Mungu alimnusuru Dr. Mpango. Basi kwa huruma na mapenzi yake Mungu wetu wa rehema, azidi kumjalia afya njema na maisha ya furaha na amani.