Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Willibrod Peter Slaa, amekosoa vikali viongozi wa sasa wa chama hicho kwa kushindwa kuwaongoza wananchi ipasavyo na kutokujenga uelewa wa kutosha juu ya wajibu wao wa kisiasa.
Akizungumza kupitia mtandao wa Clubhouse hivi karibuni, Dkt. Slaa alieleza kuwa CHADEMA imeshindwa kuwapatia wananchi ujasiri na uwezo wa kuleta mabadiliko makubwa nchini, hali iliyosababisha wananchi kubaki katika hali ya kutojiamini na kutegemea zaidi uongozi wa chama kuliko kuwa na nguvu zao wenyewe.
Katika mazungumzo yake, Dkt. Slaa alitilia mkazo umuhimu wa chama kuwa na mikakati ya kuwajengea uwezo wananchi, akieleza kuwa kwa muda mrefu wananchi wa Tanzania hawajawahi kupewa mwongozo madhubuti wa kujitegemea katika harakati za kisiasa.
"Usitegemee wananchi wawe mstari wa mbele, wanahitaji kuongozwa... CHADEMA mliwajengea uwezo? Upi? Kama mliwajengea uwezo wamefika wakashindwa kutekeleza, wananchi wajibu wao nini?" alihoji Dkt. Slaa, akisisitiza kuwa ni jukumu la viongozi wa kisiasa kuwaongoza wananchi na kuwapa moyo wa kusimama kidete kwa ajili ya haki zao.
Dkt. Slaa alitoa mfano wa matukio mbalimbali ya siku za karibuni likiwamo tukio la Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) kuchoma vitenge vilivyokuwa vimetolewa kama zawadi na Rais Samia Suluhu Hassan. Tukio kama hilo ni ishara ya namna chama kimeshindwa kuleta ushawishi wa kutosha kwa wananchi.
“Kwenye suala hili kwa mfano la kuchoma kanga na vitenge, wananchi hawakumualika Rais Samia, nyinyi ndiyo viongozi mliomualika, mlikwenda kama chama kwenda kumbana Samia kwamba ulitupa zawadi, sasa leo tunataka kuchoma hizi zawadi na mkachoma mbele yake? Wananchi mtawaingiza kwenye matatizo tu bila sababu”, amesema Dkt. Slaa na kuongeza,
“Wananchi wana jukumu lao, wananchi mliwaomba kwenye maandamano wametokea. Wananchi wanahitaji kupewa ujasiri, na kauli za vyama vya upinzani juu ya maandamano zilitokaje?"
Aidha Dkt. Slaa amezungumzia suala la maridhiano akilitaja kuwa halikuwa shirikishi kwani CHADEMA walikaa kwenye meza moja na serikali katika mchakato wa maridhiano bila kuwa wazi kwa wananchi. Alidai kuwa kitendo cha viongozi wa chama kukaa na serikali kimya kimya kiliwafanya wananchi kuendelea kukosa ujasiri wa kushiriki kikamilifu katika harakati za kisiasa.
"Leo unategemeaje wananchi walipuke wakati nyinyi wenyewe mlikuwa mnakaa meza moja na serikali mkinywa juisi... Vitendo vile vilifanya wananchi waendelee kulala," alisema Dkt. Slaa, akiongeza kuwa chama kilipaswa kuwa na mikakati ya wazi na madhubuti ya kushirikiana na wananchi ili kuongeza hamasa katika kudai haki.
Pia, Dkt. Slaa alieleza kuwa chama kinachotaka kushinda na kuongoza lazima kiwe na mbinu nyingi na za kisasa za kufanikisha malengo yake. Alihoji kama CHADEMA imewahi kuwa na mbinu zaidi ya elfu moja kama ambavyo chama tawala, CCM, hujigamba kuwa nacho.
"CCM wana mbinu elfu moja, nyinyi CHADEMA mna ngapi? Mliwahi kutoka hadharani kutuambia?" alihoji Dkt. Slaa,
Kwa upande mwingine, Dkt. Slaa alitoa changamoto kwa viongozi wa sasa wa CHADEMA kuwa wazi na kutoa taarifa zaidi kwa umma juu ya mbinu na mikakati yao ili kuwaongezea wananchi imani na ujasiri katika harakati za kisiasa. Alisema kuwa kama viongozi wa CHADEMA walitoka salama kwenye kesi ya ugaidi, basi walipaswa kutumia fursa hiyo kuonyesha wananchi jinsi walivyopambana na changamoto kubwa na kuwahamasisha kuendelea na mapambano ya kisiasa kwa
ushirikiano wa karibu.