Tiba ya Liliondo ‘isizike' mjadala wa Dowans
Joseph Sabinus
p>KATIKA moja ya makala zangu, niliwahi kuandika kuhusu tatizo la Watanzania kuvutwa na kuyumbishwa kwa hoja za msimu kadiri zinavyojitokeza. Kwamba hali hiyo, imewapa nguvu hata watawala wazembe kuongeza juhudi za kumuomba Mungu wao ili liibuke suala jipya linaloweza kuzima lile la moto linalokuwa likichemka kwa nguvu ya moto wa kasi au bungeni, kwenye vyombo vya habari na katika jamii kwa jumla.
Kama ilivyo ada, shilingi inazo pande kuu mbili; upande wa mwenge na upande wa kichwa. Ndivyo ilivyokuwa hata katika makala hiyo. Kwamba wapo walioniunga mkono na kukiri kuwa kweli, jamii yetu inaumwa ugonjwa huo wa kuvutwa na kuyumbishwa na hoja za msimu na matukio ya msimu.
Kwamba hili linapovuma, wanaliacha hili hata kama bado "changa"; wanalifuata lingine la wakati huo huo ambalo nalo hawalifikishi tamati na kujua limekwisha vipi.
Kadhalika, wapo waliosita kukubaliana na mimi na wengine wakasema nami kama mwandishi wa habari, ninayo sehemu kubwa ya kulaumiwa kwa kutokuwa chachu ya kuendeleza hoja hizo.
Nianze tu kwa kusema kwamba mimi sio malaika. Nami pia ninayo madhaifu kama walivyo wanajamii wenzangu hivyo, ninapoikosoa jamii, maana yake ni kwamba nami ninajikosoa pia maana Wazungu wanasema ‘Charity begins at home', yaani wema huanzia nyumbani.
Nipende tu kusema kuwa, takriban wiki mbili sasa, vyombo vya habari vimetawaliwa na habari kutoka Loliondo inapotolewa tiba mbadala ya Mchungaji mstaafu wa KKKT, Ambilikile Mwasapile maarufu kama Babu.
Babu ambaye anatoa tiba mbadala kwa msingi wa imani kwa Mungu, amekuwa gumzo kubwa na kimbilio kwa watu mbalimbali kwa kuwa jamii yetu inaumwa magonjwa mbalimbali yakiwamo hasa ya kimwili yanayosababishwa na mambo mbalimbali kama ugumu wa maisha na mienendo michafu ya kimaisha.
Ndani ya matatizo yanayoshuhudiwa na mashuhuda mbalimbali wa "tiba ya Babu", ni pamoja na udhaifu wa kinga mwilini, kiharusi, kisukari na magonjwa ya moyo ambayo hakika ni tatizo sugu kwa Watanzania na chanzo cha matatizo mengine ukiwamo umaskini katika jamii.
Hivi vitapatikana endapo kila mmoja atapaza sauti ya unyenyekevu na kumlilia Mungu aliponye Bara la Afrika kwa namna na njia aitakayo Mungu.
Hayo ndiyo yametokea Tanzania. Vyombo vya habari zaidi ya wiki nzima sasa vinatawaliwa na habari za tiba mbadala inayotolewa Liliondo mkoani Arusha na Mchungaji mstaafu wa KKKT, Ambilikile Mwasapile.
Tiba hiyo inayokwenda sambamba na imani ya uponyaji utokao kwa Mungu, imekuwa kivutio cha maelfu ya watu toka ndani na nje ya nchi, na inadaiwa kutoa matunda makubwa yanayoshuhudiwa na watu mbalimbali waliokuwa na mgonjwa mbalimbali. Hawa, ni watu wa kada mbalimbali.
Hilo hatukatai kujadiliwa kwa kina maana tunahitaji usalama wetu kwanza ili mambo mengine yajadiliwe kwa hoja na kwa kina, maana amani na usalama au tuseme uzima, ni mtaji wa kila jambo jema.
Hata hivyo, kuibuka kwa "uponyaji" huo ambao ni kazi ya Mkono wa Bwana unaowashukia Watanzania, ambao kamwe haupaswi kuwa mtaji wa kuacha mambo mengine muhimu na badala yake, kuganda juu ya Loliondo.
Ieleweke mapema kabisa kwamba nami ninaunga mkono na wala sipingi watu kwenda kutafuta tiba hiyo mbadala ambayo ina upekee zaidi wa kutumia nguvu ya Mungu, na si kupiga ramli hivyo ni vyema na haki watu waizungumze na huku pia, wakipanga taratibu nzuri za kuendelea na uzalishaji mali na mijadala mingine muhimu kwa taifa.
Mambo yanayolikumba taifa kama ugumu wa maisha unaowatafuna wananchi kiasi kwamba kila siku inaonekana ngumu kuliko jana, bahati mbaya au basi tuseme uzembe uliosababisha takriban watu 40 kupoteza maisha katika milipuko ya mambo iliyotokea katika Kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Kikosi cha 511KJ cha Gongo la Mboto na hata tatizo la mgawo wa umeme ambao umekwenda sambamba na nyongeza ya bei, ni mambo ambayo katu hayapaswi kuzikwa kwa njia ya tiba ya Loliondo.
Watanzania bado wanahitaji majibu ya maswali mengi kutoka kwa watawala, ikiwa ni pamoja na kujua hatima ya malipo ya mabilioni ya pesa za wavuja jasho kutokana na mikataba mibovu na kampuni za ajabuajabu ikiwamo ile ya kufua umeme wa dharura ya Dowans. Wanataka kujua what is up; and what is next (kuna nini na nini kinafuatia).
Watanzania wanayo kiu kubwa kusikia tena "ahadi zile na kama zile" za Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kama bado tatizo la umeme nchini litaendelea kuwa historia ya kukosekana au litabadilika na kutoka hapa ili sasa mgawo wa umeme na kupanda ovyovyo kwa bei yake vibadili mfumo wa masimulizi na kuwa unaoanza kwa maneno, "Hapo zamani za kele, palikuwa na mgawo wa umeme na kupanda kwa bei kila siku…"
Watanzania wanayo hamu ya kusikia Waziri Ngeleja akiendelea "kuuimba wimbo huu" japo hawaoni mchezaji wake katika uwanja ulio wazi.
Watanzania wanahitaji kujua kuna sababu gani za msingi zinazovisukuma baadhi ya vyama vya siasa kutaka kufanya maandamano na kuna sababu gani za msingi za kuwafanya walaumiwe na wasifanye hivyo.
Watanzania wanahitaji mapema kujua mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utaanzaje, utafanyikaje na utamalizika vipi ili Katiba ya nchi iwe ya wananchi wote na isiwe inayowabeba "watoto wa mama" huku wengine ambao labda ndio "watoto wa mama wa kambo, wakiachwa watembee kwenye kokote bila viatu".
Yapo mambo mengi muhimu kujadiliwa bila kuuawa kwa agenda yoyote ikiwamo agenda ya tiba ya Babu kule Loliondo.
Tiba ya Babu iheshimiwe na watu waendelee kupata huduma hiyo ili kwa mapenzi yake Mungu, mwenye kupona apone na mwenye kushindwa, ashindwe maana Bwana ndiye aliyetoa na ndiye anayetwaa.
Watanzania waende kutafuta huduma ya tiba hiyo mbadala kwa imani ya kupata nguvu za Mungu huku wakijua kuwa, imani ndiyo inayopnya na kwamba, hata kabla ya huduma hiyo, magonjwa kama malaria yalikuwapo yakiwa na tiba za kidaktari kutoka kwa wasomi waliobobea, lakini Tanzania tumezika ndugu zetu wengi hivyo, hata tunapopona, tusipone ili turudi "kuanza upya mashambulizi" ya uzembe dhidi ya kanuni za afya.
Tuache hayo, tuendelee kujadili masuala mengine ya msingi pia ikiwa ni pamoja na kwanini watoto wetu waliohitimu kidato cha nne katika mtihani wa mwaka 2010, walifeli katika kiwango cha kutisha.
Tuendelee kutafuta majibu halisi ya kwanini wafeli kiasi hicho ilihali kuna serikali? Kwanini wafeli kiasi hicho ilhali kuna wizara inayohusika na masuala ya elimu; kwanini ilhali kuna walimu na takwimu zinazoonyesha idadi ya majengo ya shule zinazidi kuongezeka?
Tusihamishe hoja na kuishia Loliondo; bali tujiulize na kutaka kupewa majibu kwamba, walimu wanatosha katika shule hizo za sekondari? Walimu wanafanya kazi katika mazingira ya kiutu yanayoonesha wanaheshimiwa na kwamba wanapaswa kutiwa moyo?
Bado tujiulize vitendea kazi kama vitabu vya ziada na kiada vipo, mishahara wanapata kwa wakati na kwa njia isioyowapa usumbufu? Kama hakuna, tujiulize kwanini baadhi ya shule zimekuwa mapango ya popo na nyingine zikikosa walimu?
Yapo mambo mengi ikiwa ni pamoja na tatizo lingine linalozidi kuibuka la ukosefu wa maji safi na salama hata katika maeneo ya mijini ambako eti kuna mabomba. Jamii ijiulize, kina mama kule vijijini watajifungua kwa kutumia mwanga wa vibatari hadi lini?
Ndiyo maana ninasema, Watanzania watumie tiba mbadala ya Loliondo, lakini wasiue wala kusahau mambo mengine muhimu ili hata hao wanaopona, Mungu awajalie wapone na kuja kuishi katika Tanzania inayofaa kuishi.
Majibu kama matatizo ya milipuko katika kambi za majeshi, bado yanahitaji kutolewa ili mzembe ajulikane na ajibu kwanini uzembe wake uwe bei ya mauti ya wengine.