Duru za siasa - Matukio

Duru za siasa - Matukio

LWAKATARE
MASHARIKI YA KATI SYRIA


Kama tulivyowahi kueleza hapo nyuma, suala la mkanda wa video linalomhusu Lwakatare baso limechukua nafasi kubwa nchini. Tulisema kuwa suala lile limeshupaliwa na Polisi kwasababu kubwa moja ambayo ni kuzima kabisa mjadala unaomhusu Kibanda.
Hakika wamefanikiwa sana kwasababu hakuna anayeongelea tena kuhusu Kibanda.

Tulisema Lwakatare amekamatwa bila maandalizi na ndivyo ilivyotokea. Amechiwa na kukamatwa tena ili kuzima hoja ya yeye kuwekwa rumande bila mashtaka. Hatutaweza kuliongelea kwa undani tukijua lipo mahakamani.

Hata hivyo kisiasa suala hili linachukua sura isiyotarajiwa.
Inaonekana kana kwamba limehusishwa sana na Chadema na hiyo ndiyo kete inayotaka kutumiwa kuwamaliza.

Kuna tatizo moja linaloikabili CDM kwasasa.
Kwanza haijulikani mkanda huo ni wa kweli au la kwa kuzingatia kuwa Ludovic na Lwakatare wameonyesha kwa kiasi fulani kufahamu baadhi ya maudhui. Kisichojulikana ni je, hii ilikuwa ni set up''mtego'' au ni hujuma ?

Swali la kujiuliza ni kuwa endapo mkanda huo utathibitika kuwa ni wa kweli, je CDM inawezaje kujiondoa katika kashfa hiyo? Tunadhani viongozi wa CDM lazima wawe makini sana, na kwavile wana wanasheria wanaoweza kufanya analysis ni muhimu sana kuwatumia ili kupata ukweli wa suala zima.

Ni kwa njia hiyo CDM wataweza kuwa salama kama hawapo salama au wanaweza kuitumia hiyo kete vizuri sana kama wapo salama.

Jambo lililowazi ni kuwa suala la Kibanda linaonekana kuzibwa na kitu kisichohusiana nalo kabisa.
Hili linaacha maswali mengi kuhusu mateso ya Kibanda.
Polisi wanatakiwa waje na jibu na si vitambaa vya kuzuia uchunguzi halali na wakina kama suala la Lwakatare.


MASHARIKI YA KATI SYRIA

Hali imekuwa ni tete sana na kuna tuhuma kuwa Asad ametumia silaha za sumu (Chemical weapon) dhidi ya wananchi wake.
Bashir Al Asad ni mtoto wa Rais Hafidh Al Asad. kiti cha urais katika nchi hiyo kimekuwa kama cha kurithi.
Ikumbukwe kuwa chama kinachotawala kinajulikana kama Ba'ath kama kile cha Saddam Hussein.

Chama hicho kimekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 41 sasa. Ingawa serikali ya Asad inaonekana kupoteza uungwaji mkono na sehemu kubwa ya wananchi, kuna makundi yanayo muunga mkono.
Vyombo vya usalama zaidi ya 10 vinamuunga mkono ikiwa ni pamoja na kundi dogo la Alawai ambalo linaundwa na wakristo wengi.

Tofauti na watu wanavyodhani, nchi za kiarabu zina dini zote kwasababu ya historia ya dunia ilivyo.
Kule Iran jews wana viti maalum katika bunge la nchi hiuo, kama alivyokuwa Tareq Azizi makamu wa rais wa Saadam Hussein n.k. Kwahiyo siasa za mashariki ya kati si za ujumla wa Waislam bali kuna michanganyiko mingi ikiwemo Orthodox kama wale wa Misri.

Makundi mengine yanayomuunga mkono Alsaad ni pamoja na wafanyabiashara na daraja la juu.
Nchi za magharibi zimewaunga wapinzani wa Asaad mkono kwa kuwapa silaha wamuondoe madarakani.

Ziara ya Obama nchini Jordan ina maana zaidi kwa kuzingatia kuwa Jordan ni sehemu muhimu sana ya kupitishia silaha kwenda kwa wapinzani.

Katika vita ya Lebanon kati ya Hezboullaha na Israel silaha nyingi za Hezbollah zilitoka Syria.
Kwa wakati huu silaha za wapinzani wa Asaad nyigni zinatoka Lebanon isyokuwa ya Hezboullah.
Inatosha kusema Lebanon na Jordan ni mikondo muhimu ya kupitishia silaha ili kuwafikia wapinzani wa Alsaad.

Pamoja na hayo Al Asaad anapokea misaada kutoka kwa Brotherhood ambao sasa wana shina la kudumu nchini Misri.
Kwahiyo suala zima la Syria ni mchanganyiko wa makundi, na kana kwamba hiyo haitoshi kuna nyongeza ifuatayo.

Kundi la Alqaeda linampiga vita Al Asaad na kiongozi wake Dr Ayaman Al Zawahir ametangaza vita rasmi dhidi ya Syria.
Kwanini Alqaeda wampige vita Asaad inaonekana kama kituko '' Bizzare'' kwasababu wengi walitegemea kumuunga mkono dhidi ya nchi za magahribi.

Sababu kubwa ni kuwa utawala wa baba yake (Hafidh Al Asaad) uliua Brotherhood katika miaka ya 1980 wapatao 10,000 katika mji wa Hama. Waliotekeleza jukumu hilo ni Alawi ambao wengi wao ni kutoka dini ya wakristo.

Na tunafahamu kuwa AlZawahir alikuwa mfungwa kwa nyakati fulani na yeye ni zao la Brotherhood.
Inawezekana kuwa miongoni mwa waliouawa ni wenzake katika harakati.

Lakini pia Syria inalaumiwa kwa kuwasaliti Wapalestina kuhusu vita yao dhidi ya Israel.
Tunakumbuka kuwa katika miaka ya '81 Israel ilichukua kwa nguvu milima ya Golan (Golan height) na kuikalia tokea wakati huo.

Milima ya Golan inatoa sehemu kubwa sana ya maji yanayotumika Israel na milima hiyo ipo katika maeneo muhimu ''strategy position'' iwe Israel kushambulia au kushambuliwa.

Kuanzia wakati huo Syria imekuwa kama imeachia eneo hilo na hili linawaudhi sana waarab wakiwemo Alqaeda.
Kw mtazamo huo ugomvi wa Syria ni faraja kwa Israel na pengine inapunguza pressure ya suala la Wapalestina kwani macho ya dunia yanaelekea Syria zaidi.

Pengine nchi za magharibi zingeweza kuitumia sana Ufaransa kupitia koloni lake la Lebanon.
Tatizo ni kuwa Syria nayo inadai Lebanon ni sehemu yake kihistoria.
Hilo linakuwa ni mwiba mkubwa kwasababu kadri nchi hizo zinavyojizatiti kukabiliana na Asad yapo mengine yanazuka.

Hofu inayofuata ni ya kuingilia kati kwa kundi la Hezboullah chini ya Imam Hassan Nasrallah.
Israel inakumbuka machungu ya vita iliyopita na hivyo isingependa kuvutika katika mzozo huo.

Wakati huo huo, Iran imekuwa inaisadia Syria kwa silaha kukabiliana na wapinzani.

Tunafahamu mtafaruku uliopo kati ya nchi za Magharibi na Iran.
Ni majuzi tu kiongozi wa kiroho Imam Ayatollah Khamenei amesema iwapo Israel itashambulia Iran basi miji ya Haifa na Tel Avivu itateketea. Hilo limekuwa linaitia hofu Israel kwa sababu ni tishio la kweli na linaweza kutokea.

Juzi Obama alikuwa Israel na katika mambo aliyofanikiwa ni kuilazimisha Israel kuomba radhi kwa Turkey kutokana na shambulio la Flotilla lililolaaniwa na jumuiya ya kimataifa.

Israel chini ya Benjamin iliwahi kukataa kata kata kuomba radhi.
Kugeuga kwa msimamo huo ni kutaka Turkey irudi kuwa mshirika wa Israel kwa hofu kuwa kadri siku zinavyosonga mbele vita eneo la mashariki ya kati litakuwa maafa kwa Israel.
Mathalan, Iran inaweza kuitumia Turkey ambayo kijeshi inasimama kidole kwa kidole na Israel (toe to toe).

Wakati huo huo kuna Hezboullah na Brotherhood achilia mbali Tunisia na majirani wengine.
Kwa maneno mengine mizozo inayoendelea mashariki ya kati inaihusu sana Israel kiusalama.

Kwa kumalizia tunasema kuwa hali ya mashariki ya kati inaingiliana sana kisiasa, kiuchumi na kijamii kwahivyo mzozo wa eneo moja ni mzozo wa eneo lote na wala haitegemewi kuwa kundi fulani linaweza kuunga mkono upande mwingine, la hasha! tumeona ya Al qaeda n.k.

Siasa za mashariki ya kati ni ngumu sana na zinaathiri sana usalama wa eneo lote na dunia kwa ujumla.

Tusemezane.
 
Duru za siasa wiki hii itaangalia mambo yafutayo
1.Mzozo wa Korea Peninsula
2. Ziara ya rais wa china nchini
3. Kuangauka kwa jengo.
 
KUANGUKA KWA JENGO DAR

Tuanze na hili lililochukua roho za wenzetu wasio na makosa. Mungu awarehemu na kuwapunzisha kwa amani.

Tukio hili la kuanguka kwa jengo limeonekana katika vyombo vyote vikubwa vya habari duniani.
Siyo kuwa ni tukio la kusikitisha tu bali ni marudio ya matukio ya namna hii.

Tunazokumbu kumbu za jengo la Chang'ombe na Msimbazi ambayo yalikuwa katika hatua za ujenzi kama hili.
Tunazohabari za majengo kadha wa kadha kuanguka achilia mbali ajali za moto n.k.

Jengo lililoanguka lililkuwa la mwekezaji binafsi aliyeshirikiana na NHC. Lilijengwa na mkanadarasi ambaye pia ni diwani.
Utaratibu wa ujenzi wa nyumba kubwa kama hizi ni mrefu na unaohitaji umakini.
Muhimu kukumbuka hapa ni kuwa NHC ni shirika la umma lililopewa dhamana ya kuendeleza ujenzi wa nyumba kwa wananchi.

NHC inamiliki asilimia 25 ya mradi huo. Likiwa ni shirika la umma huu ni mradi unaohusu uwekezaji wa mamilioni ya fedha.
Uwekezaji wake upo katika kutoa kiwanja na hadi sasa hakuna ajuaye mkataba ulikuwaje.
Mambo haya huwa yanafanywa siri kwa kujua kuwa umma ukielewa basi inaweza kuharibu ''deal''

Kwa mtazamo huo NHC haiwezi kamwe kujiondoa katika sakata hili.
Mkurugenzi wa shirika kwanza kabisa alitakiwa awe amejiuzulu kutokana na madhara yaliyotokea chini ya uongalizi wake.

Jengo lilitakiwa lijengwe ghorofa 10 na hadi linaanguka lilikuwa na ghorofa 16.
Katika taratibu za ujenzi kila hatua hukaguliwa na kuthibitishwa na wataalam kuwa mradi upo katika kiwango tarajiwa. Hapa kuna wataalam kama Engineers, watu wa builiding economic, kuna consultant ambaye lazima atakuwa mshauri wa NHC.

Wapo wataalam wa wilaya na mkoa na Jiji la Dar es Salaam nikimaanisha manispaa ya Ilala.
Kwa mtazamo huo hadi jengo linapita ghorofa 10 wataalam hao walikuwa wanafanya kazi zao kama ilivyokusudiwa wafanye.

Kwa NHC ni lazima uongozi ulikuwa unajua kinachoendelea katika mradi huo. Asilimia yoyote inatoa upper hand kwa shirika kufahamu uwekezaji umefikia hatua gani, gharama zake kulingana na mkataba na kwamba mkataba uliheshimiwa kama ulivyosainiwa. Kwahiyo NHC inawajibika kwanza kueleza nini kimetokea na si kueleza bali kuwajibishwa kueleza na kuchukuliwa hatua kama mwekezaji na shahidi muhimu.

Pili, kuna waliohusika na utaalamu wakiwemo wakaguzi wa majengo,wachora ramani na wahandisi.
Hawa nao wanatakiwa mmoja baada ya mwingine wahakikiwe kujua ushiriki wao ulikuwaje na katika hatua gani.

Tatu, manispaa ya Ilala ndiyo inatoa vibali vya uendelezaji wa maeneo. Hata kama kuna mvurugano wa nani afanye nini bado manispaa inadhama ya kujua hilo.
Hapa ndipo viongozi wote wa manispaa wanapotakiwa wawekwe katika kikaango kubaini ushiriki wa kila mmoja.

Kuna mkandarasi ambaye anatakiwa afikishe vielelezo vya namna alivyokuwa anaendeleza eneo hilo kulingana na taratibu.
Nne, kuna wataalam wa wizara ambao katika mradi kama huu lazima watakuwa wana ufahamu wa kutosha nini kimetokea na kwanini. Nani anahusika na kwa vipi.

Tano,bodi ya wanadisi inapaswa kueleza umma endapo huu ndio uhandisi uliokusudiwa na unaosimamiwa na bodi hiyo.
Inapaswa ieleze taratibu zinaotumika katika uhandisi na kutoa ushahidi usio na chembe ya shaka kuhusu ushiriki wa wahandisi wa jengo hilo kwa namna moja au nyingine.

Vinginevyo bodi hii ifutwe kwasababu hakuna mantiki ya kuwa na chombo kisichoweza kusimamia wahindisi.
Hii ni aibu kwa wasomi, wahandisi na taaluma nzima ya uhandisi.

Sita, bodi ya wakandarasi nayo pia iunatakiwa itueleze kama tatratibu zilizingatiwa katika kupata mkandarasi na endapo kandarasi alikidhi viwango viwango vilivyowekwa.

Kwa maneno machache sakata hili linawahusu watu wengi sana. Na inatokea hivyo kwasababu kuu moja.
Rushwa imezidi kila mahali na katika eneo la ujenzi huko ndiko uozo ulipo.
Ni rushwa hiyo ndiyo ilipelekea NHC kutojua nini kinaendelea katika mradi.
Ni rushwa iliyoingia katika taalauma ya uhandisi na ukandarasi.

Kutokana na taarifa ya waziri Tibaijuka ni wazi kuwa mmiliki wa majengo hayo anayo zaidi ya mawili na hivo huu ni mradi mkubwa sana kwa kundi fulani la jamii. Makundi hayo ni kama nilivyoyaanisha hapo juu.
Kuna 10% za kila aliyeruhusu mradi kuendelea kwasababu huo ndio utaratibu wetu uliopo

Huu si wakati wa kuunda kamati za kuchunguza nini kimetokea na kwanini.
Huko nyuma zimeundwa kamati na hakuna lolote lililofanyika. Huu ni wakati wa kuchukua hatua kunusuru maisha ya wananchi kwa maelefu. Ni wakati wa kunusuru sifa za wasomi wa nchi yetu na ni wakati wa kunusuru taifa na aibu hii isiyohitaji pesa za WB au IMF.

Kwa vile rushwa imetamalaki kila ofisi ya nchi yetu hili litapita kama ''upepo'' na hizi tambo tunazoziona ni kujikosha tu.
Wananchi wachukue hatua za kuiwajibisha serikali kwasababu mwisho wa yote hizi ni dalili njema sana za uozo uliovyo ndani ya serikali.

Duru za siasa inatambua kuwa ujanja utakaotumiwa na wamiliki kwa kushirikiana na mtandao wao serikalini ni kukimbia mahakamani ili kuzuia habari kuongelewa zaidi, kupata muda wa kununua wale wanaohusika kutuambia ukweli na kuzima hoja nzima kwa kutumia fedha.

Wakati hayo yakitarajiwa ni vema wananchi wakachukua hatua za shinikizo ili mkurugenzi wa NHC afikishwe kunakohusika ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi kwa uzembe pamoja na timu kubwa sana ndani ya manispaa na wizara.

(tutaendelea na mzozo wa Korea na ziara ya Rais wa China nchini)


Tusemezane
 
ZAIARA YA RAIS WA CHINA
Rais mpya wa China amefanya ziara katika nchi za Urusi na kwa Afica ametembelea Tanzania.
Kutembelea kwake Tanzania mara tu baada ya kuchukua uongozi ilikuwa ni njia mojawapo ya kuongea na bara la Africa.

Kwa maneno machache ziara yake ililenga sana bara hili na wala si Tanzania peke yake.
Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji kwasababu nyingi. Kubwa likiwa urafiki wa muda mrefu wa nchi mbili.

Rais Nyerere alikuwa swahiba mkubwa wa Mao Tsetung pamoja na waziri mkuu Chuon Lai.
Ikumbukwe kuwa Tanzania ilisimama kidete katika kuirudisha china ndania ya United Nation.
Wakati huo balozi wa Tanzania UN alikuwa SAS kama kumbu kumbu zipo sahihi.

Pengine ni kwa msimamo huo thabiti China iliwekeza mradi mkubwa sana barani Africa wa ujenzi wa reli ya TAZARA.
Mradi huu ulikuwa wa msaada na mkopo nafuu ambao ulilenga hasa katika kuzisadia nchi za kusini mwa Africa ikiwemo Zambia.

Huko nyuma wakati Tanzania ikiwa katika hali mbaya kiuchumi, China ilisimama kusaidia pale ilipowezekana.
Urafiki na undugu huu ni wa muda mrefu na hasa jinsi ujamaa wa Nyerere ulivyoangaliwa kule China.

Kwasasa China ni Uchumi mkubwa wa pili duniani. Imeelezwa kuwa kama kasi waliyo nayo kiuchumi itaendelea kama ilivyo basi katika miaka 10 ijayo China inaweza kuwa na Uchumi nambari moja duniani.

Mageuzi ya kisiasa yameisadia sana nchi hiyo kuendelea hasa katika utengenezaji bidhaa na technology ya kiwango cha juu sana. Majuzi wamezindua treni inayokwenda kwa kasi ambayo imefupisha safari ya masaa 22 kuwa masaa 8.

Kwa spidi ya treni hiyo safari ya Dar-Arusha ni takribani saa 1.5.
Utengenezaji wa bidhaa umekuwa nafuu na hivyo kuvutia makampuni mengi ya magharibi kutengeneza bidhaa zake huko. Lakini pia kumekuwa na ongezeko la watu wa daraja la kati na hivyo kufanya soko lake la ndani kuwa kubwa.

Kwa muktadha huo safari ya Rais Jimping haikuwa katika urafiki tu wa maneno.
Ililenga sana kutafuta masoko ya bidhaa zake na pia kutafuta vyanzo vya malighafi.

Pengine kwa kutumia mahusiano ya muda mrefu rais huyo ametumia mwanya huo kufikia malengo waliyojiwekea.
Siasa za wenzetu ni za kiuchumi ''economic diplomacy'' na si za bla bla.

Sisi tunaonekane kuwa ''beneficiary'' wa mikataba mbali mbali ya kutusaidia.
Ukweli ni kuwa sisi ni losers kama hatutatumia fursa hiyo nasi kutafuta mahali pa kuuza kile tulicho nacho.
Hapa sina shaka China ni soko kubwa lakini swali linabaki, je tumetumia fursa hiyo ipasavyo?

Inavyoonekana tumekuwa omba omba zaidi ya kuwa partner katika uchumi.
Mawazo haya potofu yanapelekea sisi kujiona dhalili hata kama tunacho kidogo tulichojaliwa.
Tuna utajiri mwingi wa asili, hivyo ilikuwa muafaka kuhakikisha kuwa tunautumia vyema hasa nafasi kama hizi zinapojiri.

Sidhani kama misaada ya ujenzi wa bandari ni muhimu sana.
Muhimu ni utamaduni wa kutumia kile tulicho nacho kwa umakini, uadilifu na manufaa ya taifa.
Leo ni nani anaweza kutueleza kwanini TAZARA imekufa?
Tazara imekufa kwasababu haifanyi kazi katika kiwango tarajiwa.

Tuna tatizo la kusafirisha mahindi kutoka nyanda za juu kusini, eti tunakodi malori ya jeshi kwa kazi hiyo kwasababu tu tumeshindwa kuitumia Tazara, tumeacha imeharibika kwasababu za poor management.
Tazara haina upungufu wa abiri au mizigo! ina upungufu wa management.

Sasa tunajengewa badari Bagamoyo. Sijui nani aatahakikisha kwa dhati kuwa bandari hiyo itatoa matokeo yanayotarajiwa kama tumeshindwa kuitumia ile ya Dar es Slaam vema.

Tatizo letu ni siasa kutangulia kila mahali na hili la bandari ya bagamoyo ni mojawapo.
Tuna bandari Tanga, Mtwara na kwingineko. Je, tumeshazitumia katika viwango hadi tudhani tunahitaji nyingine Bagamoyo?

Kwa mwendo huu China itatuletea Karanga tubadilishane kwa dhahabu na Almasi.

Tusemezane.
 
Mkuu nguruvi

Sekta ya ujenzi kwa ujumla wake ina madudu mengi sana...rushwa, vifaa vya ujenzi feki, wataalamu makanjanja imekuwa ni vitu vya kawaida kabisa. Mtu yuko tayari kuhonga hata milioni 200 ili apate tenda na akipata hana discipline ya kufanya kazi nzuri! Angalia hata barabara zetu zinavyojengwa siku hizi...mwaka hauishi mahandaki yanarudi upya kama kawaida...Na hakuna mwenye wasi wasi wanajua mwisho wa siku watatangaza tenda nyingine ya kufanya ukarabati!

Kwa hili la jengo lililoanguka NHC wamejiingiza kwenye biashara na kundi la wahuni ama kwa kutokujua au makusudi wakijua wanachofanya. NHC kama partner kwenye ubia huu alipaswa kufuatilia kwa karibu kuhakikisha jengo linajengwa kwa ubora na kwa mujibu wa mkataba waliosaini. Hizo ghorofa 6 za nyongeza nazo zilikuwa kwenye mkataba? Kama jibu ni hapana mapato ambayo yangepatikana yangeingia kwa nani? Sitashangaa kusikia kwamba waheshimiwa walikuwa wamepatiwa apartments kadhaa humo ndani kama "takrima"!!

Hata kama jengo hili lisingeanguka lakini hadi mwisho wa ubia huu NHC wangerudishiwa jengo ambalo ni condemned na kuishia kubomolewa kwa kuwa na kiwango duni na kutofaa kuishi binadamu.
 
Last edited by a moderator:
BARONESS MARGARETH THATCHER AFARIKI

Niwatake radhi kuwa mjadala wa Korean Peninsula utaendelea.
Kutokana na kifo cha Aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza 1979 hadi 1981 Margareth Thatcher tutaangalia kwa ufupi wasifu wake na heshima au mapungufu katika nyakati za uongozi wake.

Baroness ni heshima anayopewa mtu hasa wale wanaoingia katika kundi la Mamwinyi ambao kwa wanaume wanaitwa Lord. Uingereza ina mabunge mawili, kwanza la makabwela (House of common) halafu la Mamwinyi (House of Lord).
Lakini kuwa Baroness au Lord si lazima mtu aingie katika bunge la Mamwinyi, ni heshima kwa watu waliotoa mchango wao kwa taifa. Tafsiri ya neno baroness na wapi linatumika ina utata sana. Kwa mjane wa Lord basi awezaitwa baroness lakini si kimyume chake.Kwa muktadha wa mjadala baroness tuichukulie kama heshima aliyopewa na si vinginevyo.

Baroness Thatcher pia alikuwa Nighted, heshima ya juu sana katika nchi ya Malikia.
Thatcher alizaliwa mwaka 1925 na aliingia katika uongozi wa chama cha Conservative mwaka 1979 akifanikiwa kumuondoa Lord Carrington aliyekuwa waziri mkuu.

Ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo na hadi sasa ni waziri mkuu aliyekaa madarakani kwa muda mrefu katika karne hii kufuatana na kumbu kumbu.

Aliingia madarakani huku vyama vya wafanyakazi vikiwa na nguvu sana na migomo isyokwisha na taratibu alivisambaratisha kwa kuanzisha sera za ubinafsishaji.

Hakika huyu ndiye alikuwa kinara wa ubinafsishaji hadi kufikia mahali watu walikuwa na wasi wasi huenda akabinafsisha hata ofisi maarufu ya 10 downing street ambayo ndiyo ofisi ya waziri mkuu.

Katika mambo yaliyomuondoa madarakani, kasi ya ubinafsishaji ni mojawapo.
Aliondoka madarakani kwa kuondolewa na chama chake kama alivyondolewa Tonny Blair.

Aliyemrithi Thatcher alikuwa John Major ambaye naye alishindwa uchaguzi na Tonny Blair.
Blair kama Thatcher naye aliongoza kwa muda takribani unaokaribiana na kama ipo tofauti ni ndogo.

Katika siasa za nje Thatcher alikuwa na utata sana. Moja ya mambo anayokumbukwa nayo ni kuongoza vita dhidi ya Argentina mwaka 1982 kuhusiana na mzozo wa visiwa vya Folkland.

Pamoja na kutakiwa kufuata usuluhishi wa kidplomasia Baroness alikataa na kuingia vitani akisaidiwa na mshirika wake mkuu mbabe Ronald Reagan.

Marekani ndiyo ilisaidia sana katika kufanikisha zoezi hilo hasa kwa kutumia miundo mbinu na technology.
Hatimaye Uingereza ikaivuruga vibaya Argentina huku kukiwa na makovu ya kutosikiliza ushauri wa kidplonasia kutoka kwa viongozi wengine ambapo lawama zinamwendea mama Thatcher.

Thatcher ingawa alipinga ubaguzi wa rangi, yeye alisimama kutamka wazi kuwa Mandela alikuwa ni gaidi.
Kifo chake kimepokelewa kwa namna tofauti kwa nchi za Kiafrika kutokana na msimamo wake kuhusu suala hilo.

Kwa upande wa China, Thatcher alishindwa kuwashawishi ili Uingereza iendelee na mkataba wa miaka 50 katika visiwa vya Hong Kong, huku Ulaya akikataa kata kata Ujerumani magharibi kuungana na Ujerumani mashariki.

Yeye alimuona kiongozi wa Ujerumani wakati huo H. Kohl kama mpinzani wake jambo lililopelekea kuonekana udhaifu wake hasa kuhusu siasa za Ulaya.

Lakini pia alikuwa mshiriki mzuri sana wa Marekani na kutokana na mahusiano yake na Reagan iliyokuwa Urusi ilisambaratika na hivyo kuondoa tishio la vita baridi.

Kwa upande wa uchumi, Thatcher alijenga matabaka na hilo likabaki kuigawa Uingereza kimatabaka huku kukiwa na tabaka dogo la juu na la kubwa la chini. Kwa wenyewe wanasema alikuwa true conservative au mhafidhina haswa.

Kwa kumuangalia Thatcher kuna mambo mengi ameyaacha nyuma yake, mazuri na mbaya.
Kwahiyo Legacy yake ina mchanganyiko.

Ataingia katika kundi la viongozi manguli wa karne lakini hatafikia daraja la akina Winston Churchil.
Thatcher atafanyiwa mazishi ya kitaifa yatakayoambatana na heshima zote za kijeshi.
Atazikwa katika makaburi ya watu mashuhuri wa Uingereza.

Katika miaka hiyo Thatcher alikuwa na akina Ronald Reagan, Mikhaili Gorbachov, Tito, Willibrand, Nyerere,Boumediene na wengine kadha wa kadha.Wengi wa Watu walioko katika kundi lake kwasa sasa ni marehemu.

Thatcher aliyejulikana kama Iron lady kwa misimamo yake ameondoka na sasa kilichobaki ni wasifu wake.
Funzo moja muhimu ni kuona viongozi wote wa kisiasa wa Uingereza wakiwa pamoja katika kueleza mazuri na uzalendo wa wa Thatcher katika nchi yake. Yeye kama mwanadamu alikuwa na mazuri na mapungufu yake.

Muhimu ni kuangalia aliifanyia nini nchi yake, na je viongozi wetu wanajifunza nini kuhusu legacy pale watakapokuwa nje ya madaraka au kuondoka duniani.

Tusemezane.
 
MAATUKIO YA KIGAIDI MAREKANI

Kumetokea mlipuko wa mabomu katika mbio za masafa marefu za Marathon mjini Boston Marekani.
Hadi leo watu watatu wamepoteza maisha na wengine 178 wakiwa wamejeruhiwa, 13 katika hali mbaya.

Ni tukio la kigaidi ambalo hadi sasa ''motive'' yake haijulikani.
Mabomu yaliyolipuka ni mawili katika muda wa tofauti ya sekunde 15 umbali wa Yadi 100.

Taasisi zote za uchunguzi za Marekani zipo katika uchunguzi wa hali ya juu kwa kushirikiana na zile za majimbo.
Hadi sasa kilichopatikana ni mfuko wa kubeba mgongoni (back pack) na sampuli ya mabaki ya bomu hilo vyote vikiwa vimeharibika katika kiwango kidogo.

Mara baada ya tukio hilo mtu mmoja raia wa Saudia alijeruhiwa pia na alikuwa hospitalini chini ya ulinzi mkali.
Kuna habari za nyumba yake kufanyiwa msako na wachunguzi kuondoka na vitu.
Pia kuna habari za kijana mmoja kutoka Saudi Arabia anayeishi kwa visa kuwa katika uchunguzi.

Kwasasa FBI wanasema wanazo picha nyingi zilizotumwa kabla na baada ya tukio na wanazifanyia uchunguzi.
Jambo moja muhimu ni kuwa Camera moja iliyokuwa juu ya jengo haikuharibika na hiyo ilikuwa na picha muhimu sana kufuatana na taarifa yao.

Imeonekana kuwa bomu hilo halikuwa la kishindo kikubwa wala la kitaalam kwani limetengenezwa na pressure cooker iliyojazwa misumari na vitu vingine ili kuleta madhara zaidi kwa wanadamu.

Uchunguzi unakusanya kila punje ya kitu katoka eneo la ajali.
Hilo ni muhimu sana kwasababu kuna clue nyingi zaweza kupatikana kutoka mkusanyo wa vitu hivyo.

Kuna uwezekano wa kupata namba za pressure cooker, kampuni iliyotengeneza, maduka ilipouzwa na nani amenunu na kwa njia gani.

Wakati hayo yakiendelea kumekuwa na uchunguzi kila mahali kama vile namba za simu, nani alipiga na kwa nani.
Hizo nazo zaweza kutoa picha kwa namna fulani.

Katika suala la uchunguzi wenzetu wamepiga hatua. Ingawa hajakamatwa mtu, dhidi ya yote lazima mtu atakamatwa.
Uchunguzi wa wenzetu ni wa kitaalamu kwa kutumia watalaam na taaluma.

Kwakweli inasikitisha sana kuona sisi hatuwezi kukamata mtu aliyefanya uhuni kama tunaoushuhudia kukiwa na kila aina ya ''viashirio''. Labda kwa hili niseme sisi ni dunia ya ajabu wala siyo dunia ya tatu.

Kwanini mpaka sasa kuna ''people of interest'' na siyo watuhumiwa?
Kwa wenzetu kumkamata mtu katika tukio kama hilo kunaweza kuleta matatizo ikithibitika kuwa hana hatia.
Hivyo vyombo vinajitahidi sana katika kuhakikisha kuwa kuna uhakika wa kile kinachofanyika.

Lakini pia kuna funzo moja muhimu kutoka Marekani.
Wakati mji wa Oklaham ulipopigwa mabomu na mamia ya watu hasa watoto kupoteza maisha, watu wote walijua ni magaidi kutoka mashariki ya kati.

Baada ya uchunguzi mtuhumiwa alikamatwa 'Tom mcveigh'' ambaye ni mzungu.
Kwahiyo dhana nzima ya ugaidi ilionekana kama kuogopa kila kitu hadi kivuli chao wenyewe na kwamba si kila tukio lazima litoke nje.

Jambo moja ninaloweza kuandika leo ni kuwa FBI walisema kuwa kesi hii haitakuwa ngumu kama walivyodhani.
Kuna uwezekano wanao watuhumiwa na sasa mtandao mzima unafuatiliwa au kujua habari zaidi kuhusu tukio hilo.

Wakati hayo yakiendelea kuna mtu mmoja amekamtwa kuhusiana na kutuma barua kwa Seneta mmoja na leo hii Rais Obama zikiwa na sumu ya Ricin.

Racin ni sumu kali sana kiasi kwamba punje ya mchele ni kubwa sana kutoa roho ya mtu.
Barua zote zilikuwa na chembe hizo imethibitika.

Kuvurugiga kwa mpango huo wa sumu kunatokana na barua hizo kuwa 'intercepted' kabla ya kuwafikia walengwa.
Hakukuwa na hatari ya karibu kwa seneta na Rais Obama kusema kwa uchache na wala barua hizo hazifungamani na tukio la Boston hadi leo kwa mujibu wa taarifa.

Katikatukio la Boston siasa nazo zimo ndani yake. Ikulu ya Marekani ilitoa picha ya rais Obama akiwa amekaa na simu akiongea na maafisa usalama na wengine wakiwa katika simu.

Ingawa Republican wanonekana kuwa kimya, tayari picha hiyo imeanza kuleta mzozo wa kisiasa.
Republican wanasema hiyo ilikuwa ''show off'' wakati wa ajali na Obama ametumia maumivu ya watu kisiasa.

Ni suala la muda tu tutasikia siasa nyingi kuhusu tukio hili ambalo ni la kwanza kutokea tangu Obama ameingia madarakani. Matukio kama haya kwa siasa za Marekani hugeuzwa kuwa mitaji ya kisiasa kwa namna mbali mbali.

Funzo moja ni jinsi wenzetu walivyojiandaa katika kukabiliana na majanga.
Katika tukio lile la Boston kila resource ilitumika katika kunusuru maisa ya watu.
Na uchunguzi kama nilivyoeleza ni wa kina na wala si lelemama kama wa kwetu hapa nyumbani.

Duru inafutailia na kukuhabarisha kila mara.
 
BOSTON BOMBING
MANHUNT YAMALIZIKA.

Jiji la Boston lililzimika kufunga shughuli zake kwa siku nzima ya Ijumaa ili kupisha vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi ya kumtafuta mtuhumiwa wa pili baada ya yule wa kwanza kuuawa katika mapambano na Polisi.

Kama tulivyosema katika bandiko lililopita FBI na Polisi wa Boston walisema tukio hili halikuwa la kukanganya kama ilivyokuwa imeonekana. Mapema alhamisi FBI walitoa picha za watuhumiwa kama walivyo naswa na Camera mbali mbali hata mkanda wa video ulivyoonekana.

Hakukuwa na shaka kuwa wao walikuwa watuhumiwa kwasababu mmoja alionekana akiweka begi chini na walikuwa wakitembea kama watu wenye mipango fulani. Wachunguzi wa mambo ya usalama wanasema ilikuwa ni wazi kuwa hawa wangelionekana mapema kabla ya kulipua.

Baada ya hapo tafuta tafuta ya wapi walipo ndipo ilipoanza na ni katika chuo cha ufundi MIT kulitokea mapambano na Polisi mmoja kuuawa na mwingine aliyekuwa hayupo kazini kujeruhiwa.

Watuhumiwa ni mtu na mdogo wake mkubwa akiwa na umri wa miaka 26 na mdogo miaka 19. Wote ni wazawa wa Chechenya kule Urusi.

Mtuhumiwa wa kwanza aliuawa katika mapambano na Polisi na yule mdogo kutoroka.
Hali hiyo ililazimu msako wa nyumba hadi nyumba ikiaminika kuwa walikuwa bado katika mji wa watertown na hivyo kuto toa nafasi nyingine ya wao kutoweka.

Mtuhumiwa mdogo alitoroka na gari waliloteka na inaamika kuwa wakati wa mapambano aliendesha gari na kumkanyaga nduguye aliyekuwa majeruhi bila kufahamika kama ni makusudi au ilikuwa katika harakati za kujiokoa.

Yeye alipatikana jana akiwa katika boti nyuma ya nyumba mmoja ambapo kuna mtu aliona kitu katika boti hiyo na baada ya kusogelea aligundua kuna damu.

Polisi walifika kwa kutumia helcopter ambayo ilitoa miali maalumu kubaini kama kulikuwa na mtu.
Hata baada ya hapo ilibidi boti hiyo iondolewe kwa tahadhari kwani mtuhumiwa alirusha risasi kabla ya kuishiwa na kujisalimisha.

Mtuhumiwa sasa yupo hospitali akiuguza majeraha ya shingo na mguu aliyoyapata wakati akiwa na kaka yake siku alipouawawa.

Kupatikana kwao ni kutokana na matumizi ya teknolojia. Mara baada ya picha zao kuwekwa hadharani FBI walipokea hadi video wakiwa katika duka moja na walinunua bidhaa kwa kutumia credit card ya kughushi.

Habari zilizopelekwa Polisi zilikuwa ni nyingi na zilizotoa mwelekeo sana ingawa FBI inaonekana walishakuwa na habari zao zaidi ilikuwa suala la muda.

Watuhumiwa waliondoaka Chehenya na kuja Marekani katika miaka 1999. Mwaka jana kaka mkubwa ambaye ni marehem alirejea Chechnya na alikaa kwa miezi 6. Inasemekana aliporudi alikuwa radicalized zaidi na hilo liliwashangaza sana wenyeji.

Chechnya ni jimbo lililo karibu sana na Dagastan na nchi za kiarabu. Wakazi wake wengi ni waislam na wamehusishwa mara nyingi na tuhuma za kigaidi.

Kinachochanganya watafiti ni kuwa vijana hawa wamekulia Marekani na has mdogo ambaye hajui Chechnya kwa uhakika.
Sasa ni vipi alikuwa radicalized na nina walio nyuma yao? Kwamba hawa ni watu wanaoijua Marekani zaidi kwa tamaduni imekuwaje hadi wakafikia hatua hiyo?

FBI bado wanamlinda mtuhumiwa aliyekamatwa ili pengine kupata habari zaidi. Mtuhumiwa yupo katika hali mbaya lakini stable hivyo inatarajiwa atapona na kutoa taarifa zaidi.

Hapa kuna mambo mawili, mtuhumiwa anaweza kushtakiwa na serikali ya Marekani(Federal) na akipatikana na hati adhabu ya kifo ipo mbele yake. Au anaweza kushtakiwa Boston ambako hakuna adhabu ya kifo.

Pamoja na mashtaka ya ugaidi kuna mashtaka yanayotokana na vifo na ni wazi kuwa maisha yake yataishia magereza ima kwa kifungo cha maisha au kwa kunyongwa.

Jitihada za kupata watuhumiwa hawa zilifanikiwa kwa kutumia mbinu za kisasa na kisayansi.
Hakika kwa aliyefuatilia ni dhahiri kuwa wenzetu wamejipanga kukabiliana na majanga.

Hata utoaji wa taarifa ni wa mpangilio ukifuata muda na matukio. Kwamba taairfa za Polisi zinabaki kuwa za Polisi bila kuingiliwa na wanasiasa.Ni utaalamu wa hali ya juu sana katika kukabiliana na uhalifu.

Sina hakika kama Polisi wa nchi yetu walipata fursa ya kujifunza chochote kuhusiana na tukio hilo.
Ni wazi kuwa bado safari yetu ni ndefu na tunapaswa kukimbia wenzetu wakitembea.

Tusemezane
 
DURU ZA MASHARIKI YA KATI
TANZANIA

Vita kati ya wapinzani na serikali ya Al-Assad inaendelea. Inavyoonekana hakuna maendeleo ya aina yoyote kwa upande wa wapinzani hasa tukizingatia kuwa sasa ni takribani mwaka wa pili.

Nchi za Magharibi zimetoa msaada kwa wapinzani. Kilichojitokeza ni kuwa msaada huo haukuhusu mambo ya kijeshi.
Kuna habari kuwa sehemu kubwa ya wapinzani ni wafuasi wa Al-qaeda na nchi za magharibi zina wasi wasi na mustakabali wa nchi hiyo kama itaangukia mikononi mwa watu wenye misimamo mikali ya kisiasa inayoambatana na itikadi

Wasi wasi mkubwa ni jinsi ambavyo Israel itakuwa katika wakati mgumu hasa kwa kuzingatia mabadiliko ya kisiasa ya siku za karibuni pale mashariki ya kati.

Wiki hii kuna habari za serikali ya Syria kutumia silaha za kemikali dhidi ya wapinzani.
Habari hizo zimethibitishwa na Israel, UK na USA. Tukio hilo linaonekana kubadili hali ya mambo.
Huenda likatumika sasa dhidi ya Asaad kwasababu tu sababu za kufanya hivyo zitakuwa zimepatikana.

Kuna hoja kuwa kwanini Marekani haijaingilia kati suala hilo. Ukweli ni kuwa vita mbili za Iraq na Afghanistan zimekuwa ni mzigo na tatizo kwa nchi hiyo. Hivi sasa Obama anafanya kila jitihada za kumaliza vita ya Afghanista na asingependelea kuingiza nchi katika vita nyingine.

Kinachoweza kutumika ni ile mbinu ya Marekani kuwa msaidizi wa majeshi ya NATO kama ilivyokuwa Libya.
Ingawa inaonekana kama hakuna mkakati, ni suala la muda na sababu zimeshaanza kupatikana Alsaada atashambuliwa kama ilivyokuwa kwa Ghadaf au kule Mali.

Kitendwaili kikubwa ni kuwa nani anayeaminika kuiongoza nchi ya Syria?
Inavyoonekana hakuna mtu au watu walioandaliwa hivyo kukabidhi nchi kwa watu wengine yanaweza kujirudia yale ya Afghanistan na Osama ambaye ukweli unabaki kuwa aliandaliwa na Marekani kupambana na Soviet ya wakati huo na baadaye kuwageuka.

TANZANIA
Kumekuwa na tukio la kuuawawa kwa mawanafunzi katika chuo cha uhasibu Arusha.
Mauaji hayo hayajulikani yalitokana na nini. Kilichojitokeza ni wanafunzi waliojawa na hasira za msiaba wa mwenzao kutaka kuandamana hadi ofisi ya mkuu wa mkoa.

Hali hiyo iliweza kutulizwa na mbunge wa Arusha Lema ambaye aliitwa na wanafunzi kama mwakilishi wa wananchi.
Pamoja na mkuu wa mkoa kutaarifiwa juu ya tukio hilo, bado alifika eneo la tukio huku akiwa amejaa dharau na kauli zisizoonyesha hekima za uongozi.

Ilitegemewa kuwa mkuu wa mkoa ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.
Kwa bahati mbaya hadi siku anafika katika tukio ''hakuwa na taarifa'' za kuuawa mwananchi jambo lisilo la kawaida katika taratibu za uongozi na mantiki za kibinadamu.

Kifo cha mtu ni tukio kubwa ambalo viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wanapaswa kuliona.
Kamanda wa Polisi ni sehemu ya kamati hiyo na kwa taratibu kila asubuhi hupewa taarifa juu ya tukio na pengine alipaswa kumweleza mwenyekiti wa kamati ambaye ni mkuu wa mkoa.

Hata kwa mantiki ya kawaida bado mkuu wa mkoa alipoitwa alitakiwa awe na ufahamu anakwenda wapi na kuongelea nini.
Wasaidizi wake ikiwa ni pamoja na viongozi lukuki walipaswa wawe wamempa taarifa ya nini kimetokea.

Katika eneo la tukio,mkuu wa mkoa alipaswa kuwa kiongozi wa kwanza kuonyesha hisia za tukio na kuomboleza na wanafunzi. Yeye kama kiongozi na mzazi alipaswa afahamu anaongea na vijana ambao mara nyingi huwa na mitazamo tofauti na hawana muda wa kuficha hisia zao.

Majibu mepesi katika hali ya mtafaruku namna ile ilikuwa ni kuchochoea moto badala ya kuuzima.
Maswali yabaki kuhusu utitiri wa viongozi katika mikoa.

Hebu tuangalie kwa uchache

Inaendelea......
 
Inaendelea...

Katika mkoa kuna mkuu wa mkoa, mkuu wa Wilaya, kamanda wa Polisi wa mkoa, mkuu wa Polisi wa Wilaya.
Katika jiji la Arusha ni wazi kutakuwa na Mbunge, meya, madiwani n.k.

Haiiingii akilini kuwa hadi mwanafunzi anauawa (tukio ambalo lazima ligonge vichwa vya wahusika) si mkuu wa Wilaya au Polisi aliyekwenda kuonana na wanafunzi hao.
Japo basi Mbunge Lema alikwenda kuonana nao na kuwatuliza kwa kuanzia ili jambo lizungumzwe.

Mkanda wa video unaomwonyesha Lema akiongea na ukitizamwa kwa makini hakuna mahali ambapo mtu anaweza kusimama na kujenga hoja kuwa kulikuwa na uchochezi. Badala yake Lema alitumia fursa ya kuongea na wanafunzi hao na kuwaasa kuhusu hali ilivyo huku akisema haijulikani kwanini mwanafunzi yule aliuawa.

Kimsingi Lema kama Mbunge alifanya kazi wapiga kura wake waliotarajia aifanye.
Nayo ni kuwasiliana na mkuu wa mkoa na kumpa taarifa kuhusu hali tete ya usalama inayotokana na wanafunzi hao kuwa na jazba achilia mbali tukio zima la mwanafunzi huyo kuuawa.

Siku nne zilizopita Lema alikamatwa saa 5 usiku. Hadi sasa sababu za kukamatwa kwake hazijawekwa hadharani.
Ni dhahiri kuwa tukio la mkuu wa mkoa kushambuliwa kwa mawe huenda ndio chanzo.
Na kibaya zaidi ni zome zomea aliyokumbana nayo kiongozi huyo mpungufu wa hekima na busara.

Tuseme kuwa Lema ni mbunge ambaye upatikanaji wake hauna shaka. Katika taratibu za kawaida jeshi lingeweza kuwasiliana naye ili kupata maelezo. Endapo angekaidi basi jeshi lingekuwa na sababu za kutumia njia nyingine.

Lakini basi hiyo njia nyingine ingeweza kufanyika mchana na wala si usiku wa saa 5.30.
Pengine tukio hilo lilifanywa ili kumdhalilisha kwa namna fulani.
Hata hivyo taratibu za kumkamata mtu zinaambatana na kumweleza sababu za kukamatwa kwake.

Leo ni siku ya nne mtuhumiwa Lema yupo chini ya ulinzi bila kufunguliwa mashtaka.
Huu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na pengine matumizi mabaya ya nguvu za dola.

Kwa wananchi wengi wa Tanzania, mtu anaweza kukamatwa akaswekwa rumande bila sababu na kisha kuachiliwa huku akidhani kuwa amefanyiwa hisani na si uonevu. Tabia hii ni hutokana na upungufu wa kuelewa haki za wananchi.

Maswali ya kujiuliza ni kuwa, mbunge Lema alifanya kosa gani kuongea na watu anaowawakilisha?
Na kama ni uchochezi iweje basi hadi leo hajafunguliwa mashtaka?
Ni kwanini serikali itumie nguvu kubwa kumsaka Lema na wala si muuaji wa mwanafunzi?
Na kwamba mkuu wa mkoa alitumia busara na maarifa ya kiuongozi kuzuia mtafaruku uliojitokeza?

Maswali hayo hatuna majibu nao kwasababu sasa hivi mauaji yamekuwa jambo la kawaida na si tukio la kutisha.
Tumeona mlolongo wa matukio yakihusisha wana habari, viongozi na wanachama wa vyama vya siasa.

Tumeona hata vyama vya siasa vikitoa kauli za kukubaliana na ukiukwaji huo wa haki za binadamu.
Kwa mtazamo wa haraka suala hili linachukua mkondo wa kisiasa kuliko haki za wananchi.

Kwavile litaingia katika siasa kwa namna ambayo haikupaswa,ni wajibu wetu kuonya kuwa amani ya nchi haitegemei siasa bali ni jukumu la kila mmoja. Jukumu hilo ni zito sana kwa waele wenye dhamana.

Tukio hili halipaswi kuwa la kisiasa na kama vyama vya siasa vitalipeleka huko basi usalama wa nguruwe mwituni ni mzuri zaidi kuliko ule wa mtanzania wa kawaida.

Tukio linaiweka serikali na Chama tawala katika wakati mgumu. Ni jambo lisilowezekana kuwa serikali ya chama tawala imeshindwa kutafuta suluhu japo basi kuomboleza na wanafunzi kwa njia nzuri bali kutuma watu ambao ubinadamu wao ni kwa kuhojiwa ''in question''. Mkuu wa mkoa hawezi kutumia tambo na majigambo katika maisha ya watu!!

Mkuu wa mkoa ni mteuliwa wa rais anayetokana na CCM. Kwa maneno mengine CCM sasa imeshindwa kulinda mali na uslama wa raia hata kufanya dhihaka kali kama aliyofanya mkuu wa mkoa.

Chuki hiyo pamoja na ile ya kumkamata mbunge Lema inazidi kuwazindua watu kuhusu jinsi CCM ilivyoshindwa kusimamia utendaji wa viongozi wake pamoja na serikali inayotokana na chama hicho.

Ikumbukwe kuwa walioguswa sana na msiba huu ni wanafunzi pamoja,wazazi wa marehemu na watu wa kawaida.
Hawa ni ''jeshi'' lisiloonekana lakini wakati wa chaguzi nguvu yao ni kubwa sana kwasababu wanaishi na wapiga kura.

Kitendo cha kumkamata Lema akiwa ni kiongozi wa chama cha upinzani na huku kukiwa na hali ya sintofahamu kuhusu kiongozi mwingine Lwakatare ni muonekano wa uonevu kwa mtazamo wa average Tanzanaian.

Kwa mtazamo huo wa kushindwa kusimamia haki za raia, kukamata viongozi wa wananchi na si wahalifu, CCM inaelekea mahali ambapo ni ngumu sana kutoka. Chuki wanayoijenga itawagharimu sana na itakuwa ushahidi siku ya hukumu ya nani aongoze nchii hii. Wananchi wanaweza kuwa wamefikia mahali pa kutochagua sera za vyama bali kuchagua kuiondoa CCM

Hatudhani kuwa nguvu za dola ni suluhisho la matatizo.
Mubarak hakuweza, Kaunda hakuweza, Moi hakuweza na wengi wengineo. CCM itaweza ?

Tusemezane.
 
KUCHAFUKA KWA HALI YA SIASA BUNGENI

CCM HAWANA HOJA, CHADEMA WASIFUATE MELI ILIYOPOTEZA UELEKEO

Katika wiki chache zilizopita tumeshuhudia bunge likiwa sehemu ya matusi, kejeli, dharau na ufidhuli wa kila aina.
Hili ni bunge lililojaza wasomi wa kada ya kati na ya juu wengi wao wakiwa vijana.

Huko nyuma kumekuwa na mjadala kuhusu vijana kukabidhiwa dhamana ya kuliongoza taifa ili kuleta damu mpya inayoendana na wakati.

Kwa hali iliyokuwepo bungeni wiki zilizopita nabaki nikiridhika na msimamo wangu uongozi ni hekina na busara na wala si umri au jinsia. Kama ingelikuwa kinyume na hayo leo hii tungesikia hoja za kulisadia taifa kuliko wakati mwingine wowote ule wa taifa hili kujitawala.

Nimegusia jinsia kwasababu kuu moja, kwamba sasa ni wakati wanawake nao wapewe fursa za uongozi wa juu wa taifa hili. Endapo tunadhani kuwa uongozi una nasaba na jinsi basi itabidi tujiulize kama tunafikiri sawa sawa.

Matokeo ya kuvurugika kwa bunge ni kulegea kiti cha Spika.
Spika ni kiongozi wa umma bila kujali katoka chama gani.Ndiyo maana yeye huvaa joho lenye nembo ya taifa na wala si ya chama anachotoka. Bunge linaendeshwa kwa kanuni ili kulifanya liwe na staha na hadhi tarajiwa na wala si soko la wapuuzi na kijiwe cha wendawazimu.

Wendawazimu huo unatokana na Spika mwanamke aliyechaguliwa kwa sababu ya uanamke wake kushindwa kuongoza kwa kufuata misingi waliojiwekewa na badala yake kuhudumia chama chake kana kwamba chama ndicho kinagharamia shughuli za bunge. Bunge si mkutano wa CCM ni sehemu ya umma (public square yenye heshima yake)

Upendeleo wa wazi na kuruhusu wabunge wa CCM kuporomosha mitusi ya nguoni ni sehemu ya udhaifu mkubwa wa mama Makinda. Sijui kama mama Makinda anaelewa tatizo la nchi hii.

Kwa vile anafanya kazi karibu na wale wasiojua kwanini sisi ni masikini sidhani kama anaweza kuwa na ufahamu mwingine zaidi.

Nilitegemea wabunge wa CCM wenye serikali na chama tawala wawe mstari wa mbele kuisimamia serikali yao kufanya kile walichowaahidi wananchi. Hakika CCM ina mambo mengi sana na tungetarajia wapinzani wawe watu wa kuporomosha mitusi tunayoiona kwa vijana na wasomi kama akina Nchemba.

Kinyume chake Chadema wamekuwa wanajenga hoja zinazowagusa wananchi.
Pamoja na kufinywa na kudhulumiwa haki zao kama wabunge bado wanapopata nafasi huzikuna nafasi za Watanzania.
Chadema kama wanadamu wengine nao wamefikia kikomo cha uvumilivu na sasa wanaingia katika kujihani pengine kwa kujibu matusi kwa tusi.

Kwa wananchi wanaofuatilia bunge hakika ni wazi kuwa CCM imepoteza mwelekeo. Chama tawala kinapokuwa na mabingwa wa matusi na wala si sera basi chama hicho kipo katika wodi ya wagonjwa mahututi ''ICU'' pengine kikielekea mortuary kule walikopunzika akina UNIP, KANU n.k.

Ningewakumbusha Chadema kuwa sasa hivi wabaki katika hoja za msingi za kuelezea na kutetea hoja za kitaifa.
Ni wakati na fursa nzuri sana kwao kujipambanua kuwa wapo tayari kuliongoza taifa.

Wapo katika bahari yenye mawimbi na kina kirefu. Wasichotakiwa kukifuata ni kulilia kudandia meli iliyopoteza mwelekeo, meli inayoyumba ikiwa haina rubani.

Meli hiyo ya CCM imepoteza nguvu za mashine na inaelekea kusikojulikana.
Chadema jiepusheni na matusi, jikiteni katika kujenga hoja, taifa na wananchi wanasikia hoja zenu na si mitusi iliyobobea.

Lakini pia kuna funzo moja kubwa hapa. Je, kwa mtazamo wa Makinda kuna haja ya kupata viongozi kwa kuangalia jinsia?
Nina hakika kama hilo litakuwa kigezo basi sasa hatuna uhakika wa kuwa na mwanamke kiongozi tena.

Lau kana ni kuangalia uwezo, basi wapo akina mama wengi wenye uwezo.
Sasa ni jukumu la akina mama kumsihi mwana mama mwenzao aachie ngazi kabla hajawaharibia zaidi.

Kwa upande mwingine,lazima tujiulize hivi hawa vijana tunaoambiwa wana nguvu na fikra mpya ndio kweli tunaowaona bungeni. Kuna umuhimu wa kuwa na vijana katika uongozi au ni muhimu kuwa na uongozi wenye maono, hekima na busara!

Na mwisho tusisahu kuwa rushwa ndiyo iliyotupatia viongozi wa bunge.
Spika aliwekwa maalum na kundi lake ambalo sasa hafanyi kazi tena ya taifa bali kazi ya wale waliofanikisha upatikanaji wa kiti chake. Hayo ndiyo madhara ya rushwa, si lazima fedha au ufisadi, rushwa ya uongozi ni ghali zaidi.

Ujumbe wa leo, vijana mlioko bungeni ninyi ni sehemu ya tatizo katika taifa hili. Hamkutumwa na wananchi kukusanya mishahara minono na allowance ili muonyeshe ujahili wenu wa kuporomosha mitusi.

Mnaweza kukaa kimya na kuendelea kula posho na mishahara minono. Kutoa mitusi kwa kutumia jengo lililojengwa na kodi za wananchi, umeme na vipaza sauti vinavyolipiwa na wananchi ni kutukana wananchi kwa kiwango cha hali ya juu.

Mama Makinda na Job Ndugai, taifa hili ni moja ya mataifa masikini sna duniani.
Kuendelea kwenu kukalia kiti msichokiweza ni kuudhalilisha utu wa mwanadamu na Mtanzania.

Taifa lingewashukuru sana kama mngekaa pembeni mkaachia wenye uwezo waliongoze bunge.
Hakika uwepo wenu katika kiti cha Spika ni kuwakumbusha watanzania machungu makali wanayoishi nao kila siku.
Hamna namna ya kurudisha heshima yenu ila kwa njia ya kujiuzulu.

Mnaweza kuamua kukaidi na kukalia kiti hicho lakini muelewe taifa haliwaangalii kama viongozi bali walafi wachache wanaokusanya pesa kwa ajili ya kumalizia majengo yao.

Taifa linawangalia kama washirika wakubwa wa umasikini, maradhi na ujinga.
Taifa linawangalia kama watu waliopoteza heshima. Fikirieni ya kuwa mtaangaliwa vibaya mpaka lini?

Tusemezane
 
Well said Mkuu Nguruvi3, ulivyonena ndivyo haswa ilivyopaswa kuwa. Uongozi ni Hekima na Busara ndio maana hutokea Ubunifu wenye tija ndani yake.
Uongozi si Umri wala Jinsia. Lakini katika misingi ya demokrasia, Uongozi ni Umri na Jinsia. Kilichomuingiza Makinda bungeni ndicho hicho. Demokrasia kwa watu weusi kamwe haitoi fursa kwa Busara na Hekima kuwa vigezo vya uongozi, kigezo kikuu ni aje unaweza kuteka hisia za wapiga kura(umaarufu wa aina yoyote), na ndio maana anayeonekana ni tumaini naye anapanda meli iliyokwisha poteza mwelekeo. HISIA za wapiga kura juu ya mgombea zina nafasi kubwa sana kuliko akili zake kwa asilimia kubwa sana ya wapiga kura wote. Niliwahi kusema hapa kuwa, kuna HARAKATI ZA KISIASA(kwa tafsiri siasa ni kiini macho) na HARAKATI. Harakati za kisiasa ni utafutaji wa kuungwa mkono kwa kuteka HISIA za wengi, ndio maana tunaona watu maarufu ndaniye, na wanakubalika. Wakati HARAKATI, kama neno lilivyo kavu, ni kuipigania kweli kulinda maslahi ya jamii yote, kwa kufanya hivyo halengi hisia zetu bali AKILI zetu. Lakini katika misingi ya wengi wape, ukifanya hivyo Umeumia kama una uchu wa madaraka. Je, ni nani kwa sasa amekosa uchu huo? Ni haki yao kudandia meli iliyokwenda mrama. Na tunaposema kuteka akili za watu si kwa maneno tu, bali ni kwa vitendo pia. Matendo yako ndiyo yatakayohalalisha maneno yako, si porojo tu. KILA MTU ANA AKILI, ILA KATIKA KUELEWA INATEGEMEA UNATUMIA NJIA GANI KUMUELEWESHA.
Mungu wetu anaita sasa!
 
Last edited by a moderator:
BOSTON MARATHON
WENGINE WAKAMATWA

Katika hali ya kutafuta washiriki wa ulipuaji wa Boston, FBI wamefanikiwa kupata watu wa karibu wa Dhozokhar na Tamerlan ambao ndio waliofanya uhalifu huo. Dhozokhar bado yupo katika gereza akiendelea na kaka yake mkubwa Tamerlan ni Marehemu.

FBI wamekamata vijana watatu ambao walishiriki katika kuficha ushahidi '' obstruction of justice''.
Nao kama mwenzao Dhokar ni vijana wadogo ambao wamesema baada ya kubaini washirika wao ndio wanaotafutwa waliingia katika chumba chao na kuchuku unga wa baruti pamoja na mafuta ya vaselin na kuvitupa katika jalala.

Mara baada ya tukio katika hali ya kushangaza FBI waliwahi kuzuia taka hizo zisichukuliwe.
Tutakumbuka walifanya upekeuzi katika eneo na kuondoka na vitu ambavyo sasa tunaelewa vilikuwa ni uchafu wa mabaki ya mabomu.

Mawasiliano ya vijana hao yamepatikana ikiwa ni pamoja na maongezi ya simu, text na muonekano wao katika face book.
Wao wanadai hawakujua lolote ingawa Tamerlan alishawahi kuwaambia anajua kutengeneza bomu.

Baada ya picha za awali kutoka katika vyombo vya habari, vijana hao waliwasiliana na marehem Tamerlan ambaye aliwajibu kuwa chukueni chochote kilichopo katika chumba chake.

Utetezi wao wa kushangaza ni kuwa walifanya ukusanyaji wa vitu na kuvitupa ili ''kuwaeousha washikaji na mabalaa''
Nadhani ni suala la umri hapa kwasababu haiwezekani umwepushe mshikaji aliyeua wakati tayari wao wameshasababisha balaa.

FBI imepata mawasiliano mengi na maswali yanabaki endapo hao washirika hawakushiriki.
Hata kama hawakushiriki, ilikuwaje hawakutaarifu vyombo vya usalama hata walipobaini washikaji wamesababisha zali.
Ndivyo ambavyo mke wa Tamerlan naye anavyoonekana kuwa na mawasiliano na mumewe wakati anatafutwa ili hali alipaswa kutaarifu vyombo vya usalama.

Funzo moja kubwa kwa matukio haya ni jinsi ambavyo vyombo vya usalama vinavyoweza kuunganisha habari, kutafuta mawasiliano na kutambua wapi penye ''masilahi nayo''.

FBI walikuwa na taarifa za hawa watu hata wakati wanasafiri. Kwa sababuzisizojulikana FBI hawakuweza kufuatilia kwa ukaribu zaidi taarifa kutoka Russia ambazo zilikuwa na kila aina ya viashirio vya watu hao.

Hata hivyo wameweza kukamata kila aina ya mawasiliano na kuwatambu wahusika wa mawasiliano hayo.
Huu si mwisho wa uchunguzi, uchunguzi unaendelea hadi kubaini nani alishiriki vipi na kwanini.
Inatosha kusema kwa kuanzia na kwa muda mfupi sana FBI wameweza kutengua kitendawili.

Hapa kuna maswali kuhusu hali ya hapa nyumbani Tanzania kwa sasa.
Kila uchao kumekuwa na matukio ya uhalifu ambao kama uchunguzi wa kina na kisayansi ungefanyika basi wahusika wote wangekuwa wameshakamatwa.

Hata pale taarifa za wahusika zinapopelekwa Polisi kama alivyofanya Bashe, Dr Slaa, Mwakyembe n.k. bado Polisi wetu hawawezi kufanya uchunguzi wa kina wenye majibu.

Siamini kuwa hilo linatokea kwa kuwa na teknoloji hafifu au kutokuwa na wataalam.
Nadhani yanatoke kwa makusudi tu.

Na hali inaonekana kuwa mbaya kila siku, hakuna ajuaye hatima yetu na kwamba mikasa kama huu wa Boston tunaweza hata kubuni achilia mbali kutafuta.

Kuna tatizo! tena kubwa katika vyombo vya usalama hasa jeshi la Polisi.

Tusemezane
 
Mkuu Nguruvi3 na wana duru la siasa.
Suala la kufutwa matokeo ya kidato cha nne linaonesha ni namna gani tusivyo makini na mambo ya muhimu kwa mustakabali wa taifa letu. Kwa mtazamo wangu hili suluhisho limetolewa ili kutuliza hasira ya wananchi dhidi ya serikali kuhusiana na matokeo mabaya ya kidato cha nne. Na mbaya zaidi hakuna wanaowajibishwa kutokana na sakata hili. Kwa hali hii ya kucheza na elimu sidhani kama Watanzania tutajiuza sawasawa katika soko la ajira hasa kwenye hii jumuiya yetu ya EAC. Sijaona nchi ambau ni wanachama wa EAC wakicheza na elimu kama tunavyofanya sisi.
 
Last edited by a moderator:
Mkuu Nguruvi3 na wana duru la siasa.
Suala la kufutwa matokeo ya kidato cha nne linaonesha ni namna gani tusivyo makini na mambo ya muhimu kwa mustakabali wa taifa letu. Kwa mtazamo wangu hili suluhisho limetolewa ili kutuliza hasira ya wananchi dhidi ya serikali kuhusiana na matokeo mabaya ya kidato cha nne. Na mbaya zaidi hakuna wanaowajibishwa kutokana na sakata hili. Kwa hali hii ya kucheza na elimu sidhani kama Watanzania tutajiuza sawasawa katika soko la ajira hasa kwenye hii jumuiya yetu ya EAC. Sijaona nchi ambau ni wanachama wa EAC wakicheza na elimu kama tunavyofanya sisi.

SUALA LA MITIHANI
Kwanza niseme kuwa katika nyakati tulizo nazo hakuna silaha muhimu sana kama elimu.
Hii ni dunia ambayo inampasa kila atakaye kufanikiwa awe na mahali pa kuanzia ambapo ni elimu.
Huko twendako suala la elimu linaweza kuwa tatizo sana kwetu.

Katavi umeongelea soko la EAC, mimi naongeza kuwa hata soko la SADC bado tuna wakati mgumu sana.
Hizi si zama za bora elimu ni zama za elimu bora. Si zama za kupata certificate ni zama zinazohitaji weledi na jinsi gani elimu hiyo inatumika.

Elimu ni zaidi ya ajira.Dunia ya sasa mjasiriamali, mkulima au mfugaji anatakiwa aelewe mazingira ya dunia na kuwa na uwezo wa kutafsiri hali ya mambo pale alipo. Hilo litawezekana endapo mtu atakuwa na elimu inayomwezesha kufanya hivyo.

Hata katika suala la ajira, ukiritimba unaoliliwa na watu kuhusu nafasi za ajira kwa wazawa nao unaukomo wake.
Leo mashirika na makampuni hayaajiri yenyewe bali kutumia mawakala ili kupata watu wanaowahitaji.

Si mara moja au mbili utasikia masahili ya nafasi fulani yamefanywa na taasisi fulani au kampuni fulani mathalani pricewater. Hapo anatafutwa mtu mwenye uwezo atakayeleta tija na wala si uzawa popote alipo.

Ukiangalia upande wa elimu tuna tatizo kubwa sana la kuchanganya utaalam na siasa.
Elimu ni suala la utaalam na wala si siasa. Ni mara nyingi suala hili limeongelewa lakini ni katika mizania ya siasa na wala si utaalam.

Tume lukuki zimeundwa na kila moja inakuja na taarifa ambazo zinaishia makabatini au zingine kugeuzwa kuwa za kisiasa.
Matokeo ya mwaka huu ni mfano mzuri sana. Kufeli kwa wanafunzi kwa kiwango cha kutisha kuna sababu muhimu na lazima sababu hizo zitafutwe na wataalam na kwa njia za kitaalamu.

Kuna maswali mengi sana ya kujiuliza. Hivi tatizo ni mitihani au ni wanafunzi?
Endapo ni wanafunzi, tatizo lao ni nini hasa, kwamba hawaandaliwi katika viwango au hawajali masomo.

Je,kuna maandalizi mazuri ya wanafunzi na waliopewa dhamana hiyo wanatimiza kama ilivyokusdiwa?
Je, ni kiwango kuvunjika moyo kwa walimu kumeathiri au kutoathiri maendeleo ya wanafunzi.

Kama tatizo ni mitihani ni nani anayehusika na utungaji wa mitihani hiyo na je alitunga kutokana na mitaala ya elimu au aliazima maswali ya kutahini kutoka nchi nyingine.

Ikifika hapo utaona kuna kundi kubwa sana la watu wanaohitajika kujibu maswali hayo.
Sijui kwanini suala hili linafanywa kisiasa zaidi ya kitaalamu.
Hakuna majibu ya tatizo yanayoeleweka zaidi ya porojo za kisiasa.

Sasa tumefikia mahali ambapo eti matokeo yanafanyiwa standardization.
Ninashangaa kwasababu kama mwanafunzi alipata 10 ukafanya standardization na akapata 30 hapo utakuwa umemsaidiaje kielimu.Kinachoonekana ni ku-ignore mzizi wa tatizo na kutafuta suluhu ya muda kama kuweka band aid katika kidonda.

Pengine inafanyika hivyo ili kupata wanafunzi wa kuendelea na masomo na vyuo mbali mbali.
Lakini je mbele ya safari wanafunzi hao watakuwa tayari na wameiva kupambana na dunia ya ushindani?

Ukiliangalia suala hili kwa undani ni wazi limetekwa na siasa zaidi ya utaalam.
Mimi sikubaliani na hoja ya kuongeza viwango vya ufaulu.

Ninachoweza kusema ni kuwa itafutwe sababu iliyosababisha haya yakatokea kwanza.
Waliohusika wawajibishwe ili yasije yakatokea tena.
Tujitahmini kuwa elimu yetu ni ya viwango tarajiwa katika masoko ya ushindani?

Tuangalie mitaala yetu na kujiridhisha kama inakidhi hali na matakwa ya karne hii.
Kubadilisha namba za matokeo hakumuongezei mwanafunzi maarifa zaidi ya kumpa kichwa kuwa yeye ni bora hata kama hana ubora huo.

Ni wazi kuwa katika nchi zinazotuzunguka, sisi tuna tatizo kubwa.
Tena ni janga wala si tatizo kama tunavyoweza kusema. Suala la elimu ni la kitaalam na wataalam waachiwe na kupewa na nafasi ya kutumia utaalam wao kutusaidia na wala si wanasiasa kutafuta kura na umaarufu kwa kutumia suala nyeti na roho ya taifa kama elimu.

Tusemezane.
 
TUKIO LA BOMU ARUSHA

Wiki hii taifa limegubikwa na taarifa za kusikitisha za tukio la bomu katika uzinduzi wa kanisa jijini Arusha.
Hadi wakati huu watu watatu wamefariki na wengine wengi kuwa majeruhi.

Kwa mtazamo wa tukio ni mapema mno kusema nani kahusika na kwanini. Tuna mifano mingi kama kule Oklahama ambapo baada ya mlipuko watu wengi walijua ni tukio la kigaidi lililohusisha islamic fundamentalist. Hata hivyo baada ya uchunguzi ilibainika kuwa aliyefanya tukio hilo ni Mmarekani Thom Mcveigh aliyekuwa na chuki na serikali.

Ndivyo ilivyokuwa kule Omah ambapo magaidi wa Irleland walihusika na mlipuko ulioua watu wengi.
Kwa upande mwingine matukio ya 9/11 na lile la Boston hivi karibuni yalifanywa na watu ambao walishukiwa kuwa waislam wenye msimamo mkali na ndivyo ilivyokuwa.

Vurugu za kidini si lazima zihusishe watu wa imani tofauti. Zinaweza kuwa za washirika wa imani hiyo wanaotofautiana wenyewe kwa wenyewe. Hayo yametokea nchini kama mzozo wa Arumeru Mshariki, Dodoma na kanisa la Anglican, Sumbawanga na kwingineko kama ilivyo kwa mizozo ya Bakwata na makundi mengine, shehe kumwagiwa tindikali, masheikh kuchapwa viboko kama ilivyotokea misikitini n.k

Kinachotia mashaka sana kuhusu tukio hili ni ''nature'' yake. Siku za karibuni hali ya utengamano kitaifa imekuwa ya mashaka sana. Kumetokea mauaji ya padri Zanzibar na mwinginekule Geita, kuchoma miskiti moto,kushambuliwa kwa sheikh na malumbano yasiyoisha kuhusu imani.

Kumekuwepo pia na tatizo la makundi ya watu kuchochea vurugu hizo hadharani. Makundi hayo ni ya kidini na hata ya kisiasa kama ilivyotumika na chama tawala dhidi ya vyama vingine.

Hali hiyo imeachiwa kana kwamba imekubalika licha ya ukweli kuwa watu wanaochochea vurugu hizo wanajulikana na wanaendelea na uchochezi wao. Na hapa nisisitize kuwa makundi ya dini ya pande zote.

Tuna mifano ya wachungaji na maustadhi wakiwa wanatoa kauli za kusikitisha sana hadi mtu kufikiria mara mbili kama kweli dini ndiyo maana yake iliyokusudiwa.

Kwa upande wa serikali kumekuwa na kuogopa kukabiliana na wachafuzi hao. Serikali imekuwa inapewa kila aina ya viashirio vya kuvurugika kwa amani lakini mbinu zinazotumika hazionyeshi kama kweli ina dhamira.

Katika tukio la Arusha watu 10 wamekamatwa. Katika hali ya uchunguzi ni nadra sana kutaja majinaya wahusika.
Pengine serikali inafanya hivyo kuzuia hali mbaya endapo itabainika vinginevyo.

Lakini hii ni suluhu ya ajabu sana, kinachotakiwa kufanyika ni kutafuta wahusika na kupata chanzo cha tatizo, nani wamehusika wakiwa wapi na kwa msaada gani.

Nchi za wenzetu wapeleleiz hawawezi kukurupuka tu au wanasiasa kukurupuka kutoa majina ya watuhumiwa.
Tunayaona kila siku yanapotokea kwingine. Kufanya hivyo kunazuia kuvuruga uchunguzi.
Lakini pia ni kulinda haki za binadamu. Hivi ikitokea kuwa mtuhumiwa siye, serikali itaueleza nini umma.

Rais JK amesema kuwa serikali itawasaka usiku na mchana na hawata lala hadi ijulikane chanzo ni nini.
Sijui serikali hiyo iliyoshindwakulishughulikia tatizo la chuki miongoni mwa wanajamii itawahakikishiaje wananchi kuwa sasa inaweza!!!

Pamoja na mbinu zote zinazotumika kutuliza hali ya mambo, kuna jambo moja ambalo serikali lazima ijalaumu.
Leo wananchi hawaamini kuwa serikali inatoa taarifa za kweli kwasababu taarifa za matukio mengi zimekuwa ima za kuficha au za kupikwa.

Hivi nani atakuwa tayari kutaja wahusika hata kama anawajua iwapo serikali hiyo hiyo imeshindwa kuwakamata wahusika waliotajwa na wahanga wa matukio. Tunakumbuka kisa cha Ulimboka ambapo amemtaja mtu aliyehusika lakini hakuna hatua zilizochukuliwa zaidi ya udanganyifu wa kumakamata mtu na hadi leo haijulikani kamani yeye au siye.

Mauaji ya watu yamekuwa jambo la kawida na wahalifu wanafanya hivyo bila serikali kuchukua hatua.
Leo ni kiongozi gani atakayesimama na kuwaambia watu uchunguzi unafanyika na watulie ili hali kuna mambo yamebaki bila majibu.

Kuna kesi ya Mwangosi, Ulimboka, Kibanda, Mwakyembe, Prof Mwakyusa, Reginald Mengi na wengi tu ambazo serikali imekuwa inafanya trick za kutuliza watu na kisha mambo kwisha pole pole. Nani ataamini uchunguzi unaoendelea kwa kutaja majina mawili matatu utakuwa na maana yoyote.

Tunachotaka kusema hapa ni kuwa kumekuwa na vurugu, matukio na serikali ikifanya mizaha kama ile ya sinema ya Kova.
Leo hao hao wanasema hawalali wakiwatafuta wahalifu. Nani anakuwa na chembe ya kudhani hilo ni kweli.

Wakati tukiwapa pole waliofikwa na madhila haya, tuwaombe Watanzania waendelee kuishi kwa amani na upendo.
Jamii zetu zimeingiliana sana kiasi kwamba tukio kama hili ni msiba wa kila mmoja. Tusikubali kugawanywa kwa misingi ya imani au chochote kiwacho.

Na wala asitokee yoyote kuanza kumshuku mwingine hadi ukweli utakapotamalaki kama itatokea hivyo.
Sisi sote tusimame pamoja na kulaani uhalifu huu usio na kabila, imani au ubinadamu.

Kuparurana ni upungufu mkubwa wa ubinadamu, imani na undugu. Sisi kama taifa tusikubali kuishi kwa mapanga kama yale tunayoyaona kila siku katika TV.

Na katika kuzuia haya yasitokee lazima tuwe pamoja na kuitaka serikali iache mchezo na maisha ya wananchi wetu.
Mambo kama ya sinema ya kova ndiyo yametufikisha hapa. Na hayo yakitokea hakuna anayewajibika kana kwamba kuna baraka za serikali. Tunachokisikia ni wale wenye dhamana kuendelee kuhoji Kibanda ni nani na kupongeza waauaji kama wale wa Iringa.

Tatizo letu si hawa wanaorusha magrenedi kwasababu hao ni watu wasiozidi 100 kati ya mamilioni.
Tatizo letu ni kuwa wale tuliowapa dhamana ya kulinda mali na maisha yetu wamegeuza maisha na uhai wetu katika michezo yao ya kisiasa. Yatakapotokea tusiyoyaombea wao watakimbilia Ulaya kwani tayari wana pesa Uswiss.
Lazima tuwabane ama sivyo tuwatake watoe nafasi kwa wenye uwezo kusimamia uhai wetu na mali zetu.

Itaendelea......
 
MLIPUKO WA ARUSHA

Inaendelea....

Hapo nyuma tumesema kuwa serikali imekuwa inafanyia mizaha mambo mazito yanayoigusa jamii.
Hadi leo kuna mambo hayajapatiwa majibu licha ya ukweli kuwa yalikuwa na masilahi kwa taifa (public interest)
Haya ni pamoja na mauaji, majaribio ya mauaji, wizi na ubadhirifu, ufisadi na rushwa.

Mambo hayo yameondoa imani ya wananchi juu ya serikali yao. Kwamba, serikali sasa inaonekana kama chombo cha kupika ulaghai na wala si cha kutoa majibu kwa masuala mazito ya nchi.

Wiki hii serikali imewaachia raia wa kigeni waliokamatwa kwa tuhuma za kule Arusha.
Tayari hilo limezua minong'ono isiyokuwa ya lazima kwa serikali. Wapo wanaosema kuna jambo linafichwa.
Hata kama hakuna nani ataamini ikiwa yapo zaidi ya 20 mazito kuliko hili na yamefichwa?

Tulionya kuwa suala hili halipaswi kuwa la kisiasa au kukurupuka. Ni suala nyeti linalohitaji uadilifu.
Hadi sasa wananchi wa Tanzania wameonyesha uvumilivu na kustahamiana kwa hali ya juu sana.
Wao wanaamini kuwa hili si tukio la kawaida na nadra kufanywa na watanzania bila kuwa na motive.

Tumesema huko nyuma ilibdi kwanza uchunguzi wa kina ufanyike kabla ya kuliita tukio la kigaidi.
Maana unapoliita la kigaidi basi unatakiwa uwe na ushahidi unaolingana na tuhuma hizo.
Pengine serikali inao. Kwa kutumia busara hili lilitakiwa liwe tukio la uhalifu hadi pale itakapobainika vinginevyo.

Mbele ya wananchi na dunia ugaidi ni jambo zito linalohitaji jicho la karibu na pengine ndivyo linavyoangaliwa sasa.
Kwahiyo serikali iwe tayari kukabiliana na hoja zitokanazo na tuhuma hizo.

Ni kwa bahati nzuri kijana aliyehusika amekamatwa na kuna madai kuwa alikamatwa kukiwa na ushahidi wa kutosha.
Kwa namna yoyote kijana huyo atakuwa na habari za washirika wake wa karibu na hivyo ni matumaini ya wananchi kuwa jibu la tukio litapatikana kwa ukweli na uwazi.

Hatutegemei kupata majibu ya kupenedeza mtu au watu, tunategemea kupata majibu kwa mujibu wa tukio.
Hilo ndilo litaondoa shuku waliyo nayo wananchi juu ya serikali yao.
Litaondoa sintofahamu inayolitafuna taifa kichini chini.

Inawezekana ni tukio la chuki za kidini au tukio la chuki miongoni mwa wanadini.
Kwa hali yoyote haitegemewi kusikia hadithi kama zile za Kova ambazo zimeliondolea jeshi la polisi hadhi ya kusema na kusikika.

Ni katika kuziba ombwe la jeshi la polisi, kila mara jeshi hilo limekuwa likisema linafanya utafiti kwakushirikiana na FBI au Interpol au nchi za jirani.

Hii maana yake ni kuwa hata kama jeshi la polisi lina habari za uhakika na za kweli bado hakuna raia atakayeamini kuwa habari hizo ni za kweli. Sasa inabidi watafute kibwagizo ambacho ni taasisi nje ya jeshi ili kuaminika.

Inapofikia mahali jeshi la usalama wa raia haliaminiki hapo kuna tatizo.
Tatizo ni kuwa haliaminiki hivyo hakuna mtu anayeamini kuwa linafanya kwa mujibu au kulinda mali na usalama wa raia.

Tukio hili la Arusha ni la muhimu sana kwa namna jeshi lilivyoshughulikia.
Kwanza kukamata watu na kuutangazia umma na hivyo umma hautegemei mambo kuisha kama yale ya Ulimboka

Kinyume na hivyo jeshi litakuwa limejenga mazingira mabaya sana.
Tukio hilo litaingia katika mahakama za kiraia(Public oipinion court) litajadiliwa kwa nmna kila mmoja anavyodhani na kutolewa hukumu za uongo, uzushi na ulaghai.

Tukio linaweza kuchukuliwa na wanasiasa au viongozi wa mambo ya kiroho na kulifanyanga likatoa maana isiyotarajiwa.
Linaweza kujenga chuki ya chini chini na hivyo kuwa bomu linalosubiri kulipuka muda ukifika.

Tunaishauri serikali kutoa majibu sahihi ya tukio na si majibu ya kupendeza au kupooza hasira za wananchi.
Vyovyote iwavyo ni lazima kilelezwe chanzo, wahusika na motive yao hata kama ni mambo ya kidini ndani na nje ya tukio
Kama hakuna majibu ni vyema kusema hakukuwa na majibu yoyote pengine wananchi wanaweza kuelewa.

Kosa kubwa ni kurudia yale ya sinema ya Kova. Hili si tukio dogo, ni tukio linalogusa watu, imani na uaminifu(trust) kati ya wanajamii. Jamii ingependa kuona na kupata majibu ili kushiriki kuzuia kwa siku za baadaye.
Lakini pia ili kuondoa sintofahamu iliyopo.

Hili si tukio la kununua muda( delaying tactic) ili wananchi wasahau.
Si tukio la mauji ya kisiasa na wala serikali isidhani kuwa kwavile imekuwa inaghilibu umma basi itaweza kufunika kombe mwanaharamu apite. Si kweli, huko ni kutengeneza tatizo kubwa zaidi ya lilivyo.

Tusemezane
 
1.MASHAMBULIZI YA ISRAEL SYRIA
2.SAKATA LA GESI ASILIA MTWAR
A

Wiki takribani mbili zilizopita Israel ilifanya mashambulizi katika ardhi ya Syria.
Sababu kubwa ni kushambulia ni kile walichosema shehena za silaha zinazotoka Iran kuelekea Lebanon kusini ambako kundi la Hezbhoulla chini ya Iman Hussein Nasralla limejikita.

Tunakumbuka vita ya Israel na Hezbhoulla miaka ya karibuni ambako kwa mizania za nguvu za kijeshi ni wazi Israel ilishindwa. Hata ndani ya bunge la Israel Knest hilo lilisemwa na kuundwa tume kuchunguza chanzo cha kushindwa kupambana na Hezbhoulla licha ya ukweli kuwa silaha nyingi na nzito zilikuwa upande wa Israel.

Tukumbuke pia ya kuwa Israel inakalia sehemu ya Syria (Golan Height) kwa miaka mingi.
Huko nyuma tulisema kuwa vita ndani ya Syria ina tishio kubwa sana kwa Israel kuliko mageuzi ya mashariki ya kati yaliyohusisha nchi nyingi kama Egypt.

Golan height ipo katika eneo la mkakati(strategy position) na hivyo kuiweka Israel katika wakati mgumu kiulinzi.
Syria hawana silaha nzito lakini ni mashujaa sana wa vita ''warriors'' katika mashariki ya kati.
Pamoja na uduni wa silaha Israel inawaogopa sana pengine zaidi ya Iran.

Shambulio ndani ya Syria lina mitazamo tofauti. Israel inajikuta katika njia panda.
Kwamba, imkubali Al Saada ambaye amekaa kimya kuhusu Golan lakini akiunga mkono Iran au Wamuondoe Al Asaad na wajiandae kwa makundi mengine yenye siasa kali yanayoweza kuamsha harakati za Golan.

Utata huo pia unazikumba nchi nyingi za magharibi na ni wazi kuwa kila aina ya uangalifu lazima ichukuliwe ili kuzuia madhara yasioonekana lakini yanayotabirika kwa kuangalia historia ya mambo pale mashariki ya kati.

Kitu ambacho wengi wanasahau ni kuwa mashambulizi ya Israel katika nchi nyingine kama Syria ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa. Hivyo hakuna sababu za aina yoyote zinazoweza kuhalalisha shambulio la nchi moja dhidi ya nyingine.

Kwa bahati mbaya sana UN inaonekana kutoa pass kila ambapo Israel inapokiuka taratibu za kimataifa.
Israel imekiuka maazimio mengi sana ya baraza la usalama la UN kama vile kuongeza makazi katika maeneo ya Wapalestina n.k.

Kwa kulindwa na Marekani na mataifa mengine hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya Israel
Tukumbuke kuwa tulishajadili kuhusu mauaji ya kiongozi wa HAMAS yaliyotokea Dubai kwa mtindo wa wizi wa passport za nchi kama Uingereza, Australi na Ujerumani uliofanywa na makachero wa Israel. Suala hilo likaisha bila jumuiya ya mataifa kufanya lolote licha ya ukweli kuwa lilikuwa tukio la ugaidi kama ugaidi mwingine.

Je, kuna ugaidi mzuri na ugaidi mbaya? Tunakubali dhambi kidogo kwa kulinganisha na dhambi kubwa? Je, kuna kamimba au mimba ni mimba tu wala haina udogo!

Inavyoonekana ni kuwa kuna haki ya Israel kuonea lakini hakuna haki inapoonewa au kukabiliana na upinzani.
Yote yanawekwa chini ya kivuli cha haki za kujilinda. Hapa ni upungufu mkubwa sana wa nguvu za wanachama ndani ya UN, kwamba kuna mataifa yenye nguvu na mengine ni wasindikizaji

Hata mataifa yanayojihusisha na mgogoro wa Mashariki ya kati yanayojiita ''Quarte' nayo yanaonekana kutokwa na kauli dhidi ya uhalifu wa Israel. Kibaya zaidi ni jinsi nchi za kiarabu kupitia muungano wao wa Arab League ulivyokosa umoja katika mambo yanayowahusu au kuhusu maeneo yao au jirani kama hili tukio la mashambulio nchi Syria.

Pengine kupungua nguvu kwa siasa za Misri nako kuna changia hasa baada ya serikali ya Morsi kuanza kupata upinzani mkali. Wengi walitaraji pengine Morsi angechukua hatua kali dhidi ya Israel, hata hivyo inaonekana amepigwa pini na mataifa ya magharibi.

Ni kwa mtazamo huo siasa za dunia zinashughulishwa sana na siasa za mashariki ya kati na hilo ni eneo ambalo halipaswi kufumbiwa macho.


SAKATA LA GESI MTWARA
Sakata hili bado lina zizima kichini chini. Duru za siasa imewahi kuiongelea suala hili kwa mtazamo wa kisiasa.
Hakika ni suala la kisiasa zaidi kwasababu maamuzi mengi na hoja nyingi zinajengwa kisiasa zaidi.
Pengine lingekuwa suala la kijamii(social ) na kiuchumi, lakini kama tulivyo kila jambo linanyakuliwa na wanasiasa na linapoteza maana halisi kama lilivyo.

Tusingependa turudi nyuma kuliongelea zaidi, inatosha kusema leo serikali imeonya kuwa maandamano yoyote ni marufuku. Kwa jinsi hali ilivyo, hatudhani kuwa kutakuwa na maandamano. Kinachoweza kutokea na kusimamisha huduma za jamii kama sehemu ya kuonyesha malalamiko na manung'uniko ya wananchi wa Mtwara...

Inaendelea.....
 
sakata la gesi
Inaendelea.....

Tatizo kubwa linalowakabili wananchi wa kusini kama Mtwara si ukosefu wa maliasili au chochote ukilinganisha na mikoa mingine. Tatizo kubwa ni kukosa watu wa kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Hakuna ushahidi wowote wa kuonyesha kuwa kiwango kama cha elimu ni tatizo.

Kuna ushahidi kuwa malalamiko kuwa mawasiliano mabovu yalikuwa ni tatizo sasa imebaki historia.
Miundo mbinu kama barabara na madaraja sasa yanapitika kwa wakati wote wa mwaka.

Tunasema tatizo si elimu kwasababu wapo wasomi wengi sana wenye viwango mbali mbali wanaotoka mikoa hiyo ambao ni viongozi katika ngazi ya taifa. Kuna wabunge, mawaziri, na hata Rais wa nchi amewahi kutokea maeneo hayo.
Historia inazidi kuonyesha kuwa viongozi wengi katika ngazi za kitaifa wametokea huko siku za nyuma

Tatizo linalowakumba wananchi hao ni kukosa watu wenye weledi wa kuwaongoza katika masuala mazito kama hili la gesi. Kuna hoja za msingi sana ambazo zikiangaliwa zina mantiki ya kicuhumi, kijamii.
Kwamba sasa ni wakati wanachi wa maeneo hayo wafaidike na huduma zitokazo na rasilimali zao.
Huo ni ukweli ambao hakuna anyeweza kuupinga.

Kwanini watu wa mikoa hiyo wanapoteza nguvu za hoja? Tumesema kuwa wapo wasomi wa kujenga hoja kimantiki, kisomi na kwa weledi. Bahati mbaya sana utamaduni wa wasomi wa mikoa ya kusini ni kuhama makwao na kukimbilia mikoa mingine. Mathalan, utawakuta wote wamejazana Dar es salaam hata mikoa ya kaskazini.

Hakuna sababu ya mtu kuzuiwa kusihi popote, ieleweke kuwa maendeleo ya eno husika huletwa na watu na wazwa wa eneo hilo wenye weledi. Ndivyo ambavyo utamaduni wa kuwekeza nyumbani unavyosiaidia sana mikoa ya Kilimanjaro, Mbeya na Kagera. Kwamba wakazi wa huko hurejee makwao mara kwa mara na kila wanpostaafu hurudi kutumikia maeneo husika.

Kwavile wananchi wa kusini hawana utamaduni huo, sehemu hizo zimebaki kuwa magofu na watu ambao uwezo wao ni mdogo ingawa wanatmbua haki zao. Mfano, sasa hivi wanajenga hoja kuwa gesi ni ya Mtwara na hivyo istoke.
Hapa kuna upungufu mkubwa wa uelewa. Gesi ni ya wananchi wa Tanzania na ipo Mtwara, pengine walipaswa kusema gesi inayotoka Mtwara ifaidishe watu wa eneo hilo kwavile ndiyo rasilimali yao.

Suala la gesi ni ya Mtwara linaondoa mantiki na uzito wa hoja zao na ni rahisi sana wansiasa kuunga meneno kama vile kuligawa taifa, kuvunja amani ya taifa n.k. na kufunika hoja ya msingi kabisa.

Mfano wapili, ni ule ambao wananchi wamekuwa wantumia siku za Ijumaa kudai haki zao. Maandamano yamekuwa yanafanyika siku hizo na kuna ushahidi wa kutosha kuwa jambo hilo linachukua mkondo wa kidini bila kutarajiwa.

Hatudhani kuwa madai ya gesi ni ya kidini na hivyo kila jitihada lazima zifanyike kuepusha hali hiyo.
Wanasiasa wamekuwa wanakutana na wazee wa dini jambo ambalo si sahihi kwa kila upande.

Madai ya Mtwara ni ya mkoa bila kubagua, sasa iweje watu waanze kulifanya kama suala la dini?
Wanasiasa wanaweza kutumia udhaifu huo kutungua hoja za msingi kabisa za watu wa Mtwara.

Hapa ndipo tunaona madhara ya wasomi, wastaafu na watu wenye weledi kutelekeza makwao na kuwaacha wazee na wale wenye maono yasiyolingana na mwendo wa dunia wakijitwika ajenda na kupoteza ajenda hizo kwasababu tu ya ukosefu wa wa weledi.

Pengine ningeuliza, hivi hawa viongozi kama akina Mkapa, Nape, Kingunge na wengine kwanini hawaendi kuongea na wananchi wa nyumbani kwao? Wapo akina Membe wanaoutaka urais lakini wamejificha, wanachosubiri ni wakati ufike ili waende kuungwa mkono na watu wa makao. Wapo wapi kwasasa hivi na nini msimamo wao kuhusu hali za wananchi na matukio yanayogusa sehemu zao za uwakilishi.

Wanachopaswa ni ima kuwaeleza wananchi wa maeneo watokayo kile wasichokijua au kusikiliza kile wasichokuwa wanakijua?

Lakini pia wananchi wa maeneo ya kusini wanapswa kubeba lawama kwa kiwango chao.
Licha ya kutelekekezwa na wasomi kutoka maeneo yao, wao wamekuwa watiifu sana kwa CCM.
Kwa miongo kadhaa wamekataa mabadiliko wakiamini kuwa CCM ipo upande wao.

Ni kwanini basi wasiitumie CCM ambayo wao ni watiifu kutafuta suluhu ya matatizo yao?
Je, wataendelea kubeba bendera za kijani hadi lini wakati ambapo wanapoihitaji CCM, CCM haipo karibu nao kabisa.

Siwezi kusema kuwa Upinzani ni mwarobani lakini hilo tu linatosha kupeleka ujumbe na hivyo wangeangaliwa kwa jicho tofauti na wanavyoangaliwa sasa.

Tumeona maeneo yenye upinzani wa kisiasa yakitazamwa na wansiasa kama sehemu muhimu.
Ingawa mbinu hii ni mbaya na haifai kutumika, ninachosema hapa ni kuwa silaha ya mnyonge ni umoja.

Turufu ya kura ndiyo waliyonayo na wala si deraya au mizinga ya kijeshi au maji ya kuwasha.
Kwanini basi wasitumie kile kidogo walicho nacho kuonyesha nguvu yao?

Pengine jibu la swali litakuwa lile lile, wametelekezwa na wasomi wa nyumbani kwao.

Sisi duru za siasa tunawashauri mambo makuu yafuatayo

1. Kudai haki zao kwa misingi iliyokubalika na yenye mantiki na weledi bila kutumbukiza jambo jingine katikati
2. Kuwataka wasomi wao warejee kusadiaina nao makwao na wasisubiri wakati wa kura au misafara ya mazishi
3. Kuacha kulifanya suala la gesi lionekane la kidini au kisiasa bali wasimame kama wananchi wa Mtwara
4. Kuwaita viongozi wao kama wabunge na wawakilishi wengine na kuwashinikiza walifanyie kazi jambo hili vinginevyo wasirudi tena Mtwara, wajenge nyumba huko Dodoma.

Kwa wasomi kutoka maeneo hayo, kama hamtafanya utaratibu wa kuthamini nyumbani kwenu hakika gesi inaweza kubaki Mtwara lakini ikachotwa na wajanja na kuwaacha wananchi wenu wakiwa duni.
Kwanini ninyi hamuigi mambo mazuri yanayofanywa na wasomi kutoka mikoa mingine?

Mzee CD Msuya, waziri mkuu mstaafu yeye ni mwekahazina wa CCM wilaya ya Mwanga, na ni mjumbe wa benki ya watu wa Mwanga, ni organizer wa shughuli za maendeleo za watu wa Mwanga na anaishi nyumbani kwake kijijini Usangi Mwanga.

Mwambie Benjamin Mkapa auze kiwanja na nyumba Lushoto arudi kujenga Mikindani ili siku kama ya kesho muwe naye

Ni ukweli mchungu duru inawataka radhi wakaopata usumbufu.
 
KWANINI TUMEFIKA HAPA PA KUALIKA FBI?

Msomaji mmoja kanitumia ujumbe na kuniiuliza hivi kwanini tumefika mahali pa kuita FBI kutusaidia kutafuta suluhu za matatizo kama yale ya Zanzibar na Arusha.

Nimfahamishe msomaji wa duru kuwa matatizo ya kijamii hayazuki siku moja.
Ni mlundikano wa mambo ambayo huzaa tatizo. Kwa hapa Tanzania tatizo ni usimamizi mzuri wa vyombo vya usalama

Huko nyuma nchi yetu ilikuwa na maadui kutoka pande zote. Kulikuwa na Wareno wakisaidiwa na makaburu na hata mataifa makubwa nyakati za vita baridi. Wote hao walijaribu kulifarakanisha taifa kwa namna walizoweza na hata kufanya majaribio ya kuhujumu kama si mauaji.

Vyombo vyetu vya usalama vilikuwa macho sana kufuatilia nani anafanya nini na kwasababu zipi akiungwa mkono na akina nani. Nikumbushe kuwa kesi maarufu ya Thomas Zingira ilifuatiliwa kwa kuda mrefu.
Uchunguzi wake haukuwa wa siku moja ulichukua muda mrefu sana hadi kufikia mahali pa kumnasa kukiwa na ushahidi.

Ndivyo ilivyokuwa kwa jaribio la mapinduzi lililoandaliwa na akina Hatty McGhee na wenzake.
Walifuatiliwa kwa muda mrefu sana na hata siku walipotaka kufanya mpango wao serikali ilifahamu na siku hiyo kwa makusudi Nyerere alikwenda alikotarajiwa lakini akabadilisha njia kwa chenga tu.

Kwa bahati mbaya sana Tanzania ya leo si ile. Watu wanafanya mambo hadharani na hakuna anayejiuliza madhara yake ni nini kwa jamii. Vyombo vya usalama vimechukua jukumu la kulinda viongozi na wala si taifa.
Ushahidi wa hili upo wazi, bunge linapoomba msaada wa ulinzi ni wazi kuwa hakuna aliye salama.

Bunge na wabunge hawapaswi kusimama na kutetea nafsi zao. Wanapaswa kusimama na kutetea nafasi za wapiga kura wao. Kinyume chake leo wanaomba magari yao yapewe ulinzi zaidi eti kwa matishio ya ugaidi.

Kutokana na kupoteza uelekeo na mwelekeo wa vyombo vya usalama kama TISS na Polisi taifa linawajibika kuwaita FBI waje wachunguze tatizo linalotokana na lililopo ndani ya Tanzania.
Tukirudi nyuma miaka 25 au 30 ni wazi kuwa tunavia badala ya kukua.
Hii si Tanzania tunayoijua. Miaka 50 tunaita FBI?

Vyombo vya usalama vimekuwa na ushabiki wa kisiasa na hata kuwa sehemu ya matatizo.
Vimepoteza maana halisi ya vyombo vya usalama.
Haiwezekani chombo cha usalama kikawa kinara wa kupika hadithi, kuficha ukweli,kufanya mateso, na kuzua uongo.
Hapo legitimacy ya chombo hicho imepotea na tumebaki na vyombo vya ulinzi wa viongozi na si usalama wa taifa.

Uwepo wa FBI si kwasababu wanataka kutusadia. Wao wapo kwa usalama wa taifa na viongozi wao.
Leo tunajua kuwa Rais Obama ataitembelea Tanzania. Kwa wenzetu mipango ya usalama wake inaanza mapema kabisa.
Hizo ndizo sababu za wao kufanya uchunguzi Znz na kushiriki uchunguzi kule Arusha.

Pamoja na ukweli huo, wenzetu wa FBI wanajitosheleza sana katika uwajibikaji, imani na utendaji wao.
Labda nigusie kidogo kuwa hawa FBI wanafanya kazi pamoja na CIA na wakala wengine 16 wa usalama Marekani.

Katika safu yao ya uongozi wapo wanasheria, wachumi, wanateknohama, madaktari, wauguzi, wachunguzi (forensic), engineers, wahasibu na kila aina ya fani wakiwemo watu wa siasa za dunia na za mataifa kadha wa kadha.
Kwa ufupi ni kuwa FBI inajitosheleza sana katika utaalamu na kila mtaalamu ana wajibu na anautekeleza.

Baada ya Bomu la Boston, FBI wanafanya uchunguzi wa jinsi bomu hilo linavyofanya kazi, lilivyotengenezwa, kufuatilia nani mtaalam wa kutengeneza au mwalimu wa utengenezaji, uwezekano wa teknolojia hiyo kukua n.k.
Wapo bize wakifuatilia hali za kisiasa kujua chagizo la shambulio, nani wapo nyuma na kwanini.

Wao FBI walikuwa na taarifa tayari kuhusu waliolipua. Kilichokosekana ni kuunganisha dot kunakotokana na mapungufu ya kiutendaji kwa baadhi ya watu. Ndio maana ilikuwa rahisi kujua nani anaishi wapi na anaweza kufanya nini hadi walipowakamata wahalifu.

Kazi ya kutathmini tukio hilo itaendelea kwa muda mrefu na kila chombo kitahusika, kila mtaalamu atahusika hadi jibu lipatikane. Ni kwa utaalamu wao, baada ya shambulio la 1998 Dar na Nairobi, FBI waliweza kuja na kujua bomu lilitengenezwa wapi na nani alihusika.

Sasa ukiangalia vyombo vyetu unaweza kushangaa kama kweli tuna uwezo wa kufanya uchunguzi wa kitaalamu.
Kwanza hatuna vyombo vyenye wataalam wa kutosha. Mathalani, idara ya usalama wa taifa hivi karibuni imegubikwa na kashfa za kuajiri watu kwa kujuana na wala si sifa.

Polisi na TISS hawana wataalamu wanaoweza kufuatilia mambo kwa ukaribu.
Kashfa na vurugu za kidini hazikuanza leo. Kumekuwa kunauzwa kanda za CD,DVD na mahubiri ambayo yaliashiria kabisa kuwa lipo tatizo.

Haijulikani ni kwanini vyombo vya usalama viliachia hali hiyo hadi kufika hapa tulipofika.
Kwa watu wenye kutumia wataalam kama wa siasa, sayansi ya jamii n.k. ni wazi kuwa kulikuwa na kila kiashirio cha uvunjifu wa amani.

Itaendelea.....
 
Back
Top Bottom