nadhani maoni haya unaweza kuyasambaza kwenye mtandao
Woga ni silaha dhaifu katika maendeleo
* Tumezidi kulalama
na manyerere jackton
WATANZANIA tupo kwenye mjadala, tukitafuta njia, na kasi sahihi ya kuelekea kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki.
Kwa bahati nzuri, nimepata bahati ya kupita katika mikoa takriban yote. Nimesikia maoni ya wananchi. Nimejua furaha na karaha wanazotarajia baada ya kujiunga. Wengine wana hofu. Wengine ni majasiri, wanalitaka Shirikisho lianze hata kesho.
Wengine wanajadili Shirikisho kana kwamba kuna swali la je, mnataka shirikisho, au hamlitaki? Hakuna swali la aina hiyo. Swali lililopo, ni je, twendeje kwenye shirikisho? Twende pole pole, au twende haraka?
Kwa maana nyingine, tutake tusitake, shirikisho litakuja. Shirikisho kwa lugha nyingine, ni mwilingiliano. Utandawazi ni mwingiliano. Kinachoweza kukataliwa na Watanzania ni neno au msamiati, lakini ushirikiano lazima uwepo.
Baadhi ya Watanzania wanalikataa shirikisho kwa kutoa hoja dhaifu. Kwa mfano, wanasema tukishirikiana, Wakenya watachukua (watamaliza?) kazi zetu! Rais Yoweri Museveni anataka urais, atakuja kututawala! Shirikisho la nini wakati Wakenya wameshashika kazi zote katika hoteli, asasi na kwingineko?
Watanzania hatuna elimu kama Wakenya na Waganda- tutatawaliwa! Hatujui Kiingereza- tutashindwa kwenye usaili! Hatuna viwanda vingi! Thamani ya pesa yetu ni ndogo. Kenya wanatuudhi, wanajitangazia Mlima Kilimanjaro kuwa uko kwao!
Kwa ufupi ni kwamba zinatolewa hoja nyingi ambazo zikichunguzwa, ni hoja dhaifu. Kwa mfano, Mwalimu wa shule au chuo anaposimama na kusema elimu ya Watanzania ni ndogo, maana yake ni nini? Wanafunzi wamweleweje? Huko ni kujitukana.
Tujadili hoja moja baada ya nyingine. Tuanze la hili la Wakenya kuteka kazi za Watanzania. Wakati Watanzania wanaogopa kupoteza kazi kwa Wakenya baada ya kuanza kwa Shirikisho, mambo ni kinyume. Kazi zimeshatekwa. Kwa nini zimetekwa? Zimetekwa kwa sababu sisi Watanzania hatuna uzalendo. Idara ya Uhamiaji ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haiongozwi na Wakenya wala menejimenti ya kigeni. Ni Watanzania wanaoiongoza. Wanaoruhusu wageni hawa kuja kuchukua kazi hata za kufua shuka, ni Watanzania. Vinginevyo tuambiwe kwamba wote waliopo Uhamiaji ni wageni, wanawapendelea wageni wenzao.
Saluni katika miji ya Arusha, Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya na kwingineko, zimeshikwa na Wakenya, Warundi na Wakongo. Nani kawakaribisha? Je, udhaifu wa Uhamiaji, ambao ni udhaifu wa Watanzania, ni kigezo cha kulichukia Shirikisho la Afrika Mashariki?
Tunalalamika kuwa Wakenya wanautumia Mlima Kilimanjaro kujinufaisha! Hivi sisi tulitarajia nini? Kama tunathamini usingizi na kujisahau kujitangaza nje ya mipaka? Tunalalamika Kenya kutangaza Kilimanjaro ipo kwao, tunasahau kuwa hata hapa hapa nchini, Arusha wanajitangaza kuwa Mbuga ya Serengeti ipo Arusha! Wakazi wa Mkoa wa Mara kama hawaoni sababu ya kuukanusha uwongo huo, nani awasaidie kuifanya kazi hiyo? Kila kitu kinanunuliwa Arusha, Mara wamelala, nani awaamshe? Ukilala utaibiwa tu.
Rais Museveni kawa gumzo. Watu wanapoteza muda wanasema, hatutaki shirikisho kwa sababu Museveni ametangaza kwamba anataka awe rais wa kwanza wa shirikisho. Huku ni kupoteza muda. Nasema hivyo kwa sababu bado hakujawekwa vigezo na sifa za rais wa Shirikisho. Yawezekana sifa ikawa kwamba rais wa kwanza wa shirikisho lazima awe mwanamke! Au Rais wa kwanza wa shirikisho, lazima awe ni rais mstaafu kama Mzee Mwinyi, Moi, Dk. Salmin na kadhalika. Hivi kweli Museveni kutangaza nia tu ya kuwa rais ndiyo sababu ya kuchukia ujio wa shirikisho?
Hoja ya kwamba Watanzania tutashindwa ndani ya shirikisho kwa sababu ya kutojua Kiingereza, hiki nacho ni kioja. Hizi ni hoja dhaifu mno. Tena zinatolewa na wasomi, wakiwamo wa vyuo vikuu na wahadhiri.
Kwanza, Watanzania wangapi wanajua kwamba kidato cha sita Tanzania ni sawa na mwaka wa pili katika Chuo kikuu nchini Kenya? Wangapi wanajua kuwa mwanafunzi aliyehitimu sekondari Kenya, hawezi kupokewa chuo kikuu Uingereza hadi apate miaka kadhaa ya kupigwa msasa? Nani anayejua kuwa pale Tunguu, Zanzibar Wakenya hawapokewi hadi kwanza wasome ili elimu yao iwafikishwe kwenye kiwango cha kukubaliwa kujiunga chuo kikuu? Haya tunayajua, au tunasema tu elimu ya Tanzania ni ndogo kwa hisia? Ni hatari sana kujadili mambo kwa hisia.
Sijui ni nani alituloga, hadi tukaamini kuwa Kiingereza ndiyo chanzo cha shibe, maisha bora, dawa, ondoleo la dhambi na mambo mengine kama hayo?
Kama Watanzania tu wavivu, Kiingereza kitatufaa nini?
Hivi kweli tunahitaji kujua Kiingereza ndipo tuweze kulima kwa njia za kisasa na kupata ziada? Kule Sumbawanga ambako mahindi yanaoza kwa kukosa wanunuzi, wanalima sana kwa sababu wanazungumza Kiingereza?
Pemba ambako nyanya chungu zinaagizwa kutoka Tanga, ilhali ardhi ipo, wanafanya hivyo kwa sababu hawajui kuzungumza Kiingereza? Umasikini wa Pemba unasababishwa na Kiswahili? Je, si kweli kwamba uvivu na kutotaka kubadilika ndiyo sababu kuu?
Hoteli zetu zinatoa huduma mbaya zisizo na mfano. Wahudumu hawazingatii maadili ya kazi zao. Glasi chafu. Majibu mabaya. Hakuna unyenyekevu. Haya yako karibu sehemu zote za Tanzania. Je, hali hii ni kwa sababu hatujui Kiingereza?
Na kama tuliolaaniwa, Kiingereza tunakililia kwa sababu moja tu-kwenye usaili! Hivi nani kasema kwenye shirikisho, bila kupata kazi inayohitaji usaili, hatuwezi kushindana? Ujasiriamali utawezekana vipi kama tutaendelea kuwa na fikra za aina hii? Kwa nini kila mtu anawaza kuajiriwa, badala ya kuajiri?
Nani anaweza kufuga kuku 100,000; kisha akashindwa kuuza mayai Kenya kwa sababu hajui Kiingereza? Nani atakayevumbua dawa ya kutibu ukimwi, kisha akose wateja kwa sababu hajui kuzungumza Kiingereza? Mbona wakarimani tunao. Wataajiriwa na nani? Tunakuwa wavivu wa kuzalisha, kisha tunasingizia lugha.
Mhitimu wa VETA Kenya aliyefundishwa kutengenza gari au dirisha kwa Kiingereza au Kinandi, ana tofauti gani na wa Tanzania aliyefundishwa kwa Kiswahili au Kikurya?
Kenya hawalali. Malori yanasafiri usiku na mchana. Usiku mabasi yako barabarani. Sisi ni tofauti. Pale Mombo wilayani Korogwe, kulikuwa na kituko. Kiongozi mmoja, kwa wivu tu wa mkewe, alizomoka na kupiga marufuku kina mama kuuza vyakula kwa wenye malori nyakati za usiku! Kina mama wale wameamua kujiajiri. Wameamua kuukosa usingizi, lakini kiongozi kwa wivu wake tu wa kimapenzi, anapiga marufuku biashara hiyo. Hapa tukidhibitiwa na Wakenya tutamlalamikia nani?
Nchi gani iliyoendelea kwa kuhamasisha watu wake kuuchapa usingizi? Nchi gani iliyoenelea ambayo watu wake wanafanya kazi kwa saa 12 tu? Je, udhaifu huu ndiyo tunaujengea hoja ya kulikataa shirikisho?
Wapo wanaopinga shirikisho, wakidai kwamba hatutajiandaa! Wengine wanasema kwa kuwa kuna mtafaruku kaskazini kwa Uganda; Kenya, Rwanda na Burundi ni wakabila; na Muungano wa Tanzania bado una dosari, basi tusubiri kwanza matatizo hayo yamalizike ndipo tuungane!
Kama Watanzania wanahofu kuambukizwa ukabila kutoka Kenya, Rwanda na Burundi, kwa nini wasiwe na hofu ya kuambukiza amani, upendo, utulivu na mshikamano katika nchi hizo?
Madai ya kwamba tusubiri kwanza tofauti kwenye Muungano zimalizike ndipo tuingie kwenye shirikisho, ni ya kuchangamsha baraza. Hao Wamarekani, au Waingereza walioungana mamia ya miaka iliyopita, tangu lini wametulia? Je, hatusikii chokochoko za kila mara kwa Waingereza?
Mbona mwaka 1961 tulijitawala bila kuwa na wasomi na wataalamu wengine? Mbona mambo yalienda vema hadi wasomi wetu walipoanza kuiharibu nchi? Hawa wote wanaoruhusu wageni kuja kuajiriwa kwa kazi zisizostahili, walionunua rada, waliosaini mikataba ya kipuuzi kwenye madini, waliobariki ujio wa Net Group Solution, IPTL, Richmond, waliotuwekea mezani mapanki, si ni hawa hawa wasomi baada ya Uhuru?
Je, ni kweli hatuna wasomi, au wapo lakini wengi wao ni wazandiki, mafisadi, wachumia tumbo na wasiokuwa na huruma kwa makabwela waliogharamia elimu zao?
Udhaifu huu wa kukosa uzalendo, uzandiki, ufisadi na uchumia tumbo, ndizo hoja zinazotumiwa kulipinga shirikisho?
Kama ni wasomi, Tanzania ina wasomi wengi, tena wenye uelewa wa hali ya juu. Kinachowakwaza baadhi ya wasomi wa Tanzania, kwanza ni kukosa uzalendo, na pili ni ubinafsi. Hawafanyi mambo kwa ajili ya Tanzania ya leo na ijayo. Wanafanya kwa ajili ya matumbo yao. Ndiyo maana wako radhi kugawa rasilimali za nchi bila soni, alimradi tu wahakikishiwe mlo.
Pale wasomi waliposimama kutetea maslahi ya Tanzania, mafanikio yalionekana, lakini pale walipoamua kutuweka kwenye mabalaa kama ya mikataba ya madini, maumivu tumeyashuhudia.
Tumekosa ujasiri. Tunajitahidi kutafuta vi-jisababu visivyo vya msingi, kuhalalisha udhaifu wetu.
Nasema hivyo kwa sababu Shirikisho si fomula kama ya hesabu. Si kwamba kila shirikisho lazima liwe 2+2=4. Shirikisho la Afrika Mashariki linaweza kuwa na mfumo wake mzuri, utakaolinda maslahi ya kila nchi.
Kwa mfano, suala la ardhi hilo linaweza lisiwe ndani ya masuala ya shirikisho. Ardhi ya Watanzania itaendelea kuwa mali ya Watanzania. Kwa namna gani hilo na mengine yatawezekana, ndilo suala la Watanzania kulijadili. Tutafute fomula.
Je, Zanzibar na visiwa vingine, vitakuwa katika nafasi gani ndani ya Shirikisho? Hayo ndiyo mambo ya kujadili na kuyapatia fomula inayofaa.
Changamoto kubwa inayotukabili Watanzania, ni kufunguka akili na kuingia katika ushindani wa maendeleo. Tujifungue akili, tusafiri kwenda huku na kule duniani kote. Tufanye biashara kwa juhudi. Tujaze ndege za Dubai kama wanavyofanya Wakenya na Waganda.
Tuzaliwe upya. Tuwe wazalendo. Tuipende nchi yetu. Kila Mtanzania katika nafasi yake, ahakikishe anafanya jambo kwa manufaa ya nchi yake. Uhamiaji wanapoachia kazi zote zishikwe na wageni, watambue kuwa wanawaumiza Watanzania wenzao. Tuzalishe zaidi, tufanye kazi kwa juhudi, maarifa na uadilifu. Bila kubadilika, kamwe tutabaki kuwa mabingwa wa kulalama, ilhali wenzetu wakizidi kuchanja mbuga kuelekea kwenye maendeleo.
Udhaufu wetu wenyewe, tusiuingize kwenye hofu ya kuundwa kwa shirikisho. Mkazi wa Mtwara, Abdallaha Chiwaula, amewahi kusema: Woga ni silaha dhaifu katika maendeleo Nani nasema bila kubadilika kwa hiari, wakati utatubadili kwa nguvu!
manyerere@hotmail.com
0713 335 469
.tamati