Elias Msuya
Platinum Member
- Dec 23, 2011
- 267
- 1,014
Kwa miaka kadhaa, jina la Edwin Watenya Sifuna limekuwa miongoni mwa yanayotajwa zaidi katika siasa za Kenya.
Wakati wengi walimfahamu kama Katibu Mkuu wa Orange Democratic Movement (ODM) na mmoja wa watetezi wakubwa wa Raila Odinga, leo anatajwa kama mwanasiasa anayejaribu kujijenga kuwa mbadala wa kisiasa dhidi ya Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Safari yake haijawa rahisi, bali migogoro, uaminifu kwa chama, mapambano ya ndani, na hatimaye kuvunjika kwa uhusiano wake na uongozi mpya wa ODM baada ya kifo cha Raila Odinga.
Kutoka mwanasheria hadi msemaji wa ODM
Edwin Sifuna alianza kujijengea jina kupitia taaluma yake ya sheria kabla ya kuingia kikamilifu katika siasa.
Umahiri wake wa kujenga hoja na kujibu mashambulizi ya wapinzani ulimfanya kuwa mmoja wa wasemaji muhimu wa ODM wakati chama hicho kikiongozwa na Raila Odinga.
Katika kipindi ambacho ODM ilikuwa inakabiliana na serikali mbalimbali, Sifuna alijitokeza kama mmoja wa vijana waliokuwa tayari kuingia kwenye mijadala mikali ya kisiasa bila woga.
Mara nyingi alikuwa mstari wa mbele kutetea msimamo wa chama dhidi ya serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na baadaye utawala wa William Ruto.
Mwaka 2021 aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa ODM, nafasi iliyompa jukumu la kusimamia shughuli za kila siku za chama na kukifanya kiendelee kuwa nguvu kubwa ya upinzani nchini Kenya.
Mwanasiasa aliyekuwa karibu na Raila
Wachambuzi wengi walimwona Sifuna kama mmoja wa viongozi vijana waliokuwa na uhusiano wa karibu na Raila Odinga.
Katika uchaguzi wa 2022 na hata baada ya kushindwa kwa Raila, Sifuna aliendelea kuwa mmoja wa watetezi wakubwa wa sera za ODM na mkosoaji mkali wa serikali ya William Ruto.
Alijenga taswira ya mwanasiasa ambaye hakuwa tayari kulegeza msimamo wake hata wakati viongozi wengine wa ODM walipoanza kuonyesha utayari wa kushirikiana na serikali.
Mbali na msimamo wake, Sifuna alipewa nguvu na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Raila Odinga ambaye Julai 25, 2026 akihutubia mkutano wa hadhara Kakamega, aliwakemea wanaomkosoa kiongozi huyo.
“Kama Sifuna ameongea yuko na haki ya kuongea, kama wewe unatofautiana naye kimaoni, sema yako. Si hiyo ndiyo demokrasia? Mimi sijasema eti usiongee kwenye chama, sema, hata kama unaona Baba anafanya makosa, sema,” alisema Raila.
Kifo cha Raila na mwanzo wa mgogoro
Kifo cha Raila Odinga mwaka 2025 kilibadilisha kabisa mwelekeo wa siasa ndani ya ODM.
Bila kiongozi aliyekuwa nguzo ya chama kwa zaidi ya miongo mitatu, makundi mbalimbali ndani ya ODM yalianza kupigania ushawishi kuhusu mustakabali wa chama.
Sifuna alionekana kuamini kuwa ODM ilipaswa kubaki chama cha upinzani na kuendelea kusimamia misingi ambayo Raila alikuwa akiitetea kwa miaka mingi.
Lakini viongozi wengine waliona kuna umuhimu wa kuendeleza ushirikiano na serikali ya Rais William Ruto, jambo lililoibua mgawanyiko mkubwa ndani ya chama.
Julai 11, 2026 ODM ilitangaza kuwa hakitasimamisha mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa Kenya wa mwaka 2027, badala yake itamuunga mkono Rais William Ruto kuwania muhula wa pili madarakani.
Kauli hiyo ilitolewa na kiongozi mwandamizi wa ODM, Oburu Oginga, akisema uamuzi huo umetokana na mazungumzo ya kisiasa yanayoendelea kati ya chama hicho na viongozi wa serikali.
Soma zaidi: Chama cha ODM kumuunga mkono Ruto Uchaguzi Mkuu wa 2027
Kuondolewa katika nafasi ya Katibu Mkuu
Migogoro hiyo ilifikia kilele mwaka 2026 wakati Kamati Kuu ya Taifa ya ODM (NEC) ilipomwondoa Edwin Sifuna katika nafasi ya Katibu Mkuu kwa madai ya utovu wa nidhamu na kukiuka taratibu za chama.
Sifuna alipinga hatua hiyo mahakamani na kudai kuwa taratibu hazikufuatwa ipasavyo. Baadaye, baada ya mchakato mwingine wa ndani wa chama, uongozi wa ODM ulimwondoa rasmi tena, na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikatambua mabadiliko hayo.
Kwa wafuasi wake, kuondolewa kwake kulionekana kama adhabu ya msimamo wake wa kupinga ushirikiano wa ODM na serikali ya Ruto. Kwa uongozi wa chama, hatua hiyo ilikuwa utekelezaji wa nidhamu ya chama.
Mwanzo wa safari mpya
Baada ya kupoteza nafasi yake ndani ya ODM, wengi walidhani ushawishi wa Sifuna ungepungua.
Badala yake, Sifuna alijiunga na vuguvugu la viongozi vijana walioasi ODM maarufu, Linda Wananchi na kuendeleza mashambulizi kwa Serikali ya Ruto.
Soma zaidi: Edwin Sifuna: Haiwezekani tumpatie Ruto nafasi arudi kwenye hiyo kiti
Sifuna atapenya vuuguvugu linaloongozwa na Kenyatta dhidi ya Ruto?
Katika hatua hiyo, Sifuna ametajwa kuandaliwa kuwa mgombea urais kupitia majadiliano ya kuunganisha upinzani dhidi ya Rais William Ruto yanayoongozwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta
Hatua hiyo ilidhihirika mwanzoni mwa Agosti 2026, wakati Uhuru aliposhiriki na kuongoza kikao cha Baraza la Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.
Kikao hicho kilitafsiriwa na wachambuzi wengi kama mwanzo wa kurejea kwake katika siasa za ndani, huku kikiwa sehemu ya mikakati ya kuunganisha makundi mbalimbali ya upinzani kuelekea uchaguzi wa 2027.
Ingawa Uhuru hajatangaza hadharani kumuunga mkono mgombea yeyote wa urais, amekuwa akihusishwa na juhudi za kusuka muungano unaojumuisha viongozi mbalimbali wa upinzani, akiwemo aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Ushirikiano huo umeibua mjadala mkubwa kwa sababu Gachagua alikuwa mmoja wa washirika wakubwa wa William Ruto mwaka 2022, lakini sasa ameibuka kuwa mmoja wa wakosoaji wakuu wa serikali yake.
Hata hivyo, bado haijafahamika ikiwa Sifuna, Gachagua na viongozi wengine wataafikiana kuhusu mgombea mmoja wa urais au kila mmoja atafuata mkondo wake.