SoC02 Elimu changamoto ya maendeleo

SoC02 Elimu changamoto ya maendeleo

Stories of Change - 2022 Competition
Joined
Aug 19, 2022
Posts
1
Reaction score
0
Elimu ni nguzo muhimu inayohitajika katika kujenga maendeleo ya taifa lolote duiani. Halikadhalika kwa nchi yetu ya Tanzania, elimu ni msingi mkubwa unaohitajiwa.

Lakini kwa masikitiko makubwa, bado elimu inayotolea nchini mwetu haijaweza kuwa yenye tija toshelezi katika kuleta maendeleo katika nchi yetu. Hii ni kwa sababu kuna changamoto katika sekta yetu ya elimu kuanzia mitaala inayotumika kama miongozo mama katika kufundisha, vitendea kazi na nyenzo muhimu hitajiwa katika ufundishaji, weledi, mwamko na hamasa ya waalimu na watoa mafunzo kwa ujumla pamoja na muda unaotumika mtu kupata elimu ama kujifunza kuanzia ngazi ya chini kabisa yaani shule ya awali kwa mfumo wa elimu rasmi.

Ningependa kuyazungumzia kwa undani haya machahe miongoni mwa changamoto nyingi zinazoikabili sekta yetu ya elimu na namna changamoto hizi zinavyoathiri maendeleo ya nchi yetu katika nyanja tofauti tofauti. Sambamba na hayo, kuwasilisha mapendekezo juu ya nini kifanyike kupatikana ufumbuzi.

Mitaala; kama mipangilio ya muongozo ya namna gani mwanafunzi atafundishwa somo fulani kuanzia mwanzo hadi mwisho wa somo hilo kwa mwaka husika wa elimu, mitaala ya ufundishaji imeonekana kutokuwa toshelezi. Hii ni kwa sababu, mitaala iliopo imeonekana wazi kushindwa kuakisi na Kwenda sambamba na kasi inayohitajika katika dunia ya leo inayokuwa kwa kasi.

Halikadhalika imeshindwa kumfanya mwanafunzi kuwa mbunifu, mwenye fikra pana na mwenye uwezo wa kutengeneza fursa kuweza kujiajiari ama kuisadia jamii inayomzungua kutatua changamoto zinazo endana na fani aliyosomea pasi na elimu aliyokuwa nayo.

Mathalani, tumeona miradi mingiya maendeleo ikiendelea hapa nchini ikiwa inaongozwa na wataalamu wa kigeni kutoka nje ya nchi, lakini katika fani hizo hizo katika vyuo vyetu vikuu mbalimbali tumekuwa tunazalisha wahitimu wa taaluma fanani kila mwaka. Hivyo tunatumia pesa nyingi kuwalipa wataalamu wa kigeni pesa ambazo tungeliwalipa wataalamu wazawa wafanisi ,pesa zingeweza kubaki kwenye mzunguko wa uzalishaji na uchumi wa ndani ,hivyo kukuza uchumi wa ndani.

Cha kusikitisha, wahitimu wengi kati ya hao badala ya kuweza kutumika katika miradi ya maendeleo iknayoendela hapa nchini, wamejikuta katika ajira ambazo hazifanani na tasnia zao ama hawana ajira kabisa. Wengi wanaobahatika kupata ajira ya fani bobezi huishiwa ngazi za usaidizi na sio wasimamizi wakuu wa miradi mikubwa inayoendela nchini mwetu kama ya uhandishi, tehama na nyanja nyinginezo. Hii ni kutokana na kushindwa kukidhi uhitaji wa taaluma ya fani husika mbali ya kuwa ni muhitimu rasmi wa fani hiyo.

Kuna ngazi nne katika elimu rasmi hapa nchini kuanzia shule ya awali, msingi, shule ya sekondari na sekondari ya juu Pamoja na ngazi ya chuo. Lakini ukitazama mitaala iliyopo haimuandai mwanafunzi kutoka ngazi moja Kwenda ngazi nyingine. Kumekuwa na marejeo ya vitu vinavyofundishwa kutoka ngazi moja kwenda ngazi nyingine. Hili linaenda kusababisha upotevu wa muda badala yake, tunahitaji mitaala inayoakisi mwendelezo wa elimu.

Mifano halisi ni, masomo yanayofundishwa shule ya awali yanalandana na masomo ya darasa la kwanza katika shule ya msingi. Halikadhalika, masomo na mada nyingi za darasa la tano hadi darasa la saba yameonekana kufundishwa tena kidato cha kwanza hadi cha nne tofauti ikiwa ni lugha na uwasilishaji. Kama haitoshi, mada hizo hizo zinajitokeza tena kidato cha tano na sita zikiwa na muendelezo wa uwasilishaji na maudhui.

Changamoto hii inaweza kutatuliwa kwa kuwa na mkusanyiko wa maudhui yote ya mada Fulani kwa somo hisika na kupangwa kwa muendelezo ili mwanafunzi aweze kusoma kutoka ngazi moja Kwenda nyingine kwa kuelewa lakini pasi na marurio marudio. Hili linaweza Kwenda sambamba na chaguzi za masomo mapema kuanzia shule ya msingi ili mwanafunzi aweze kusoma masomo machache yanayoendana na kwa undani zaidi.

Vitendea kazi duni; vitendea kazi na nyenzo muhimi hitajiwa katika ufundishaji bado vimekuwa sio toshelezi na vinavyoendana na ukuajia kwa kasi wa teknolojia zitumikazo kufundishia.

Inasikitisha kwamba, mpaka sasa bado kuna shule zinashindwa kufanya mitihani ya vitendo/majaribio ya kisayansi kwa kukosa vifaa. Bado shule nyingi ,baadhi mijini na aghalabu vijijini zinafanya mitihani ya majaribio kwa nadharia na sio kwa vitendo. Hii ni kutokana na kukosa kemikali hitajiwa, nyenzo ama vifaa kazi kwa ajili ya kuendesha majiribio hayo.

Kama haitoshi, bado mpaka sasa wanafunzi hususan ngazi ya shule ya msingi wanalazimika kusoma masomo ya tehama kwa nadharia. Upatikanaji wa kompyuta , komyuta mpakato na vishkwambi mashuleni bado sio wenye kukidhi hitajio la wanafunzi waliopo shule zetu.

Hii ni changamoto kubwa kwa sekta na wizara yetu ya elimu ikishirikiana na wizara ya teknologia kupambana na kutenga fundu la kutosha katika bajeti zao katika kila mwaka wa fedha kuongeza vitendea kazi na nyenzo muhimu hitajiwa katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu ya vitendo na majaribio toshelezi kuakisi ukuaji wa kasi wa sayansi ,tehama na elimu kwa ujumla duniani.

Weledi ,hamasa na mwamko katika kufundisha; changamoto nyingine inayoikabili sekta yetu ya elimu ni weledi ,hamasa na mwamko ya waalimu na watoa magunzo kwa ujumla. Japo kuwa serikali imekuwa ikijitahidi kuwaweka waalimu katika mazingira mazuri ya kufundishia sambamba na malipo na mishahara kwa ujumla, bado vyote hivi havijaweza kufikia kiwango toshelezi cha kuambana na ugumu wa maisha.

Hili hupelekea waalimu kukosa hamasa ya ziada katika kutekeleza majukumu yao kama wito. Mwalimu ni zaidi ya chaki na ubao, mwalimu ni mlezi wa pili wa mwanafunzi ,hivyo akikosa hamasa na morali katika ufundishaji ataishia kuwasilisha somo aliloliandaa ili kutekeleza jukumu lake bila kujali saikolojia ya mwanafunzi , nani kaelewa nan ani hajaelewa.

Hivyo basi, waalimu wanahitaji semina za mara kwa mara za kuwakumbusha kazi yao ni wito zaidi ya jukumu.

Halikadhalika, matamasha mashuleni yatasaidia kuwaweka waalimu na wanafunzi karibu na kuwajenga kisaikolojia na kusaidia muamko na hamasa ya pande zote mbili, waalimu na wanafunzi. Lakini pia, kuwepo na mwalimu bora mashuleni wa kila mwezi na akapewa utambulisho, cheti na pongezi kama motisha ya utendaji bora itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza hamasa na ari ya waalimumashuleni. Swala hili limeonekana likiongeza hamasa na morali kwa wafanyakazi na mashirika mbalimbali hususani yasiyo ya kiserikali kwa kuwatambuwa wafanyakazi bora wa kila mwezi, kuwapa vyeti Pamoja ana bonsai mbalimbali, hivyo ni matumaini yangu itafanya kazi vivo hivyo kwa waalimu wetu mashuleni.

Muda wa utoaji elimu; muda unaotumika mtu kupata elimu rasmi kuanzia ngazi ya shule ya awalihadi ngazi ya chuo imeonekana ni mrefu nab ado kumekuwa na marudio na marudio ya masomo yanayofundishwa. Swala la muda, sio tu linachajihishwa na marudio ya mada na masomo yanayofundishwa, bali pia imechangiwa na utumiaji wa lugha mbili, Kiswahili kwenye shule ya msingi na kuhamia kwenye Kiingereza kuanzia sekondari hadi ngazi ya chuo.

Hivyobasi kuna haja ya lazma ya kubaki na lugha moja ya kufundishia inayojitosheleza na itakayoenda sambamba na mahitaji ya dunia ya leo.

Kwa dhati kabisa, napendekeza kubaki na Kiswahili kwa kuwa hatutapoteza muda wa kuwafundisha wanafunzi shule ya msingi kwa kiwahili halafu kufanya kinachoonekana ni kuwafundisha vitu hivyo hivyo kiingereza ngazi ya sekondari.

Kiswahili ni lugha kubwa yenye historian a inayojitosheleza kutumika kufikisha taarifa hivyo basi na tukitumie Kiswahili chetu kitufae.

Badala ya kupoteza muda shule ya awali mwaka mmoya hadi miwili, shule ya msingi miaka saba , sekondari ya sekondari ya juu miaka sita kwa ujumla jumlisha na miaka mitatu hadi mitano ya ngazi ya stashahada kulingana na fani husika, tunaweza kupunguza Zaidi ya miaka mitano tukitumia tugha moja kufundishia. Na mtoto akianza shule mapema atamaliza mapema, hivyo atakuwa na miaka mingi ya ujana kuwekeza katika kulitumikia taifa lake kama mzalishaji akiwa ameajiriwa, mfanyabiashara mwenye elimu ama mjasiriamali mbobezi.

Kwa kumalizia, ningependa kutilia mkazo wanafunzi kuchukuwa mapema michipuo ya masomo wanayotaka kubobea kuanzia kidato cha kwanza na sio cha tatu.Lakini yote haya yanategemeana na kupatia ufumbuzi changamoto nilizotangulia kuzizungumzia hapo juu.

Tuijenge elimu yetu ,tuiboreshe, tuikuze ili itukuze itujenge tulijenge taifa letu.
Wino umenitupa mkono, napenda kuwasilisha shukrani zangu za dhati kupata fursa hii.

18/08/2022
NASRA ABUBAKAR SULLE 0657 577 404 , 0744 156915​
 
Upvote 0
Back
Top Bottom