SoC04 Elimu yetu yahitaji mabadiliko makubwa ili kuharakisha maendeleo ya nchi

SoC04 Elimu yetu yahitaji mabadiliko makubwa ili kuharakisha maendeleo ya nchi

Tanzania Tuitakayo competition threads

Erastojhn

JF-Expert Member
Joined
Apr 1, 2012
Posts
223
Reaction score
208
Elimu ndio silaha na nguzo kuu ya taifa lolote hapa duniani. Tanzania kama nchi inapaswa kulitazama suala la ubora na aina ya elimu wapewayo wananchi kama inakidhi mahitaji ya sasa ya nchi hasa ukizingatia dunia kuwa karibu zaidi katika nyanja mbalimbali mfano ajira, biashara na mawasiliano. Kwa bahati mbaya elimu yetu iko 'ICU' na serikali haioneshi kushtushwa na hali na madhara makubwa kwa wananchi wake siku za usoni. Tunapaswa kuchukua hatua zifuatazo ili kulinusuru taifa maana ujinga ni adui wa maendeleo na ili taifa liendelee haraka lazima liwekeze kwenye elimu bora na ya kisasa inayolenga kumkomboa Mtanzania kifikra na kiuchumi kwa faida ya Tanzania na dunia kwa ujumla. Inashangaza serikali inawekeza pesa nyingi kwenye matumizi ya anasa kuliko kuwekeza zaidi kwenye elimu.

Napendekeza yafuatayo yafanyike katika ku'revolutionize' elimu yetu. Bila mabadiliko makubwa kwenye elimu, taifa letu litaendelea kubaki nyuma kwa miaka mingi na sera na mipango ya serikali bila kuwa na elimu bora haitaweza kuharakisha maendeleo ya wananchi kwani tatizo kuu linaanzia kwenye uduni wa elimu yetu.

  1. Lugha ya kufundishia: Ni lazima sasa serikali ikaanzisha lugha ya Kiingereza kama lugha rasmi ya kufundishia kuanzia shule za awali tofauti na ilivyo sasa. Hii itaongeza uelewa zaidi kwa wanafunzi wanapojiunga na masomo ya sekondari. Ni aibu kwa sasa nchi yetu imetengeneza matabaka katika eneo hili. Miaka ya nyuma nilipokuwa nasoma shule ya msingi watoto wa viongozi wote walikuwa wakisoma shule za msingi za serikali, hali ni tofauti kabisa kwa sasa. Leo karibu watoto wote wa viongozi na wenye nafuu ya kiuchumi au wa matajiri wanasoma kuanzia shule za awali kwa kutumia lugha ya Kiingereza. Huu ni ubaguzi na unafiki mkubwa sana kwa viongozi wetu ambao tulitegemea wawe mfano kwa wananchi wanaowaongoza. Wao watoto wao wanasoma kwa lugha ya Kiingereza kwa sababu wanajua faida ya lugha hii hasa ikianza kufundishwa shule za awali na msingi katika masomo yote isipokuwa somo la Kiswahili. Ila la kushangaza hawataki kubadili lugha ya kufundishia katika shule za serikali ili hata watoto wa maskini wapate fursa kama watoto wao ya kukifahamu Kiingereza vyema ili kiwasaidie katika mawasiliano au masomo ya sekondari na elimu ya juu kwa ujumla. Leo mtoto wa darasa la saba ambaye hajapata fursa ya kuendelea na masomo hawezi kupata faida lukuki za walau kukijua Kiingereza. Mfano hata ukimnunulia smartphone ambamo kuna elimu pana nje ya mfumo wa shule na kwa bahati mbaya sehemu kubwa ya elimu mitandaoni inapatikana katika lugha ya Kiingereza. Mimi binafsi nimefaidika sana na elimu ya kwenye intaneti (online) kwa mambo mbalimbali, nimejifunza mengi kutoka karibu kila kona ya dunia kwa sababu ya kukifahamu Kiingereza vizuri. Serikali ama kwa maksudi imeamua kutengeneza 'classes' katika jamii baina ya wenye nguvu za kimamlaka na matajiri au wenye ahuweni ya maisha (middle class) na mafukara na wananchi wa kipato cha chini. Hivi serikali ikianzisha medium ya Kiingereza kuanzia shule za nursery wananchi wenye kiu na Kiingereza ambao wamepeleka watoto wao shule za 'English medium' wangeokoa mabilioni mangapi ya pesa wanazolipa kama ada ambazo ni kubwa katika shule hizo?
  2. Tubadili mtaala kwa kujifunza kwa waliofanikiwa sana katika elimu: Tuna mifano mingi ya nchi ambazo zimefanikiwa sana katika elimu duniani na zimepiga hatua kubwa kimaendeleo. Nchi kama China, Denmark, Norway, India, Finland ni mfano ambapo kama tuko serious kama nchi tulipaswa kuwatuma wataalam wetu kwenda katika baadhi ya nchi hizo kujifunza kwa kina kisha tuka'export' ujuzi wao kwa faida ya vizazi vyetu vijavyo. Katika elimu hakuna shortcuts lazima tupange mipango ya muda wa kati na ya muda mrefu iwe kama sera au dira ya nchi ili hata kunapokuwa na mabadiliko ya kiuongozi serikali mpya inayoundwa ifuate sera ya nchi iliyokubaliwa na wadau wengi ili kufanikisha malengo kwa asilimia kubwa.
  3. Tuboreshe na kutanua wigo wa elimu ya awali (Nursery school): Tafiti mbalimbali zimeonesha kuwa kuna uwezekano mkubwa sana wa mtoto aliyepitia masomo ya chekechea kusoma hadi elimu ya chuo na utafiti mwingine umeonesha kuwa kati ya umri wa miaka 0-3 kuna mabadiliko makubwa ya kiakili na kifikra anayopitia mtoto. Hivyo, kukiwa na mazingira mazuri ya kujifunzia katika umri huo mdogo uwezo wa mtoto kitaaluma huongezeka. Kwa sababu hizi muhimu na nyingine inaonesha kuwa Taifa linalowekeza vema katika elimu ya awali litavuna faida kubwa baadaye kwa kuwezesha watoto kufika mbali zaidi kielimu na hivyo kuliletea taifa maendeleo makubwa siku za usoni. Serikali inapaswa kujenga shule nyingi za awali zilizo bora nchi nzima ili watoto wengi wapate elimu hiyo kabla ya kuingia darasa la kwanza.
  4. Maslahi bora kwa walimu wetu: Mbali na kuchukua walimu ambao walifaulu vizuri shuleni na kuboresha vyuo vinavyowaandaa, ni muhimu sana kuboresha mishahara na maslahi mengine ya walimu ili tuweze kupata ubora zaidi katika suala zima la ufundishaji wa wanafunzi wetu.
  5. Tutoe elimu ya vitendo (vocational) kulingana na mahitaji ya sasa: Ni muhimu serikali ikaanzisha kozi mbalimbali kwenye vyuo vyetu vya veta nk ambazo zitajibu mahitaji ya sasa ya Watanzania. Mfano kuwa uhitaji mkubwa wa mafundi wa kutengeneza simu, hivyo serikali ikianzisha kozi kama hizi itasaidia sana kutoa ajira nyingi kwa vijana wetu nchini kote. Kozi za aina hii ni nyingi, mfano ujuzi wa ufugaji samaki, ufugaji wa kisasa wa mifugo, biashara na fursa kwenye internet, mbinu bora za kilimo cha kisasa nk. Hii itasaidia kuwapa ujuzi vijana wetu wengi na hivyo kwa kiasi kikubwa kutatua tatizo kubwa la ukosefu wa ajira au hali ya vijana wetu kushindwa kujiajiri.
Katika kuhitimisha kwangu napenda kueleza yafuatayo: nchi yetu iko nyuma sana sana kielimu katika ranks za dunia. It's never too late, tunayo nafasi ya kwanza kukiri kuwa tumekosea na kuuangusha uma wa Watanzania. Iwapo tungewekeza vya kutosha kwenye elimu tungekuwa tumetatua matatizo mengi ambayo leo yapo kwa sababu ya ujinga. China ilikaa chini zaidi ya miaka 40 iliyopita na kupitisha mageuzi makubwa katika elimu yao ikiwa ni pamoja na kutuma wanafunzi wa Kichina kwa maelfu kwenda kusoma katika nchi za kimagharibi kupata ujuzi wao na kisha kurejea nchini mwao kuijenga China. Na kipindi hicho walipokaa na kupitisha maazimio kadhaa katika elimu, China ilikuwa bado ni nchi ndogo kiuchumi. Miaka 40+ baadae wameona faida ya walichokifanya katika elimu na leo China imepiga hatua kubwa katika nyanja karibu zote huku ikiwa na uchumi wa pili kwa ukubwa duniani. Hii inamaanisha inawezekana kuinua taifa tukiweka siasa pembeni na kukubali kubadilika. Inchi yetu ina utajiri mwingi haiwezi kushindwa ikiamua kuwekeza na kufanya an overhaul ya elimu yetu kwa faida hasa ya vizazi vijavyo. Tunaweza, watu tunao, pesa zipo, unakosekana utashi tu wa kisiasa. Elimu pekee iliyo bora itatupeleka katika Tanzania tuitakayo na kwa hakika italeta faida kubwa ambazo nchi nyingine zilipata baada ya kuwekeza kwenye elimu.
 
Upvote 1
. Leo mtoto wa darasa la saba ambaye hajapata fursa ya kuendelea na masomo hawezi kupata faida lukuki za walau kukijua Kiingereza. Mfano hata ukimnunulia smartphone ambamo kuna elimu pana nje ya mfumo wa shule na kwa bahati mbaya sehemu kubwa ya elimu mitandaoni inapatikana katika lugha ya Kiingereza. Mimi binafsi nimefaidika sana na elimu ya kwenye intaneti (online) kwa mambo mbalimbali, nimejifunza mengi kutoka karibu kila kona ya dunia kwa sababu ya kukifahamu Kiingereza vizuri
Hakika, kiingereza ni muhimu hasa katika kujifunza.

Lakini swali, kuna tatizo gani tukianza na Kiswahili msingi halafu Kiingereza atakidaka sekondari hadi anamaliza kidato cha nne?? Maana yote hii bado ni elimu ya MSINGI. La kwanza hadi kidato cha nne.

Je mazingira yetu tayari yanaruhusu mtoto kuanza na kizungu mwanzo mwisho?

maelfu kwenda kusoma katika nchi za kimagharibi kupata ujuzi wao na kisha kurejea nchini mwao kuijenga China. Na kipindi hicho walipokaa na kupitisha maazimio kadhaa katika elimu, China ilikuwa bado ni nchi ndogo kiuchumi.
Nakubali na kuzipenda pointi za kujifunza kwa waliofanikiwa na ku'import ujuzi. Insha nzuri
 
Back
Top Bottom