Damaso
JF-Expert Member
- Jul 18, 2018
- 3,978
- 6,739
Ni saa 10 na nusu alfajiri ninaamka kujiandaa kwa ajili ya kwenda harakati, nafuata taratibu zangu za kila siku, napiga goti namshukuru Mungu kwa uzima naingia bafuni kujishikashika na sabuni pamoja na maji ya baridi ili kuzimua akili ikae mguu sawa. Huwa nachukua nusu saa tu kujiandaa na kwenye saa 11 kamili ninakuwa njia kuelekea ofisini ila kuna kitu nimekiona hakipo sawa kwa zaidi ya miaka miwili.
Tokea kumekuwepo na utiritiri wa hizi shule za binafsi maarufu kwa jina la English Mediums basi sio ugeni kukutana na gari la shule (School bus), mabasi ya njano, haswa majira haya ya saa 11 na saa 11 na nusu zikiwa na watoto wadogo wakienda shule. Ni jambo la kufikirisha sana, kiasi kwamba ukitazama ndani ya magari hayo utakuwa kitoto kimeuchapa usingizi bila wasiwasi, hajafunga mkanda, kiufupi usalama ni mdogo kwa watoto wetu.
Masuala ya msingi ambalo nimepata kuona tunawaumiza watoto wetu ni mambo mawili:
- Suala la kuamka kuwahi shule, kwa hakika ninathubutu kusema kuwa Mtoto anayesoma shule ya Msingi Muungano anaenjoy Maisha ya shule kuliko ambaye anasoma St. X English Medium. Unaweza kukataa ila nitakupa scenario hizi kadhaa uone mtoto wa kidumu na mfagio anaishi huku wenzake wakiishia. Mtoto anayesoma Muungano anaweza kuamka saa 12 na nusu tena kwa bakora za kutosha kutoka kwa Bi Mkubwa na darasani akaingia saa 1 na nusu, Maisha yanasonga. Mapumziko kwake ni kwenda kucheza mpira na kula barafu za mama Aisha. Turejee kwa Mtotoanayesoma St. X English Medium ambapo tokea saa 11 na nusu au saa 12 anazunguka na basi mji mzima na akiingia darasani saa 1 kamili, mapumziko yao watakunywa uji na kupumzika kweli. Wadau wa elimu tazameni kwa ukaribu jambo hilo, binafsi kuna shule zaidi ya tano ambazo saa 12 kasoro mbasi yao yanazunguka na watoto wakiwa wameuchapa usingizi wa kutosha. Montesorri, Jabal Hira, pamoja na Buyegi Archbishop Mayala nimepata kupishana na magari yenu mara kadhaa alfajiri watoto wakiwa wameuchapa.
- Suala ya mabegi makubwa na mazito, nina Rafiki yangu ambaye mtoto wake amepata ulemavu kwenye mgongo, mtoto wa darasa la nne ila anabeba begi zito utadhani utingo. Hakuna maana ya uwepo wa ratba za masomo (timetable) halafu wanafunzi wakapewa maelekezo kuwa abebe vifaa vyote vya shule kila siku. Kwanini shule zisitengeneze makabati ambayo watoto watahifadhi vifaa vyao na kutembea na vifaa kiasi tu. Kuna wakati Bismarck na Tulele walikuwa wanaongoza kwa watoto wao kubeba vitu vizito, yaani begi utadhani mkimbizi!? Askari wa Barabarani kuweni makini na mabasi haya kwani sidhani kama ni utaratibu kuendesha watoto kwa mtindo wenye hatari namna hiyo. Simamisha gari kisha ingia watazame watoto waulize kama mikanda inafaya kazi, je kuna Fire extinguisher na vifaa vya usalama, ongea na msimamizi wa watoto upate kujua hali halisi ya watoto.
Mamlaka husika zifanye jitihada za msingi katika hili, watoto wetu tunawapatia ulemavu kwa uzembe wa kijinga jinga, watoto wapate usingizi wa kutosha, waamke mapema ila sio saa 10 au 11 kwa kigezo cha kuwahi shule! Hakuna tuzo ya mwanafunzi aliyewahi shule. Tuache kuweka pamba masikioni.
SIO KWA UBAYA! TUNAREKEBISHANA TU!