Vigogo TANROADS wajigawia 'vijisenti'
Mwandishi Wetu Julai 29, 2009
Kigogo wizarani ashirikishwa
WAKATI kukiwa na malalamiko lukuki kuhusu hali mbaya ya miundombinu ya barabara nchini, vigogo katika Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) pamoja na Wizarani wanapongezana kwa kupeana mamilioni ya fedha kupitia utaratibu wa honoraria.
Miongoni mwa malipo ya aina hiyo ni shilingi milioni 40 zilizolipwa Desemba 23, mwaka jana kwa vigogo sita baada ya kuidhinishwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa TANROADS nchini, Ephraem Mrema.
Malipo hayo yalifanyika kufuatia barua kumbukumbu namba trd/hq/a/c/03/1 ya Desemba 17, 2008 ya Kaimu Afisa Utawala, ambaye hata hivyo hakuonyesha jina lake, kwenda kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa TANROADS.
Katika barua hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari, Honoraria, Kaimu Afisa Utawala huyo (Ag HRA) anatoa sababu za pendekezo lake la kupatiwa vigogo hao honoraria hiyo kuwa ni kutokana na mchango wao mkubwa walioutoa hadi kufanikisha nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi wa TANROADS.
Mgawo wa awali wa honoraria hiyo unaonyesha kuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu, Omar Chambo alipwe shilingi milioni nane lakini ikafanyiwa marekebisho na Afisa Mtendaji Mkuu alipoipitisha Desemba 18, 2008 ambapo alimuidhinishia shilingi milioni 10.
Wengine katika mgawo huo wa honoraria ambao kila mmoja aliidhinishiwa kulipwa shilingi milioni sita na Afisa Mtendaji huyo wameorodheshwa kama ifuatavyo J.M.E Mwakitosi (Kaimu DAP wakati huo), Loyce Lugoye, Agnes Meena, N. J. Kipanda na Peter Mhimba