Ilikuwa yapata mida ya saa saba za usiku breki za gari aina ya spacio nyeupe zilifunga mbele ya jengo kubwa la ghorofa moja,jengo hili lilionekana kuachwa ukiwa huku likitapakaa giza na kuwa kama halijamalizwa.
Watu wanne tulishuka garini huku kiongozi wetu Evelyn akituongoza kuelekea kwenye jengo hilo.
Nilipata kudalizi mazingira ya nje ya jengo hili,miti na vichaka vya hapa na pale vilijenga taswira ya kutisha na kuwa kama watu wakitutazama!, kibaridi chepesi nacho hakikuwa mbali tayari kilipokea miili yetu nakuanza kutulaki bila hiana,hakukuwa na nyumba nyengine jirani kitu kilichofanya nianze kuhisi jengo hili labda lilikuwa ofisi mpaka kuja kutengwa huku pekee!.
Mwenyeji wetu aliendelea kutuongoza mpaka kwenye ukumbi mmoja mkubwa uliopatikana kwenye jengo hili,alisimama Kisha akatugeukia "kwa siku ya leo tutajihifadhi hapa,kesho tutapata eneo bora zaidi" alinena eve huku akituangalia kama tulikubaliana na swala lake!.
Hakuna aliepinga,kimya chetu kilimaanisha kukubaliana na swala lake.
Aligeuka Tena nakuendelea kupiga tambo zilizofuata ngazi iliyokuwa ikielekea juu ya jengo hili,Napo tulifikia kwenye ukumbi japo wenyewe haukuwa ukumbi mpana zaidi wa lile jengo la chini.. niliyapitisha macho yangu huku na kule nakuona mablangeti kadhaa,tochi na maji kwenye dumu yakiwa juu ya kiti cha mbao.
Mara hii eve aliikaribia tochi nakuiwasha kisha akaitundika ukutani hivyo walau mwangaza ulipata kuwepo maeneo yale,aliyaendea mablangeti yale Kisha akamkabidhi kila mtu blangeti moja. Alitutazama kwa tuo Kisha akatuambia
"Mnaweza kupumzika!".
Sote tulimtazama nakuwa Kama watu wenye maswali,ndipo mimi nikaamua kuwatangulia wenzangu kuuliza.
"Unafikiri hili litakuwa eneo salama kwetu..?"
"Ndio maana tupo hapa" alijibu eve.
Kilipita kimya kifupi Kisha Jeff akaongeza swali jengine kumuelekea eve "asubuhi tutakwenda wapi..?"
Eve alijisaula halafu akajibu "eneo salama zaidi ya hili!".
Eve alijibu huku akimshika mkono anitha ambae waliongozana mpaka kwenye moja ya kona kulipokuwa na mabox yaliyopangwa.. walituacha huku mi na Jeff tukiwatizama.
Kwa sauti ya chini Jeff akaninong'oneza "unafikiri kwa kiasi gani tunapaswa kumuamini huyu mwanamke..?"
"Tutamwamini zaidi mpaka pale tutakapojua ukweli kuhusu yeye" nilimjibu Jeff huku nikimtazama ambapo mara hii alikuwa amejifunika blanket lake mwili mzima nakuacha kichwa chake kikiwa wazi.
Punde hiyohiyo eve alirudi tulipokuwa lakini kabla hajatufikia akatuita
"Gentlemen"
Tulibaki tukimtazama bila kumjibu chochote mpaka alivyosimama mbele yetu Kisha akaongezea "nafikiri ni muda wa kupumzisha vichwa vyenu" tuliendelea kumtumbulia macho ambayo hayakuonyesha kuwa na usingizi.
"Bado hujatukata kiu" nikatupia sentensi hiyo fupi.
"Kiu ipi..?" Akauliza eve huku akijifanya Kama hakuelewa vyema sentensi yangu.
"Kiu ya kukufahamu vyema na kuwafahamu maadui zetu!" Niliongeza.
Eve akaachia tabasam hafifu usoni pake Kisha Kama asiejali akatuacha na kuendea tochi kisha akaizima!. Nilimpa ishara Jeff kuwa akapumzike nae akafanya hivyo kwa kuchagua moja ya kona na kwenda kujibwaga.
Tulibaki mimi na eve,nikiwa nimesimama nyuma yake kwa takribani tofauti ya tambo kumi hivi..
"Jonas" eve aliniita huku akigeuka na kunitazama mahala nilipo ambapo mwanga hafifu wa mbalamwezi changa ulipambana na kiza kutumulika.
Sikuitika bali nami nilimtizama kwa tuo nikingoja aseme kile alichokusudia..
Kabla ya kusema chochote alinisogelea kwa mara nyengine akaachia tabasam ambalo nililisoma halikuwa tabasam halisi Kisha kwa kutumia mkono wake wa kulia akaushika mkono wangu uliokuwa na bandeji ndogo akanitazama kwa tuo Kisha akahamishia macho yake kwenye uso wangu palipokuwa na mkwaruzo. Taratibu akauvuta mkono wangu na kunisogeza zaidi kisha akaninong'oneza kwenye sikio langu la kushoto
"Pole mpenzi".
Baada ya sentensi hiyo fupi akauachia mkono wangu nakuanza kuongoza akielekea nje ya jengo lakini kabla hata hajazifikia ngazi nilimfuata na kumshika bega lake la kushoto na kumgeuza anigeukie!.
Tulibaki tumetazamana huku nusu ya mwili wake ukiwa umezielekea ngazi na nusu akinielekea mimi!.
Sikusema chochote wala nae hakusema chochote,punde akaamua aendelee na safari yake niliyomkatisha.
Nilimuangalia akizishuka ngazi kwa mwendo wa wastani huku nami hasira za mkizi zikianza kunivamia baada ya kuona eve hataki kuleta ushirikiano katika hili!. Nilishusha pumzi ndefu Kisha nikaamua nimfate hukohuko.
Nilimuona akiliendea gari na kufungua buti kisha akatoa box la chuma ambalo sikujua ndani yake kulikuwa na nini!,mawazo yangu hayakutaka kujishighulisha na kile alichokuwa anakifanya bali zaidi nilitaka ayajibu maswali yangu.
Nilimsogelea na kumuangalia tena
"Kwanini hutaki kujibu maswali yangu..?" Nilimuuliza kwa sauti ya ukali kidogo.
"Jonas" aliita Kisha akatulia,halafu akaendelea "Mimi nashughulikia usalama wenu zaidi na wala sio maswali yenu!" Alinijibu huku akionyesha msisitizo!.
Akafunga buti la gari na kulichukua box lile la chuma akiniacha nikiwa nimesimama mkabala na gari.
Sikulizika mara hii nilimfata kwa tambo kubwakubwa na kwenda kusimama mbele yake, nilimtazama machoni huku nikionyesha kutokujali mzigo wake alioubeba ulionyesha kuanza kumzidia!.
"Usiponiambia ukweli kuhusu wewe na watu wanaokufatilia basi sitaambatana na wewe".
Hakujibu chochote bali alijivuta kwa pembeni nakuendelea na safari yake.. niliendelea kumtizama mpaka alipoishilia kwa ndani.
Nikiwa nimesimama pale mawazo na hasira zilizidi kunipanda na kutamani hata nitokomee kusikojulikana lakini nilimfikiria rafiki yangu Jeff ambae nilimuimgiza kwenye mkasa huu!,mkasa ambao hivi sasa ulimfanya aiche nyumba yake nzuri nakuja kulala kwenye hili jengo lenye giza. Nafsi ilinisunta na kujiona mwenye hatia kuhusu rafiki yangu jeff.
Kuhusu anitha sikuhofu sana kwani sote tulikutana kwenye mkasa huu japo mpaka Sasa sikujua kipi haswa kilimsibu!.
Nikiwa nawaza hayo hatua za eve zikanigutua tena,mara hii tena alikuwa akitoka kwenye lile pagala na kuiendea gari Kisha akafungua mlango wa mbele na kutoa begi dogo la mgongoni akalibeba nakuanza kurejea aliponifikia akasimama na kunitazama na kunena!.
"Nipo hapa kuhakikisha usalama wenu niliouvuruga,ila kuhusu mimi na hao watu niachie mimi Jonas" aliongea hayo nakuonyesha msisitizo.
Hapohapo nami nikamdakia
"Usitufanye sisi watoto wadogo utupeleke vile utakavyo!"
Hakuongeza chochote zaidi ya kuendelea na hatua zake zilizompoteza kizani akizamia kwenye gofu hili.
Niliendelea kubaki pale nje huku hasira zangu zikizidi kunitiririka hadi kuanza kuhisi koo langu likipatwa na maumivu hafifu.
Nililiangalia pagala lile na kuikumbuka nyumba yangu iliyokuwa na kuta zenye rangi ya maziwa kwa ndani,nilivikumbuka vito vyangu vichache vilivyopatikana ambavyo nilivipata kwa kazi yangu ya udereva taksi.. hata kitanda changu kilichonipokea kila siku baada ya mihangaiko ya huku na kule,leo hii nilikiacha mkiwa na kuja kujilaza katika jengo hili lisiloisha.
Ambalo lingetosha kunitesa kwa baridi kutokana na kutokuzibwa maeneo mengi tena huku mbu wenye uchu wakiifaidi damu yangu!. Niliiwaza kazi yangu ya udereva ambayo hata boss wangu sahivi hakujua nipo wapi.. sikujua alifanya nini sahivi,labda kunitafuta huku na kule akijaribu kuniulizia!. Nilijikuta nikiwaza maswali ambayo sikuwa na majibu yake.
Punde nilianza kurejea taratibu kwenye jengo hili,nilipita kwenye lango lake ambalo bado lilikuwa wazi yeyote angeweza kupita na kufanya atakavyo.. niliamua kujituliza kwenye ngazi ambazo ziliekea kwenye floor ya juu. Nilikaa pale nakushika kichwa changu kilichojazwa mawazo na maswali lukuki ambayo yalihitaji majibu,ila mjibuji alionekana kuwa mkaidi,hata kufanya safari yangu iishie katika ngazi hizi kwani nilihisi kumfata huko alipo kulikuwa kwenda kujiongezea hasira zaidi.
Zilipita dakika kadhaa nikiwa nimekaa katika ngazi huku nikizitazama nguzo mbili zilizomulikwa na mwanga hafifu wa mbalamwezi,sakafu ya zege ilitapakaa vumbi na vipande vichache vya mbao!.
Punde hii nilihisi mkono ukinishika bega langu lakushoto!,nilipogeuka nilikutana na uso wa eve ulionisabahi na kuisikia sauti yake ikiniuliza
"Hauhisi baridi..?"
Sikujibu chochote
Eve alikuja na blanket langu nililokuwa nimelitupa chini,akanifunika kuanzia mabegani kwangu Kisha akaketi upande wangu wakulia na kunisogelea hata mwili wake kugusana na mwili wangu!.
Nilimtizama nae akanitazama.. bila hata kujali akakilaza kichwa chake kwenye bega langu!,kikapita kimya ambacho kilipambwa na kelele za chura waliokuwa wametapakaa kwenye vichaka huko nje.
"Nisamehe mpenzi kwa kukutia kwenye huu mkasa!" Alinena eve huku akiendelea kukiegemeza kichwa chake kwangu.
Nilitulia pasipo kujibu chochote,
"Sikudhamiria kufanya hivyo ila nakuhakikishia usalama wako utakuwa juu yangu mpaka hili liishe!".
Aliendelea.
Alitamka maneno hayo huku alionekana kujidhibiti vilivyo,laiti angelijua maneno hayo kwangu yalipita patupu nakuwa kama simuelewi alichonena!.
Kilipita kimya tena ndipo akabadili mwelekeo wa maongezi.
"Ilikuwa nzuri sana siku ile kwenye gari!" Alinena huku akiwa amenishika kwa kunikumbatia kwa pembeni na kunitazama. Napo sikumjibu chochote!.
Alipoona kimya akaongeza "it was so sex".
Hilo neno sikusubiri lipite,kwa sauti ya kukereka nikaongeza
"Ndio ilikuwa nzuri sana haswa pale ulipoipenyeza risasi ya kifua kwenye mwili wa yule mtu mwenye miraba minne!"
Sote tukabaki tumetazamana,lakini macho yake hayakuwa na ujali katika sentensi yangu!,hata midomo yake ilionyesha hilo kwa kuanza kuliangua tabasam hafifu!.. Kisha akaacha kuniangalia na kuangalia mbele zilipo zile nguzo kubwa mbili.
Swali jengine likamtuka "kwani hukupenda..?"
Swali lake la kuniuliza kuhusu kupenda ndilo swali ambalo sikulipenda zaidi toka nimfahamu Evelyn!.
Nilijikwatua toka kwenye mikono yake nakusimama kisha nikaanza kupandisha ngazi!.
Ghafla katika punde hiyohiyo ilisikika mivumo ya gari ambayo iliivutia macho yangu kutazama nje,ndipo macho yangu yakapokelewa na mianga ya taa za gari mbili zilizokuwa zikija kwa spidi katika jengo tulilomo!,eve nae alinyanyuka kwa haraka huku akitazama nje nilikotazama.
Tuliziona gari zile zikifunga breki kwa kuliweka gari letu katikati pale lilipokuwa limepaki!,walichomoka wanaume waliovalia suti huku wakiwa na mitutu mikononi mwao kisha wakalishambulia gari letu kwa kulipiga risasi kadhaa!.
Nilimuona eve akitimua mbio akipanda ngazi nakuelekea katika lile box lake la chuma,akalifungua nakutoa bunduki aina ya pisto mbili akanirushia moja kisha moja akaitia kiunoni mwake na kutoa bunduki nyengine kubwa yenye mkanda nakuivaa,kwa haraka Tena akatoa bastora mbili moja akamkabidhi Jeff ambae bado lenge la usingizi lilikuwa limemvaa!,na nyengine alimkabidhi anitha ambae alikuwa akitweta kwa uoga baada ya kusikia milio ya bunduki huko nje!.
Eve alimuangalia anitha alieshangaa kifaa kile ambacho hakujua kukitumia!.. eve alilitambua hilo na kumuambia "utabonyeza hilo tufe huku ukimuelekezea adui"
Anitha alibaki akikodoa tu..
Eve alinyanyuka huku akifunga sanduku lile alinitazama huku akinijia na kuniambia nimfuate,tulishuka ngazi kwa tahadhari huku tukiwaacha Jeff na anitha katika floor ya juu.
Tulipoziacha ngazi tuliinama huku tukitembea harakaharaka,tulipoufikia mlango wa kuingilia tulitulia mimi nikaegama upande mmoja wa ukuta nae eve akafanya hivyohivyo katika upande wa pili.. kwa tahadhari akachungulia nje huku akiitoa bastora yake kiunoni na kuikamata vilivyo mikononi pake,nami nikaikamata vyema bastora yangu Kisha kwa tahadhari nikachugulia nje kulipokuwa na adui zetu ambao walionekana Kama wakijadili kitu na kutawanyika kuanza kuusogelea mlango wa jengo tulimokuwepo..
Walipotawanyika ndipo nikapata wasaa wa kumuona tena yule mzungu mwenye pua ndefu akiwa sambamba na wale watu japo yeye alibaki nyuma kwenye gari akiendelea kuvuta sigara huku akishikilia mikononi pake bunduki ambayo sikuielewa ni aina gani ya bunduki.
Eve alinitazama Kisha kwa sauti ya chini akaniambia "risasi yangu ya kwanza itakuwa ishara ya wewe kushambulia"
Niliitikia kwa kichwa kisha nikayarudisha macho yangu nje ambapo adui zetu bado waliendelea kusogea kwa tahadhari huku wengine wakitambaa kwenye majani!.
Kwa haraka haraka nilipata kuwahesabu nakugundua walikuwa watu saba tu!,mapigo ya moyo yalianza kunipwita kwa pupa nilipoanza kuona ugumu wa kupona mbele ya watu hawa wasiokuwa na chembe ya huruma!.
Kwa mara nyengine nikajikuta nikijilaumu kwa kuongozana na eve mwanamke mwenye mabalaa!,hata ule usemi wake wa kunena kuwa hapa kulikuwa ni eneo salama niliuona ni ulaghai tupu!,nilitulia na kumeza funda la mate kisha nikavuta pumzi ndefu wakati huohuo nilimuona eve akichungulia kwa kuibia kisha ukafuata mlio wa bastora yake ambayo haukupita patupu baada ya kusikia kelele za mtu akilala kwa maumivu!.
Ilifuata milio mingi ya bunduki zikipiga hovyo eneo tulilopo,huku nikizisikia baadhi ya risasi zikitua kwenye ukuta nilioegemea!.
Jambo hili lilinitisha zaidi katika maisha yangu ni kama vile nilimuona malaika wa mauti akipiga hesabu za kifo changu mbele ya macho yangu!,kijasho hafifu kikanikumba nakujikuta hata pumzi zangu zikitetereka.
Punde milio ya risasi ikakoma na kubaki sauti ya yule mtu aliepigwa risasi ikigugumia!.. bila kulaza damu eve akajibu pigo jengine kwa kufyatua risasi iliyopita patupu pasipo kulenga!,adui zetu nao wakajibu mapigo.
Eve alinitazama kwa jicho la mkazo lililodumu kwa sekunde moja tu!,nilijua alitaka niuvae ujasiri nami niziteme cheche za kile nilichokishika mkononi.. nilimtizama pia Kisha kwa kuibia nikachungulia nje hapohapo nilipokelewa na milio ya risasi iliyoelekezwa kwangu.. kwa haraka niliurudisha uso wangu nakusikilizia risasi tena zikikita katika ukuta nilioegemea,nilishusha pumzi nakuvuta miguu yangu kwa kuiweka sawa.
Mashambulio yalikwama kwa pande zote mbili ukabaki mchezo wa kuviziana,niliihamisha shingo yangu na kwenda kuchungulia katika dirisha lililokuwa karibu nami! Hapo nikauona mgongo wa adui yangu ukiwa umejisaula huku wenyewe ukihisi upo mahali salama,bila hata kufikiri mara mbilimbi niliionyoosha bunduki yangu na kubonyeza tufe langu lilloiachia rasasi iliyokwenda kutua kwenye mgongo wa adui yule!.
Sauti yake mbaya ya makelele ilisikika ikiyoyoma kwa sekunde kadhaa Kisha tena kimya kikatawala,nilipomtupia jicho eve alinionyesha kitabasam ushenzi ambacho sikujua kina maana gani.
Tuliendelea kujibanza pale huku milio michache ya bunduki ikitawala punde nilisikia sauti za miruzi ikipigwa huko nje!.. adui zetu walikuwa wakipeana ishara ambapo hatukujua zilikuwa ishara za nini hapo ndipo nikamuona eve akitupia jicho kuangalia kama Kuna chochote.. aliporudisha macho yake yalionyesha kama hali ya hatari ambapo alinionyesha ishara ya kwamba adui zetu walianza kusogea ili kutafuta wigo wa kuweza kutushambulia!.
Ilipigwa risasi moja iliyopita mlangoni na kwenda kupiga hadi katika nguzo moja kati ya zile nguzo mbili!,hapo ndipo nilihisi kuwa adui zetu walisogea karibu zaidi.. eve akajibu mapigo kwa kuachia risasi moja ambayo ilipiga bila shabaha,nami nikaunga kwa kuachia risasi nyengine moja ili kuwatuliza adui zetu.
Huko juu sijui Jeff na anitha walikuwa na hali gani, nafikiri milio ya bunduki ilizidi kuwatisha zaidi.
Eve alinipa ishara kuwa nishambulie nami nikafanya hivyo,akapata upenyo wa kuvuka mlango na kutua upande niliopo.. niliacha kushambulia na kumtizama,akavua bunduki yake ile kubwa na kunikabidhi baada ya kuikoki akasema kwa kuninong'oneza
"Hakikisha havuki mtu kwenye huu mlango!"
Nilipigwa na butwaa kuona nakabidhiwa ulinzi wa kulinda watu wenye siraha na wazoefu katika mapambano wasipite kwenye mlango uliowazi!!,nilijikuta nikilamba lips zangu za midomo huku nikimtizama eve aliekuwa akinipa maelekezo ambayo hata sikuwa bayana kutatilia maanani isipokuwa niliwaza umauti tupu!.
Eve alichomoka na kuambaambaa mpaka kwenye moja ya dirisha akachungulia kwa nje kisha nikamuona akishambulia kwa bastora yake na kutulia nami nikachungulia kwenye dirisha la karibu yangu sikuambulia chochote!. Punde nikasikia kama mtu akinyata kuukaribia mlango!. Nilitulia na kujiweka sawa minyato nayo ikatulia zikapita sekunde tano minyato ikarudi tena. Nikautanguliza mdomo wa bunduki yangu kuchungulia nje kisha jicho langu likafuata!.
Hapohapo nilipotazama vizuri niliona mguu wa mtu ukiwa umeegemea nguzo ndogo ya jengo hili iliyokuwepo nje, taratibu nikaichomoa bastora yangu ndogo kisha nikasema na mguu ule!.
Sauti ya ukelele uliambaa tena kwa uchungu huku kikifuata kishindo cha mtu kuanguka kama gunia! "Puu" hapohapo alipoanguka niliweza kuuona ubavu wake wa kulia ukinielekea nao pia nikasema nao kwa kuachia risasi mbili zilizosema na adui huyu hata kushindwa kutoa tena ukelele!. Damu zake zilitapakaa eneo hili la mbele ya jengo huku mashambulizi yakifunguliwa kama mvua zilizokuwa zikinyesha pasipo mpangilio!.
Hakika mashambulizi ya muda huu yaliongea dhamiri nzima ya neno mauti!.. zilikita risasi juu,chini hata na katikati.. ukuta nilioegemea ndio Kinga pekee niliyoitegemea,mapigo ya moyo yalifuruma kwa nguvu kwani adui hivi sasa hakunirihusu hata upenyo wa kuchungulia!.
Mara hii niliamua kuuachia mlango na kwenda kwenye kona nyengine ya dirisha nilitulia hapo nikisubiri adui atie mguu wake tu nami niipeperushe nafsi yake!.
Sikujua wapi eve alikuwa,huu ndio muda ambao nilihitaji mwanamke huyu arudi na akae karibu yangu,nilisahau kama alikuwa ni yule niliemuita shetani.. nilijikuta nikiropoka tu kwa sauti kali "eve"
Hazikupita hata sekunde nyingi eve alikuwa pembeni yangu akihema kwa pupa!.. nilimtizama Kisha akazungumza huku akihema
"Nilikuwa nikitafuta njia ya kutorokea lakini naona adui kazunguka kote!"
Sentensi yake hiyo ilikuwa kama kitu kizito kilichogonga kisogoni pangu!.. Sasa niliuona mwili wangu ukienda kutobolewa na risasi za adui!.
Eve hakuwaza mara hii aliishika bunduki ile kubwa aliyonipa na kulikaribia dirisha nakuanza kushambulia!. Nilibaki nikimtizama kama mwenye kupoteza matumaini!
"Jonas"
"Jonas"
"Jonas"
Iliita sauti ya eve mara ya tatu ndio nikagutuka,nikamuangalia na kuniambia "adui mlangoni"
Kauli yake ilinifanya niinyanyue bunduki yangu na kupiga pale mlangoni pasipo uangalizi ambapo niligundua ilisaidia kumzuia adui alietaka kuingia ndani!.
Mara nilimuona Jeff akishuka ngazi pekee nakutufata tulipo!.
Huku jasho na mitetemo ikimtoka alinikaribia na kuniangalia nae akaanza kushambulia huko nje!.
Hili ni moja kati ya jambo lililonipa tumaini katika vita hii!,rafiki yangu huyu hii ndio ilikuwa moja ya sifa yake hakupenda nipambabe peke yangu,siku zote alikuwa upande wangu.
Eve aliacha kushambulia na kumuuliza Jeff "Anitha yuko wapi..?"
Yupo juu alijibu Jeff huku akishambulia.
Niliitazama bastora yangu na kugundua kuwa iliishiwa risasi hata bila kuuliza eve aliliona hilo na kunipatia risasi nyengine.
Ukali wa mashambulizi ulizidi kupamba moto adui akitaka kuingia ndani nasi tukijitahidi kuuzima moto huo kwa kujibu mashambulizi.
Ulifika wakati ambao sitaweza kuusahau maishani mwangu!,wakati ambao ulikuwa ni mgumu kama huu Jeff aliamua kurudi floor ya juu kufuata risasi zaidi ndipo kwa bahati mbaya risasi za adui ziliufakamia mwili wake na kumtuliaza chini!. Macho yangu yalikumbwa na mshangao baada ya kumuona rafiki yangu kipenzi akitapatapa huku damu zikimmwagika!.
Nilimkaribia huku nikimuita jina lake
"Jeff"
"Jeff"
Hakuitika zaidi ya kutapatapa,nilitamani kulia lakini hakuna chozi lilipita hata nilizisahau sauti za milio ya bunduki zilizozidi toka kwa adui ghafla nilisikia sauti ya eve ikinena kwa nguvu
"Jonas take cover"
Nilisikia ila sikufanya chochote ndo kwanza nilibaki nimeushika mwili wa rafiki yangu jeff!. Punde hiyohiyo nilishangaa nikipigwa kumbo na eve lililonipeleka chini.. risasi kadhaa zilitukosasa.
Mara hii hakukuwa na kusubiri eve alinivuta huku akishambulia adui ambao sahivi walikuwa mlangoni wakichungulia na kushambulia!.
Nilikuwa nyuma ya eve,eve akiwa mbele yangu akishambuliana na adui huku tukizipanda ngazi.. tulipanda mpaka juu huku tukiuacha ule upande wa juu ukitawaliwa na adui!..
Eve alibaki kwenye ngazi akijibanza na kurushiana risasi na adui punde aling'aka "chukua kamba kwenye box" kwa haraka nililifikia box lile nikakutana na risasi nyingi nikajizolea na kuziweka mfukoni Kisha nikaichukua kamba.. nilipotoa macho yangu kwenye box hili la chuma ndipo nikamuona anitha akiwa amejibanza kwenye kona huku akitetemeka asijui cha kufanya.. nilinyanyuka bila hata ya kuuliza kamba ile ilihitaji nini tayari nilijua Kama hii ilitakiwa ifanyiwe nini.. nilienda kwenye moja ya nguzo iliyokuwepo juu ya ghorafa hili ambayo ilikuwa nyuma kwenye miisho ya kuta,nikaifunga na kuitupa kwa nje Kisha nikachungulia urefu uliofika ile kamba mpaka kule chini bado iliacha nafasi kubwa!.
Sikujali nilienda nikamvuta anitha na kumwambia aitumie kamba ile kushuka chini,alipochungulia isita kidogo lakini alipoyarudisha macho yake ilitosha kumwambia kuwa hiyo ndio njia!.. nae bila hiana huku akitetemeka aliishika kamba Ile nakuanza kishuka..
Wakati akishuka nilidalizi ili nione Kama Kuna adui yoyote alievizia! Lakini angalabu adui hawa walikuwa hawajafika eneo hili la nyuma ya jengo hili..
Anitha alifanikiwa kushuka salama nakuishika bastora yake tayari kwa ulinzi japo kwa kutetemeka!. Nilimrudia eve na kumpiga begani nae akaongeza mashambulizi huku akirudi nyuma.
Niliishika kamba kwa dhati nami nikaanza kutelemka mpaka chini!. Mikito ya risasi iliendelea kulindima,macho yangu juu kutazama Kama eve angelianza kushuka lakini kilipita kimya pasipo majibu!. Hapo nilianza kuuona ugumu ambao alikutananao huko alipo. Isingekuwa rahisi kumuepuka adui hivyo akiwa pekee! Akili ilinicheza ndipo nikaamua nikawachokozea adui nikiwa huku chini.. nilitembea kwa kufuata kuta nilipofika kwenye Kona niliona maadui walivyojidhatiti kumshambulia eve.
Niliinua bastora yangu nakuanza kushambulia pia!,adui walihaha nakuanza kujificha baada ya kugundua kuwa wamepata adui mpya!.
Huu ndio wakati eve alipata upenyo na kudandia kamba nakutufika..
Hatukuchukua muda baada ya mashambulizi mawili matatu tu tuliwakimbia adui zetu na kutokomea machakani....