Fahamu kuhusu makosa ya rushwa na adhabu zake kwa mujibu wa sheria

Fahamu kuhusu makosa ya rushwa na adhabu zake kwa mujibu wa sheria

Mr George Francis

JF-Expert Member
Joined
Jun 27, 2022
Posts
234
Reaction score
376
FAHAMU KUHUSU MAKOSA YA RUSHWA NA ADHABU ZAKE KWA MUJIBU WA SHERIA

SEHEMU YA NNE (4)

mr.georgefrancis21@gmail.com

Ni siku nyingine tena tunakutana katika muendelezo wa mada yetu ambapo hapa tunapata elimu kuhusu makosa ya rushwa na adhabu zake kama kichwa cha somo kinavyoeleza.

Sasa bila kupoteza muda tuendelee na mada yetu kwa kuangazia makosa yafuatayo:

11. Umiliki wa mali ambazo upatikanaji wake haueleweki. Ni kosa kwa Mtumishi wa umma kuwa na mali au pesa nyingi zaidi kuliko kipato chake halali cha sasa au kilichopita na hana maelezo ya kuridhisha kuhusu alivyozipata.

Mahakama ikijiridhisha kuwa kuna mtu anamiliki mali au pesa fulani kwa niaba ya mtuhumiwa au alipewa hizo mali ambazo upatikanaji wake haueleweki kama zawadi kutoka kwa mtuhumiwa na kama hakuna ushahidi unaojitoshereza kuhalalisha umiliki wake basi mali hizo zitachukuliwa kuwa ni mali zinazomilikiwa na mtuhumiwa hivyo kuwa sehemu ya kesi husika inayomkabili mtuhumiwa.

✓ADHABU:
Mtu atakayekutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni kumi (10,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka saba (7) au vyote kwa pamoja.
• Lakini pamoja na adhabu hiyo Mahakama inaweza kuamuru mali hizo za mtuhumiwa zitaifishwe na kuwa mali za serikali. Kuhusiana na kosa hili kuna maelezo mengi muhimu, siwezi kuelezea kilakitu lakini ili kuongeza maarifa zaidi kuhusu kosa hili soma kifungu cha 27(1) hadi (9) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

12. Matumizi mabaya ya mali za umma. Mtumishi wa umma au mtumishi katika taasisi binafsi ambaye kwa kukosa uaminifu au kwa udanganyifu akafuja mali za umma zilizowekwa chini yake au akabadilisha umiliki wa mali hizo na kuwa mali zake au akaruhusu mtu mwingine kufanya hivyo atakuwa anatenda kosa.

✓ADHABU:
Mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake faini isiyozidi shilingi milioni kumi (10,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka saba (7) au vyote kwa pamoja.
• Pamoja na adhabu hii lakini pia Mahakama inaweza kuamuru kuwa mali zilizofujwa ama kubalidilishwa umiliki wake na mtuhumiwa zirejeshwe kwa mmiliki wake halali au mtuhumiwa kuamriwa kulipa fidia kama mali hizo hazipatikani.

Hapa pia kuna options nyingine ambazo Mahakama inaweza kuamua. Lakini ili kuongeza maarifa zaidi kuhusiana na kosa hili, hunabudi kusoma kifungu cha 28(1)(2)(3) &(4)(a)(b)(c)&(d) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

13. Kubadilisha matumizi. Mtumishi wa umma au mtumishi wa taasisi binafsi anayebadilisha mali za serikali au idara ya serikali taasisi binafsi kutoka katika matumizi ya vile ilivyokusudiwa kuwa na kufanya kutumika kwa matumizi yake binafsi au kwa faida ya mtu mwingine kupitia nafasi yake atakuwa ametenda kosa.

✓ADHABU:
Mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni mbili (2,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka miwili (2) au vyote kwa pamoja. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 29 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

14. Kusaidia au kufadhili kutenda kosa. Mtu yeyote anayemsaidia au kufadhili mtu mwingine kutenda kosa la rushwa kinyume cha sheria hii ya kuzuia na Kupambana na Rushwa naye pia atakuwa ametenda kosa la rushwa.

✓ADHABU:
Ukikutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni mbili (2,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka miwili (2) au vyote kwa pamoja. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 30 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Ahsante kwa kuendelea kuwa nami, tukutane katika sehemu inayofuata ya mada hii ili tumalizie mada yetu.

Mungu akubariki sana.

NAME: Mr George Francis
EMAIL: mr.georgefrancis21@gmail.com
 
FAHAMU KUHUSU MAKOSA YA RUSHWA NA ADHABU ZAKE KWA MUJIBU WA SHERIA.

SEHEMU YA TANO (5)

mr.georgefrancis21@gmail.com

Karibu tena mpenzi msomaji wangu. Leo tunakwenda kumalizia mada yetu ya makosa ya rushwa na adhabu zake kwa mujibu wa sheria.

Tumalizie mada yetu kwa kuangazia makosa yafuatayo;

15. Matumizi mabaya ya madaraka. Mtu anayetumia mamlaka au madaraka aliyopewa na umma katika kutekeleza au kushindwa kutimiza majukumu yake kwa manufaa yake binafsi au kwa manufaa ya mtu mwingine binafsi atakuwa ametenda kosa la rushwa.

✓ADHABU:
Ukikutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni tano (5,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka mitatu (3) au vyote kwa pamoja. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

16. Kula njama ya rushwa. Mtu yeyote anayekula njama na mtu mwingine kwaajili ya kufanikisha kutenda kosa lolote ndani ya sheria hii ya kuzuia na Kupambana na Rushwa atakuwa ametenda kosa la rushwa.

✓ADHABU:
Ukikutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni tano (5,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

17. Kushawishi ili kupata upendeleo. Mtu yeyote anyetoa au kupokea rushwa ili mtumishi wa umma atumie nafasi yake vibaya na kumpatia upendeleo fulani kutoka katika utawala au mamlaka za umma kwaajili yake au kwaajili ya mtu mwingine atakuwa anatenda kosa.

✓ ADHABU:
Ukikutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni tatu (3,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka miwili (2) au vyote kwa pamoja. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 33 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

18. Kuhamisha mali iliyopatikana kwa njia ya rushwa. Ni kosa kwa mtu yeyote kubadilisha umiliki au kuhamisha mali iliyopatikana kwa njia ya rushwa kwa lengo la kuficha au kupoteza uhalisia wa mali hiyo au kumsaidia mtu mwingine anayetuhumiwa na kosa la rushwa kuhepuka kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kosa la rushwa alilotenda.

Mtu yeyote anayechukua , anayemiliki au kutumia mali au pesa ambayo anajua fika kwamba mali au pesa hiyo imepatikana kwa njia ya rushwa atakuwa ametenda kosa.

✓ADHABU:
Mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni kumi (10,000,000/=) au kifungo kisichozidi miaka saba (7) au vyote kwa pamoja.

•Kuhusiana na notisi anayoweza kuitoa mkurugenzi mkuu wa mashtaka au defense anayoweza kutumia mtuhumiwa ili kujitetea kuhusiana na kosa hili katika kifungu hiki nikuombe ukasome kifungu cha 34(5)&(6) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Lakini kupata maarifa zaidi kuhusu kosa hili kwa ujumla soma kifungu chote cha 34(1) hadi (6) cha Sheria hii ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

19. Kujifanya ni afisa wa TAKUKURU. Mtu yeyote anayejifanya kuwa ni afisa wa TAKUKURU au mtu mwenye mamlaka chini fulani chini ya sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa au sheria nyingine yoyote inayohusiana na kuzuia na kupambana na rushwa chini ya mamlaka ya sheria hizo atakuwa ametenda kosa.

✓ADHABU:
Mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni mbili (2,000,000/=) au kifungo cha mwaka mmoja au vyote kwa pamoja. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 36(a)&(b) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

EMAIL: mr.georgefrancis21@gmail.com

20. Kufichua taarifa kwa mtu anayechunguzwa. Mtu yeyote anayetoa taarifa kwa mtu anayechunguzwa kwa kufanya au kujihusisha na vitendo vya rushwa bila ruhusa ya kufanya hivyo atakuwa ametenda kosa chini ya sheria hiii ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

✓ADHABU:
Mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kutenda kosa hili adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi laki moja (100,000/=) au kifungo kisichozidi mwaka mmoja (1) au vyote kwa pamoja.

Lakini mtuhumiwa wa kosa hili anaweza kutoingia hatiani endapo mtuhumiwa wa kosa husika alishapelekewa wito wa Mahakamani au kuna vitisho vinavyoweza kuhatarisha usalama wa mtuhumiwa au sababu nyinginezo kama zilivyobainishwa katika kifungu hiki.

Kuongeza maarifa zaidi kuhusu kosa hili hunabudi kusoma kifungu cha 37(1) hadi (3) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Baada ya kuangazia makosa hayo lakini kifungu cha 39 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kinamtaka kila mtu kutoa taarifa pale unapofahamu kuwepo kwa vitendo vya rushwa au kufahamu nia ovu ya mtu kutaka kutenda kosa la rushwa. Huu ni wajibu wa kila mtu na upo kisheria. Hivyo mimi na wewe sote tuna wajibu wa kutoa taarafa kwa mamlaka husika pale tunaposhuhudia vitendo hivi vya rushwa.

Usiogope kutoa taarifa kwasababu ya tunapaswa kuwa wazarendo lakini pia kwasababu sheria inamlinda mtoa taarifa au shahidi wa kosa lolote la rushwa.

✓Kifungu cha 52(3) kinasema kuwa mtu yeyote atakayemdhuru au kumtishia mtu aliyetoa taarifa za kufanyika au kuwepo kwa mpango wa kufanyika vitendo vya rushwa atakuwa ametenda kosa na adhabu yake ni faini ya shilingi laki tano (500,000/=) au kifungo cha mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.

Hadi hapa tumefikia mwisho wa mada yetu. Ahsante kwa kuwa nami tangu mwanzo hadi hapa tulipoishia. Kama umekosa sehemu yoyote unaweza kunitafuta kupitia mawasiliano yangu hapo chini nitakutumia sehemu nyingine zilizopita.

NB: Kataa kutoa ama kupokea rushwa. Toa taarifa kwa mamlaka husika unapokutana na kadhia ya kuombwa kutoa au kupokea rushwa.

Kila mtu apate anachostahili kulingana na anavyostahili na sio kwasababu ya kutoa rushwa.

Mwenyezi Mungu azidi kutubariki sote na kutupatia nguvu katika vita hivyo dhidi ya adui yetu rushwa.

NAME. Mr George Francis
EMAIL: mr.georgefrancis21@gmail.com
 
Back
Top Bottom