Ajali hiyo ilitokea Machi 10, 2019, muda mfupi baada ya ndege hiyo kuondoka Addis Ababa nchini Ethiopia kuelekea Nairobi. Abiria na wafanyakazi wote 157 waliokuwa ndani ya ndege hiyo walifariki.
Kulingana na kampuni ya mawakili inayowawakilisha familia hizo, mchakato wa kisheria nchini Marekani sasa umekamilika na Boeing inatarajiwa kuanza kutoa malipo ya mwisho.
Kwa wastani, kila mwathiriwa anahusishwa na kiasi cha takriban dola milioni 2.73 (Sh353 milioni) kutoka kwenye mifuko ya fidia iliyoanzishwa baada ya ajali hizo.
Fidia hiyo inahusishwa na makubaliano ya Boeing na Wizara ya Sheria ya Marekani kufuatia ajali mbili za ndege aina ya 737 MAX—Ethiopian Airlines Flight 302 na Lion Air Flight 610 ya Indonesia iliyoua watu 189 mwaka 2018.
Uchunguzi wa ajali hizo ulihusisha mfumo wa MCAS na ukazua maswali makubwa kuhusu muundo wa ndege, mafunzo ya marubani, usimamizi wa usalama na mchakato wa kuidhinisha ndege hiyo.
Mbali na fidia kwa waathiriwa, Boeing imekubali kutumia dola milioni 455 (takriban Sh58.9 bilioni) kuboresha mifumo yake ya usalama, uzingatiaji wa kanuni na udhibiti wa ubora.
Kwa familia za Wakenya waliopoteza wapendwa wao, malipo hayo yanakuja karibu miaka saba baada ya ajali, huku yakifungua ukurasa mwingine wa mchakato mrefu wa kutafuta haki na uwajibikaji.
Swali kwa mwananchi: Je, fidia ya kifedha inaweza kweli kufidia hasara ya maisha ya mpendwa, au ni hatua tu ya kusaidia familia kukabiliana na madhara ya janga kama hili?
Source: citizendigital