Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,771
- 41,027
Na. M. M. Mwanakijiji
Mojawapo ya masimulizi ya kiimani ambayo yalinivutia sana tangu zamani ni safari ya wana wa Israeli kutoka Misri kwenda nchi ya ahadi wakiongozwa na Nabii Musa. Simulizi hili nimelisoma mara nyingi na kila ninapolisoma Napata mafunzo mapya. Hata hivyo mojawapo ya mafunzo ambayo naweza kutumia kuelezea siasa zetu za leo katika Tanzania ni ile tabia ya baadhi ya wana wa Israeli kulalamika lalamika kila mambo yalipokuwa magumu walipokuwa njiani.
Musa alipowajia wana wa Israeli na ujumbe kuwa kuna nchi ya ahadi inawangojea wengi walifurahia na kwa kweli walifuata maelezo yake yote na hata ile siku ya kutoka Misri jamii nzima walikuwa tayari kutoka. Wote walikuwa na hamu ya kwenda kule ambako hakuna utumwa, na kule ambapo wangekuwa hai. Waliambiwa nchi wanayoiendea ilikuwa inatiririka maziwa na asali (Kut. 3:8,17). Kwa kweli waliitamani sana hiyo nchi. Na waliondoka Misri wakifurahia kuwa wanaenda mahali ambapo watafurahia maisha kweli kweli.
Walipoondoka na kuvuka bahari ya shamu walishuhudia muujiza mkubwa wa bahari kufunguka na wao kupita kwenye nchi kavu. Lakini muujiza mkubwa ni jinsi gani majeshi ya farao yaliangamia na wana wa Israeli walikuwa wamevuka ng’ambo ya pili. Ukisoma kitabu cha Kutoka 15 utaona jinsi wana wa Israeli walivyoimba kwa shangwe wakifurahia jinsi walivyoona matendo makuu ya Mungu. Wana wa Israeli walipenda mabadiliko na mafanikio lakini hawakuwa tayari kulipa gharama.
Hili tunaliona kwenye sura mbili zinazofuatia tukio la wao kuvuka Bahari ya Shamu. Kwenye sura ya 16 na sura ya 17 tunakutana na wana wa Israeli baada ya kupata shida kidogo walipoanza kulalamika na kunung’unika. Walijisikia njaa kidogo wakaanza kukumbuka “masufuria ya nyama” waliyokuwa wakila kule utumwani Misri. Mara kadhaa katika safari yao walijikuwa wanakumbuka Misri na kutamani kurudi kule walikotoka kwa sababu walikuwa na uhakika wa kula kwao, kulala kwao – hata kama walikuwa utumwani!
Ndugu zangu, naomba kupendekeza kuwa kweli wapo Watanzania wanaotaka mabadiliko na maendeleo lakini pia wapo wengine ambao kwao mabadiliko ni lazima yawe rahisi, yasiyo na jasho na yasiyo na uchungu. Wanataka kuendelea bila kulia, wanataka kufanikiwa bila kuinama au kunyanyua! Hawa ndugu zetu miaka hii mitano kwao maisha yalikuwa magumu sana kiasi kwamba walianza kukumbuka “masufuria ya nyama”.
NI kweli maelfu walitoka Misri lakini Misri haikutoka mioyoni ma wengi katika Israeli. Hata ukisoma Qurani Tukufu utakutana na wana wa Israeli wakilalamika tena kuwa hawakuwa tayari kwenda kwenye nchi waliyoahidiwa kwa sababu walikuwa wanaogopa kuna majibut majabari kule. Kwamba, walimuambia Musa kuwa kama anataka wao waende kwenye hiyo nchi basi Musa na Mungu wake waende wakapigane na majitu hao wakati wao (wana wa Israeli) watakaa hapo hapo wakisubiria! Kwa mujibu wa Qurani hii ilikuwa ni sababu ya wana wa Israeli kuharamishwa kuingia nchi ya ahadi kwa miaka arobani wakibakia kutangatanga (Qurani 5:20-26).
Leo hii katika Tanzania wapo watu ambao wanajua kukatisha tamaa wengine; watu hawa wanabeza SGR kuwa haiwezekani; wanatuambia hatuwezi kuendelea bila kusaidiwa; wanatuambia sisi ni maskini na kuwa hatuwezi kabisa! Wanarudisha hofu na hali ya kutokujiamini miongoni mwetu na kwa bahati mbaya wapo ambao wanawaamini. Nikiri tu kuwa mojawapo ya vitu vilivyokuwa vinanipa moyo sana ni lugha ya kujiamini ya hayati Rais Magufuli. Kwa uzuri au kwa ubaya alikuwa anajiamini kupitiliza! Sidhani kama alikuwa na mazoea ya kutumia lugha ya “haiwezekani” au “hatuwezi”. Kwake yeye mengi yalikuwa ni mambo ya kuthubutu kuyafanya. Inawezekana hata sasa kuna watu hawakubali hatua mbalimbali anazochukua Rais Samia; na hawa nao wanaanza kuwa na wasiwasi kwa sababu hawaamini kuwa anaenda kuendelea kulisogeza taifa mbele.
Binafsi kwa wakati huu ninamuona Rais Samia kama Yoshua aliyechukua nafasi ya Musa. Yoshua mwana wa Nuni na Kalebu mwana wa Yefune walikuwa ni watu wawili ambao walileta taarifa ya kujiamini baada ya kwenda kupeleleza nchi ya ahadi. Wakati wenzao walirudi na taarifa ya kutisha ya kuwa nchi ya ahadi imejaa mijitu mikubwa kiasi kwamba wao walikuwa wadogo kama “panzi” Yoshua na Kalebu walisema hata kama hivyo ni kweli bado wao walikuwa wana uwezo wa kushinda. Yoshua hakuwa Musa na hakufanya mambo kama Musa; alijua jukumu lake lakini alienda kufanya vitu tofauti na Musa. Mama Samia – kama nilivyoeleza huko nyuma – si lazima afanye kila kitu kama Magufuli wala haitaji kuzungumza kama Magufuli; anajua ajenda anayoitekeleza na anajua Watanzania wanatarajia nini kwake.
Wakati umefika wa kuanza kuwakatalia wale wote ambao wanataka turudi kwenye maisha ya utawala wa kifisadi ambapo baadhi yetu walikuwa wanakesha kwenye masufuria ya nyama! Kibarua alicho nacho Rais Samia ni kuweza kujua ni kina nani hawa ambao wanaotamani turudi kwenye fikra za kitumwa na za kimaskini; tukumbuke; siyo wote walioondoka Misri, walitoka kweli Misri! Kwani wengi bado walikuwa wanakumbuka Misri kwa mioyo yenye kuitamani; na wapo wanaotamani turudi kwenye ufisadi. Tukirudi tumekwisha; vinginevyo tunaweza tukajikuta tunatangatanga miaka arobaini!
Tujiandae kwa Deep Green, Tangold na Meremeta 2.0? Angalau Serikali inaonesha kushtushwa na kilichojaribiwa Wizara ya Fedha…
Niandikie:klhnews@gmail.com