Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,922
- 3,252
Katika hotuba yake ya hivi karibuni mkoani Njombe, Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson alitoa maagizo yanayoshtua. Baada ya kuwaonya watumishi wa umma dhidi ya kuvujisha "siri za serikali," alitangaza kwa fahari kuwa zaidi ya vijana 400 wa Kitanzania wamekamatwa kwa kutoa lugha za matusi kwenye mitandao ya kijamii, huku akiahidi kuwa kamatakamata zaidi itafuata.
Tena alisisitiza kuwa kutokana na uwekezaji wa teknolojia uliofanywa na Serikali, watakaokiuka sheria watakamatwa, akitumia msemo “wataookotwa.”
Ni kauli iliyomshtua pia Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara alipochangia bungeni jijini Dodoma hivi karibuni Juni 2026, akihoji uhalali wa mtendai wa Serikali kutoa kauli za watu kuokotwa, ilihali taarifa za watu kutekwa na kupotea zikiwa bado zinasambaa.
Soma pia: Msigwa: Vijana msinitukane mtakamatwa tu
Tumeshuhudia mapema mwaka huu, miili kadhaa ya watu wakiokotwa kwenye mito hapa Dar es Salaam wakiwa wameuawa na wengine wakiwa wamekatwa viungo, hivyo kauli kama hizo za kutosha zinapotolewa na mtendaji wa Serikali hadharani, ndipo ujue tumefikia kwenye kilele cha ukatili kama taifa.
Hata hao vijana 400 ambao Msigwa anasema walikamatwa, haijulikani kama walifikishwa mahakamani au walipelekwa wapi.
Wakati serikali ikifunika matendo haya kwa kisingizio cha kulinda maadili na amani ya umma, ukweli uliojificha uko wazi: utawala unahofia sana ukosoaji wa kidijitali. Kwa kufanya kufadhaika kwa asili na kwa uwazi kwa kizazi hiki kuwa kosa la jinai, serikali haikiuki tu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania—ambayo inahakikisha haki ya uhuru wa kujieleza—bali inahujumu kikamilifu mustakabali wa kiuchumi wa nchi.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 3.-(1) inasema, “Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia naya kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.”
Ibara ya 18.-(1) inasema, “Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati. (2) Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.”
Pamojana na uhuru na haki ya watu kutoa maoni, lakini Msigwa anasimama hadharani, anawatishia wananchi wanaotoa maoni yao, eti kisa tu hayamfurahishi yeye na mabosi wake. Anasema vijana wamemtukana, lakini hajawahi kusema wametukana tusi gani. Yeye mwenyewe amewahi kuwatukana vijana kwa kuwaita Nguchiro. Je, na yeye “aokotwe?”
Soma pia: Gerson Msigwa awajia juu waliomkosoa kuita wananchi Nguchiro
Ukandamizwaji wa mitandao ya jamii
Wakati dunia ikiwa imepiga hatua kubwa katika Tehama, Tanzania inakwenda kinyume cha maendeleo hayo, kwa kufungia mitandao ya jamii. Kwa mfano mtandao wa X (Twitter) haupatikani hadi utumie VPN, Tik Tok mpaa Jamii Forums zilifungiwa, kwa sababu tu vijana wengi wako huko wanatoa maoni yao. Yaani Serikali haitaki watu wafikiri tofauti.Msigwa anajitapa kwamba Serikali imefanya uwekezjai mkubwa wa kukamata watu wanaotoa maoni yao mtandaoni. Sio kuwekeza kuwawezesha vijana kujiajiri mitandaoni, hapana. Wao wanacho waza ni kukamata watu kufunga na “kuwaokota.”
Wenzetu huko duniani, wanawezekeza kuitumia mitandao ya jamii kujenga uchumi wao, sisi tunawekeza teknolojia ya kamata kamata na kufungia mitandao. Aibu gani hii?!
Mifano ya Kenya na Afrika Kusini
Sio lazima kutazama nchi za Ulaya na Marekani kuona faida za kiuchumi za uhuru wa kidijitali; inatosha kuwatazama majirani zetu.
Kenya, ambayo mara nyingi inajulikana kama "Silicon Savannah," ina moja ya idadi kubwa ya watu mtandaoni waliochangamka na wanaotoa maoni ya kisiasa kwa uwazi zaidi duniani. Vijana wa Kikenya mara kwa mara hutumia mitandao kama X na TikTok kuikosoa vikali serikali yao, kufichua ufisadi, na kuandaa maandamano ya kidijitali.
Badala ya kuwakamata kwa wingi, serikali ya Kenya imewekeza kwenye uchumi wa kidijitali. Kupitia mipango kama ‘Ajira Digital Programme,’ serikali inatoa mafunzo kwa zaidi ya vijana milioni moja ili kupata kazi za kidijitali za masafa (remote jobs).
Ubunifu wa teknolojia za kifedha (Fintech) kama M-Pesa na mfumo unaokua kwa kasi wa kampuni changa (start-ups) kwa sasa unatoa ajira kwa mamia ya maelfu ya vijana wa Kikenya katika utengenezaji wa programu, masoko ya kidijitali, na kazi za kimkataba (gig economy). Serikali inaelewa kuwa vijana walio na uhuru wa kuzungumza pia wako huru kubuni.
Vivyo hivyo, nchini Afrika Kusini, ukosefu wa ajira kwa vijana ni janga kubwa, lakini uchumi wa kidijitali unatumika kama njia muhimu ya kujikwamua.
Afrika Kusini inajivunia uchumi unaokua wa wabunifu wa maudhui (creator economy) na sekta kubwa ya usafiri wa mtandaoni (kama Bolt na Uber) ambayo hutoa kazi zinazobadilika kulingana na muda kwa mamia ya maelfu ya vijana.
Katiba ya Afrika Kusini inalinda kwa nguvu uhuru wa kujieleza. Vijana wa Afrika Kusini wanapowakejeli wanasiasa au kudai huduma bora mtandaoni, hujibiwa kwa mijadala ya kisiasa, si kuvamiwa na polisi. Uhuru huu unaruhusu utengenezaji wa maudhui ya kidijitali—kuanzia YouTube hadi podikasti (podcasts)—kuwa njia halali na yenye faida ya kujipatia kipato badala ya kuwa hatari ya kisheria.
Mfumo wa Kidunia: Amerika na Ulaya
Ulimwenguni kote, uhusiano kati ya uhuru wa kujieleza na utawala wa kiteknolojia hauwezi kupingika.
Nchini Marekani, ulinzi kamili wa uhuru wa kujieleza kupitia Marekebisho ya Kwanza ya Katiba (First Amendment) ulitengeneza mazingira bora kwa ukuaji wa uchumi wa kidijitali wa kisasa. Mitandao ambayo vijana wa Kitanzania wanakamatwa kwa kuitumia sasa—X, Instagram, TikTok, YouTube—ilijengwa katika mazingira ambapo kuhoji mamlaka ni haki ya msingi.
Uchumi wa wabunifu wa maudhui nchini Marekani pekee una thamani ya makumi ya mabilioni ya dola, ukiajiri mamilioni ya vijana wanaoingiza kipato kupitia maoni, sanaa, na hata ukosoaji wao wa kisiasa.
Barani Ulaya, mataifa ya kidemokrasia yanawekeza kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya ujuzi wa kidijitali kwa vijana wao. Wakati Umoja wa Ulaya unadhibiti intaneti kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya faragha ya data (GDPR) na usalama wa watumiaji (Digital Services Act), kimsingi unalinda uhuru wa kujieleza kisiasa. Vituo vya teknolojia (Tech hubs) katika miji ya Berlin, London, na Paris vinastawi kwa sababu wajasiriamali vijana wanatambua kuwa kuhoji hali ilivyo ndiyo hasa maana ya ubunifu.
Gharama Kandamizi ya Udhibiti
Serikali inapokamata vijana 400 kwa "lugha ya kashfa," inatengeneza hali ya woga inayoenea mbali zaidi ya siasa.
Uchumi wa kidijitali unahitaji kuthubutu, ubunifu, na mabadilishano huru ya mawazo. Ikiwa kijana wa Kitanzania anayetengeneza programu (software developer) au maudhui (content creator) anahofia sana kuwa neno lililokosewa au ukosoaji wa huduma mbovu za umma utampeleka jela, atajizuia mwenyewe. Hatanzisha podikasti hiyo; hatajenga programu hiyo ya kijamii (civic-tech app); hatashiriki katika uchumi wa kidijitali wa kimataifa (gig economy).
Kwa kugeuza mfumo wa haki kuwa silaha dhidi ya vijana wake, serikali ya Tanzania inatengeneza mazingira ambapo wawekezaji wa kimataifa wa teknolojia wanaona hatari za kisheria badala ya fursa.
Kuanzisha Wizara ya Vijana sio suluhisho
Baada ya machafuko ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 yaliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali, Rais Samia Suluhu Hassna alianzisha Wizara ya Maendeleo ya Vijana iliyoko chini ya Ofisi ya Rais.Wizara hii imekuja kufuatia maandamano ya Oktoba 29, 2025 ambayo yalihusisha vijana, jambo lililoishtua Serikali na kubaini kuwa, vijana sio kundi la kuacha nyuma. Tumeona Waziri wake, Joel Nanaula akifanya ziara mikoani akikutana na vijana ili kuelewa kero zao. Je, hilo ndilo suluhisho la kukabili kero za vijana hasa ukosefu wa ajira?
Pamoja na mipango na mikakati mizuri ya Serikali, haiwezekani kutatua kero za vijana, huku umefungia uhuru wa maoni mitandaoni na hadharani. Ieleweke kwamba Serikali haiwezi kuajiri vijana wote, ila inawa jibu wa kuweka mazingira wezeshi ili vijana wenyewe wajiajiri.
Mazingira wezeshi ni pamoja kuruhusu uhuru wa maoni hadharani, mitandaoni. Eneo kubwa la ajira kwa vijana katika ulimwengu wa sasa wa teknolojia ni mitandao ya jamii. Huko ndiko vijana wanaweza kujiajiri kwa kuanzisha Startups, kutangaza biashara zao, kufanya maigizo na vichekesho na mwisho wa siku wanaingiza kipato.
Kauli ya Msigwa kwamba wamekamata watu 400 na wataendelea kuwakamata ni tisho kubwa kwa vijana na huenda ikaua kabisa moyo wa ubunifu kwa vijana na hatimaye inazidisha chuki ya vijana kwa Serikali.
Hata ile ruzuku kwa ajili ya waunda maudhui (content creators) iliyotangazwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, inaweza isizae matunda yanayokusudiwa, kama vijana watakosa uhuru wa kufanya kazi zao.