Godbless Lema awali aliteuliwa kuwa mjumbe wa kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA kabla ya uteuzi wake
kutenguliwa na Msajili wa vyama vya siasa, na kisha baadaye kuteuliwa tena kwa ajili ya kukaimu nafasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa chama hicho kanda ya Kaskazini. wakati wa uchaguzi mkuu ndani ya chama hicho uliofanyika January 2025, Lema alikuwa ni miongoni mwa makada ambao walikuwa wakimuunga mkono Tundu Lissu alipokuwa akigombea nafasi ya uenyekiti hadi kushinda dhidi ya Freeman Mbowe aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo kwa miaka 21.
Mnamo tarehe 14 Januari, 2025 Lema alifanya
mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es salaam ambapo pamoja na mambo mengine alitumia fursa hiyo kutangaza msimamo wake dhidi ya kumuunga mkono Tundu Lissu alipokuwa akigombea uenyekiti CHADEMA Januari, 2025.
“Niko hapa kuweka bayana kwamba, ninamuunga mkono Lissu. Najua nitakuwa kwenye wakati mgumu sana mbele ya kaka yangu (Mbowe), lakini niweke wazi kuwa ninamuunga mkono Lissu na nitampigania kwenye harakati hizi za kuwa mwenyekiti.
Video iliyochapishwa TikTok ikimhusisha Lema
Tarehe 08, Julai 2025 mtumiaji wa mtandao wa TikTok kwa jina la
'Mapinduzi 64' alichapisha kipande cha video kinachomuonesha Lema akisema Lissu hawezi kuwa kiongozi kwa sababu hana pesa, hawezi kuendesha chama.
Je, ni upi uhalisia wa video hiyo?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck kupitia marejeo ya video umejiridhisha kuwa video hiyo imepotoshwa uhalisia wake kutoka kwenye
hotuba ya Lema aliyoitoa Januari 14, 2025 mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Video imepotoshwa kwa kukata vipande kutoka kwenye hotuba hiyo na kuviunganisha isivyo stahili hatimaye kubadili ujumbe uliokusudiwa na Lema.
Sehemu ya kipande hicho, Lema alimtaka aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe apumzike kugombea nafasi ya uenyekiti na amuachie Makamu wa CHADEMA Bara Tundu Lissu kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho.
"Watu wamepatikana wanataka nafasi yake na huwezi kumtilia mashaka Lissu ambaye amekuwa Makamu Mwenyekiti, Mnadhimu Mkuu wa Chama, Mwanasheria Mkuu wa Chama n.k, usipomuamini Makamu wako kumuachia Chama ni nani unaweza kumuamini ukamuachia chama?”
Aidha alisisitiza kufanya maamuzi ya kuchagua kiongozi pasipo kujali uwezo wa kifedha kwani chama hakipaswi kujengwa na pesa ya mtu mmoja bali kwa michango kutoka kwa wananchama.
"Nimeona hoja nyingi kwenye mitandao wanasema Lissu hana pesa, kwa hiyo Lissu hawezi kuendesha chama, kama kuna kitu ambacho wajumbe wanatakiwa wakifikirie na wakafanye maamuzi ya kumchagua Lissu, ni Lissu kutokuwa na Pesa ili wajumbe wajue chama chao hakipaswi kujengwa na pesa ya mtu mmoja, chama chao kinapaswa kujengwa kwa 'mobilization' ya 'fund' kutoka kwa wanachama"
Rejea
hapa kupata video ya alichokisema Lema kuanzia dakika ya 12
View: https://www.youtube.com/live/n4jGmCXtOsc?si=a7oqu40DW5t9s2Ne&t=746