Josephat Gwajima ni Askofu na mwanzilishi wa kanisa la 'Glory of Christ Tanzania Church' GCTC (Ufufuo na Uzima Ministries), kadhalika ni mwanasiasa ambaye mwaka 2020 alichaguliwa kuwa
mbunge wa jimbo la Kawe kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM.
Leo Januari 16, 2025 Askofu Gwajima amezungumza mbashara kupitia mtandao wa
YouTube ambapo pamoja na mambo mengine amezungumzia hoja ya CHADEMA kutaka reforms haipaswi kupuuzwa, akionya kuwa kushinda uchaguzi bila upinzani haiwezi kuleta mshikamano wa kitaifa unaohitajika kwa maendeleo.
Taarifa inayosambazwa kuhusu Askofu Gwajima
Baadhi ya watumiaji wa mtandao wa Facebook wamekuwa wakisambaza taarifa inayosema Askofu Gwajima ametoa wito kwa wananchi wote kushiriki uchaguzi mkuu kwa amani, utulivu na mshikamano, huku ikitumia utambulisho wa grafiki ya Jambo TV.
Je, ni upi uhalisia wa taarifa hiyo?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck kwwa kutumia utafutaji wa maneno muhimu (Key word search) pamoja na marejeo ya video, umejiridhisha kuwa taarifa inapotosha uhalisia wa kilichozungumzwa na Askofu Gwajima.
Vilevile grafiki iliyotumika kusambaza taarifa hiyo ni ya kughushi kwani haijachapishwa katika kurasa rasmi za mitandao ya kijamii ya
Jambo TV.
Aidha katika mkutano wake, Askofu Gwajima akizungumza kuhusu uchaguzi amekishauri Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali kuruhusu kufanyika kwa mabadiliko ya sheria (reforms) japo kwa uchache ili kuwezesha vyama vyote kushiriki uchaguzi mkuu wa 2025 na kuondoa migawanyiko nchini.
"Mnajua vyema kwamba Chadema wamesema hawaingii kwenye uchaguzi mpaka tufanye Reforms na modality yao wanayoisema, wanasema watazuia uchaguzi.
Nataka nitoa ushauri kwa unyenyekevu sana, ni kweli Sisi CCM tunaweza kuamua kuendelea na uchaguzi na tukafanya uchaguzi na tukashinda lakini kushinda uchaguzi sio jambo kubwa sana, kuitawala nchi ambayo imemegukameguka kwasababu ha makovu ya uchaguzi ndiyo jambo kubwa zaidi, kuiletea nchi maendeleo iliyomeguka kutokana na makovu na majeraha ya uchaguzi ni kazi ngumu sana.
Sisi kama CCM tunaweza kuamua kwamba tuendelee- tutaendelea na tutashinda. Lakini ebu jaribu kuwaza tangu siku unapoapishwa kuna watu wanaendelea kukupinga mpaka utakapomaliza miaka yako mitano, yaani kuna watu hawakuingia kwenye uchaguzi, hawakushiriki, pengine hawakutambui halafu wanaanza kukupinga tangu siku unapoapishwa mpaka utakapotoka miaka mitano.
Maendeleo utayaletaje? Utapata matatizo na Jumuiya za kimataifa na ndani ya nje utapata matatizo utashindwa kwenda kwa kasi kwa maendeleo yetu kama inavyotakiwa na itakuwa sio vizuri.
Mimi nashauri kwamba, CCM ina wanachama zaidi ya milioni kumi na kitu, hatuhitaji kuogopa, tuamue kuwaruhusu hawa wa Chadema kuwapa reforms chache ambazo zinaweza kufanyika kwasasa, tuwape a minimal reform, haichukui muda. Tuwape, tuingie nao kwenye uchaguzi.
Kwani wewe hufahamu kwamba CCM ina wanachama zaidi ya Milioni kumi na kitu?ambao wapo tayari? kwanini tuingine kwenye mchezo halafu tunayecheza naye hayumo? Ni sawasawa na kuingia kwenye mechi huku kuna Simba, huko inatakiwa iwe Yanga, halafu Yanga haipo, tunacheza wenyewe halafu tunapiga goli, si mechi.
Nashauri sana badala ya kuendelea na No Reforms, No election, CCM awepo mtu wa kutafakari. Mimi kama mwanachama wa CCM na kama Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM na pia Mtanzania, nashauri sana tungeamua kukubali kufanya hiyo reforms, najua shughuli za Bunge zimesitishwa lakini uhai wa Bunge bado upo mpaka mwezi wa nane, zitafutwe wiki mbili au tatu, zitengenezwe reforms wanazozihitaji hata kama sio zote, lakini ziwe chache zitakazowafanya waingie kwenye uchaguzi halafu waingie tuwapige, reforms zimefanyika, wameingia, tunawapiga."
Rejea
hapa kutazama alichokizungumza kuanzia dakika ya 30:07
View: https://www.youtube.com/live/jINnZ9eLnwE?si=B5OnT77DwOhHvJv-