KESI YA MZEE MNYOKA 40 (
Gily anatudhamini)
Tito aliongea hayo akijaribu kumsogelea Joyce
“usisogee!” alisema George huku akimkonyeza Joyce ambaye alienda kuchukua silaha za walinzi wa Johnson kisha wakaanza kutembea kutoka nje,
‘MY DAUGHTER ! ‘’ alisema Tito, Oscar alijitahidi kumeza mate huku akipigwa na butwaa,
“kumbe! Sikujua, kwanini nimekuwa mzembe kiasi hiki kutomjua Joyce tangu mwanzo’ Oscar aliwaza,
Na hatimaye walifika nje na kuanza kuwafunga kamba Tito na walinzi wa Bwana Johnson kisha wakamfunga Bwana Johnson mwenyewe,
Wakati Tito anazidi kushangaa Joyce alienda kwenye ile gari yao na kutoka na kijikoti cha kijeshi pamoja na bastola mbili kisha akapiga saluti kwa Oscar
‘naitwa Joyce, NSA level 4 ! alisema huku akijitambulisha kwa Oscar na kumkabidhi Oscar kile kikoti ambacho alikivaa huku Tito akizidi kuchanganyikiwa..
“kwahiyo kumbe wewe Oscar ulikua mpelelezi .. hahahahahaha dah! Mimi ni mpumbavu! Mimi ni mjinga!’ alisema Tito kwa uchungu!
Oscar alivaa vidude vya mawasiliano na kisha akachukua jukumu lake kama kiongozi..
“nendeni kule chini mkafunge milango yote vizuri na kuhakikisha ulinzi upo kila sehemu” aliongea Oscar huku jicho lake likimtazama Joyce
Baada ya saa moja Bwana Allan alifika pamoja na kikosi chake na kuwachukua akina Tito na genge lake na kuwaondoa chini ya ulinzi mkali..
Oscar walirudi kwenye ambulace yao na kuanza safari pole pole hakuna aliyeongea chochote..
BAADA YA SIKU CHACHE
Tito alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani pamoja kufilisiwa mali zake zote, alimtaja Askofu Mjimbi ambaye alikutwa akiwa amejipiga risasi ya kichwa na kufariki. Bwana Johnson alirudishwa na kufunguliwa kesi upya nchini uingereza,
Oscar alikua amefanya mpango wa kuonana na Joyce kabla hajaondoka lakini kwa sababu ambazo hakuzielewa Joyce hakupatikana tena kwenye simu yake
Siku hiyo aliamua liwalo na liwe na hivyo akajitosa kwenda kumvaa Bwana Allan..
‘oscar, ni wewe tu hujafika hapa ofisini tangu tukio lile, nikajua bado umepumzika! Hata hivyo afadhali umekuja maana ni wewe ulibakia tu, ili na mimi nikapumzike!” alisema allan akimkaribisha Oscar,
“kwani kuna nini!” aliuliza Oscar hata akasahau jambo lililomleta
“ Namba moja ametoa zawadi kwenu na ofa, na kwa kazi kubwa mliyofanya, zipo nyingi ila tuanze na hii kwanza, “ alisema akitoa kwenye droo yake picha moja ya nyumba nzuri sana yenye uzio mpana,
‘Ipo hapa mjini maelezo yapo nyuma ya hiyo picha,’ alisema halafu
Na hii hapa.. alisema huku akitoa hundi ya pesa dola za kimarekani elfu 50,
“hayo ndio yametoka kwa namba moja , mimi zawadi yangu kwako Binafsi ni hii hapa!” alisema akitoa bahasha nyingine akimkabidhi Oscar,
Oscar aliichukua na kutaka kuifungua..
“hapana hii utafungua nyumbani, haya sasa niambie kitu gani kimekuleta”
aliuliza Allan akimtazama Oscar machoni..
Oscar hakujua anzie wapi
“mkuu ni kuhusu Joyce!” alisema Oscar.
‘ana nini!” aliuliza Allan kwa ufupi
“aah hapatikani na sijawahi kumuona tena tangu siku ile, na kwao hayupo, na George pia hapatikani!’ alisema Oscar kwa aibu kidogo..
‘nilikuambia umebaki mwenyewe,” sijui kama ulielewa, anyway nenda zako nyumbani ,kumbuka hiyo bahasha ukafungue kwako..
Alisema Allan akinyoosha mkono wake,
Oscar alimjua vyema bosi wake huyo hivyo akatoka kwa upole na kushika mlango tayari kutoka
‘take care!” alisema Allana akimuaga.
Oscar alifika nyumbani kwake na kutazama ile picha ya nyumba hakika ilikua nzuri sana na zaidi sana ilikua eneo zuri sana kama mlimani hivi,
Aligeuza ile picha na kuona namba ya simu, alikua anataka kupiga ndipo akakumbuka kuwa hajafungua ile bahasha!
Haraka alichukua ile bahasha na kuifungua..
Ndani yake kulikua na passport mpya ya kusafiria yenye picha yake pamoja yenye jina JACOB LAURENCE ISAYA ikimtambulisha kama mfanyabiashara pamoja na kitambulisho cha kupigia kura na kadi ya benki vyote vikiwa na jina hilo hilo!
“Asante Mungu!” Oscar aliruka kwa furaha kwani tayari hii ilimaanisha anapata likizo ndefu ,
‘Joyce uko wapi?’ aliwaza huku akichukua vitu vyake alivyoona kuwa ni muhimu na kuondoka tayari kuhamia nyumba yake hiyo mpya!
Alitoka nje na kuitazama nyumba yake hii aliyokaa karibia miaka mitatu, kisha akatoa simu yake na kupiga ile namba
“njoo tegeta kwa ndevu , hapa uliza kwa Waroma halafu kuna njia inashuka kama unaenda mji mpya utaona kama mlima hivi nipo hapo” sauti ya mwanaume upande wa pili ilisikika
Oscar aliendesha gari lake kwa kasi na baada ya masaa mawili alifika na kweli alikuta nyumba kama vile vile alivyoiona kweny picha ilikua nzuri sana,
‘bila shaka ni bwana Jacob eeh?’ alisema Yule mzee
“ndio hujakosea kabisa’ alisema oscar akimsalimia Yule mzee,
Alimtembeza nyumba nzima na kisha akamkabidhi funguo na kuaga..
“mzee sasa mbona haraka!’ alisema oscar
“nimeambiwa nikupe ufunguo halafu niende kazi yangu ilikua kulinda tu hapa!” alisema Yule mzee
Na huku akitoka kwa haraka Oscar alitabasamu tu huku akijiachia kwenye nyumba yake hiyo,
Akili yake sasa ilikua kwa Joyce alijaribu kutuma emails, na meseji za whatsap lakini hazikujibiwa na Joyce hakuwa online kabisa
Simu yake iliita na kwa haraka aliipokea bila kuangalia mpigaji
“joyce !?” alijikuta akiuliza
“ utakuwa mwehu, umeacha hati yako ya nyumba Mr Jacob, nakutumia mtu akuletee, huyo mwenzako nae kawa chizi kama wewe!” alisema Bwana Allan, kisha akakata simu!
“huyo mwenzako nae kawa chizi kama wewe!’ oscar aliirudia hii kauli kichwani mwake
“kwa maana hiyo anajua alipo si ndio!?” alijiuliza akikaa vizuri kwenye kochi lake
Aliletewa ile hati na Paulo mfanyakazi mwenzake pale ofisini ambaye nae alisema hajui chochote kuhusu Joyce alipo,
“kila mmoja alikuja kivyake pale kama wewe na kisha akaondoka na bahasha yake akasepa” alisema Paulo huku akirudi zake ofisini..