Hadithi: Mzaha wa damu

Hadithi: Mzaha wa damu

MZAHA WA DAMU 03
By CK Allan


Baada ya kuichaji na kuweka sawa sasa niliingia kwenye mtandao wa facebook na kuanza kutafuta jina Ephraim, nilipitia akaunti zenye majina ya Ephraim kwamba angalau ningepata yenye picha yangu au picha ya mtu ambaye ningeweza kumfahamu
Nilipitia akaunti nyingi lakini sikuweza kuona yenye picha yangu hata hivyo nilitengeneza akaunti kwa jina la Ephraim Tito kisha nikaendelea kutafuta akaunti ya Ephraim, nakumbuka nilitafuta hadi simu ikaisha chaji nikaiweka kwenye chaji kisha nikarudi kupumzika ndani, nilijikuta nikipitiwa na usingizi na ghafla ndoto ikanijia nikajiona nimeshika ile simu na kuingia kwenye mtandao wa facebook kisha nikaenda kwenye sehemu ya kuingia na kuweka taarifa zangu
Jina la kwanza: Ephraim
Jina la pili : Tito
Jina la mwisho: Kikulwe
Tarehe ya kuzaliwa : 25/9/1987
Jinsia :me
Nilijikuta najaza hizo taarifa kwenye ile simu kisha nikatengeneza neno la siri na wakati naingia nikajikuta nastuka tena huku nikitweta
Haraka sana nilichukua kalamu na kuandika zile taarifa kisha nikachomoa ile simu haraka kwenye chaji na kuingia kwenye mtandao wa facebook, nilienda sehemu ya kutafuta marafiki na kuandika Ephraim Kikulwe, zikatokea akaunti nyingi tu nikaanza kupitia moja baada ya nyingine mara ghafla macho yangu yakatua kwenye akaunti moja hivi iliandikwa jina la Kikulwe Ephraim, nilibaki kuduwaa kwenye picha ya mtumiaji niliona picha ya mtu aliyefanana na mimi akiwa katika kiti cha ofisini hivi, sasa nilianza kutafuta kupekua na kupekua picha mbali mbali katika akaunti hiyo, niliona mara ya mwisho kutumiwa akaunti hiyo ilikua oktoba 10/2019
Huku picha ya mwisho ikiwa imepigwa nje ya jengo lilionekana kama ukumbi hivi ukiwa umepambwa huku kukiwa na maneno yalisomekana
“karibu Waziri mkuu Kongwa tunakusubiri”
Sasa sikuweza kuvumilia nilitoka nje na kwenda kuwaonyesha mzee Tito na mkewe kuhusu yale yote niliyoyaona,
“hakuna shaka huyu ni wewe na mwaka Jana mheshimiwa waziri Mkuu mama Zawadi Macha alitembelea wilaya zote kukagua miradi ya maendeleo sasa bila shaka hii ilikua mojawapo ya ziara zake” alisema mzee Tito
“kwahiyo huyu ni Mimi na kwenye hii picha hapa naona kuna watu wengine hebu subiri ..” nilisema huku nikishusha zile picha kuelekea chini
Mara niliona picha yangu tena lakini safari hii ilikua kuna mwanamke kaiweka kwenye ukurasa wake kisha akahusisha na akaunti yangu ambapo kwa lugha ya mtandao waliita “kutag” picha hii aliituma wiki chache zilizokua zimepita
“ni mwaka mmoja umepita bila uwepo wako, Nimekumis, Ofisini tumekumis, SITAACHA kukuombea Pumziko la milele akupe yeye Bwana na Mwanga wa Mbinguni akuangazie tutaonana Mbinguni”
Nilijikuta nguvu zikiniishia na kisha nikaona giza likinifunika mboni za macho yangu baadae sikuelewa tena kilichoendelea.
Nilikuja kuzinduka baadae sana huku nikiwa kitandani kwangu, niliangalia saa ilikua saa 11 jioni
Nilitoka nje na kumkuta mama Tito akiwa anapasua kuni, nilienda kumsaidia huku akiwa haamini kuniona tena nikiwa na afya njema
“mzee yuko wapi?” nilimuuliza sasa nikiwa nachukua ile shoka
“ah itakuwa yupo chumbani kwake” alisema na kabla sijajibu mzee Tito alitokea akiwa na uso wa bashasha
“Ephraim umeamka, ooh afadhali” alisema huku akichukua zile kuni zilizokwisha kupasuliwa na kuingiza ndani
Baada ya muda tulimaliza sasa na kurudi ndani,
“wakati umelala ulikua unamtaja sana Josephine , je ni nani huyu?” mzee Tito aliongea akiwa sasa ananitazama usoni
“nani Josephine? Oooh simu , simu iko wapi ile simu?” nilikimbia chumbani tena na kuchukua ile simu pale kitandani
Kisha nikaingia tena kwenye ule mtandao wa facebook
Nilitafuta ile akaunti tena na sasa wote watatu tukawa tumeduwaa
“ndio huyu, anaitwa Josephine Mpanji, namjuaaaa!” nilijikuta napiga kelele za furaha!


“huyu ni mchumba wangu, angalia hapa, sasa nilishusha chini zaidi na kuangalia picha zake mbali mbali na kulikua na picha ambayo nilikua namvalisha pete ya uchumba katika kanisa la st Gasper Dodoma, haraka nilirudi kwenye ukurasa wake na kutafuta namba ya simu kisha nikaihifadhi na sasa tukashauriana na Mzee Tito kupiga ile namba!

“kwasasa huwezi kuongea nae moja kwa moja kwakuwa huwezi kujua wale watu waliokudhuru pengine bado wanaendelea kukufuatilia hivyo tutaweka sauti ya juu kisha niongee nae mimi lakini kwanza tuandae mazingira ya namna ya kuongea nae bila kuleta taharuki” alisema mzee Tito,
tuliandaa mzingira yote ya maswali anayoweza kuuliza kisha simu ikapigwa
“halo habari ya jioni”
Ilisikika sauti ya mwanamke upande wa pili na sasa nilisikia moyo wangu ukipiga paa baada ya kusikia sauti hiyo
“ndio mimi naitwa mzee Tito Nipo Moro goro”
‘ndio mzee Tito ,sidhani kama nakufahamu” sauti ya upande wa pili ilisikika
“ni kweli , hunifahamu, nimekupigia simu kunisaidia jambo moja” alisema Tito
“ndio mzee Tito nakusikiliza” alisema
“nina kijana wangu ambapo wakati Ephraim anapata matatizo hakuwepo nchini sasa alikua na baadhi ya mizigo ambayo ametoka nayo nje ya nchi yeye anasema kuwa ameagizwa na Ephraim, sasa kwa bahati mbaya kutokana na changamoto ya Corona amewahi kuondoka na akaniachia namba hii alisema nikutafute” alisema mzee Tito huku nikimuonyeshea alama ya “dole” kuwa ameongea vizuri
“sawa mzee Tito ni mizigo gani?” aliuliza
”kwakweli hata mimi sijui, imefungwa tu kwenye boksi” alijibu mzee Tito
“sasa ulitakaje mzee Tito” aliuliza
“kwani uko wapi sasa hivi?” aliuliza mzeee Tito
“kwakweli nipo nyumbani Mbeya, baada ya Ephraim kupotea na unajua ilikua bado wiki moja tufunge ndoa, sikuwa sawa, kwahiyo nikashindwa kabisa kufanya kazi nikaomba likizo nipo tu kwakweli sielewi” sauti ilisikika upende wa pili na sasa nilishindwa kuvumilia na kujikuta nataka kumnyang’anya simu mzee Tito
“sasa mama naomba unisikilize vizuri, naomba kwanza kama hapo ulipo upo na watu usogee sehemu ambayo unaweza kuongea ukiwa mwenyewe bila kusikika
Sawa nitakupigia baada ya dakika chache
‘sasa tufanyaje?” alisema mzee Tito
“nadhani tumuamini tu hakuna namna nyingine sema usimwambie moja kwa moja maana…”
Tulikatishwa na sauti ya simu sasa Josephine alikuwa anapiga simu
“haya niambie mzee Tito” ilisikika upande wa pili
“kuna jambo inabidi ujue nadhani najua alipo Ephraim hakufa kama ambavyo unajua” alianza mzee Tito kwa upole
“unsemaje wewe mzee?, walimuua Ephraim, walimpoteza, tena kwa kisa ambacho sio cha kweli? Hakufanya Ephraim aiiiiii, aiiiiii!” alianza kulia Josephine
“ndio maana nikakupigia Josephine, ni wewe pekee ambaye unaweza kumrudisha tena katika hali yake ya kawaida,” alisema mzee Tito
“unanidanganya najua unanidanganya!’ alisema tena
“muda sio mrefu utaamini lakini nataka unihakikishie jambo moja!” alisema mzee Tito
“ndio jambo gani!”
“kwanza unihakikishie kuwa hutamwambia mtu kuhusu jambo hili halafu tutaongea zaidi juu ya nini cha kufanya” alisema Mzee Tito
“na mimi naomba unihakikishie jambo moja kwanza kabla hatujaendelea” alisema Josephine
“jambo gani?” mzee Tito aliuliza sasa akiweka simu karibu ili tusikie wote
“nataka kujua kama kweli Ephraim yuko hai”
“sawa, hii namba iko whatsap?” aliuliza mzee Tito
“ndio” alijibu
Mzee Tito alikata simu yake kisha akanigeukia,
Sawa ngoja nilichukua ile simu nakuingia chumbani na kuwasha taa kisha nikavua shati, na kurekodi video fupi nikihakikisha Josephine anaona baadhi ya makovu na alama mbali mbali mwilini mwangu ili aweze kuhakikisha kuwa mimi ni mzima wa afya kabisa lakini niliyepitia katika changamoto mbali mbali
Tulimtumia ile video kwa njia ya whatsap na baada ya muda akapiga simu
 
MZAHA WA DAMU 04
By CK Allan
“ni kweli kabisa huyo ni Ephraim ni kweli ni yeye! Niambie yuko wapi niambie yuko wapi!” alisema Josephine akilia machozi
“sasa hapo ndipo ambapo unaharibu kumbuka tulishakubaliana basi nakataka simu” alisema mzee Tito
“hapana mzee Tito hujui tu namna gani huyu mtu alikuwa wa muhimu kwangu” alisema Josephine na sasa mimi pia nilishindwa kuvumilia na kukwapua ile simu
“mpenzi!” nilisema kwa utulivu
“ephraim! Ni wewe kweli nimesikia sauti yako sasa nimeamini, hakika nimeamini” alisema Josephine akizidi kulia
“nisikilize” nilisema
“naamini umeshalia imetosha Josephine, kwasasa hutakiwi kulia tena bali tuangalie jinsi gani ya kurudia maisha yetu ya kawaida, kwasasa naomba uje hapa nilipo nitakuelekeza kila hatua namna ya kufika lakini usimwambie mtu yoyote juu ya safari hii” nilisema
“nipo tayari Ephraim hata usiku huu kukuona mpenzi wangu, nipo tayari!” alisema Josephine huku akilia kwa kwikwi
Tuliongea zaidi kisha nikampa maelekezo namna ya kufika kutokea mbeya kwa msaada wa Mzee Tito, na kisha akaahidi kufika pale baada ya siku tatu
Sasa nilijihisi kutua mzigo ni kweli facebook imenikutanisha na mtu ambaye nilikua namuwaza wakati wote na sasa niliamini kupitia huyu , kila kitu kitarudi katika hali yake ya kawaida,

Oktoba 20, 2020
Tayari tulikua mjini Manyoro mimi na Mzee Tito baada ya kuwasalimia marafiki zake kadhaa tulielekea stendi kumsubiri Josephine, nilishindwa kukaa kwenye kiti na wakati wote nilikua naangalia saa kupitia simu yangu ya mkononi Josephine alikua amepanda basi la Blessed ambalo hupita majira ya 11 jioni,
“Ephraim bado muda kijana wangu, atafika tu muda si mrefu!” alisema mzee Tito akitabasamu
Nilirudi kwenye benchi na huku nikiwa naona kana kwamba muda hausogei,
Sasa nilijikuta nasimamama baada ya kuona basi kwa mbali likiwa linakuja kwa kasi kuelekea stendi tulipokuwa,
“mzee wanapita hawa, wanampitisha mbona?” nilisema huku nikijiandaa kusimamisha lile gari , mzee Tito ailinitazama tu huku akicheka
Mara pole pole ile basi alipunguza mwendo na kuingia stendi
sasa nilisimama na kukimbia huku nikiwapiga vikumbo waliokuwa wanauza maji na matunda na kuwahi mlangoni pa basi, naam na hatimaye alishuka Josephine akiwa katika muonekano wa kupendeza kama ilivyo kawaida yake alisimama pale mlangoni akiangaza macho huko na huko na sasa akashuka chini huku akiwa amebeba begi lake mgongoni na mkoba mkononi huku mkono mwingine akiwa na mfuko wa plastic , sikusubiri muda mrefu nilimfuata pale pale alipo na kumkumbatia kwa nguvu, zaidi ya dakika tano tulikumbatiana tuu huku kila mmoja akitoka machozi sasa ilibidi mzee Tito aingilie kati kututenganisha maana tayari watu walishatuzunguuka na wengine walikua katika harakati za kutoa simu zao ili waturekodi, haraka mzee Tito aliivuta bajaji moja iliyokuwa jirani kisha akapakia ile mizigo na kisha tukaingia sote na kuondoka
“tupeleke uzunguni pale!” alisema mzee Tito
“ipi mzee, ile ya bar au ile lodge?” aliuliza dereva wa bajaji
‘ile yenye bar” alisema mzee Tito
Tulifika ple kwenye ile bar mzee Tito akalipa kisha tukashuka na kuingia ndani, tuliagiza nyama choma na vinywaji na sasa tukaanza hadithi za hapa na pale
Mzee Tito alikuwa muongeaji mkuu huku akifanya utani wa hapa na pale na sasa nilitambua kuwa mzee Tito alikua mwenyeji sana wa maeneo yale niliona wahudumu wakimchangamkia sana mzee Tito na kumbe alikuwa mnywaji mzuri wa pombe
“hakika huwezi kujua mpaka siku utakapojua!” niliwaza
“endeleeni mimi nikatafute usafiri leo hatulali huku kabisa!” alisema mzee Tito
“yeah ni kweli” tulisema wote kwa pamoja mimi na Josephine huku tukitazamana
Baada ya nusu saa mzee Tito alirejea akiwa na vijana wawili waliokuwa wamevaa majaketi
“sasa mkwe sisi tunakaa porini, sio kijijini kwahyio utakaa kwenye piki piki zaidi ya masaa matatu!” alisema mzee Tito


“hakuna shida mimi ni kamanda muulize Ephraim tulivyokuwa tunapiga kazi vijiji vyote vya wilaya ya Kongwa kwenye …

‘project ya E-vision, kufunga mfumo wa malipo ya dawa kwenye zahanati za vijini, wawili wawili mimi na wewe na Chidy alikua na Cindy..” nilianza kutoa hadithi kuhusu tulivyofanya ile project

sasa mzee Tito na Josephine walibaki kuduwaa, ni wazi kumbu kumbu zangu zilikuwa zinarejea.
Mimi na Josephine tulipanda kwenye piki piki moja mzee Tito alipanda piki piki nyingine pamoja na mizigo ya Josephine safari ya kwenda kijijini kwetu ‘mafichoni’ ikaanza ,
Na hatimaye majira ya saa 3 usiku hivi tulikua mbele ya nyumba ya mzee Tito, ilikuwa safari ndefu lakini kutokana na uzoefu wa wale jamaa tulitumia masaa mawili na dakika kadhaa tu kufika msituni kwetu,
“zawadi mama nimekuletea anti yako huyu hapa” nilisema sasa nikimtambulisha Josephine kwa zawadi
“zawadi nimekuja anti yangu, nimekuletea zawadi nzuri sana” alisema Josephine akifungua begi lake na kutoa mfuko mdogo hivi
“Ephraim aliniambia unapenda sana midoli haya hii napa” alisema akitoa midoli na kumpa zawadi ambaye alikimbilia chumbani kwake kwa furaha
Baada ya chakula cha usiku hadithi zilianza rasmi na Josephine akaanza kuhadithia kuhusu yeye na mimi, sio akina mzee Tito tu bali hata mimi nilikuwa na hamu ya kujua kule ambapo nilitoka na pengine kila kitu ambacho kimenikuta
“mimi nilitokea Mbeya kwa maana ya nyumbani kwa baba na mama, nilimaliza chuo cha mipango Dodoma mwaka 2014 na kuajiriwa mwaka 2015 , ajira ya kwanza nilipangwa Mbeya , lakini baba yangu alikua Dodoma baada ya kuhamishiwa uko, kwahiyo nikahamia Dodoma mwaka 2015 mwezi wa sita,
Nilikuwa nimeajiriwa kama afisa Tehama msaidizi wilaya ofisi yangu ilikuwa katika jengo la halmshauri ya mji wa Kongwa na baba yangu alikuwa daktari bingwa upasuaji wa moyo hospitali kuu Dodoma,
Kwakweli sikupenda kabisa wanaume, na nilikuwa nimepanga kuolewa nikifikisha miaka 30 na wakati huo naanza kazi nilikuwa na miaka 25 tu,
Ofisi yetu tulikuwa watatu mimi, Cindy na Rashidi ambaye tulipenda kumuita Chidy
Sasa mwaka 2016 serikali ilitoa mfumo wa udhibiti mishahara kwa kuunganisha taarifa za wafanyakazi wote na hazina, kwahiyo maafisa Tehama wote wilaya walitakiwa kupata mafunzo ili kuunganisha taarifa hizo halmashauri, kwakuwa ofisi lazima zibaki na watu ndipo sasa ikalazimu serikali kuongeza mtaalam mmoja mmoja kila wilaya kwa ajili ya kuwafundisha na kuwatrain maafisa waliopo, ndipo sasa kwa wilaya ya Kongwa akaletwa huyu jamaa hapa Ephraim, nakumbuka mimi ndio nilipewa kazi ya kwenda kumchukua uwanja wa ndege , alionekana ni mpole sana lakini baada ya muda mfupi niligundua ni mtu alikua anapenda utani sana, kwa ufupi pamoja na kwamba alikuwa ni mkubwa wetu ofisini lakini tulikuwa huru sana akiwepo ofisini, Chidy na Cindy walibadilishiwa majukumu na ofisini nikabaki mimi na Ephraim tu, tulizoeana sana na Ephraim, ingawa hakuna aliyekuwa tayari kuonyesha hisia wazi wazi lakini tulipendana sana, na sasa hata kabla ya kuambiana wazi wazi tayari kulikuwa na minong’ono pale ofisini kuwa mimi na Ephraim tulikuwa wapenzi..
Sasa Josephine alikuwa akitiririka hadithi yake iliyotufanya kutazamana na kutabasamu
“ siku hiyo nakumbuka ilikuwa mwaka 2017 tulikuwa tumetoka kwenye mizunguuko ya kufunga mifumo ya kusambaza dawa kwenye zahanati zote za kongwa, tulikua tunamalizia kijiji cha mwisho ili kurudi wilayani njiani tukavamiwa na majambazi! Ilikuwa ni siku ngumu sana,
Tulikuwa tumefunga zawadi mbali mbali kwenye gari tulizotoka nazo kijijini..
‘ni kweli Josephine, tulikuwa na kuku tulipewa na mzee mleli, na ndizi na miwa nakumbuka!” nilisema
“ni kweli kabisa, sasa tuligoma kushuka kwenye gari na tukamuamrisha dereva kufunga vioo vyote” hata hivyo jambo la ajabu lilitokea
Nakumbuka Ephraim alinikumbatia na kunipa mabusu kadhaa hivi kisha akaniambia maneno ambayo siwezi kusahau hadi leo alisema ananipenda sana na kama lolote likitokea basi nijue kuwa alinipenda sana kuliko mwanamke yoyote kisha akafungua mlango na kutoka nje kuwafuata wale majambazi! Chidy alijaribu kumvuta nje lakini yeye aliufunga mlango kwa nguvu..
 
MZAHA WA DAMU 05
Majambazi walikuwa watatu na mmoja tu ndio alikuwa na bunduki huku wengine wakiwa na mapanga na fimbo hatukujua kitu gani kitatokea kwa Ephraim, mara ghafla tukamuona akipiga magoti na kuweka mikono kichwani huku akijaribu kuongea lugha ambayo hatukusikia hata hivyo ni kama walikuwa wameshindwa kuelewana na wale jamaa kwani sasa Yule aliyekuwa na bunduki alibaki huku akiwa amemlenga kichwani wakati wale wawili wakija kwa kasi kuelekea kwenye gari, hatukuweza kwenda mbele kwakuwa walikuwa wameweka magogo na tusingeweza kurudi nyuma na kumuacha Ephraim pale chini
Mara wakati tunashangaa Ephraim alisimama pale chini kwa kasi ya ajabu na kumpiga teke la mkono na kuifanya ile bunduki kupaa na kuanguka pembeni kisha wakati Yule jambazi anababaika kwa mstuko akarusha ngumi ya shingo iliyomfanya kupepesuka na kisha akaruka juu na kumpiga teke la tumbo na kuanguka chini kwa maumivu na sasa Chidy nae akatoka nje ya gari wakati huo dereva nae alishuka huku akiwa ameshika spana akitulinda mimi na Cindy, tayari kule Ephraim alishachukua ile bunduki , na kisha kumuweka chini ya ulinzi Yule jamaa na sasa ilikuwa rahisi tu kuwanyang’anya silaha zao na kisha kuwageuzia kibao na kuwaweka chini ya ulinzi , dereva nae alishuka akiwa na spana kubwa mkononi na kumpiga kichwani Yule jamaa aliayekuwa upande wetu na sasa wote watatu wakawa wamedhibitiwa, tulipiga simu polisi na baada ya muda mfupi waliwasili na kuwachukua. Tulirudi salama na kuendelea na maisha ya ofisini mara kwa mara na sasa upendo kati yetu ulikua wazi na hatimaye nilienda kumtambulisha Ephraim kwa baba yangu , hata hivyo tayari alikuwa amepata hadithi nzima ya matukio yaliyotokea kule kwenye ile safari na hivyo tayari ilikua rahisi tu kumtambulisha kwake.
Maisha yaliendelea na hatimaye tukatangaza uchumba na wiki moja kabla ya harusi ndio tulikuwa tunajiandaa kumpokea Waziri Mkuu mama Zawadi Macha, wakati tunajiandaa mkuu wa wilaya alikua mara kwa mara anatutembelea ofisini na kuweka mazingira sawa ya kumpokea Mgeni nakumbuka siku hiyo ilikuwa tunaboresha mifumo ya komputa ofisini kwa mkuu wa wilaya, baada ya kazi ya masaa mawili ya kufunga waya,tulienda ukumbi mdogo kupata chai na mkuu wa wilaya alikuwepo, alikuwa ni mwanamke wa miaka kama 43 hivi na alikuwa mcheshi sana , nakumbuka kila saa alikua anamuita Ephraim mume, mara baada ya kugundua Ephraim alitoka wilaya ambayo mumewe alizaliwa, wakati tunaendelea na kazi angeweza kumuita Ephraim kwa utani
“haya mume umalize kazi uje kula usije kufa huku” ama angeweza hata kusema “mume ukapumzike sasa kesho pia ni siku” Ephraim kwakuwa nae alipenda sana utani basi alijibu tu na kisha kazi ikaendelea na tukamaliza salama na kuondoka huku madam akichukua namba zetu za simu kwa mawasiliano zaidi.
Ikiwa imebaki wiki mbili tufunge ndoa yetu nakumbuka siku hiyo tukiwa tunatoka ofisini tulikuwa tunajadiliana mambo kadhaa na tukajikuta tunamtaja mkuu wa wilaya
“hivi kwanini kwanza tumesahau kumualika?” Nilimuuliza Ephraim
“ah ngoja tumualike mke mkubwa huyu!” alisema Ephraim huku akitoa simu yake na kumtumia meseji , haikujibiwa kwa muda huo na tukagawanyika mimi nikaenda kwangu na kesho yake nakumbuka Ephraim alienda kufanya maboresho (updates) ya komputa za hospitali ya wilaya na mimi nilikua ofisini,
Mpaka kufikia jioni ya siku hiyo hakukuwa na mawasiliano kati yangu na Ephraim, usiku kwenye majira ya saa moja hivi Ephraim alinipigia akisema kuwa mkuu wa wilaya alikuwa amejibu ile meseji na kuwa alisema atajitahidi kuhuduhuria kisha akanifowardia zile meseji zake nakumbuka moja ilisema
“kwahiyo umeona mimi mzee sana umeamua kuoa kigori eeh?”
Kulikuwa na meseji nyingine ambazo kesho yake nilizisoma kwenye simu ya Ephraim na kwa hakika kama ningekuwa simjui Ephraim au Yule mkuu wa wilaya basi ningehisi lazima walikua na mahusiano ya kimapenzi, hata hivyo hakuna aliyejali kwani kila mmoja alikuwa bize na shughuli zake na hakukua na mtu aliyedhani suala lile lingekuja kuwa mtihani na madhara makubwa sana kwake
Ilikuwa imebaki siku moja sasa kabla ya kumpokea waziri mkuu mama Zawadi Macha, tulitoka kukagua ukumbi na kujaribu vifaa vyetu tulitoka nje ya ukumbi na kupiga picha tukiwa na watu wengine pale ukumbini, sasa wakati tunarudi ndani Ephraim aliniambia kuna mtu amempigia simu anashida sana ya haraka akamsaidie sikumuuliza kwa undani ila alisema kuna komputa ilikua imegoma kuwaka na ilikua na ripoti muhimu ya kusomwa kesho kwahiyo aliitwa haraka kwenda kurestore na kufanya backup.. nasikitika kuwa sikuwahi kumuona tena Ephraim toka siku ile!

“kama ujuavyo kunapokuwa na ujio wa kiongozi mkubwa watu wanakuwa na heka heka za hapa na pale kuhakikisha kuwa kila idara inakutwa na hati safi, basi tulijikuta hadi usiku wa manane tunafanya kazi na hakuna aliyekumbuka kumuulizia Ephraim kwa kudhani kuwa pengine atakuwa sehemu akifanya kazi,
Ni mpaka nilipojaribu kutuma sms bila kujibiwa na kuamua kupiga simu hazikupatikana, na sikuwa na namna isipokuwa kwenda nyumbani kwake na kukuta mlango umefungwa, kwakuwa ilikuwa ni usiku sana nilirudi nyumbani kulala lakini sikupata usingizi nilikuwa tu kitandani huku simu ikiwa mkononi nikiamini Ephraim angepiga simu wakati wowote lakini haikuwa hivyo, asubuhi saa 12 na nusu tayari dereva alikua mlangoni akigonga ili kuniwahisha kazini kwani tayari waziri mkuu alitegemewa kufika saa nne., nakumbuka njiani dereva alikua akiniuliza alipo Ephraim
“yaani anauliziwa sana, mkurugenzi anasema ikifika saa moja kamili hajatokea basi atachukuliwa hatua” alikua anaongea dereva huku sasa nikijaribu kumpigia lakini sikumpata,
“itakuwa yupo ofisini anamalizia kazi zake huyu,na bila shaka nitamkuta ofisini” niliwaza huku nikishuka kwenye gari haraka haraka kuwahi mapokezi
Nilifika haraka na kuangalia kwenye kitabu cha mahudhurio sikuona jina lake, niliingia ndani sehemu tuliyokuwa tunaweka funguo na nilipigwa na butwaa kuona ufunguo ukiwa umening’inia pale pale kama nilivyouacha jana..
Niliuchukua na kwenda kufungua ofisi yetu na kisha kuwapisha watu wa usafi na kujaribu kupita ofisi mbali mbali, na sasa nilianza kupata wasi wasi kwani kila niliyekutana nae aliniuliza alipo Ephraim, sasa sikuwa na namna ilibidi kwenda kwa mkurugenzi na kumueleza hali halisi ambapo sasa alishauri kufanya kila kilichowezekana ili ziara ya waziri mkuu ipite halafu tushughulikie suala la Ephraim, nilienda ukumbini huku nikiwa sina fuaraha wala amani, akili yangu ilikuwa inaniambia Ephraim alikuwa sehemu Fulani akifanya kazi muhimu sana , kwani pamoja na kuwa alikua mtu wa kupenda utani sana, lakini alikua anafanya kazi sana na alikua hapendi kuwa na kiporo kama akiamua kufanya jambo lake
“kwakuwa tayari kazi kubwa tulishaifanya hakukuwa na jambo gumu siku hiyo nilifanya kazi vizuri kuhakikisha pengo la Ephraim linazibika hadi pale waziri mkuu alipoondoka nikarudi tena kwa mkurugenzi,
“Josephine kwanza kale chakula, pumzika leo hii umefanya kazi kubwa sana, niachie hili suala nalishughulikia kwa karibu sana, hapa tayari nimewasiliana na ocd anakuja hapa muda si mrefu” alisema mkurugenzi huku akinishika begani
“ngoja nimsubiri tu” nilisema sasa nikijiweka vizuri kwenye kiti, wakati huo simu yake ya mkononi iliita kisha akaongea kwa karibu dakika 10 hivi huku akiwa ananitazama sana
Baada ya kumaliza akaanza kuniambia maneno ambayo sikuyaelewa hadi leo
‘ephraim alionekana jana akiondoka na gari moja hivi lililokuwa linaendeshwa na mwanamke, walipita njia kuu kana kwamba wanaelekea chuo kikuu hivi cha Dodoma, na kwa tararibu za polisi inatakiwa walau yapite masaa 48 hivi kwa mtu mzima na masaa 24 kwa mtoto mdogo kuweza kufungua faili la kupotea,
Kwahiyo nikuombe Josephine, kwasasa kapumzike mimi niko hapa naweza kukusaidia kwa chochote, na tutampata Ephraim” alisema huku akifunga tai yake vizuri, nilisimama na kuondoka na kwenda hadi hospitali alikokuwa anafanya kazi baba na kumueleza tukio zima,
Alinisihi kwanza nirudi nyumbani nikapumzike kisha atakuja tuongee, lakini alisema Ephraim alikuwa na sababu maalum iliyompelekea kuzima simu, na atarudi tu wakati ukifika
Sikuwa na jinsi isipokuwa kurudi nyumbani na kesho yake niliandika barua ya kuomba ruhusa ya wiki kwa ajili ya sherehe ya harusi na kisha nikarudi kwangu rasmi sasa nikitegemea Ephraim ataonekana! Lakini hakuonekana na hatimaye siku tatu zikakatika na sasa ikabidi wazazi wa pande zote mbili wakutane na kuahirisha harusi!

msako ukaanza kwa kushirikiana na vyombo vya usalama lakini hakukuwa na dalili zozote, za Ephraim kupatikana, na hatimaye nikajikuta nashindwa kufanya kazi kabisa, na mwishowe nikaomba likizo ya mwezi mmoja na hata ulipoisha sikuweza tena kurudi kazini nikarudi nyumbani Mbeya kukaa na mama yangu. Ndio sasa mpaka hivi tumewasiliana juzi nafurahi kukuona Ephraim naamini kabisa utakumbuka kila kitu na kuweza kutuelezea kitu gani hasa kilitokea siku ile! Alisema Josephine akiwa anatoka machozi kutokana na maelezo aliyokuwa akiyatoa,
“haya ilikuwaje mpaka ukajikuta uko hapa Ephraim?” aliuliza Josephine akinitazama
 
MZAHA WA DAMU 06
By CK Allan
“Tutaongea mengi Josphine lakini mzee Tito akueleze kwanza kwa ufupi pale aliponiokota nikiwa sijitambui” nilisema mzee Tito akiwa ananitazama na kama ishara ya kukubaliana na mimi alianza kumsimulia Josephine ile hadithi yake ya kusisimua kama alivyonieleza mimi siku ile nilipozinduka.
Josephine alibakia ameduwaa huku akishika mdomo wake na baadae alisimama wima huku akizunguka zunguka ,
“sasa Napata picha Ephraim’ alisema Josephine
“baada ya wewe kupotea siku hiyo alikuja madam cathe ofisini akiwa na bahasha mkononi mwake, baada ya kunipa pole alisema kuwa anasikitika sana kwa kila kitu kilichotokea halafu akaniachia hiyo bahasha, na ndani yake kulikuwa na milioni tatu na laki mbili, hata hivyo alionyesha hali ya kuwa na wasi wasi na alikuwa kama hajiamini hivi, na kwa mara ya kwanza alikuja akiwa amevaa miwani nyeusi, kitu ambacho hakikua kawaida yake….”
“madam Cathe ndio nani..?” nilimuuliza sasa nikimshangaa
“Ephraim, humjui madam Cathe si ndio Yule mkuu wa wilaya?” alisema sasa na tayari nilijikuta nakumbuka sura yake na umbo lake Yule madam,
Alikuwa mrefu hivi maji ya kunde na alipenda kuvaa suruali na sasa nilijikuta nakumbuka jinsi tulivyokuwa tunafanya kazi na kutaniana siku ile wakati tukiwa nyumbani kwake..
“Catherine mwanjewa, mkuu wa wilaya ya Kongwa .. kwanini lakini ? kwanini lakini? Why?’ nilijikuta sasa nikisema kwa sauti huku machozi yakinilenga lenga, pale ndani wote walibaki kunitazama tu bila kuongea chochote na sasa bila kutegemea nilijikuta matukio yote yakirejea kichwani mwangu kama filamu..
“nimekumbuka kila kitu!”

nilisema sasa nikikaa chini na kuanza kuwaeleza kila kitu nilichokuwa nakikumbuka, kama vile Josephine hakuwa akiniamini aliweka simu yake tayari kurekodi maelezo yangu,


“sikilizeni, siku ile baada ya kutoka kufunga ile projector kubwa ambayo ndio ingetumika kusomea ripoti ya mkurugenzi, nilisahau kuhifadhi ile ripoti kwenye flash kwa ajili ya backup kwahiyo nikatoka na kwenda kwa mkurugenzi nikaiweka kwenye flash yangu na kuisukumia mfukoni, sasa nilirudi kule ukumbini ili nifunge zile komputa mbili na kuweka projector ndogo kule nyuma, wewe ulikua na afisa elimu pale mbele kwenye meza ya mapambo, wakati namalizia kule nyuma simu iliita na ilikua namba ngeni alikua ni mwanaume alijitambulisha kuwa amekuja na msafara wa waziri mkuu walikua na shida ya komputa yao kuna mafaili ya muhimu wameyapoteza ghafla kwenye mojawapo ya komputa zao walisema wapo karibu na halmashauri wakanielekeza aina ya gari walipo na sehemu walipokuwa wamepaki
Wakati nataka kutoka ndio ukaniambia tupige kwanza picha pale nje ya ukumbi ili tufanye preview ya ukumbi kwahiyo baada ya picha jamaa wakanipigia tena , ndio nikakuambia naondoka nilisogea tu hatua chache na wakati natokea barabani wakanipigia tena na kuniuliza kama ndio mimi ninayekuja nikiwa nimevaa fulana ya bluu na jeans na raba nyeusi nikawajibu ndio wakaniambia wameniona nisimame pale pale na kweli baada ya dakika moja hivi gari nyeupe ilipaki mbele yangu na mlango ukafunguliwa bila mtu yoyote kushuka, nilisogea na kuingia kwakuwa sikuwa na hofu ya kitu chochote, ndani kulikuwa na watu wawili mbele na wengine wawili nyuma kwahiyo tulikuwa jumla ya watu watano , sikuwa namfahamu yeyote kati ya wale jamaa na wakati nikiwa katika hatua za kutaka kuuliza jamaa mmoja alitoa soda kwenye mfuko aliokuwa nao, na kuwapa wale jamaa kule mbele kisha akatoa soda nyingine kwenye mfuko wa pembeni na kuwapa wale jamaa kule nyuma kisha akanipa na mimi huku akitabasamu halafu akaniambia ninywe kwanza tupoze koo kisha tutafute mahali tukae turejeshe mafaili
“unajua broo sisi wote hapa tunaumiza kichwa itakuwaje kama yasiporudi hata hivyo tumepata story zako kuwa unaweza sana hizi kazi, usijali tutakulipa pesa nzuri, maliza soda twende zetu” alisema na mimi sikua na wasi wasi nikanywa ile soda kisha dereva akaondoa gari kwa mwendo wa kawaida tu kuelekea maeneo ya stendi , mara nilianza kuona giza na kizungu zungu halafu nikajiona kama napaa angali hivi, halafu nikapoteza fahamu ni mpaka nilipokuja kuzinduka baadae nikiwa nimefungwa mikono na miguu kwenye kiti kwenye chumba ambacho sikuelewa ni wapi
Nilijaribu kupiga kelele na ndipo jamaa wawili wakatokea
“oi nipo wapi ? imekuwaje mbona niko hivi nimefanyaje kwani mbona niko hapa mmenifunga hivi?’ niliuliza huku nikiwa najaribu kupambana na zile kamba

Wale jamaa hawakunijibu badala yake mmoja alitoa simu na kutoka nje, kisha baadae akarudi tena akiwa Na mwanaume mmoja hivi wa makamo miaka kama 50 hivi
Alikuja moja kwa moja na kunipiga teke kichwani lililonifanya kuanguka mzima mzima nikiwa kwenye kile kiti , wakati naugulia maumivu sasa alinizaba kibao usoni mpaka nikashindwa kuona kwa muda, nilipiga kelele za maumivu huku nikimuuliza sababu za yeye kufanya hivyo, hakujibu aliendelea kunishambulia na sasa ilibidi wale vijana wake kumshikilia na kunikalisha tena pale kwenye kiti huku damu zikiwa zinatoka puani na mdomoni
Yule mzee alinikaba shingoni na kuniuliza kwanini natembea na mke wake!
“mzee sijawahi kutembea na mke wa mtu mimi!” nilisema kwa tabu huku nikijitahidi kuachia pumzi yangu
“unasemaje wewe kifaranga? Huko chuoni ulifundishwa kutengeneza komputa au kutengeneza wake za watu?” alifoka tena huku akiniongezea ngumi yam domo, niliskia maumivu makali sana
Kwa bahati nzuri kamba zilifunguka mikononi mwangu nikaweza kuzuia baadhi ya mashambulizi yake, hata hivyo Yule mzee alionekana kuwa na hasira sana na bila shaka angeniua pale pale isingekuwa kuzuiliwa na vijana wake niliweka mikono yangu pamoja ishara ya kumsihi Yule mzee anisikilize huku sasa nikiwa nalia kweli kweli,
“tafdhali mzee nisikilize, mimi sijui hata huyo mwanamke unayemzungumzia!” nilijaribu kujitetea
“humjui? Humjui hawara yako Cathe? Hivi ninyi vijana wa siku hizi hamuogopi kabisa kutembea na wanawake ambao hamjui kabisa waume zao wanafanya nini na wapi?” alisema sasa akimkonyeza kijana wake ambaye alileta simu yangu
“toa lock, toa lock!” alisema Yule mzee akinipa ile simu yangu
Nilitoa ile nywila kwenye simu yangu huku nikiwa na najifuta damu zilizokuwa zinachuruzika usoni
Yule mzee alifungua sehemu ya ujumbe mfupi na kunisomea kwa sauti meseji zilizokuwa zinatoka kwa mkuu wa wilaya Cathe
“we mwanaume unaniacha kweli? Siamini unamuoa huyo, kwani kanizidi nini au mimi nimezeeka sana?”
“mwanaume wewe huridhiki kweli mapenzi ninayokupa bado unaoa tu!”
“haya ulale sasa mume, kesho uwahi kurekebisha zile komputa hatuhitaji kwere kwenye wilaya yetu”
“umefanya kazi nzuri leo mume, natamani nikupe zawadi kubwa hadi ndoa isifungwe”
Mzee aliendelea kusoma zile meseji kwa sauti huku vijana wake wakicheka na sasa na mimi nilijikuta nacheka, nilicheka kweli mpaka sasa Yule mzee akabaki kuduwaa na wale watu wake kisha akarudisha ile simu na kunisogelea tena
“kwahiyo unanicheka? Baada ya kutembela na mke wangu, unanicheka si ndio?”
Aliuliza Yule mzee huku akiachia kibao kingine kikali
“mzee huu ulikua utani tuu, sijawahi kutoka na madam, ni utani tuli…” nilikatishwa na teke kali ambalo lilinipata sawia maeneo ya kwenye kidevu na kunipeleka chini, nilijikuta naona giza mbele yangu na nikajikuta nazimia
Sikuelewa chochote kilichoendelea mpaka siku hiyo nilipojikuta hapa kwa mzee Tito miezi kadhaa iliyopita
Nilisema huku kila mmoja akinitazama,
“pole sana kijana wangu, kwa maana hiyo Yule alikua mume wa madam Cathe ?” aliuliza mzee Tito
“ngoja,” Josephine aliongea huku akitoa simu yake na kubonyeza bonyeza kisha baada ya dakika kama tatu hivi akanionyesha picha ya mzee mmoja akiwa ndani ya suti pembeni yake kulikua na mwanamke ameshika maiki
“ndio ni huyu mzee, na huyu ni madam Cathe” nilisema sasa
“aisee, SASA NIMEELEWA KILA KITU!” alisema Josephine
“nini tena!” tulijikuta tunauliza kwa pamoja mimi na mzee Tito
“wakati naamua kuacha kazi madam aliniita nyumbani kwake na kuniomba nisiache kazi, nakumbuka siku hiyo nilimkuta huyu mzee akiwa pale, alikua ananitazama sana na kila baada ya dakika kadhaa aliondoka pale sebuleni na kurudi baadae alirudi akiwa amevaa miwani alidai kuwa alikua anasumbuliwa na mafua na macho yalikua yakitoa machozi
Sasa mkuu wa wilaya baada ya kuniomba sana kubaki nilikataa kwa kumwambia kuwa nisingeweza kufanya kazi huku nikiwa sijamuona Ephraim , angalau angekuwa amekufa labda
 
MZAHA WA DAMU 07

By CK Allan
Yule madam alinisihi sana akishirikiana na Yule mume wake nakumbuka ni kama kuna kitu Yule mzee alitaka kusema lakini alishindwa ila nilidhani kuwa ni huruma tu walikua nayo juu yangu, wakati narudi mbeya baada ya mwezi mmoja hivi, madam Cathe alinipigia simu kuwa ameongea na mkurugenzi na badala ya kuachishwa kazi nitapewa ruhusa maalum ya matibabu na mshahara wangu hautafungwa na yeye kama mkuu wa wilaya ataniongezea laki 5 kila mwezi ili zinisaidie mpaka nitakapoamua kurudi kazini, na siku nitakayorudi tu nitaenda masomoni na atagharamia yeye aliniambia kuwa ananisaidia kama mdogo wake tu kwa kuwa niliishi nae vizuri,
Ni kweli mpaka leo mshahara wangu unaingia na laki 5 kutoka kwa mkuu wa wilaya alisema Josephine
“aisee sasa una mpango gani?” aliuliza mzee Tito
“sijajua bado! Lakini naamini hakuna kitakachoharibika, mimi na Josephine tutashauriana jambo la kufanya” nilisema huku nikimgeukia Josephine na kumkumbatia, tayari ilikuwa ni usiku sana mimi na Josephine tulielekea chumbani kwangu na sasa mambo mengine yakaendelea
Niliamka na kuangalia saa ilikua saa 3 kasoro asubuhi Josephine hakuwepo kitandani nilitoka hadi nje na kumkuta akiwa jikoni na mama Tito wakiendelea kuandaa chakula cha asubuhi ile
Baada ya salamu nilirudi zangu chumbani na kuendelea kutafakari mambo yote yaliyokuwa yametokea, kwasasa mawazo yalikuwa kwa mama na baba yangu pamoja na mdogo wangu Janeth, niliwaza jinsi mama yangu alivyolia na baada ya kupokea taarifa za kupotea kwangu, na mdogo wangu Janeth je atakuwa katika hali gani na kama alimaliza masomo yake ama la, Mara ya mwisho Janeth alikuja Dodoma wakati namvalisha pete ya uchumba Josephine, alikuwa kidato cha tano shule ya wasichana ST Thomas Morogoro, kwa kiasi kikubwa mimi ndie nilikuwa namlipia ada na mahitaji yake muhimu, hata hivyo baada ya sherehe za uchumba alibaki kwa siku kadhaa akiwa anaishi na Josephine na nakumbuka tulipanga kufunga Ndoa yetu wakati ambao Janeth angeweza kuhudhuria, baada ya kifungua kinywa sasa nilikuwa na shauku ya kutaka kujua kuhusu familia yangu
“naomba usinifiche kitu kuhusu baba na mama, na janeth” nilisema sasa huku mapigo yangu ya moyo yakiongezeka, sikutaka kusikia habari mbaya juu tena
“Ephraim usijali, wote ni wazima kabisa lakini…” alisema Josephine
“lakini nini?... lakini nini?” nilimuuliza sasa nikiwa na wasi wasi
“Janeth, alishindwa kabisa kuendelea na masomo na mpaka sasa akili yake haiko sawa kabisa, yupo Milembe Dodoma!,” alisema Josephine akiwa na huzuni na tayari machozi yalikua yanatoka
“dah,” nilijikuta naishiwa maneno ya kusema
“ndio hivyo Ephraim, angalia mimi mwenyewe nilishindwa kuendelea na kazi, kwahiyo hata Janeth hatuwezi kumlaumu, sio makosa yake!” alisema Josephine
“ni kweli , naomba turudi mjini” nilisema
“ni kweli lakini nilikua naomba kwanza upone kabisa kisha tukubaliane kitu cha kufanya ili tusije kufanya makosa tena, je wale waliotaka kukudhuru kama bado wanaendelea kukufuata?” aliuliza Josephine
“sikiliza kwa jinsi ilivyo ni kuwa Yule mzee alikuwa anafuatilia simu ya mke wake, na akawa anasoma zile meseji zetu kwahiyo yeye alichukulia ni kweli ndio akaamua kufanya alichofanya, baadae ndio akajua ukweli kuwa ilikua ni mzaha, ndio maana akaamua kukutafuta, lakini ilikuwa ameshachelewa” nilimwambia
‘itakuwa hivyo, na je wewe unaamua nini?” aliuliza Josephine
“kwasasa naomba kitu kimoja, turudi Dar kwa baba na mama , then tufanye utararibu wa kwenda Dodoma baada ya hapo tutajua!” nilisema
“vipi kuhusu kazini?” aliuliza Josephine
“sijajua bado” nilisema nikisimama na kujiangalia tena kwenye kioo, makovu yalikuwa yananikaribisha na kunicheka hivi!

Ni kweli baada ya wiki moja mimi na Josephine tulirudi Dar, ilikuwa ni huzuni sana kuagana na mzee Tito na mke wake ambao nao walikua na hadithi ya kusikitisha, katika maisha yao kwani mzee Tito baada ya kustaafu serikalini, alikuwa akirudi kwake mwanza na familia yake na kwa bahati mbaya walipata ajali ya meli ya Mv Bukoba, na yeye peke yake alipona katika ajali hiyo pamoja na mwanamke mwingine ambaye ndie mke wake kwa sasa, anadai alijikuta akiwa ameshikilia kipande cha mbao ambacho kilikua kinaelea na mke wake huyo alikua ameshikilia mbao nyingine,

kutokana na hadithi ya mzee Tito anasema kuwa hata mke wake huyo alipoteza familia yake yote katika ajali hiyo na baada ya heka heka waliokolewa na kuwekwa sehemu moja, na siku ya kutolewa hospitali walitolewa kwa pamoja kama mke na mume.
“hatukuwa na sababu ya kuanza kubishana na wauguzi kuwa sisi hatukufahamiana isitoshe kila mmoja alikuwa amepoteza familia yake akishuhudia, kwahiyo tulipofika mwanza mjini niliamua kurudi Dar na kuuza kila kitu changu na kutafuta shamba mbali kabisa, hatukutaka kukaa na watu kabisa , mke wangu alikuwa anaweza kuzimia hata mara tatu kwa siku, lakini mwishowe tulihamia huku na maisha yanaendelea” nilikuwa nakumbuka maneno ya mzee Tito nikiwa kwenye gari nikirudi Dar, ilikuwa ni safari ndefu kwani sasa akili na mawazo yangu yalikuwa yakiwaza kuhusu wazazi wangu na Janeth.


Tulifika majira ya saa moja usiku na kuchukua bajaji kuelekea kimara mwisho ambapo ndipo kulikuwa nyumbani kwetu, kwasasa nilikuwa mzima kabisa isipokuwa nilibakiwa na makovu mwilini na kidole changu cha mwisho ambacho kilikuwa kimepinda na hakikuweza kunyooka vizuri, sasa tulikuwa nje ya geti na kumshauri dereva wa bajaji apige honi na baada ya muda mfupi ilisikika sauti ya mtu akitembea kuja kufungua lile geti, alikuwa ni baba yangu ambaye alifungua geti kisha akasogea pale tulipo na kabla hajafika Josephine alishuka akiwa na begi lake, tayari tulikuwa tumeshalijadili hili mimi nilibaki ndani ya bajaji kisha nikavaa kofia yangu na kujifunika kwa kikoi baada ya Josephine kunipa ishara nikashuka kwenye bajaji na mfuko mmoja uliobaki, halafu tukasogea ndani, nilimpungia mzee Tito mkono kisha akatangulia na kupiga hatua kuelekea ndani,
“shosti uko wapi?” Josephine alikuwa anaita kwa sauti baada ya kuingia ndani, tofauti na wanawake wengine Josephine alikuwa amemzoea mama yangu kama mama yake mzazi, suala hili lilichagizwa na zoezi la matibabu la Janeth kule Dodoma ambalo liliwafanya kukutana mara kwa mara, kila wakati mama alipokuwa anaenda Dodoma waliwasiliana na Josephine na walienda wote,
“haya shoga yanguu mie huyoo haya mbona usiku usiku wewe mwanamke?” mama alikuwa anauliza akitokea jikoni
“shosti nimekuja mjini kutembea ngoja nije huko jikoni” Josephine aliondoka na kuelekea Jikoni na sasa nikabaki nikiwa na mzee Tito, mipango yetu ilikuwa imekwenda kama tulivyopanga mzee Tito alikuwa akinitazama tu na sasa nilitoa simu yangu na kumtumia ujumbe Josephine..
“kazi ianze”
“sawa baba” alijibu
Na baada ya muda Josephine alitoka
“aah mzee naomba mtoe huyu rafiki yangu mpaka kwenye duka la dawa karibu hapo kuna dawa zake akanunue kikaratasi anacho mwenyewe, tumezisahahu bahati mbaya” alisema Josphine na mzee Tito bila hiyana akasimama na mimi nikamfuata tukatoka nje ya geti na Josephine alimwambia kuwa mimi nilikua nasumbuliwa na jino na nilikuwa sipendi kuongea, hata hivyo kutokana na jinsi nilivyojifunika kichwani na suruali ya jeans niliyovaa bila shaka mzee Tito alijua mimi ni mwanamke “rafiki yake Josephine” na mzee wangu mimi kama kawaida hakuwa mtu wa kujali mambo, niliijua ile mitaa vizuri na nilijua hata duka ambalo tulikuwa tunaelekea, baada ya hatua kadhaa tulipita grocery moja hivi kwa mama Temba nikasimama
“ah mzee tuingie hapa” nilisema na kidogo mzee Tito alistuka baada ya kugundua ni sauti ya kiume, tuliingia na kuangalia sehemu iliyokuwa tulivu na kukaa baada ya dakika mbili mhudumu alikuja baba yangu alikuwa anakunywa pombe ingawa hakuwa mlevi lakini siku iyo aliagiza malta tu na mimi nikaagiza wine, baada ya mhudumu kuondoka sasa nikatoa ule mtandio na ile kofia na kutazamana uso kwa uso na mzee Tito!


Sasa mzee Tito alisimama akzunguka kisha akakaa tena na kusimama halafu akawa kama mtu aliyechanganyikiwa, baada ya muda akakaa tena
“mzee, nilisema huku nikishindwa kujizuia na kumkumbatia kwa nguvu!” tulikumbatiana kwa muda sasa huku mzee Tito akimshukuru Mungu,
“Najua yapo mengi sana unayo kijana wangu lakini nataka tu kujua sasa imekuwaje” alisema mzee Tito
“mzee kwanza unajua kwanini nimeanza kwako na sio kwa mama, nimesikia kila kitu kilichomtokea Janeth na najua hali ya mama, sipendi kumpoteza”
Nilisema nikiwa nimetazamana na mzee
 
MZAHA WA DAMU 08

By CK Allan
“Ni kweli na mama yako presha bado inamsumbua, na baada ya kupata taarifa kuwa tukaahirishe harusi hali yake ilikua mbaya akalazwa Dodoma karibia mwezi mzima, na Janeth nae ikawa hivyo ulivyosikia, kwakweli tunashukuru Josephine alikuwa karibu sana na sisi” alisema mzee Tito
“tulipanga hivi kwamba wewe ujue hizi taarifa pembeni ukiwa na mimi, halafu mama ataambiwa na Josephine kule wakati…..” nilikatishwa na mlio wa simu ya baba ambapo mama alikuwa anapiga
Haraka baba alipokea na kuweka sikioni
“Jesca tunakuja tupo jirani tu hapa” alisema baba
“ni kweli?, nauliza ni kweli?” mama sasa alikuwa akiongea kwa kukata kata
“mke wangu tunakuja” alisema mzee kisha akalipa vinywaji tukaondoka
Sasa tulitembea haraka haraka na kufika nyumbani tayari mama alikuwa mlangoni akisubiri
Bila kupoteza muda mama alinipokea kwa kunikumbatia kwa nguvu kisha akanikagua usoni sasa machozi yalikuwa yakimtoka
“ni wewe Ephraim mwanangu, ni wewe, sitaki kujua wamekufanyaje, nshukuru Mungu uko hai mwanangu!” mama alisema na sasa akashindwa kujizuia na kuingia ndani! Sote tuliingia ndani na kumkuta mama akiwa ameinama kwenye kochi alikuwa akifanya sala na kumshukuru Mungu, tulibaki tumeduwaa tu na kumuacha mama amalizie maombi yake, baada ya dakika zipatazo 10 mama alimaliza maombi yake na kisha akasimama na kunikumbatia tena kisha
“sasa kalete chakula Josephine” alisema huku akiwa anajifuta machozi
Sasa ilikuwa haihitaji daktari kuweza kung’amua kuwa mama hakuwa sawa, tayari alikuwa anaongea sana kupita kawaida! Tulianza kula chakula lakini yeye alikuwa akinitazama tu na kuniongezea chakula chake
‘mama mimi tayari nimekula kula basi na wewe” nilisema sasa nikijaribu kumpa mama yangu chakula alikula kidogo na sasa bila kutegemea mama akaanguka chini , mzee tito alikimbilia chumbani haraka na kisha akatoka akiwa na ufunguo wa gari na kunirushia
Katoe gari haraka huku yeye na Josephine wakimuweka sawa pale kwenye kochi
Nilikimbia haraka na kuwasha gari kisha nikafungua geti nikatoa gari nje ya geti na wakati huo tayari baba na Josephine walikuwa wamemshika na kumtoa nje kumpakia kwenye gari, nilifunga geti na kuondoa gari haraka kuelekea hospitali
“Tunaenda kwa Dokta Longino !” alisema mzee akinielekeza
“si hapa Bucha?” nilisema sasa nikivuta mafuta na kufunga mkanda vizuri
“ndio lakini amehamia kwenye lile jengo la nyuma ndio zahanati yake ilipo” alisema baba
Kutoka kwetu mpaka hapo ilikuwa ni dakika tano tu kwa gari lakini nilitumia dakika tatu na sekunde kadhaa tukawa tayari nje ya geti la kituo cha afya cha FARAJA HEALTH CARE tuliingia ndani haraka na Josephine alipiga kelele kwa wahudumu kuwa ni dharula na haraka wakatoka wakiwa na kitanda kilichokuwa na magurudumu na kumuweka mama yangu na kumkimbiza haraka kwenda chumba cha matibabu ya dharula
‘hii sasa hatari, mama yangu atapona?” nilijaribu kumuuliza nesi mmoja aliyekuwepo pale
“usijali kaka madaktari wake wanafanya kila wanachoweza, huyu ni mgonjwa wetu, kwani si mama Ephraim huyu, maskini toka mwanae apatwe na matatizo mama wa watu amekuwa akipata shida sana ya moyo” alisema Yule nesi
“ah” niliguna kisha nikaondoka na kusogea pale alipokuwa amekaa mzee na Josephine, walikuwa wanaonekana kuchanganyikiwa sasa kile ambacho tulikuwa tunahofia zaidi ndicho ambacho kimetokea, tulikaa pale kwa zaidi ya nusu saa bila daktari yeyote kutoka nje na hivyo kuzidisha wasi wasi na sasa baba yangu alikuwa akisimama na kukaa kila baada ya sekunde kadhaa na hatimaye wakati tunajiuliza kitu gani kilichotokea dokta Longino alitokea akiwa na uso wenye tabasamu kidogo
na sasa aliponiona alishtuka na kunisogelea
“Ephraim? Ah nimeshangaa kujiuliza kitu gani kimemtokea mama kwa ghafla sasa kumbe ni furaha ya mama iliyopilitiliza! Hakika Mungu ni mwema!” alisema
“nashukuru sana Dokta” nilisema
“tunakusikiliza dokta” alisema baba
“mama anaendelea vizuri na kwasasa amewekewa mashine ya kupumua ili kuweza kurudisha mapigo yake katika hali ya kawaida, ambapo tunategemea kwenye saa 8 hivi au 9 usiku tunaweza kuitoa kama hali isipobadilika na sasa tunaweza kwenda ofisini kwangu kuongea zaidi

Aliongea Yule daktari ambaye mara nyingi alituzoea kutokana na mama kutibiwa pale mara nyingi, tulipita vyumba kadhaa na kufika ofisini kwa dokta Longino.
“haya mzee Tito nipe habari za Ephraim!” alianza dokta Longino
“mama, sijui hata nisemeje lakini mimi pia ndio nimemuona usiku huu na tulikuwa hatujaongea chochote bado wakati tunapata chakula ndio ikawa hivi ilivyokuwa, kwakweli hata mimi natamani kusikia kila kitu kilichomtokea Mwanangu” alisema baba akinitazama kwa jicho lililojaa shauku
“kwakweli baba tutaongea kila kitu ila kwa ufupi nilivamiwa na majambazi ambao walikuwa wamenifananisha na mtu mwingine ambaye walikuwa wametumwa kwake kumshambulia, na walinipiga na kunijeruhi sana na kisha wakaenda kunitupa huko porini karibu na Morogoro wakidhani kuwa nimekufa, lakini kwa bahati kuna mzee aliniokota na kunihudumia na kunitunza mpaka nikapona, na hatimaye nilimtafuta Josephine kwenye mitandao ndio akanifuata na tuko hapa leo”
Nilisema huku dokta Longino na mzee wakiwa kama bado wanasubiri niongee jamabo ambalo labda sikuongea,
“lakini jambo la ajabu mzee ambaye ameniokoa na kunihudumia kwa kipindi chote kile na yeye anaitwa Tito!” nilisema sasa nikiachia tabasamu kali nikimtazama Josephine ambaye nae alikuwa akitabasamu
“kwasasa tuangalie hali ya mama kila kitu kitakaa sawa tu baba huko baadae” nilisema
“kwanini usije na mzee Tito na mkewe huku mjini?” aliuliza baba
“kwakweli tungependa sana lakini na yeye ana changamoto inayomfanya yeye na mkewe waishi huko porini labda huko mbeleni” niliwaambia kisha nikawasimulia kwa ufupi kuhusu maisha yao jinsi walivyonusurika kufa maji katika ajali ya mv Bukoba,
“nawaomba sana kama hamtajali mkapumzike mzee Tito kesho asubuhi mama atakuwa sawa kabisa” alisema daktari Longino
“hapana tutabaki tuu” tulijikuta tunasema kwa pamoja mpaka dokta akashangaa
Haya basi jamani ngoja tuone kama atakuwa ametolewa kule kwenye chumba maalum halafu tumtafutie chumba ambacho mnaweza kuwa nae, nisubirini hapa” alisema dokta Longino
Hakuwa amebadilika sana dokta Longino bado alikuwa vile vile na urembo wake, na hakika usingeweza kufikiri kama atazeeka hivi karibuni, nakumbuka tangu nikiwa mdogo nilikuwa nakuja kupatiwa matibabu katika zahanati ya dokta Longino, enzi hizo walikuwa kwenye jengo la kawaida tu, tofauti na sasa ambapo walikuwa wamehamishia huduma katika jengo jipya la kisasa kabisa na pia waliweza kuwa na vyumba vitatu vya wagonjwa maalum, Baada ya dakika kadhaa dokta Longino alirejea akiwa na nesi mmoja ambapo alitukabidhi kwake
“mama ameshatolewa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu, hapa kwetu huwa hatuna wagonjwa mahututi, tuna wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu, kwahiyo sasa mama yupo chumba maalum ambapo na ninyi mnaweza kuwa nae ila tu msimuongeleshe kwasasa” alisema Dokta Longino, kwa maelezo ya mzee alisema kwamba alisoma darasa moja enzi hizo pamoja na baba yake Dokta Longino, na ni yeye alikuwa mpambe katika harusi yao, na hata hivyo wakati wakiwa wanarudi kumsindikiza Longino shule ya wasichana Korogwe, alikokuwa anasoma gari yao ilitumbukia mto wami na kisha wote kupoteza maisha, na sasa Longino alilelewa na baba yake mdogo kwa kipindi chote hata hivyo alienda nchini India kusomea udaktari na hakurejea tena isipokuwa alimuwezesha Longino kusomea udaktari na kumuwezesha kufungua kituo kidogo cha afya, na sasa longino alikuwa anamchukulia baba yangu kama baba yake mzazi, na hata pale hospitali tulilipia dawa tu lakini hatukulipa vipimo wala kitanda kama walivyokuwa wakifanya wagonjwa wengine,
Nilikuwa nikiwaza haya yote huku tukipandisha ngazi kuelekea vilipo vyumba vya wagonjwa maalum na kisha kwa msaada wa nesi tuliingia chumbani na kumuona mama akiwa amelala na kuwekewa mashine maalum ya kupumua
“hali yake iko sawa sema tu tumempa dawa maalum ili apumzike, mapigo yake yako sawa, tafadhali msije kumuamsha” alisema Yule nesi kisha akapiga hatua kuondoka
Tulifika kitandani na kumuangalia mama kisha baadae tukaenda kukaa kwenye sofa iliyokuwa pale pembeni, pembeni kulikuwa na kitanda kingine ambacho tulimshawishi baba akakubali kulala na mimi na Josephine tukaanza kupiga hadithi za hapa na pale kwenye sofa mpaka usingizi ukatupitia,
Nilikuja kuamka asubuhi nikiwa peke yangu kwenye sofa, mbele yangu mama yangu alikuwa amekaa akipiga hadithi na Josephine, baba hakuwepo
 
Back
Top Bottom