MZAHA WA DAMU 09
By CK Allan
“mama, mama” nilisema sasa nikiruka pale kwenye sofa na kwenda kumkumbatia mama yangu
“mwanangu nimepona kabisa poleni sana nimewasumbua kwa kuwalaza hospitali jamani” alisema
‘tafadhali mama usiseme hivyo” tulisema wote kwa pamoja mimi na Josephine
“oneni mpaka mnaongea kwa pamoja” mama alisema akiwa anatushika mikono
“shosti, umeniogopesha ujue” alisema Josephine sasa akimtania mama
“vipi mzee Tito kaenda kuzimua?” nilisema nikimuulizia baba
“hahaha hana ujasiri huo, tangu lile tatizo litokee Tito kaacha kabisa kunywa pombe anaenda kanisani asubuhi mchana na jioni,hivyo kapitia kanisani ibada ya asubuhi kisha apitie nyumbani kuchukua nguo zangu kadhaa za kubadili leo tunaweza kuruhusiwa” alisema mama akijiweka vizuri pale kitandani
“hahaha mzee Tito kaokoka! Kweli Mungu yupo!” nilisema huku tukicheka wote pale
Baada ya dakika kadhaa Dokta Longino alikuja,
“aisee poleni kwa uchovu, nikasema leo sikuamshi hata kidogo” alisema dokta Longino
“hahaha ni kweli, nimelala sana” nilisema nikiona aibu kidogo
‘mama leo anarudi nyumbani , sioni haja ya kuendelea kumuweka hapa ana hamu sana na mwanae , Furaha hebu niletee faili la mama” alisema Dokta Longino huku akiwa anaendelea kumpima mama mapigo yake ya moyo kwa kifaa chake alichokuwa ameshika mkononi na kuweka masikioni,
Baada ya saa moja baba alirejea akiwa na mfuko mdogo wa plastic ambapo aliuweka pale kisha nikatoka na mzee na kumuacha mama akiwa na Josephine kwa ajili ya kujiandaa kurudi nyumbani.
Saa tano na dakika kadhaa hivi sasa tulikuwa nyumbani mama yangu alikuwa amepona kabisa na kurudi katika hali yake ya kawaida ilikuwa ni jumamosi na hivyo alituambia kesho twende nae kanisani kwa ajili ya kumtolea Mungu sadaka ya shukrani kwani alikuwa ameweka nadhiri yake kama nikirudi hai basi kama ujuavyo walokole tena, mama nae alikuwa mmoja wao! Basi tulianza maongezi yetu huku mama akiwa anasikiliza kwa makini na kila wakati mwingine angetoka kwenda chumbani kwake kisha kurejea tena,
Sebuleni kusikiliza maongezi yale baba sasa alibaki na mshangao mkubwa na kila wakati nilipokuwa nikimtaja mkuu wa wilaya na mume wake, baba na mama walitazamana na sasa na mimi nikawa namtazama Josephine na kukonyezana kuashiria kuwa kuna kitu tulikuwa tumegundua na hatimaye baada ya maongezi sasa mzee Mzee Tito nae akaanza kuhadithia habari zake ambazo zilibaki kutuweka sisi mdomo wazi
‘mwaka Jana ile mwezi wa 12 , baada ya kupokea simu kutoka kwa Padri Jacob, kuwa ndoa inaahirishwa kwasababu ulikuwa umepotea ghafla, nakumbuka tulipata simu kwenye saa nane hivi mchana, sikuwa na jinsi isipokuwa kuondoka jioni ile kwenda Dodoma, na tulifika majira ya saa 5 usiku na hatukutaka kumsumbua Josephine usiku ule hivyo tukaanza kutafuta mahali pa kulala, lakini kabla hatujaanza kuzunguuka Josephine alinipigia kuniuliza tumeshafika wapi, basi tukamulekeza na akatuelekeza sehemu ya kwenda kumbe tayari alishalipia hoteli basi tukaenda mpaka hoteli husika na baada ya kujitambulisha mapokezi tulipewa ufunguo wetu na kwenda kwenye chumba tulichokuwa tumeandaliwa,
Asubuhi sana alikuja Josephine akiwa na baba yake na tukapata wasaa wa kuongea nao huku kila mmoja akitoa pole kwa mwenzake, kwa bahati siku ile Padri Jacob alikuwa ameenda Dumila kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Padri mwenzao, na hivyo ikatupasa kubaki Dodoma kwa Siku kadhaa, kesho yake Josephine alinipigia akisema kuna mtu alitaka kuonana na sisi na amemtumia namba yetu aje pale hotelini, na ndipo siku iyo akaja huyo mkuu wa wilaya na mume wake kwenye majira ya saa 12 jioni hivi pale hotelini,
Walikuwa wanakusifia jinsi ulivyokuwa mchapakazi sana na jinsi ulivyomsaidia kumfungia mifumo ya komputa zake ofisini na mambo mengine, alitueleza jinsi ulivyomualika kwenye harusi yake na jinsi yeye na mume wake walivyojisikia vibaya kutokana na wewe kupotea katika mazingira ya kutatanisha, sisi tulimshukuru mkuu wa wilaya na wakati anaondoka alituachia laki 5 nakumbuka, na kisha akasema tutawasiliana zaidi tukirudi Dar, na mara baada ya kumaliza mambo yote tulirejea Dar, na baada ya wiki moja tena ndio mkuu wa shule wa Janeth akatupigia simu twende siku hiyo hiyo Janeth anaumwa, hakukuwa na namna tukarudi Morogoro shuleni na tulimkuta Janeth katika hali mbaya, imagine alishindwa kumtambua hata mama yake, tuliondoka na matron mpaka Dodoma na baada ya vipimo vya kiafya walisema hakukuwa na ugonjwa wowote na hivyo apatiwe tiba ya akili
Tuliwasiliana na Josephine ambaye alisema ana wiki moja tangu aache kazi na yuko mbeya, hata hivyo alisema kesho ataanza safari kuja Dodoma , na akatuunganisha na baba yake ambaye alikuwa na rafiki zake pale Milembe, na ikatubidi kwenda pale kumpeleka Janeth, ilikuwa ni mwendo wa saa Moja na nusu kutoka pale Dodoma mjini kwenda Milembe, kama ujuavyo tulitoka Dar mbio mbio, sikuchukua leseni wala kadi ya gari, sasa wakati tunakaribia Kongwa mbele yetu kulikua na gari dogo kutokana na mawazo na haraka sikutazama indicator kuwa alikuwa anaingia kulia, na ilitakiwa nipunguze mwendo kumuacha avuke mimi nikaunganisha na kumkwangua na taa ya upande wa kushoto kwa Yule jamaa ikapasuka na mimi vile vile taa upande wa kulia ikapasuka sikuwa na jinsi isipokuwa kupaki pembeni na kumbe aliyekuwa anaendesha ile gari alikuwa mwanamke akaanza kuvurumisha matusi na japokuwa nilimuomba radhi lakini hakujali na ukizingatia tulikua karibu na makazi ya watu tayari umati ulikuwa umejaa pale na hatimaye polisi wakawa wamefika, kama ujuavyo polisi jambo la kwanza walitaka leseni na kadi ya gari, na hapo ndipo nilikumbuka kuwa sikuwa na chochote, na pasipo kujali polisi mmoja akaingia kwenye gari kuiendesha kuelekea kituo cha polisi na mimi nikapakiwa kwenye ile gari ya Yule mama na polisi mwingine kuelekea kituoni!
Nilikiri kosa na Yule mama akasema hataki kesi anataka tu gari yake itengenezwe labda kutokana na hali ambayo alituona tunayo au alidhani kuwa nisingeweza kulipa, polisi nao waliamua kuongeza kosa ikiwemo kuendesha gari bila leseni na kuendesha gari ambayo sikuwa na umiliki nayo, kwa haraka matengenezo ya gari pamoja na kununua taa mpya walikadiria kama laki 9 pamoja na faini ambayo ilikua zaidi ya laki moja,
Sikuwa na pesa iyo kwa wakati ule na ingenichukua angalau siku tatu au nne kutafuta ile pesa, niliomba masaa mawili ya kutafuta ile pesa huku nikiacha gari langu kama dhamana, nilikuwa nawaza wapi naweza kupata pesa ile kwa wakati, wakati tunajadiliana na mke wangu mara tukamkumbuka mkuu wa wilaya na bila kusita niliingia kwenye gari na kufunga vioo kisha nikampigia madam Cathe, na kwa bahati alipokea na nilipojitambulisha tu alinielewa nilimueleza kila kitu na alisikitika sana, alininiambia nisubiri ndani ya robo saa hivi au nusu saa
Hivi analishughulikia, nakumbuka baada ya kama dakika ishirini hivi ilikuja gari ndogo aina Toyota harrier nyeusi na mtu mmoja akashuka na kuingia pale kituoni na baada ya dakika kadhaa alitoka akiwa na Yule polisi ambaye alikuja nae mpaka pale tulipokuwepo, tulishangaa Yule polisi akituomba radhi sana na kusema hakujua, alirudia zaidi ya mara tatu akituomba radhi kisha Yule kijana akatuambia tuhamishe mizigo kwenye gari lile alilokuja nalo na kisha akasema tumuachie ufunguo Yule polisi ili akalifanyie matengenezo na tutalipitia hapo kituoni baada ya siku mbili! Hivyo tulimtoa Janeth na kwa bahati alikuwa amepitiwa na usingizi na kumhamishia kwenye ile gari na kisha Yule dereva ambaye baadae alijitambulisha anaitwa Jack akatupeleka mpaka hospitali ya Milembe na kwa kuwa tayari tulishaunganishwa na daktari pale Janeth akapokelewa!
Hata hivyo baadae tuliambiwa bili ya matibabu itatoka kesho yake na sisi tutafute sehemu ya kupumzika twende tena kesho yake asubuh,
Tulirudi kwa Yule kijana na baadae alinipa simu nikaongea na mkuu wa wilaya ambaye alisema asingeweza kufika pale kwakuwa hakuwepo Dodoma bali alikuwa Mwanza kwenye kikao cha wakuu wa wilaya na waziri wa Tamisemi, alidai hata wakati ule napiga simu ilikuwa ni bahati tu walikua kwenye mapumziko ya chakula, nakumbuka alisema Yule kijana atatupeleka sehemu ya kulala na kisha kesho asubuhi atatufuata tena kutupeleka hospitali na tusisite kumjulisha chochote,
Kwa bahati Josephine nae alifika kesho yake na tukakutana hospitali na pesa ya awali ya matibabu ilikuwa laki 4 na 70 hivi nakumbuka alilipa Josephine yote na hatukuona ulazima wa kumsumbua tena mkuu wa wilaya, kama ujuavyo huku nyumbani tulikuwa tumewaachia majirani tu na hatukuwa na jambo la kufanya pale hospitali daktari alisema tunaweza kumuona mara moja tu kwa mwezi na si zaidi, na kwahiyo hatukuwa na sababu ya kukaa Dodoma, tuliwasiliana na mkuu wa wilaya tena na akatupatia pole sana akasema bado hajarudi ila atamtembelea Janeth hospitali kwa niaba yetu, basi tulipitia gari letu pale kituoni na ilikua bado kidogo nilisahau!
“kwanini?”
nilimuuliza mzee nikiwa nimehamasika
“hawakubadilisha taa tu, walibadili vifaa vyote mpaka matairi na kulipiga rangi kwa upya!”
alisema mzee Tito akicheka
‘pamoja na hayo walituwekea mafuta full tenki ambayo nilifika nayo Dar bila kuongeza!
Alimalizia mzee Tito huku akinitazama usoni kwa macho kama yaliyokuwa yanauliza
“kwani wewe unasemaje?”