Si kwa sababu ni mgombea urais anayependwa sana.
Wala kwamba ni mwanasheria nguli.
Ama kutokana na jinsi anavyojenga hoja.
Au mvuto mwingine wowote alionao! Hapana.
Bali ni kwa sababu mida hii alitakiwa awe kaoza kaburini, lakini Mungu akampandisha tokea huko!
Alitakiwa awe kanyamaza lakini bado anasema!
Alitakiwa awe kasahaulika, lakini ndiye anayeongelewa kuliko wengine wote.
Ukisoma Neno la Mungu utaona mfanano wa karibu na kisa cha ndugu yetu mpendwa.
"Basi watu wengi katika wayahudi walipata kujua ya kuwa yeye yuko huko, nao wakaja, si kwa ajili yake Yesu tu, ila wamwone na Lazaro, ambaye Yesu alimfufua.
Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri la kumuua na Lazaro naye; maana kwa ajili yake wengi katika wayahudi walijitenga, wakamwamini Yesu"
(Yoh.12:9‐11)
Sasa tujihoji, kwa nini watu walimiminika kwa Yesu baada ya tukio lile?
Jibu, hawakutaka kumwona Yeye pekee, ila na Lazaro aliyemfufua.
Kwa hiyo kumbe kuishi kwa Lazaro kuliutangaza utukufu wa Mungu. Na ndiyo sababu wakuu wakapendekeza Lazaro naye auawe haraka.
Nilipokumbuka ndiyo maana nikasema; nikimwangalia Lissu nauona utukufu wa Mungu.
Ndiyo kisa cha mimi na wengine tunatamani kumwona siyo yeye Lissu tu, lakini na huyo Mungu wake aliyemwokoa!