Umeandika nini? Hakuwa Tanzania una maana gani? Mtu kama hakuwa mtu mwema watu wangemlilia leo?
Kama alikuwa mwema au mbaya, kwa sasa hayo yapo mbele ya Muumba wake. Sisi tunamsindikiza tu aende kwa amani kule ambako kila mmoja wetu ataenda.
Lakini tutambue kuwa kila mtu, hata awe mbaya vipi, kuna watakaomlilia. Kuna msemo wa Kiswahili, 'baniani mbaya kiatu chake dawa', maana yake hakuna aliye mbaya akakosa uzuri. Jambazi anaweza kuwa mbaya kwa anaowaibia, lakini akawa mwema kwa watoto wake maana akiiba, alichoiba anaenda kukitumia kwa manufaa ya familia yake.
Wapo wanaohuzunika kwa sababu kweli wameguswa na mazuri ya marehemu. Wapo wanaohuzunika kwa sababu hawana uhakika na manufaa waliyokuwa wanayapata kwenye utawala wa Magufuli, kama watayapata tena, na hawa ni wengi sana.
Wapo waliomchukia kwa sababu aliwatenda isivyo haki. Lakini pia wapo waliomchukia kwa sababu uwepo wake uliwazuia kupata manufaa binafsi, yawe ya halali au ya dhuluma.
Ukweli unabakia pale pale, katika misiba mikubwa mitatu tuliyoipata - Mwalimu, Mkapa na Magufuli; hakika Mwalimu alililiwa na wote, japo hakuwa madarakani. Sikuwahi kumsikia hata mmoja akinena kuwa, ni aheri Mwalimu ametutoka. Mwalimu kabla ya kifo chake alisema, 'najua watanzania watanililia sana, lakini nami nitawaombea kwa Mungu'. Kwa matendo na unyofu wake, alikuwa na uhakika atamfikia Mungu.
Mwalimu alipostaafu, alipewa zawadi mbalimbali na taasisi mbalimbali lakini ama alizikataa ama alizipokea na kuzigawa. Nakumbuka alipokea trekta toka JKT kisha akakipatia kijiji ili wawe wanasombea maji. Kwa maneno yake alisema, 'Biblia inasema, ni aheri kwa ngamia kupenya tundu la sindano kuliko tajiri kuuona ufalme wa mbingu. Mnanipa vitu vyote hivi, mnataka niwe tajiri? Mimi nautamani ufalme wa mbinguni'.
Msiba huu ndiyo msiba pekee ulioonesha hali ambayo siyo ya kawaida kabisa, siyo hali ya kawaida mtu akifariki. Kuna watu wamesema wazi kabisa kuwa wanamshukuru Mungu amezisikia sala zao. Maana yake walikuwa wakiombea asiwepo Duniani!!!
Siwezi kusema neno hasa. Wala siwezi kuwalaani watu hao maana huna uhakika walipitia kwenye tanuru la namna gani wakati wa utawala wa Magufuli.
Huwezi kuelewa magumu aliyopitia Tundu Lisu, ni yeye na Mungu wake ndio wanajua.
Huwezi kujua wala kuhisi simanzi na magumu waliyoyapitia wazazi, wadogo na ndugu wa karibu wa Ben Saanane. Ni Mungu pekee yake ndiye anajua.
Ni vigumu kujua mateso ya nafsi waliyopitia wanafamilia wa Azory, yule diwani aliyeuawa na wanaCCM katili Dar, yule diwani aliyeuawa Kilosa, na yule mwenyekiti wa CHADEMA liyekatwa shingo kwa msumeno kule Arusha.
Fikiria mtoto wako, kaka yako, baba yako, mdogo wako - anauawa kwa kutakatwa na msumeno. Halafu hawa wote wakaambiwa kuwa ndugu yenu ameuawa na wanaCCM, na wauaji hawataguswa kwa sababu ndiyo watawala. Je, watu hawa watasikitikia vifo vya watawala ambao wanaamini walikuwa na mkono kwenye kifo cha ndugu yao? Hawa si ajabu, wakapiga magoti na kusema, 'Bwana tunakushukuru, kwa kuwa sauti ya mtu mnyonge imepata thamani mbele yako Bwana wa majeshi'.
Lakini hakika, ninyi nyote mlioguswa na magumu ya utawala wa marehemu kwa kuonewa, thawabu yenu ni kubwa mbinguni kama mtaweza kunena katika nafsi zetu, 'hakika bwana tuliumia na kuhuzunika sana lakini kwa kuwa wewe Yesu Kristu Bwana wetu, hata wakati ukiyandea mauti, ukiwa juu ya msalaba ulisema, Baba uwasamehe kwa kuwa hawajui watendalo. Basi nasi kwaajili ya neno hili, tunasema tumeyasamehe yote maana ni katika kusamehe, nasi tunasamehewa.