Mwanasheria Mkuu wa Serikali atoa ufafanuzi kuhusu nafasi ya Makamu wa Rais
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, ametoa ufafanuzi wa kisheria kuhusu lini nafasi ya Makamu wa Rais inakuwa wazi, akisema tarehe rasmi ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Makamu wa Rais ni
Septemba 4, 2026, kwa mujibu wa Ibara ya 149(2) ya Katiba, baada ya Rais kukubali tarehe hiyo. Amesema kwa maana hiyo, aliyekuwa Makamu wa Rais ataendelea kuwepo madarakani hadi Septemba 4, 2026, huku akieleza kuwa kumekuwa na upotoshaji mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu suala hilo.
Johari amesema Ibara ya 50(4) inaweka utaratibu wa kujaza nafasi ya Makamu wa Rais endapo nafasi hiyo iko wazi kutokana na kifo au kujiuzulu. Hata hivyo, amesema katika kutafsiri Katiba, vifungu vyake vinapaswa kusomwa kwa pamoja kwa kuzingatia
Doctrine of Harmonious Construction, yaani msingi wa kutafsiri vifungu kwa namna inayoviweka katika uwiano. Amesema kwa msingi huo, suala la nafasi ya Makamu wa Rais haliwezi kuangaliwa kwa Ibara ya 50(4) pekee.
Ameeleza kuwa ili kubaini sifa za mtu anayestahili kushika nafasi ya Makamu wa Rais, ni muhimu pia kuangalia Ibara ya 47(4), inayosema mtu hatateuliwa
kugombea au kushika nafasi hiyo bila kuwa na sifa zinazotakiwa. Johari amesema hivyo anapingana na tafsiri kwamba Ibara hiyo inahusu kipindi cha kugombea pekee, akisisitiza kuwa kifungu hicho kimetaja wazi pia suala la kushika nafasi ya Makamu wa Rais.
Johari ameongeza kuwa Ibara ya 47(4) inaweka sifa za mtu anayestahili kuteuliwa kugombea au kushika nafasi ya Makamu wa Rais, ikiwemo kuwa raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano, kuwa na umri wa miaka 40, kuwa mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa na kuwa na sifa za kuwa Mbunge au Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi. Amesema mtu akipoteza sifa hizo, ikiwemo uraia wa Tanzania, suala hilo linaweza kuathiri nafasi yake.
Soma kuhusu > Dkt. Emmannuel Nchimbi afukuzwa uanachama wa CCM
Amesema kiti cha Makamu wa Rais kinaweza kuwa wazi kwa sababu mbalimbali, ikiwemo
muda wa madaraka kumalizika, kifo, kuapishwa kuwa Rais, kutiwa hatiani kwa kosa la jinai, kuondolewa madarakani au kuacha kushika nafasi hiyo kwa mujibu wa Katiba. Johari amesema kipengele hicho cha mwisho kinabeba mazingira mengine yanayoweza kumfanya mtu kushindwa kuendelea na nafasi hiyo.
Kwa upande mwingine, amesema kipengele cha Ibara ya 47(4) kinapaswa kusomwa pamoja na Ibara ya 50(4), akieleza kuwa mtu akipoteza sifa za kushika nafasi ya Makamu wa Rais, kiti hicho kinaweza kuwa wazi. Johari amesema kuvuliwa uanachama wa chama cha siasa ni miongoni mwa mazingira yanayoweza kuathiri sifa hizo, na kwamba vifungu hivyo vinapaswa kutafsiriwa kwa pamoja.
Ametolea mfano uteuzi wa aliyekuwa Makamu wa Rais,
Philip Isdor Mpango, akisema mwaka 2021 Rais Samia Suluhu Hassan aliwasilisha jina lake Bungeni kwa mujibu wa Ibara hiyo hiyo ya 50(4), licha ya mazingira hayo kutotajwa moja kwa moja katika kifungu hicho. Amesema Bunge lilimthibitisha Mpango Machi 30, 2021, na siku iliyofuata, Machi 31, 2021, akaapishwa na Jaji Mkuu.