Kuna Mzee mmoja alikuwa anafanya kazi serikalini. Alikuwa mtu mkubwa kicheo.
Akawa kapandishwa cheo kikubwa kabisa kazini kwake.
Akapewa nyumba nzuri sana Oysterbay.
Karibu kabisa na ubalozi wa Marekani.
Watoto wake wakafurahi sana. Wakaona wanaenda kuhamia Oysterbay, tena karibu kabisa na Ubalozi wa Marekani.
Lakini, yule Mzee hakuwa mtu wa kupenda makuu.
Alisema anapapenda pale alipokuwa anaishi, maana pana sehemu kubwa, tena amezoeana sana na majirani. Wanaishi vizuri.
Zaidi, hakuona sababu za kuhamahama nyumba za serikali kwani alikuwa anakaribia kustaafu.
Watoto wake wakakasirika sana.
Wakasema Baba unaacha nafasi ya kuhamia Oysterbay, tena mtaa wa Laibon ukae jirani na rais Mwinyi na ubalozi wa Marekani?
Baba yao akasema ameshaamua.
Basi muda kidogo tu, ubalozi wa Marekani ukapigwa bomu. Ile nyumba ikapasukapasuka vibaya sana kwa sababu ilikuwa karibu sana na ubalozi wa Marekani.
Kama yule Mzee angehamia pale, familia yake ingeweza kuumia vibaya sana.
Watoto wale wakamuona yule mzee kama alikuwa na uwezo wa kuona yajayo.
Unaweza kutamani kitu kizuri, ukasononeka kukikosa.
Kumbe, usalama wako unakuja unapokikosa hicho kitu.
Ukikipata unapata balaa.