SoC04 Harakati ya Kuwawezesha Watoto na Familia za Mitaani

SoC04 Harakati ya Kuwawezesha Watoto na Familia za Mitaani

Tanzania Tuitakayo competition threads
Joined
Jun 25, 2023
Posts
45
Reaction score
32
Utangulizi
Wapo watoto wa mitaani lakini pia zipo familia za mitaani. Hizi ni familia zilizokumbwa na majanga asilia kama vile mafuriko, matetemeko ya ardhi, njaa, ukame, umaskini, magonjwa, vimbunga, na kadhalika lakini pia zilizokumbwa na majanga ya kibinadamu kama vile migogoro binafsi na ya kifamilia, changamoto binafsi na za kifamilia, kuyumba kiuchumi, vita, na kadhalika.

Jua, mvua, mawingu na upepo vyote huishia kwenye miili ya watoto na familia hizi; baada ya majanga haya kusababisha watoto na familia za mitaani kukosa haki za kibinadamu ambazo ni mahitaji muhimu ambayo ni:-​
  1. Chakula​
  2. Mavazi na​
  3. Makazi​

Mara nyingi; watoto na familia za mitaani, huitwa wa mitaani kwasababu usiku ndipo hutafuta mahali pa kulala, ambapo mahali hapo panaweza kuwa chini ya madaraja, kwenye vituo vya usafiri, sokoni, nje ya maduka na kwingineko; kisha asubuhi na mchana kutwa mpaka jioni hushinda mitaani wakizunguka huku na huko; kuombaomba, kutafuta vibarua lakini mbaya zaidi wengine hujikita kwenye uhalifu kama vile wizi, matumizi ya dawa za kulevya, biashara haramu, na kadhalika.

Watoto wa mitaani na familia za mitaani, uhusisha watu wa rika zote wasio na makazi maalum; kuanzia watoto wa miaka miwili na mitatu mpaka watu wazima kasoro watoto wachanga na wadogo sana, ambao wakionekana kuzagaa zagaa wakiwa wametupwa au kutelekezwa; huwa ni rahisi jamii kuwakimbilia na kuwapeleka mahali salama kama vile katika vituo vya watoto yatima.

Hawakupanga, hawakuchagua, hawakutaka wala hawakupenda kuwa watoto wala familia za mitaani; walijikuta mitaa ndiyo imewapokea, imewalea, imewateka na kuwafanya baba na mama zao, ndugu, rafiki na jamaa zao. Mitaa imewaathiri watu hawa mithili ya dawa za kulevya, hata kuwafanya wao kwa akili zao washindwe kutoka katika wimbi la watoto na familia za mitaani.

Makombo ya vyakula, mabaki ya vyakula, viporo, ukoko na vyakula visivyostahili ndivyo vyakula vyao, huku mavazi wanayovaa yakiwa chakavu, yaliyochanika na machafu yasiyostahili.

Jukumu la kuwasaidia watoto na familia za mitaani si jukumu la serikali au chama tawala, hili ni jukumu la kila Mtanzania kwa moyo mkunjufu kuwasaidia watu hawa kwa namna anavyoweza.

Mtanzania mwenzangu; tunapata wapi ujasiri wa kula chakula na kusaza kisha kumwaga, au kujaza mavazi yasiyovaliwa kabatini huku yupo Mtanzania mwenzetu ambaye hajui atakula nini au atavaa nini?

Hawakupenda kuwa kama walivyo, hawakupenda kukosa mahitaji ya mioyo yao, hawakupenda mioyo yao kuraruriwa kwa maumivu makali wanayoyapata sasa; lakini MUNGU ANAYEPANGA NDIYE MWAMUZI WA YOTE na Aliwaweka kwa makusudi, kwani hakuna tajiri kama asingekuwepo mtu wa hali ya chini.

Maumivu wanayoyapitia yanafanana na mtu aliye peku asiye na viatu, atembeaye juu ya miiba mikali iliyochongoka sana, anayesikia maumivu makali kwenye nafsi yake, apazaye sauti kulia; si kilio cha uchungu, bali kilio cha maumivu ya moyo lakini sauti yake haisikiki kwani kila mtu amemgeuzia kisogo. Hujitaidi kupapasa kwa mikono ili kujipambania atoke eneo hilo lakini pia mikono huishia kuchomwa na miiba, anapojaribu kukaa au kulala ili apumzike, makalio na mwili mzima pia huchomwa na miiba.

Nyakati za usiku hujificha kwenye madaraja na popote wanapopata nafasi, hulia machozi ya damu huku wakificha nyuso zao kwenye mashati yao na nguo zao zilizoraruka, kisha asubuhi hufuta machozi yao, huingia tena mtaani kwa nyuso zenye tabasamu bandia zilizoficha machozi, maumivu na sauti za vilio kwenye mioyo ya watu hawa.

Kwa muda mrefu sana sauti za watu wengi zimepazwa huku mawe mbalimbali yakitupwa gizani kuhusu kuwasaidia watoto na familia za mitaani; kila mtu akimwangalia mwenzake, labda huyu ndiye anayehusika kuwasaidia watu hawa, hali iliyopelekea kukosekana kwa msaada wa moja kwa moja na wa kudumu kwa familia na watoto wa mitaani.

Kupitia andiko hili, naomba nitume salamu zangu na maombi yangu yanayowalenga UONGOZI WA JAMII FORUMS na JAMII FORUMS kwa ujumla moja kwa moja; kuwasaidia watoto wa mitaani pamoja na familia za mitaani.

Kama jina lake lilivyo, JAMII FORUMS hujikita katika masuala mbalimbali ya KIJAMII; Siasa, Uchumi, Elimu, Afya, Ustawi wa Jamii, Maendeleo, Ulinzi, Usalama, na kadhalika.

JAMII FORUMS ina utajiri wa mamilioni ya wadau kutoka nchini Tanzania, barani Afrika na duniani kote, huku wadau wake wakiwa ni watu binafsi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na za mataifa mbalimbali, taasisi, mashirika, balozi, wanamichezo, wasanii, viongozi pamoja na wadau muhimu ambao ni wanachama (members) wa JAMII FORUMS.

IMG_20240505_154710.jpg

(Chanzo Picha: Jamii Forums)

Kwa maelezo haya, ni dhahiri kuwa UONGOZI WA JAMII FORUMS, JAMII FORUMS YENYEWE PAMOJA NA WADAU WA JAMII FORUMS, tunao uwezo wa kuanzisha HARAKATI YA KUWAWEZESHA WATOTO NA FAMILIA ZA MITAANI; ili waweze kutoka katika hali hii ngumu wanayoipitia sasa nchini Tanzania.

Harakati hii inatakiwa kuwa katika hatua nne kama ifuatavyo:-

Hatua ya kwanza, ni kuanzisha Street-Based Rehabilitations. Hivi ni vituo maalum ambavyo vitahusika na hatua ya kwanza ya kuwarejesha kisaikolojia kwanza, kwani wapo wengine ambao tayari kisaikolojia wameathiriwa na maisha hayo ambayo ni vigumu kuyaacha. Hawa ni watoto na familia za mitaani ambao wanatakiwa waweze kuishi maisha ya kawaida; kupitia mafunzo na huduma stahiki wanazohitajika kupewa kisaikolojia. Hatua hii inahusisha wote; watoto, vijana na watu wazima waliotoka mitaani.

Hatua ya pili, ni kufanya tathmini za familia, asili na chimbuko la kila mmoja, ili kwa wale ambao familia zao zipo ila waliondoka nyumbani kwa makosa, utukutu, migogoro, kufukuzwa na mambo kama hayo waweze kupatanishwa tena na familia zao. Hatua hii inahusisha wote; watoto, vijana na watu wazima waliotoka mitaani.

Hatua ya tatu, ni kuwatenga watoto wadogo zaidi wanaotakiwa kuanza shule na kupata haki za watoto ambao familia zao hazijulikani; kisha kuwapeleka katika vituo maalum kwa ajili ya uangalizi maalum kama vile vituo vya watoto yatima. Hatua hii itahusisha watoto waliotoka mitaani.

Hatua ya nne, ni kuanzisha Art Spaces and Cultural Tourism Enterprise(s), ambazo zitawasaidia wale ambao tayari wamekaa sawa kisaikolojia na tayari wamekubali kwa 100% kuacha maisha ya mitaani; ili waweze kujikita katika sanaa zinazokuza na kueneza Lugha ya Kiswahili na Asili ya Kiswahili; uandishi, uchoraji, uimbaji, ufumaji, uigizaji, michezo mbalimbali, upishi, na sanaa nyingine nyingi kisha kuuza na kufanya maonesho hasa kwa wageni lakini pia wenyeji (Cultural Tourism Programs). Baada ya muda kidogo itatakiwa ifanyike tathmini wale ambao tayari kiuchumi wameweza kupiga hatua na wanataka waende wakajitegemee, kisha kuwaruhusu wakafanye hivyo ili kuendelea kuwasaidia wengine zaidi. Hatua hii itahusisha vijana na watu wazima waliotoka mitaani.

Hitimisho
Tanzania Tuitakayo, si jukumu la serikali pekee, bali ni jukumu langu mimi, sisi, wewe, nyinyi, yeye, wao na yule.​
 
Upvote 3
Jukumu la kuwasaidia watoto na familia za mitaani si jukumu la serikali au chama tawala, hili ni jukumu la kila Mtanzania kwa moyo mkunjufu kuwasaidia watu hawa kwa namna anavyoweza.
Nakubaliana nawe, jukumu la kila mmoja.
Hawakupenda kuwa kama walivyo, hawakupenda kukosa mahitaji ya mioyo yao, hawakupenda mioyo yao kuraruriwa kwa maumivu makali wanayoyapata sasa; lakini MUNGU ANAYEPANGA NDIYE MWAMUZI WA YOTE na Aliwaweka kwa makusudi, kwani hakuna tajiri kama asingekuwepo mtu wa hali ya chini
Tuwe makini, tusije kusema amepanga Mungu, kumbe Mungu mwenyewe ametuachia wanadamu tujisahihishe na kujiwekea mifumo inayofaa. Likiamuliwa duniani Mbingu inatia tiki✔


Hatua ya kwanza, ni kuanzisha Street-Based Rehabilitations. Hivi ni vituo maalum ambavyo vitahusika na hatua ya kwanza ya kuwarejesha kisaikolojia kwanza, kwani wapo wengine ambao tayari kisaikolojia wameathiriwa na maisha hayo ambayo ni vigumu kuyaacha. Hawa ni watoto na familia za mitaani ambao wanatakiwa waweze kuishi maisha ya kawaida; kupitia mafunzo na huduma stahiki wanazohitajika kupewa kisaikolojia. Hatua hii inahusisha wote; watoto, vijana na watu wazima waliotoka mitaani.
Safi, akili kwanza kama nchi za Scandinavia wametumia mbinu hii ili kuondoa tatizo la kutokuwa na mahala pa kulala.

Hitimisho
Tanzania Tuitakayo, si jukumu la serikali pekee, bali ni jukumu langu mimi, sisi, we
Perfecto!, hujaacha kitu katika hitimisho.
 
Asante sana ndugu yangu
Nakubaliana nawe, jukumu la kila mmoja.

Tuwe makini, tusije kusema amepanga Mungu, kumbe Mungu mwenyewe ametuachia wanadamu tujisahihishe na kujiwekea mifumo inayofaa. Likiamuliwa duniani Mbingu inatia tiki✔



Safi, akili kwanza kama nchi za Scandinavia wametumia mbinu hii ili kuondoa tatizo la kutokuwa na mahala pa kulala.


Perfecto!, hujaacha kitu katika hitimisho.
 
Back
Top Bottom