Wanajamvi,
Kama heading ya uzi huu inavyojieleza, ni kwamba hakuna haja ya upinzani ku panic kabisa! Hayo ni ya wana ccm kuyafanya, na kamwe siyo upinzani. Wao ccm, kwani wamezuiwa siasa? Wamekuwa wakifanya kampeni toka awamu hii iingie madarakani. Sasahivi, wananchi kama ni kuona na kusikia, basi wameshasikia na kuona vya kutosha kupitia kwa wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi, makatibu uenezi na katibu mkuu wa ccm, ndo wamekuwa wakitamba siyo tu kwenye vyombo vya habari vya binafsi ambavyo viliingiwa na woga, bali hata Tv yetu ya Taifa TBC, ambayo inawndeshwa kwa kodi zetu wote bila kujali vyama vyetu, wala itikadi zetu! Kwahiyo wao ccm ndo wanaotakiwa kupanic maana wanarudia yale yale ambayo wananchi wamelazimika baada ya kulazimishwa, wameshayaona na kuyasikia kwa miaka minne mfululizo...Ni wazi sauti nyingine zikija watakuwa na shauku kubwa. Hiyo ni kawaida kwa hulka ya mwanadamu. Ni kiumbe mwenye kutafuta habari kila uchao! It is a human psychology.
Sasa nimeona watu wanasumbuka sana kuhusiana na suala la nani atakuwa mgombea kwa upande wa upinzani. Vyama vya ACT-Wazalendo, pamoja na kile chama kikuu cha upinzani nchini, yani CHADEMA vikizungumziwa na kuhusishwa na wagombea wawili maarufu sana, yani Tundu Antipas Lissu, sambamba na Bernard Membe, ambaye inasemekana yumo ACT-Wazalendo.
Tathimini rahisi, inaonyesha wazi kabisa kuwa ACT-Wazalendo, ni chama mbadala cha CUF. Na ndiyo kinategemewa kumsimamisha mgombea kule Zanzibar, kama sikosei, mgombea huyo ni Maalim Seif Sharif Hamad. Kwahiyo kwa upande huo wa kushirikiana inapokuja kwa upande wa Zanzibar, ni suala la kawaida tu. Na ndiyo maana halitabadilika, kwasababu ACT-Wazalendo wameisha wafuta.
Na kwa upande wa bara, mambo yalikuwa ni kati ya Lipumba, na mgombea wa CHADEMA, ambapo CHADEMA walikuwa ndo wanaotoa mgombea wa urais kwa upande wa bara. Last time Lowassa, kabla ya hapo Slaa nk.
Lakini tofauti iliyoko kwa sasa, ni Bernard Kamilius Membe. Huyu yeye ndiye anayeleta mjadala mkali. Ni mjadala ambao unachochewa sana na wana ccm wenyewe! Nadhani kisaikojia, ni umbea kwasababu yao yamewashinda! Wanatafuta wa kujifananisha nao! kwasababu wao wameshamaliza upande wao na watu kuzimwa hata nafasi ya kuchukuwa fomu za kugombea kwenye nafasi ya urais, yani fomu zikafichwa na katibu mkuu akasema wazi kabisa! Na ndiyo matokeo yake Bernard Membe kujitoa. Huyu tayari ana watu wengi tu ndani ya ccm wanaoona ameonewa na ccm. Jambo lilokuwa ni kinyume hata na katiba yao ya chama. Pia woga unaonyesha udhaifu mkubwa! Hata JK mwenyewe tuliyemuita “dhaifu”, yeye alikubali kina Shibuda wakajitosa na kuchukuwa fomu! Woga wa sasa, unaonyesha kutokukubalika ndani ya chama!
Kwa maoni yangu, hata kama vyama hivi vikiamuwa kuwasimamisha wagombea wao, bado idadi ya kura watakazozipata, zitawazidi ccm. Huu ni ukweli mchungu kwa ccm na ndiyo maana wanahaha sana kuleta mijadala ya kuwachanganya na kutaka kuleta migawanyiko! Lakini hili halitafanya kazi wala kufanikiwa, maana siku ya kufa nyani, miti yote huteleza! Kwanza kuna kura nyingi sana za wana ccm ambao hawakuona umuhimu wa Lissu kutaka kuuwawa! Na hata matendo ya serikali na bunge, yameonyesha wazi kabisa, wananchi wanajuwa kwasababu kwa miaka hiyo minne, wamekuwa wakilishwa propaganda za upande mmoja!, na sasa mahakama nayo inaweza kutupiwa macho pamoja na polisi.
Kule Kenya, hili liliwahi kutokea pia, na ndipo hapo chama cha KANU kilipoanguka chali! Kama sikosei, mara ya pili, ilibidi wafanye muungano, kwasababu mara ya kwanza, kura zao zote, ziliwashinda KANU, lakini wao walikuwa hawajaungana, na hivyo KANU kubakia madarakani. Sisi hapo tunaweza kurekebisha.
Kwa upande wa Tanzania, siasa zetu ni za tofauti kidogo na zile za Taifa la Kenya. Sisi kwanza siasa za ukabila siyo kivile! Pamoja na kwamba ccm wamejitahidi sana kuzitumia dhidi ya upinzani, Lakini hazijafanikiwa, na ndiyo maana upinzani ulipata nguvu na kuongeza wabunge wengi, na umaarufu mkubwa, sana hadi ccm kutishika! Na hata wengine wakisema uchaguzi uliopita, kama siyo kwa “goli la mkono”, ambalo Nape, January pamoja na Kinana, walifanya kazi ya ziada, basi leo hii ccm ingekuwa ndo upinzani.
Sasa miaka mitano ndo hiyo imeshakata, Kinana ni juzi tu kaomba msamaha, ni baada ya Nape na January kufanya hivyo! Lakini nao walifanya kwa shingo upande tu. Kwasababu, nguvu za mwenyekiti ni kubwa mnoo! Na wao alifanya marekebisho zaidi. Na ukizingatia yeye ndo mkuu wa serikali, na hao kina Nape na January, wamekulia humo ccm, hivyo hawana ujanja, siasa ndo maisha yao! Na hivyo wamekuwa kama “mateka” wa kifikra na hata kimwili! Hao nao sura zao halisi zingeonekana kama wengine wangeruhusiwa kuchukuwa fomu ya kugombea urais ndani ya ccm. Hata mzee Makamba naye ni hivyo hivyo tu, wengi tulimsikia kwenye zile tape walizodukuliwa wakati wakimsema mwenyekiti wao! Mzee Mkapa yeye hata kama alidukuliwa, hawakutuhubutu kuweka wazi kama hao wengine, lakini naye alizungumzia umuhimu wa kuwa na tume huru ya uchaguzi nchini! Hilo kina kitu linaelezea kabisa! Siyo kauli ya bahati mbaya tu.
Kura za ccm ndizo zitakazogawanywa, cha msingi, kuwepo na makubaliano baina ya wapinzani mapema iwezekanavyo! Ninayo imani kwamba, uchaguzi huu utatuletea viongozi wanaowakilisha kada zote za wananchi pamoja na masilahi yao! Yale ya moja kwa moja kwenye jamii, na pia kama watanzania kwa ujumla! Hili amelizungumzia vyema sana Sheick Ponda kwenye ule waraka wa “Shura ya Maimamu”, ambapo walizungumzia kuhusu upatikanaji wa katiba mpya baada ya uchaguzi mkuu! Lakini pia umuhimu wa kuweka kanuni za kipindi cha mpito, ili tupate serikali itakayotuongoza kuelekea kwenye katiba mpya ya wananchi kutoka kwa wananchi.
Hapa ina maana kwamba kuna mengi yanayowaunganisha watanzania dhidi ya ccm kuliko yale yanayowatenganisha! Hayo ya kututenganisha, ni machache sana ambayo siyo lazima kupewa kipaumbele! Maana yenyewe ni ya kuwagawanya wapinzani ili kuwadhibiti! Kuwagawanya watanzania, ili kuwaondolea sauti na umoja wa kudai haki, uhuru na maendeleo ya nchi! Yani “devide and rule”. Kwetu ni tofauti kabisa na kule Kenya ambapo siasa za ukabila ndizo zinawaumbuwa na zimekuwa zikifanya hivyo kwa muda mrefu. “Coalitions”, ama miungano yao, ni ya misingi ya kikabila. Mfano Kaleinjin na Wakikuyu, Vs Waluo na makabila mengine madogo nk. Na Kwahiyo sisi tuna nafasi nzuri zaidi kwa wapinzani kuiangusha ccm, na bado tukapata serikali itakayowatumikia wananchi vyema, na kwa mujibu wa katiba ya nchi! Na hao wakifanya uzembe, tuwe na nafasi na uwezo wa kuwandoa madarakani kwenye sanduku la kura kwa mujibu wa katiba.
Siyo siri, chama cha CUF, kilikuwa na wanachama wengi wa maeneo ya mwambao wa Pwani! Na hivyo wengi kuwa waislam. Majimbo mengi ya waislam, ni hao CUF waliyabeba, lakini mengine machache, ccm wamekuwa wakitumia ujinga na umasikini kuendelea ku watawala. Ni tofauti na baadhi ya sehemu na mikoa ambako wameshaifuta kabisa ccm kwenye misamiati yao. Hata hivyo, kama nilivyosema hapo awali, ACT-Wazalendo ndiyo ambao sasa wameichukuwa nafasi hiyo ya chama cha CUF. “It has simply been replaced”, haswa baada ya Maalim Seif kuondoka huko, na
Zitto kuitumia nafasi hiyo kumsajili.
Sasa endapo ACT-Wazalendo watamsimamisha Membe, nadhani siyo mbaya hata kidogo kwa upande wa CHADEMA na upinzani kwa ujumla!Kwanza kuna malalamiko mengi sana ya uwepo wa udini. Malalamiko ambayo yanaelekezwa kwa utawa wa ccm! Na wala siyo mara ya kwanza! Na ndiyo maana hata CUF ilipata nguvu sana! Malalamiko yao hayajaanza leo chini ya utawala wa ccm! Hawa watu sauti zao lazima zitakuwa zinataka mwakilishi. Hata waislam wale ambao walikuwa hawaipigii CUF kura, na wakawa wanaipigia ccm, basi sasa wataipigia kura ACT-Wazalendo.
Hata wale ccm wasioipenda CHADEMA baada ya kulishwa sumu mbaya na chama chao, wataipigia kura ACT-Wazalendo kumfuata Membe...Maana tunafahamu propaganda za ccm inapokuja kwenye udini na ukabila! Tuhuma zao wenyewe, lakini wamekuwa wakiwasingizia upinzani. Sasa ccm mmetawala toka uhuru, upinzani ndo umeleta shida za waislam toka lini? Hili huwa najiuliza sana wakati ccm inapokuja na mgombea wao huku wakitutajia maendeleo waliyoyaleta, na kujifananisha na upinzani ambao hawajawahi kuongoza nchi. Mbona hawakubaliani na ukweli pia hata umasikini na unyonge ni wao waliowasababushia watanzania? Hili lenyewe, lilitakiwa liwe sababu nzuri kabisa ya kuwa na uchaguzi huru! Maana nani mwingine ambaye ameshafanya “mazuri” zaidi yao tokea December 31st 1961? Nani mwingine ameshawahi kufanya “mabaya”?
Hivyo kwa maoni yangu, ni kweli kabisa kuwa uchaguzi wa huru na haki, utawaondoa ccm madarakani, upinzani uungane, ama usiungane, moto ni ule ule! Membe atakula vichwa vya ccm, chadema nao watakula vichwa vya ccm. Hata yule Sipunda anaweza kula vichwa!
Cha msingi, ni makubaliano yafanyike mapema! Makubaliano ambayo yatahusisha nia ya dhati kabisa ya pande zote mbili! Nia za kuwa na tume huru ya uchaguzi pamoja na katiba mpya ya wananchi kutoka kwa wananchi! Na siyo hii ya mkoloni yenye viraka vya ccm, ambayo inaendelea kutushikia chini kiasi cha kwamba uhuru wetu ukawa mashakani! Waliotufanya wanyonge, ndo hao hao wanaoendelea kuutetea unyonge wetu ili tubakie nao! Unyonge wa watanzania ndiyo sababu kubwa ya wao kuendelea kuwepo madarakani pamoja na umasikini wetu.
Sababu ziko nyingi sana, ila nimeamuwa kuanzia na hizi!
Nguruvi3