Nduguze Ballali waonywa
na Mwandishi Wetu
DADA wawili wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), waliokuwa wamepanga kuitisha mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wiki ijayo, wameonywa kuhusu uamuzi wao huo.
Onyo hilo limetolewa kwao kwa njia ya simu na watu mbalimbali waliowasiliana nao wakiwa Washington, Marekani, uliko msiba wa Ballali ambaye anatarajiwa kuzikwa leo.
Aidha, onyo hilo pia lilitolewa jana kwa njia ya simu na watu waliojitambulisha kuwa ni wasomaji wa Tanzania Daima, ambao walieleza wasiwasi wao wa wazi kuhusu uamuzi wa ndugu hao wa Ballali ambao taarifa za wao kuja kuzungumza na waandishi wa habari ziliandikwa jana na gazeti hili pekee.
"Mhariri, mimi ni msomaji mzuri wa gazeti lako. Ninapenda kukuomba uwafikishie salamu zangu hao dada wawili wa marehemu Ballali. Wasije wakajikuta wakifikwa na matatizo, kwa sababu ya uamuzi wao wa kuitisha mkutano na waandishi wa habari kama mlivyoandika," alisema mwanamke mmoja ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake.
Alipoulizwa ni kwa nini alikuwa akifikiria kuwa ni jambo la hatari kwa kina dada hao kuzungumza na Watanzania kuhusu kile kilichomfika ndugu yao Ballali, msomaji huyo alisema hali ya hewa kisiasa imechafuka, hivyo kulikuwa na uwezekano mkubwa kwa wao kudhurika, hata kabla hawajafanikiwa kuzungumza kile walichokipanga.
Watu wengine wawili waliozungumza na Tanzania Daima nao walieleza wasiwasi kama huo, na mmoja wao akafikia hatua ya kuwataka wanawake hao ambao hivi sasa wako Washington wakiomboleza msiba wa kaka yao, wafikishe kila wanalofahamu kuhusu mazingira ya kifo hicho cha Ballali kupitia mtandao wa intaneti.
"Mhariri naomba uwataarifu dada zake Ballali kutothubutu kuzungumza na waandishi wa habari hapa Dar es Salaam. Kama wana lolote la kusema kuhusu mazingira ya kifo cha ndugu yao, hawana budi kufanya hivyo kwa njia ya mtandao ambao katika siku za karibuni, imekuwa njia muafaka zaidi na salama kuitumia kufikisha ujumbe," alisema muonyaji mmoja.
Tanzania Daima ilipowasiliana kwa simu na ndugu mmoja wa Ballali aliyeko Washington katika msiba wa gavana huyo wa zamani wa BoT na kumweleza kuhusu wasiwasi huo, naye alikiri kupokea simu kadhaa kutoka kwa watu mbalimbali waliosoma gazeti hili hapa nchini au kwa njia ya mtandao wa intaneti.
"Hata sisi hapa tumepokea simu nyingi zikitutahadharisha kuhusu hatua hiyo ya kuzungumza na waandishi wa habari. Kwa hiyo suala hilo bado linajadiliwa na uamuzi wa kuzungumza au kutozungumza na waandishi wa habari utaangaliwa na ikibidi unaweza ukabadilishwa," alisema.
Kuhusu uamuzi wa Ballali kuzikwa Washington, ndugu huyo wa Ballali alisema hata wao walifikia hatua ya kukubaliana na uamuzi wa yeye mwenyewe kutaka akifa azikwe huko kutokana na kuchafuka kwa jina lake, kutokana na kuhusishwa kwake na tuhuma mbalimbali za ufisadi.
Mwanafamilia huyo juzi aliieleza Tanzania Daima kwamba, Ballali alifikia uamuzi huo wa kuzikwa Marekani, kutokana na kufadhaishwa na namna jina lake lilivyokuwa likihusishwa na tuhuma nzito za ufisadi.
"Yeye mwenyewe ndiye aliyeamua azikwe huku Washington. Siku zote amekuwa akitueleza namna alivyokuwa akifadhaishwa sana kutokana na kuchafuliwa kwa jina lake, hata baada ya kuitumikia nchi yake kwa juhudi kubwa, moyo mkunjufu na kwa uadilifu wa hali ya juu.
"Alitueleza hapa kwamba hajapata kuiibia nchi yake hata senti moja. Hapo ndipo aliposema akifa angetaka azikwe huku huku Washington na si nyumbani, ambako alihusishwa na kila aina ya tuhuma," alisema mwanafamilia huyo juzi, kauli ambayo jana aliendelea kuisisitiza.
Akizungumza jana, alisema alimuona Ballali kwa mara ya mwisho akiwa hai, Alhamisi ya wiki iliyopita, ikiwa ni siku moja tu kabla ya kufikwa na mauti.
"Nilipomuona Alhamisi iliyopita nilimkuta akiwa amewekewa ‘drip' nyumbani kwake, ikiwa ni kama siku moja au mbili tangu alipotolewa hospitalini, baada ya madaktari kumweleza kuwa walikuwa hawana lolote la kufanya," alisema ndugu huyo.
Aidha, jamaa huyo wa Ballali alikanusha taarifa kwamba, Ballali alikufa baada ya mashine za kumsaidia kuishi kuzimwa kutokana na uamuzi uliofikiwa kwa pamoja kati ya wanafamilia na madaktari.
"Hapana, hakuwa katika mashine wakati akifariki. Alifia nyumbani kwake Washington na si Boston kama ilivyotangazwa na BoT," alisema.
Mbali ya hayo, ndugu huyo wa Ballali aliieleza Tanzania Daima kwamba, mke wa Ballali, Anna Muganda, alikuwa ameomba msiba wa mumewe ufanywe kwa faragha, ukiwahusisha ndugu, marafiki na jamaa zao wa karibu.
Alisema kutokana na hali hiyo, shughuli hizo za msiba zilikuwa zikifanyika pasipo kuwapo kwa shughuli zozote za wazi kama vile kuchukua picha za video au kupiga picha nyingine za kawaida.
Aliieleza Tanzania Daima kwamba, kwa muda wote huo wa msiba, Anna alikuwa mtulivu na alikuwa amezima simu zake zote na hakuwa tayari kuzungumza na vyombo vya habari kabla ya kumzika mumewe leo hii.
Alisema pia kwamba, mama mzazi wa Ballali ambaye hivi sasa anaishi Boko, jijini Dar es Salaam, akiwa na umri wa miaka 94 alikuwa ameshindwa kusafiri kutokana na uzee.
Pamoja na hilo, aliieleza Tanzania Daima kwamba, taarifa walizokuwa nazo ni kwamba Katibu wa Gavana wa Benki Kuu, jana alikuwa amekwenda Boko kuhani, ikiwa ni pamoja na kutoa ubani kwa ajili ya msiba huo.
Habari kutoka Boston na Washington ambazo Tanzania Daima imeshapata kuziandika, zinaeleza kwamba, kulikuwa na taarifa zilizokuwa zikisema kwamba, Ballali alikuwa akisumbuliwa na aina moja ya saratani kwa muda mrefu. Hata hivyo wakati kukiwa na taarifa hizo, baadhi ya ndugu, marafiki na jamaa zake wamekuwa wakieleza wasiwasi wao kwamba, Ballali alilishwa aina fulani ya sumu isiyojulikana, siku kadhaa kabla hajakimbizwa Marekani kwa matibabu. Taarifa hizi za kulishwa sumu zimekuwa zikienea kwa haraka katika maeneo tofauti na baadhi ya watu tayari wametaka kufanyika kwa uchunguzi wa kina kujua ni kitu gani hasa kilikuwa kimempata