Kyoma,
Mengi sijui alikuwa na biashara gani na Mwinyi, lakini utagundua wazi uhasimu wake na Rai ni nini. Rai walikuwa wapambe wa Mkapa kabla ya Mkapa kuwageuka wakati Jenerali alipohoji mambo ya uongozi, uadilifu na Utendaji na kuitwa Banyamulyenge!
Mkapa na Mengi hawaivi na ugomvi au kidonda chao kamwe hakitapona. Ndio maana tangu mwaka jana Mengi amekuwa akimshikia Bango Mkapa left and right kupitia This Day. Mengi ni kweli alikopa pesa za CIS pale BOT, sijui kama kesharudisha zote au bado analipa deni. Mengi anaendelea kujenga maadui wengine zaidi ya Mkapa. Hawa Ajenda 21 wanamkalia kooni, lakini anawapiku. Hivyo mpira bado advantage Mengi.
Sijui uhusiano wa Mengi na jenerali ukoje sasa hivi, lakini wote wawili saa adui yao ni mmoja, Mkapa!
Kishoka
Kusema ukweli, hata mimi undani haswa wa mahusiano kati ya Mengi na Ulimwengu, au Mengi na Mkapa, au Mkapa na Ulimwengu siufahamu. Ninachofahamu ni kuwa Mengi ni Mfanya biashara. Mfanya biashara yeyote lengo lake ni kupata faida. Njia inayotumika kupata faida, inatofautiana kutokana na asili au maadili ya Mfanyabiashara mwenyewe. Wengine wanaiba, wanafanya biashara haramu, na wengine biashara halali, nakadhalika ilimradi wanapata faida. Sijuhi Mengi yuko katika kundi gani, ila nijuacho ni kuwa, Mfanya biashara yeyote anapoingiliwa katika mkondo wa kupata faida, lazima ajibu mapigo.
Mkapa ni Mwanasiasa. Kama ilivyo kwa Mfanya biashara, Mwanasiasa yeyote lengo lake kuu ni kupata madaraka. Wengine wanaiba kura, wanatumia mtutu wa Bunduki, wanatembeza rupia, au ubabe, au kujipendekeza na kujidhalilisha utu wao, ili wapate madaraka. Na wengine (wachache, kama wapo) wanapata madaraka kwa njia halali. Unaweza kumuweka Mkapa katika kundi utakalo, lakini kinachojulikana ni kuwa, mwanasiasa yeyote anapoingiliwa au kutekenywa wakati anapotafuta au akiwa madarakani, lazima ajibu mapigo.
Ingawa aliwahi kushika nyazifa mbali mbali, Kwa maoni yangu, nadhani Ulimwengu ni Mwandishi wa habari zaidi kuzidi alivyo Mwanasiasa. Waandishi wa habari wana kazi kubwa na pana katika jamii, lakini moja wapo, ambayo binafsi nadhani ni kubwa, ni kuwahabarisha wanajamii. Hapo ndipo jamii inapata habari za uongo, kutunga, umbea, kuchochea, kuchokoza, udaku, na za kujidhalilisha kama hii tahariri ya Rai. Wakati mwingine, jamii inapata habari za ukweli kutegemeana na uadilifu wa mwandishi au chombo cha habari husika.
Kwa maoni yangu, nadhani vyombo vya habari vya IPP vinaweza kuwa haviendeshwi kwa faida, lakini viko kwa ajili ya kulinda na kuingiza faida katika biashara ya Mengi. Baadhi ya wadau walivilalamikia sana, humu humu Jambo Forums, wakati wa kampeni za Kikwete. Sasa hivi ametulia anamsakama Mkapa kweli kweli. Hii ina uzuri na ubaya wake. Ubaya ni kwamba, mnaweza kumpata Rais anayetaka kupambana na mafisadi na kuwasambalatisha. Lakini anapomaliza muda wake, wanamuandama kwa kutumia vyombo vyao vya habari.
Uzuri ni kwamba, hata kama ni kweli Rais alipambana na baadhi ya michezo michafu ya Wafanyabiashara, lakini na yeye akaendekeza ufisadi, akimaliza muda wake, wanampiga makonzi kama wanavyomfanya Mkapa sasa hivi. Si unajua tena, vita ya Panzi furaha ya Kunguru. Joseph Mihangwa, mwandishi wa makala Raia Mwema, anasema ni "kunyukana". Ukiangalia utaona kuwa, katika nchi zilizoendelea kama Marekani, viongozi wengi wanaotumikia vifungo jela, ni matokeo ya "minyukano" ya mafisadi.
Ingekuwa Marekani, kiongozi kama Andrew Chenge angekwisha sogelewa na Wazee wa kazi, na kumwambia tutakupunguzia kifungo (badala ya miaka 50, utalamba 5), twambie ni hakina nani ulishirikiana nao na fedha zao ziko wapi? Hivi ndivyo aliyekuwa Spika wa Bunge la Marekani, Tom Delay anavyonyemelewa na Wazee wa Federal Gov. Wamesitisha kifungo cha Jack Abramoff, gwiji la kuhonga viongozi, ili waangalie kama wanaweza kumtia hatiani Tom Delay (wananyukana).
Habari nzuri kwa Marekani ni kuwa, wana utaratibu mzuri wa kuwalinda viongozi wao na raia wema wasio na hatia. Siyo rahisi chombo chochote cha habari kumpaka raia au kiongozi yeyote matope bila kulipia gharama zake. Habari mbaya kwa Tanzania ni kuwa, sasa hivi tunafurahi jinsi Mengi anavyoibua ufisadi wa Mkapa, lakini siku akitokea kiongozi mzuri akapakwa matope na wamiliki wa vyombo vya habari, kwa sababu tu, aliingilia mkondo wao wa kupata faida, Tanzania hatuna utaratibu wowote wa kumlinda.
Hii ni changamoto ambayo inabidi tuifanyie kazi kama taifa. Binafsi siamini kama Mengi anasukumwa na dhamiri ya kuchukia ufisadi. Mbona anashangilia utawala wa Kikwete? Zaidi ya yote, binafsi siko moyoni mwa Mkapa, Mengi, au Ulimwengu, lakini naweza kuwahukumu kutokana na matendo yao. Kimatendo, nadhani Mengi na Mkapa wanabadilika kutokana na nyakati, pamoja na mazingira. Nadhani ni kwa sababu ya dhana ya faida na madaraka.
Nilisoma makala za Ulimwengu wakati wa kampeni ya 1995, jinsi alivyokuwa akimkampenia Mkapa. Nilisoma makala za Ulimwengu wakati Mkapa yuko madarakani. Nazisoma makala za Ulimwengu sasa hivi. Sijaona kilichobadilika katika maandishi. Nakumbuka makala moja iliyoandikwa na Ulimwengu 1995 ikijibu hoja za wapinzani kuwa Mkapa hajulikani. Ulimwengu alijenga hoja za kwa nini aliamini Mkapa ndiye aliyefaa miongoni mwa wale waliojitokeza.
Mkapa aliposhinda, Ulimwengu aliendeleza taaluma yake pamoja na makala zake, na baadae kipindi chake cha TV, kuihabarisha jamii na kumkumbusha Mkapa kutimiza ahadi yake kwa wananchi. Nilisoma makala za Ulimwengu baada ya kuzama kwa MV Bukoba jinsi alivyokuwa na imani na Serikali, na nilisoma makala ya Ulimwengu iliyokuwa na kichwa cha habari "simuogopi Nzwanzugwanko". Kwa kifupi, Ulimwengu alikataa kata kata kujidhalilisha, na akaamua kusimamia hoja zake alizozijenga wakati anampigia kampeni Mkapa.
Sijuhi mahusiano ya Mkapa na Ulimwengu sasa hivi, lakini nakuhakikishia kuwa, kama Ulimwengu angekuwa mwandishi mithili ya huyo aliyeandika tahariri hii ya Rai, wangekuwa maswahiba wakubwa na Mkapa mpaka leo. Si unakumbuka makala iliyoandikwa na Salva Rweyemamu kuhusu Kikwete, alafu ikaletwa hapa Jambo Forums, mpaka baadhi ya wadau wakawa wanauliza maswali kama aliyeandika ni Salva wanayemfahamu. Lakini sasa hivi si tunajua kwa nini Salva alikuwa anaandika makala kama zile.
Hawa akina Chenge na Lowasa wangeweza kuwashawishi waadishi wa habari wenye vipaji mithili ya Ulimwengu, nadhani wangekula kuku kwa mlija. Lakini utamlipa nini, au utampa cheo gani mtu kama Ulimwengu zaidi ya chakula cha ubongo? Si unaona Marekani, waandishi wa habari uchwara na "talk show hosts" ni matajiri wa kupindukia!