Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,922
- 3,252
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, amemjibu Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, kuhusu hali ya miundombinu ya barabara nchini, akisema bado kuna changamoto ya ubovu wa barabara katika maeneo mbalimbali.
Hoja hiyo imekuja baada ya Heche kulalamikia hali ya barabara kupitia mitandao ya kijamii, ambapo Msigwa alijibu kwenye maoni ya chapisho hilo, akieleza juhudi za serikali katika ujenzi wa barabara na kumtaka Heche azungumzie pia miradi inayoendelea kutekelezwa.
Akijibu hoja hiyo Oktoba 13,2026 jijini Arusha, Heche amesema ubovu wa barabara ni miongoni mwa mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika kujadili sababu za ajali za barabarani, badala ya kuhusisha ajali hizo na uzembe wa madereva pekee.
Heche pia amelinganisha ujenzi wa reli wakati wa ukoloni na kipindi cha baada ya uhuru, akieleza kuwa wakoloni waliweza kujenga reli kwa muda mfupi, huku Tanzania ikiwa imetimiza miaka 65 ya uhuru, lakini urefu wa reli iliyojengwa katika kipindi hicho ni mdogo ikilinganishwa na reli zilizojengwa wakati wa ukoloni.
Hali hiyo imeibua mvutano wa hoja za kisiasa kati ya Heche na Msigwa kuhusu maendeleo ya miundombinu nchini. Wakati Msigwa akisisitiza juhudi za serikali katika ujenzi wa barabara na miradi mingine ya maendeleo, Heche amekuwa akiibua changamoto za ubovu wa barabara na kuhoji kasi ya maendeleo ya miundombinu nchini.
Chanzo: Jambo TV