HESLB yakwepa kuhojiwa kuhusu upendeleo wa mikopo

BARD AI

JF-Expert Member
Joined
Jul 24, 2018
Posts
3,591
Reaction score
8,826

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameionya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) akidai inaingilia kazi ya timu aliyoiunda kuchunguza uhalali wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi.

Timu hiyo iliundwa Julai 31 mwaka huu, baada ya kuwapo malalamiko mbalimbali ya utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa baadhi ya wanafunzi wenye sifa kukosa mkopo na wale wasio na sifa wakipata.

Wakati timu hiyo ya wataalamu watatu ikiendelea na uchunguzi wa kupitia utoaji wa mikopo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2017/18 hadi 2021/22, Waziri Mkenda ameibuka na kudai kuwa uongozi wa HESLB hautoi ushirikiano kwa timu hiyo.

Timu hiyo ya watu watatu ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, Profesa Allan Mushi, Idd Makame kutoka Zanzibar na Dk Martin Chegeni ambao wote ni wataalamu wa mifumo waliobobea katika sayansi ya kompyuta na takwimu.

Juzi, Waziri Mkenda akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alidai timu hiyo imekuwa ikipata vikwazo mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Tulipendekeza uchunguzi huu uangalie miaka yote mitano ambayo lengo lake ni kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu zinatolewa kwa haki ili kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji makubwa,” alisema.

Pia, alisema wamelenga kuhakikisha hakuna fursa kwa kiongozi yeyote (akitumia mfano mwenyewe) kuwapa kipaumbele ndugu zake katika utoaji wa mikopo wakati mtu ambaye hana uhusiano hapati, licha ya kuwa na vigezo.

“Tunataka tuhakikishe kile ambacho Serikali inatenga kinakwenda kwa walengwa,” alisema.

Waziri huyo alisema bodi inapaswa kuiacha kamati hiyo ifanye kazi kwa sababu taarifa iliyoombwa ni ya wizara na itafanyiwa kazi ndani ya wizara.

“Sasa natoa onyo dhidi ya ushawishi unaoendelea, asije mtu akazuia kamati kufanya kazi. Ushawishi huo inaashiria uwepo wa madudu na nikiona hali hiyo inaendelea sitasita kuchukua hatua kali sana,” alisema.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru hakuweza kupatikana kuzungumzia madai hayo, huku msemaji wa bodi hiyo, Omega Ngole alipopigiwa simu ya kiganjani alipokea na kuomba atumiwe ujumbe mfupi wa maandishi.

Mwananchi ilimtumia ujumbe huo mfupi wa maandishi saa 12:41 jioni na akapigiwa kuelezwa ausome ili kuufanyia kazi, lakini hakuujibu na hata alipopigiwa tena saa 12:52 jioni hakupokea simu.

Itakumbukwa, wakati akiiunda timu hiyo, Waziri Mkenda alisema timu hiyo itapitia malalamiko ya wanafunzi mbalimbali ambao wamekuwa wakiyatoa kuhusu upendeleo wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wasio na sifa huku wale wenye sifa stahiki wakikosa mikopo hiyo.

Alisema timu hiyo itaangalia vigezo vilivyoainishwa ili kuona kama kuna taarifa nyingine za ziada zinazoweza kutumika katika utoaji wa mikopo ili fedha zinazotolewa na Serikali zikopeshwe kwa haki.

Hata hivyo, wakati Profesa Mkenda akionya bodi hiyo kutoingilia timu ya uchunguzi, Oktoba 19 HESLB ilitoa taarifa kuanza kutoa majina ya wanafunzi wahitaji waliowasilisha maombi yao ya mkopo wa masomo kwa ajili ya mwaka wa masomo 2022/23.

“Leo (Oktoba 19) tumeanza kutoa updates (taarifa) kwa makundi yote yaliyopangiwa mikopo, ambao bado tunaendelea kufanyia kazi na wale wanaotakiwa kufanya marekebisho, kila mmoja anapata taarifa kupitia akaunti yake ileile aliyotumia kuomba mkopo, hauhitaji kufika ofisini kwetu,” inaeleza taarifa hiyo ya HESLB.

“Mwaka huu kama miaka iliyopita, fedha inayohitajika kwa mahitaji ya mwanafunzi wa muhula wa kwanza imepokelewa, tunakamilisha uandaaji wa malipo ya muhula wa kwanza na fedha zitaanza kuwafikia wanafunzi katika vyuo mwishoni mwa wiki hii.”

Kupitia taarifa hiyo, bodi ilivikumbusha vyuo ambavyo havijawasilisha matokeo ya mtihani ya wanafunzi wanufaika wanaoendelea na masomo, wawakilishe matokeo yao mapema ili kuwawezesha wao kufanya malipo ndani ya wakati.

“Hadi sasa vyuo 11 havijawasilisha matokeo yao, tunawakumbusha na tunasisitiza waharakishe kuwasilisha matokeo ili tukamilishe malipo ya wanafunzi waliofaulu kuendelea na masomo,” inaeleza taarifa hiyo.

MWANANCHI
 


Kwanini msitenge pesa ya kutosha kila Mtu akapata uo mkopo hayo mambo mengine Ni siasa tu.
 
Serikali ingerudia utaratibu wa awali wa kutoa ufadhili kwa wanafunzi waliodahiliwa kwenye vyuo vya umma pekee maana ndo vinaendeshwa kwa kodi za wananchi kwa kupitia wizara ya elimu. Hiyo bodi ya mikopo ingeachwa ihudumie wanafunzi waliopata nafasi kwenye vyuo binafsi. Hii ingeleta hata ushindani wa kuwania nafasi kwenye vyuo vya umma na kuwapa nafasi watoto wa wananchi wa kawaida wenye uwezo mkubwa darasani kupata haki ya elimu bila vipingamizi.​
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…