Dalili za VVU
Baada ya maambukizi ya awali, inawezekana mtu asionyeshe dalili yoyote kwa muda mrefu. Hata hivyo, ndani ya wiki chache baada ya kuambukizwa virusi husika, watu wengi hupata ugonjwa wa mithili ya mafua, ambao unaweza kudumu kwa wiki kadhaa. Dalili za mwanzo za UKIMWI au VVU ni pamoja na:
Homa
Maumivu ya kichwa
Maumivu ya misuli na viungo
Upele
Maumivu ya koo na maumivu ya vidonda kinywani
Kuvimba kwa tezi za limfu , haswa kwenye shingo
Kuharisha
Kupungua uzito
Kikohozi na kupumua kwa shida
Katika hatua hii ya awali, VVU huzaliana kwa haraka na kuenea mwilini kote, na kusababisha kupungua kwa kinga ya mwili.
Unaambukizwaje VVU na kuwa kwenye hatari ya kuugua UKIMWI?
Mtu anaweza kuambukizwa VVU na mtu mwingine aliye na kiwango cha virusi hivyo kinachoweza kutambulika (detectable viral load). Majimaji fulani ya mwili yanaweza kuwa na virusi husika, kwa mfano:
Damu
Shahawa na majimaji kabla ya shahawa
Majimaji kwenye njia ya haja kubwa
Majimaji ya ukeni
Maziwa ya mama
Majimaji haya yanapaswa kuingia kwenye mkondo wa damu ya mtu ili maambukizi yatokee. Hivyo basi, maambukizi yanaweza kutokea kwa njia ya kujamiiana, majeraha mabichi, au kudungwa sindano iliyotumika kwa mtu aliyeathirika na VVU. Aidha, mama anaweza kuambukiza mtoto wake VVU wakati wa ujauzito, kuzaa, au kunyonyesha.