1: HATUA ZA MAKUNDI:
Kwanza turekebishe jina, kuna watu wanasema tunaingia AFCON mara ya pili, wakati ule mwaka 1980 ilikuwa ni African Cup, jina AFCON limekuja miaka ya karibuni.
Thread zilizopita zimeongelea sana kuhusu Peter Tino, mchezaji aliyeifungia Taifa Stars bao lililotupeleka Nigeria. Hebu tujikumbushe mambo yalivyotokea na JF ionekane ni mahala pa kukimbilia data.
Kwanza kabisa, ingawa watu wanasema ni mwaka 1980 ukweli ni kwamba mechi tunayoisema ilifanyika mwishoni mwa mwaka1979, tena tukiwa na uchumi mbovu kutokana na kumalizika kwa vita ya Tanzania na Uganda.
Mechi ile tulikuwa tunahitaji draw ili tuingie finali na Zambia walikuwa wanahitaji ushindi na mechi ilifanyikia Ndola, Zambia.
Katika dakika ya 20, Zambia wakapata bao la kuongoza Hadi half-time Zambia (1) na Tanzania (0).
Kipindi cha pili timu zote ziliongeza kasi lakini Zambia ikiutawala mpira zaidi na ikishangiliwa uwanja mzima. Kuna waandishi husema mshambulia hatari wa Zambia, Godfrey Chitalu, hakufua dafu. Huu si ukweli.
Zambia ilitawala mchezo na golikipa wa Tanzania, Juma Pondamali alipohojiwa na waandishia alisema alimwogopa sana Godfrey Chitalu kwani alikuwa anapiga mikwaju hatari na yeye anaipangua.
Hadi watu wanaanza kuondoak uwanjani na wengine kuacha kusikiliza redio walijua Taifa Stars imetolewa. Ndipo zikiwa zimebaki dakika 2 kumalizika mchezo, Peter Tion akaifungia Taifa Stars bao lililotupeleka Nigeria.
Formation ya wakati huo ilikuwa ni 4-2-4. List ya mchezo huo kama nitaikumbuka vizuri ninaiandika humu, kama ina makosa madogo wanaokumbuka wanisahihishe.
01: Juma Pondamali, (Pan)
02: Leopard Tasso, (Balimi-Bukoba)
03: Mohammed Kajole, (Simba)
04: Salim Amir, (Costal Union)
05: Jella Mtagwa, (Pan)
06: Leodegar Tenga, (Pan)
07: Hussein Ngulungu, (Pan)
08: Omari Hussein, (Yanga)
09: Peter Tino, (African Sports)
10: Mohamed Salim, (Costal Union)
11: Thuweni Ally, (Simba)
2: FINALI (NIGERIA):
Baada ya kufuzu hiyo mechi ya mwaka 1979, ndipo fainal zenyewe za AFRICAN CUP zikafanyika March 1980. Mambo yalikuwa hivi huko Nigeria. Tanzania ilipangwa na wenyeji Nigeria, Egypt na Ivory Coast, siku hizi inaitwa Cote d'Ivoire (tamka kwodivaa).
Mechi ya ufunguzi, March 08, 1980, Tanzania tukacheza na Nigeria kwenye uwanja uitwa Surulele, Tanzania tukachapwa 3-1. Nigeria ilikuwa a washambuliaji hatari kama Ousegun, kwa kifupi Segun, Tunde Obamidele. Bao la pekee la Tanzania likafungwa na Thuwein Ally, mzanzibari pekee katika timu ya Taifa.
Mechi ya pili March 08, 1980, Tanzania tukacheza na Ivory Coast, tukachapwa 2-1. Hapo pia bao la pekee la Tanzania likafungwa na yuleyule Thuwein Ally. Kimsingi tukawa tumeshatolewa mashindanoni tukabaki kukamilisha ratiba.
Mechi ya tatu nimekosa kumbukumbu ilichezwa lini lakini cha uhakika ni kwamba Tanzania itulicheza na Egypt, tukatoka sare 1-1. Hapa tena bao la pekee la Tanzania likafungwa na yuleyule Thuwein Ally.
3: JUMA PONDAMALI, PETER TINO, THUWEIN ALLY, ABDALAH KIBADENI:
NImesoma mahala kwamba Peter Tino ameenziwa, sijui ni kweli au la maana sijaipitia vizuri taarifa hiyo. Lakini tukifanya tathmini vizuri, pale Zambia aliyengara alikuwa ni golikipa Juma Pondamali maana Taifa Stars ilizidiwa kasi kwa muda mwingi wa mchezo na Pondamali ndiye aliyeokoa michomo mingi ya wazambia.
Mwishoni wlalipobadili mbinu ndipo Peter Tino akasawazisha. Kama ni man of the Match alikuwa ni Juma Pondamali na si Peter Tino maana alikokoa magoli mengi ya wazi tena wakati mwingine defense imeshapitwa yote.
Kule Nigeria tumeona kwamba Tanzania ilikuwa inapata goli moja kila mechi, mfungaji akiwa ni Thuwein Ally. Huyu alikuwa ni mchezaji wa Simba akitokea KMKM ya Zanzibar.
Yale magoli matatu yalimfanya Thuwein Ally asifike maana hakuwa anajulikana sana na ndiyo yalifanya aonekane Simba imepata mchezji mzuri.
Sifa ya Thuwein Ally ilikuwa ni mashuti makali ya mguu wake wa kushoto. Kuna shuti alipigia free kick pale CCM Kirumba wapo wanaoamini lilikuwa ni moja ya mashuti makali kupigwa hapa nchini.
Hivyo, kule Nigeria, Thuwein Ally alituletea sifa Tanzania na hata jina lake likabadilika kuwa mfungaji wa magoli matatu kule Nigeria. Hivyo, kwa washabiki wa kipndi kile Thuwein Ally alivuma kuliko Peter Tino.
Peter Tino hakuvuma sana wakati ule kwa sababu hata timu aliyokuwa yaani African Sports ya Tanga, ukiachilia uhasama na Coastal Union, haikuwa tishio.
Kimsingi, Peter Tino hakuvuma sana zaidi ya hilo goli la pale Zambia. Mtu aliyekuja kuvuma alikuwa ni beki (centre half) Jelah Mtagwa ambaye hadi aliwekwa kwenye Stamp ya Posta, yaani ukituma barua lazima uone picha ya Jellah Mtagwa.
Leodgar Tenga hakuendelea sana a mpira liukweli ni kama vile alistaafu mpira kipindi hicho aana nadhani alijikita zaidi na tmasomo pale Chuo Kikuu.
4: ZAMOYONI MOGELA:
Mwaka 1980 wote uliisha baridi namna hiyo ndipo mwaka uliofuata (1981) akaibuka mshambuliaji Zamoyoni Mogela, kwenye mashindano ya CECAFA, ambako kama Thuwein Ally, zile mechi tatu alikuwa lazima afunge goli hadi kikamfanya aitwe Golden Boy.
Kimsingi Peter Tino na Thuwein Ally walikuja kipindi ambapo Abdalah Kibadeni umarufu wake ulikuwa unaondoka na hasa alipoanza ukocha kwa Majimaji ya Songea mwaka 1978.
Hivyo, mwaka 1978 hadi 1980 hakukuwa na mshambulia anayemiliki jina ndiyo maana mtu akiibuka kwenye mechi moja anatawala kidogo kama Peter Tino na Thuwein Ally.
Lakini Thuwein Ally alimzidi umaarufu Peter Tino kama ilivyoelezwa huko juu, kutokana na magoli matutu kule Nigeria. Lakini hawa wote wawili walizidiwa na Zamoyoni Mogela kuanzia Novemba 1980 hadi Mogela alivyoacha mpira.
Kama mnakumbuka mwaka 2011, Zamoyoni Mogella alipewa nishani ya kitaifa kuwa mchezaji bora kwa miaka 50 ya uhuru. Hawakukosea waliofanya hivyo.
Kuna wanaosimulia goli ambalo Zamoyoni Mogela alimfuga golikipa Juma Mhina wa Pamba pale CC ingekuwa sasa hivi lilikuwa linafungwa Ulaya, alimfunga baada ya kuipiga chenga difensi nzima ya Pamba na kumdanganya kipa kwenye upenyo mdogo akaingizia hapohapo goli.
Peter Tino alikuja kuhamia Pan mwaka 1981 na hata hivyo hakufua dafu kwa Mogela ambaye kila timu ilikuwa inamuwekea beki maarufu. Yanga ilikuwa inamuwekea beke aliyeitwa Athuma Chama akisaidiwa na Yusuf Bana.
Peter Tino alizidiwa hata na Madaraka Selemani wa CDA ya wakati huo aliyeweza kupiga chenga defense nzima. Peter Tino alisaidiwa sana na urefu wake. Hivyo, suala la Peter Tino unaweza kuliangalia namna hii.
WANASIASA KUVURUGA UZALENDO:
Kingine ni kwamba wakti ule kulikuwa na chama kimoja tu CCM na hata kama kama timu ilisaidiwa au kuhamasishwa waljitokeza kwa nadra sana akijitahidi ni Waziri anayehusika na michezo. Ungeonekana ni kichaa kutojua Taifa stars inacheza, achilia mbali kutoishangilia.
Leo soka imeanza kuingiliwa na wanasiasa, tena wengine hata hawana historia ya mpira na historia hii inayoelezwa humu huenda ni ngeni kwao. Walikuwa wapi wakati huo, jibu mnalo.
Licha ya hayo UCHADEMA na UCCM unaonekana. Akitokea sana mwanasiasa wa chama tofauti akajikita inaonekana anavutia chama chake na ni kweli mwakani atafanya kampeni kwamba kawezesha yeye na chama chake.
Matokeo yako kama timu imewezeshwa na mwanasiasa wa CHADEMA basi yule wa CCM yuko radhi timu ifungwe ilie CHADEMA isije ikachukua sifa hiyo!
Kimsingi, wanasiasa wa vyama vyote wanavurugua utamu wa mpira na walitakiwa wabaki hukohuko kwenye majukwaa ya siasa.
NAWASILISHA.