Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
''Mwalimu Nyerere na Historia'' (1980)
Kitabu cha Prof. G.A. Mhina
Lakini kwa kuwa ni kitabu cha picha nilikisoma mara moja tu katika miaka ya 1980 na kikabakia Maktaba.
Sikukigusa tena.
Jana nimeona picha za TANU katika mtandao na haraka nikatambua kuwa picha hizi nimepata kuziona katika kitabu hicho hapo juu.
Ndipo nilipokitafuta kitabu hiki na kuanza kukipitia.
Kwa hakika nilistarehe sana na picha nilizozikuta ndani ya kitabu hiki ikawa kama vile naziona picha zile kwa mara ya kwanza.
Katika moja ya picha ambayo ilinivutia kwa kosa nililoliona katika maelezo ya picha hiyo ni hiyo hapo chini:
Maelezo ya picha hii ya waasisi wa TANU ni kuwa hao ni waanzilishi wa TAA.Vipi linaweza kufanyika kosa kama hili?
Picha hii ya Waasisi wa TANU mwaka wa 1954 ni maarufu sana.
Hili mosi.
Pili hapajakuwapo na picha ya waasisi wa African Association iliyoanzishwa mwaka wa 1929.
Ingawa nimabahatika kupata picha mbili za waasisi wa chama hicho - picha ya Kleist Sykes na picha ya Mzee bin Sudi.
Tukirejea kwenye picha hiyo ya Waasisi wa TANU kuna kisa kirefu kuhusu picha hiyo iliyowekwa hapo.
Picha hiyo imechezewa kwa kutiwa mkono.
Katika picha yenyewe ya Waasisi wa TANU Ally Sykes, Tewa Said Tewa na Kasella Bantu hawamo.
Hawa walijitoa kwa kjuwa walikuwa ni watumishi wa serikali na sheria ilikuw ainawakataza kujihusisha na siasa.
Ilipokuwa inapigwa picha wao walikaa pembeni.
Angalia picha halisi hapo chini:
Kazi hii ilifanywa na Idara ya Picha Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.
Siku zote kila nikiangalia picha hiyo iliyotiwa mkono hujiuliza kama haja ilikuw akuwaweka waasisi wote wa TANU kwa nini hazikuwekwa pia picha za Ally Sykes na Tewa Said Tewa.
Tuendelee kubakia katika hili suala la picha hii ya Waasisi wa TANU.
Katika kitabu cha maisha ya Julius Nyerere, ''Nyerere Biography,'' kitabu kinaeleza kuwa picha hii ilipigwa na kamera ya Denis Phombeah yeye mwenyewe akiwa mpigaji wa picha hiyo.
Abbas Sykes alikuwapo katika mkutano wa kuasisi TANU lakini hakuwa mjumbe bali kijana mdogo wa kutumwa na kaka yake Abdul Sykes na wajumbe wengine wa mkutano kufanya hiki na kile katika mkutano ule.
Abbas Sykes amenieleza kuwa picha ya Waasisi wa TANU ilipigwa na mpiga picha maarufu Dar es Salaam jina lake Gomez.
Abbas Sykes anaeleza kuwa walimsubiri Gomez ambae studio yake ilikuwa Acacia Avenue kwa muda hakutokea.
Abdul Sykes akamwambia Abbas achukue baiskeli ya TAA amfate wakapishana.
Wakati Abbas Sykes anamfuata Gomez yeye kumbe alikuwa njiani akija New Street kuwapiga picha waasisi wa TANU.
Katika kitabu hiki cha ''Nyerere na Watanzania,'' kuna picha hapo chini ya baiskeli ya kwanza ya TANU.Bila shaka hii ndiyo baiskeli ya kijana mdogo Abbas Sykes alipanda kumfata mpiga picha Gomez:
Baiskeli ya TANU
Picha niliyopigwa na Gomez 1956
Mwandishi ni huyo kushoto kulia ni ndugu yangu Kapufi Yunge
Mama anasema nilikuwa situlii kwenye kiti ndipo Gomez akanipa kitabu nishike.
Studio ya Gomez ilikuwapo hadi miaka ya 1980.