Na bahati mbaya Uhuru ulipiganiwa na nchi nzima bila kujali dini za wahusika kisha yeye analazimisha watambulike waislamu pekee wa pwani na daslam ndio wapigania Uhuru wa kweli...
Yule msshamba kutoka butiama aliwazidi wote japo wao walikuwa mjini akawa mwenyekiti pendwa kabisa...
Avriel,
Historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika haiko kama hivyo unavyotamani wewe iwe.
Historia ya TANU mimi naijua vizuri sana kwa kuwa waasisi wake mimi ni wazee wangu.
Nilipoona imeandikwa sivyo ndipo niliponyanyua kalamu na kuandika kusahihisha historia hiyo iliyokuwapo.
Hebu soma kipande hiki hapo chini nimemuandikia kijana mmoja leo asubuhi.
Soma na unifahamishe kama historia hii inafanana hata kwa mbali na historia ya TANU na uhuru unayoijua wewe:
"Napenda kuchangia kidogo niyajuayo kuhusu Chief David Kidaha Makwaia.
Kwanza mimi nilipata bahati ya kukutana na Chief Kidaha hapa Dar es Salaam
mwaka wa 1968.
Mwanae Edward Makwaia nilikuwa nasomanae darasa moja St. Josephs Convent School basi siku moja akaniambia kuwa baba yake amekuja kutoka Nairobi kwa hiyo nimsindikize kwenda kumwamkia.
Hivi ndivyo nilivyobahatika kumuona Chief Kidaha.
Lakini wakati ule mimi mtoto sikuwa najua kwa nini Chief Kidaha alikuwa anaishi
Kenya.
Chief Kidaha baada ya uhuru aliwekwa kizuizini Tunduru kupitia Preventive Dentition Act ya 1962 na baada ya kutoka aliamua kuhama nchi na kwenda Kenya.
Chief Kidaha Kidaha ni mtoto wa Chief Makwaia Mohamed Mwandu wa Busiya.
1566962505965-png.1191693
mohamedsaidsalum.blogspot.com
CHIEF EDWARD ANTHONY MAKWAIA WA BUSIYA
Chief Makwaia Mohamed Mwandu Nimeona tangazo la Busiya Chiefdom katika mitandao ya kijamii na nikaangalia, ‘’clip,’’ yake. Hili ni ta...
mohamedsaidsalum.blogspot.com mohamedsaidsalum.blogspot.com
Wakati nafanya utafiti wa kitabu cha Abdul Sykes katika miaka ya 1980s nilikutana na Chief Kidaha Makwaia kwenye Nyaraka za Sykes kupitia barua aliyoandika Dr. Wilbard Mwanjisi.
Dr. Mwanjisi alipochaguliwa kuwa Rais wa Tanganyika African Government Servant
Association (TAGSA) mwaka wa 1951 aliandika makala kali sana katika jarida la chama, makala ambayo aliwashambulia Waingereza kiasi Rashid Kawawa akiwa mwanakamati wa Halmashauri Kuu ya TAGSA aliandika barua kuonya kuwa makala hiyo isichapwe bila ya kujadiliwa na Halmashauri Kuu ya TAGSA.
Katika makala hii Dr. Mwanjisi aliitaja hotuba ya Chief Kidaha Makwaia ndania ya LEGCO kuwa ni hotuba muhimu sana na akamsifia Chief Kidaha Makwaia kuwa ni mwanasiasa makini wa kupigiwa mfano (‘Doctor Mwanjisi Speaks to TAGSA’ 22 nd December, 1951(Sykes' Papers),
Katika hotuba hiyo Chief Kidaha alikuwa anaishauri serikali ya Kiingereza kuondoa ile sheria ambayo ilikuwa inawapiga marufuku Waafrika wafanyakazi wa serikali kujishughulisha na siasa.
Kitu ''interesting,'' katika kipindi hiki ni kuwa Chief Kidaha alikuwa na mazungumzo na Katibu wa TAA, Abdul Sykes, mazungumzo haya yakifanyika nyumbani kwa Abdul Sykes, Abdul akijaribu kumshawishi Chief Kidaha aingie TAA ili wamchague kama Rais kisha waunde TANU na kudai uhuru wa Tanganyika.
Mazungumzo haya hayakufanikiwa.
Baada ya uhuru Dr. Mwanjisi na yeye aliwekwa kizuizini na kama alivyofanya Chief Kidaha baada ya kutoka kizuizini alikwenda kuishi Kenya.
Na bahati mbaya sana waandishi wa historia ya TANU hawakutaka kufanya mahojiano yoyote na marehemu Ally Sykes katika historia ya TANU na kwa hili historia iliyokuja kuandikwa ikakosa mengi muhimu katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.
Hii ndiyo sababu Chief Kidaha Makwaia haonekani kokote katika historia ya kuunda TANU na kudai uhuru wa Tanganyika.
Ningependa kuhitimisha kwa kueleza kuwa baada ya kutawazwa kwa Malkia Elizabeth, uongozi wa TAA ulituma salamu za pongezi kwa Malkia kwa kutawazwa kwake barua ya pongezi ilitiwa sahihi na Rais wa TAA Julius Nyerere, Makamu wa Rais Abdulwahid Sykes, Katibu Mkuu Dome Okochi Budohi, Naibu Katibu Dossa Aziz, Mweka Hazina John Rupia, Naibu Mweka Hazina Ally Sykes."
Bwana Avriel,
Hii ndiyo historia ya TANU na nimezishika nyaraka hizo kwa mikono yangu na nimezisoma kwa macho yangu nazijua fika kama primary source zilizonisaidia kuandika historia hii.
Soma kitabu cha Abdul Sykes ndani kuna mengi yatakayokushangaza.
Hayo hapo juu ni Waingereza wanasema, "tip of the ice berg," yaani ni kitu kiduchu na ni kidogo sana.
Haifai mtu kunga'nga'nia ujinga wakati elimu ya kujifunza ukawa mwerevu ipo na ya bure.
Mimi hapa natoa elimu, darsa la historia bila khiyana bure kabisa sitozi senti moja.
Vyuo Vikuu Marekani na kwingi duniani huniita kwa gharama zao kusomesha hii historia wenyewe wanaita, "corrective history."