Mkataba huo ulikuwa ni wa miezi sita kuanzia mwezi wa nane 2024, Agosti 2024 Mkandarasi alianza kujenga barabara hiyo kwa kasi akileta vifusi na kuchimba mitaro hali iliyoleta matumaini kwa wakazi wa eneo hilo licha ya kuwa alizuia njia hiyo kupitika kwa muda mrefu.
Alichimba mitaro na kumwaga vifusi na udongo katikati ya barabara na kuanza kujenga mitaro ya baadhi ya sehemu.
KWANINI BARABARA IMESIMAMA?
Taarifa zinasema kuwa mkandarasi huyo ameishiwa pesa ya kuendeleza barabara hiyo, hivyo kuitelekeza.
Baadhi ya wakazi wa eneo hili na watoa huduma za usafiri wanasema matatizo ya uhaba wa pesa yalianza kuonekana tangu barabara hiyo inajengwa kwani hata vibarua walikuwa hawalipwi.
‘Huyu mkandarasi amekimbia hana pesa, kuna wakati alipigana na vibarua wake hapa, wakimdai pesa. Walipigana sana hapa’ – anasema mwendesha Bajaji.
Kiongozi mmoja wa Mtaa huu anadai mkandarasi mzawa ambaye alikataa kumtaja jina, hana pesa na ametelekeza barabara hiyo ambayo sasa imekuwa changamoto mara mbili zaidi ya ilivyokuwa mwanzo.
‘Kabla hajaja barabara ilikuwa mbaya lakini ilikuwa inapitika bila shida yoyote, lakini sasa ni kero.
‘MKANDARASI AMEKUJA KUHARIBU SI KUTENGENEZA’
Alipoanza kujenga barabara hii alifunga kabisa njia kasoro kwa watembea kwa miguu tu, alisababisha watu wenye magari wanaoishi pembezoni mwa barabara hiyo kutafuta maeneo mengine ya kuegesha magari na kurudi majumbani mwao kwa miguu, kero hii ilichukua takribani miezi miwili wenye magari kushindwa kupita.
Hata sasa wenye magari wanalazimika kuzunguka ili waweze kupita hivyo sehemu ya dakika moja au mbili kufika nyumbani inachukua takribani dakika kumi kuzunguka
Hali ilivyo sasa, hata Bodaboda zinapita kwa tabu kwani njia imejaa tope na barabara imeharibika mara mbili zaidi ya ilivyokuwa awali.
Mkandarasi amefanya maisha yamekuwa magumu kwani hata kwa walio na biashara pembezoni sasa hawapati wateja kama ilivyokuwa awali.
Je, nini kinaendelea? Ni kweli Mkandarasi kaishiwa na mbona TARURA wapo kimya?