KERO Hivi wafanyabiashara wa barabarani hawawezi kuuza bila kufungulia sauti ya spika juu?

KERO Hivi wafanyabiashara wa barabarani hawawezi kuuza bila kufungulia sauti ya spika juu?

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua
A

Anonymous

Guest
Naishi Mbagala, na nina dukuduku pamoja na maoni binafsi ambayo ningependa yawafikie wananchi wenzangu na mamlaka husika, ili ikiwezekana hatua zichukuliwe na marekebisho yafanyike.

Kumekuwa na tabia ya wafanyabiashara, hasa wale walio pembezoni mwa barabara, kutumia redio zenye matangazo ya biashara kwa sauti kubwa sana. Unapopita katika maeneo hayo, kelele zinakuwa nyingi kiasi cha kukosa utulivu na kuhisi kuchanganyikiwa.

Mfano mzuri ni maeneo ya Mbagala Zakhiem na Rangi Tatu, ambako kelele hizo zimekuwa kero kwa watu wanaopita na wanaoishi au kufanya kazi katika maeneo hayo. Wakati mwingine unajiuliza wafanyabiashara na watu wengine wanawezaje kuvumilia kelele hizo kuanzia asubuhi hadi usiku.

Kwa mtazamo wangu, hali hii ni aina ya uchafuzi wa mazingira kwa kelele (noise pollution), kwani inaweza kusababisha usumbufu, maumivu ya kichwa na kuathiri utulivu wa watu.

Maswali ya kujiuliza
  1. Je, biashara haiwezi kufanyika bila kutumia redio zenye matangazo ya sauti kubwa?
  2. Je, wafanyabiashara hawawezi kufungua maduka yao, kupanga bidhaa na kuwakaribisha wateja bila kusababisha kelele kwa watu wengine?
  3. Je, mamlaka husika hazioni tatizo hili, na kama wanaliona, ni hatua gani zinazochukuliwa kulidhibiti?
  4. Je, uchafuzi wa mazingira kwa kelele si tatizo linalopaswa kupewa uzito nchini kwetu, au kwa nini hali hii inaonekana kupuuzwa?
Athari kwa afya na ustawi wa jamii
Kwa mtazamo wangu, kelele hizi zinaweza kuathiri ustawi wa watu wanaoishi, kufanya kazi au kutumia muda mwingi katika maeneo hayo. Kelele za mara kwa mara zinaweza kuchangia msongo wa mawazo, kukosa utulivu na matatizo ya usingizi, hasa kwa watu wanaokaa katika mazingira hayo kwa muda mrefu.

Nimeona ni vyema kutumia jukwaa hili kueleza dukuduku langu na kuomba suala hili lijadiliwe kwa lengo la kupata suluhisho. Biashara ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi, lakini ni vyema ziendeshwe kwa kuzingatia pia haki ya watu wengine ya kupata utulivu katika mazingira yao.

Naiomba jamii na mamlaka husika kulichukulia suala hili kwa uzito na kuweka utaratibu unaowezesha wafanyabiashara kutangaza bidhaa zao bila kusababisha usumbufu kwa wananchi.
 
Back
Top Bottom