Kikao cha Waziri Mgimwa, TRA balaa
MAWAKALA wa ushuru wa forodha (clearing agents) wenye uzalendo wameshtukia njama za kuwatumia kukwepa kodi kifisadi kupitia bandari ya Dar es Salaam na kuibua kiwewe kwa wahusika, imefahamika.
Hayo yalibainika katika kikao cha mawakala hao wakiwakilishwa na maofisa waandamizi wa kampuni zao na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, kikao kilichohudhuriwa pia na wakuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kwamba mawakala hao wapatao 150 walishtukia njama za wenzao waliojaribu kumpotosha waziri ili wazuie operesheni ya TRA ya kuhakiki upya makontena yaliyokuwa yapitishwe bila kukaguliwa.
Baada ya kuwasikiliza mawakala hao na TRA, Waziri Mgimwa ambaye awali alionekana kutaka kulainika, alitaka sheria ifuate mkondo wake na operesheni ya kukagua upya makontena uendelee ili kujiridhisha hakuna ukwepaji kodi wowote na watakaobainika wachukuliwe hatua.
Baada ya Tanzania Daima kuandika habari za ukwepaji kodi kutumia utaratibu halali wa TRA kutoa mizigo inayolipiwa kodi bila kukaguliwa, mamlaka hiyo ilisitisha ghafla utaratibu huo ili kuchunguza madai ya kuwapo ukwepaji kodi mkubwa unaotajwa kuwahusisha vigogo ndani ya serikali na watu wazito.
"Wenzetu waliingia katika kikao hicho wakiwa na mbinu chafu za kutaka kumtumia waziri awatishe TRA ili makontena yao yanayokaribia 500 yatoke. Tukashtukia na kumwambia waziri utaratibu ufuatwe na yote yakaguliwe upya kujua yana nini ndani.
"Wamedanganya kuwa baadhi ya makontena wamedanganya yana viatu toka Dubai lakini ndani kuna magari, mengine wanasema kuna nguo za watoto kumbe kuna vitenge na vifaa vya electronics. Sasa kisheria ukishusha thamani ya mzigo TRA wanapandisha lakini udanganyifu wa aina ya mzigo ni kosa la jinai unataifishwa na kushtakiwa," anasema mtoa habari wetu.
Katika kikao hicho, mawakala hao walimpongeza Kamishna Mkuu wa TRA na wizara kwa kazi nzuri, lakini walilalamikia kitendo cha baadhi ya vigogo wa juu kuwaingilia katika kazi zao na hivyo kusababisha uhalifu unaofanywa na wakwepa kodi kuendelea kufanyika.
"Waliondoka wakiwa wameinamisha vichwa chini ila wanachofanya sasa ni kueneza propaganda kwenye magazeti kwamba kuna usumbufu unaosababishwa na TRA bandarini kumbe ni kuwabana wasikwepe kodi, hata kama kunakuwa na usumbufu, lakini ni vizuri kuokoa kodi," anasema.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, wahusika walikuwa wakitumia mwanya huo kwa kuficha thamani halisi ya mizigo na wakati mwingine kudanganya hata aina ya mizigo iliyomo ndani ya makontena na mara nyingi kwa kutumia nyaraka za kughushi.
Kampuni inayotajwa kuhusika kwa kiasi kikubwa ni ile maarufu kwa uuzaji wa bidhaa za nyumbani na wahusika wanaelezwa kujisahau sana na kufanya hadharani kwa kutumia majina ya vigogo wa juu serikalini.
"Nasikia mpango wa haraka walionao ni kuwahonga maofisa wa TRA wanaopangwa kwenda kufanya ukaguzi ili wakubaliane na kilichokuwa kimeandikwa kwenye nyaraka zao," anaeleza mtoa habari wetu.
Hata hivyo hali inaelezwa kuwa tete ndani ya TRA kutokana na taarifa hizo kuvuja na kuwafanya vigogo kuhaha na baadhi kutaka hata kuitelekeza mizigo yao na wengine kuwasababishia hasara kubwa wafanyabiashara waliowatumia.
"Waziri Harrison Mwakyembe aliambiwa haya yote alipokutana na wakurugenzi wa Clearing & Forwarding lakini pamoja na kujiita mpambanaji wa ufisadi alipuuzia kwa sababu zake mwenyewe mpaka vyombo vya habari viliporipoti na ndipo TRA wamechukua hatua," anaeleza mtoa habari huyo.
Kwa takriban miaka mitatu iliyopita serikali kama njia ya kuondoa mizigo bandarini mapema kwa kuepusha mlundikano na msongamano wa mizigo bandarini iliruhusu baadhi ya mizigo ya wateja wakubwa iwe inachukuliwa bandarini bila kukaguliwa.
Kitendo hiki japo kilionekana kuwa na lengo zuri kilikosolewa na wengi kwa madai kuwa kingeweza kutumika vibaya na baadhi ya hao wateja wakubwa kwa kukwepa kodi.
Mmoja wa wateja wakubwa aliyelalamikiwa hata na baadhi ya vyombo vya habari ambaye anajishughulisha na biashara ya vifaa vya nyumbani, sasa anafanya biashara ya uwakala wa mizigo.
Katika kikao ambacho waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe alifanya na wakurugenzi wa makampuni ya mawakala wa forodha moja ya mambo yaliyojitokeza ni kutaja kwa majina kampuni za mfanyabiashara huyo na nyingine yenye kumiliki Bandari kavu (ICD), kuwa zinalindwa na wakubwa.
Wakati ICD hiyo ya kuweka magari ikituhumiwa kwa utawala wa kudhalilisha na kuwatisha Watanzania bila aibu, kampuni hiyo ya vifaa vya nyumbani inatuhumiwa na mawakala wa forodha kwa ukwepaji wa kodi.
Inadaiwa kampuni hiyo inayomilikiwa na ndugu wawili wenye asili ya Kiarabu kuwa imekuwa na mtindo wa kuingia makubaliano na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa na wadogo hasa wanaofanya kwenye eneo la Kariakoo kwamba mara waagizapo mizigo yao hasa kutoka China na Dubai watumie kampuni yake au kampuni zake dada ambazo zingine zina leseni za kutolea mizigo bandarini kama njia ya kulipa kodi kidogo.
Wateja wanaokubali kutumia mpango huu haramu hulipa kwao sh milioni 17 kwa kontena moja la futi 40 na sh milioni 12 kwa kontena moja la futi 20.
Kampuni hizo zinazodaiwa kulindwa na wakubwa zinalipia TRA sh milioni nane kwa kontena la futi 40 na milioni nne kwa kontena la futi 20 pamoja na gharama za bandarini ambazo si zaidi ya sh milioni 1.2.
"Inashangaza serikali kila siku inahaha kutafuta vyanzo vipya vya kuongeza mapato wakati hiki kilichoko tena chenye uhakika kikidhalilishwa na walafi wachache kwa kushirikiana na wenye mamlaka," alisema mtoa habari wetu.