Wild Flower
JF-Expert Member
- Jul 20, 2023
- 977
- 1,966
Shirika la kutetea haki za Wafanyakazi wa majumbani la Wote Sawa chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake Angela Benedicto, limesema Serikali imetoa tangazo ambalo utekelezaji wake umeshaanza ambalo linamtaka mwajiri aliyeajiri mfanyanyakazi wa nyumbani (house girl) na haishi kwako, umlipe mshahara wa kima cha chini Tsh.160,000 na kama anaishi kwako utamlipa mshahara wenye kima cha chini shilingi elfu 80.
Mfanyakazi wa ndani aliyeajiriwa na Maafisa wenye stahiki (Majaji, Wabunge, Mawaziri na Viongozi wengine wa juu wa Serikali atalipwa kima cha chini cha mshahara cha Tsh. 265,000 na walioajiriwa na Wanadiplomasia (wakiwemo Mabalozi) na Wafanyabiashara wakubwa watalipwa kima cha chini cha shilingi 328,000.
Haya yamebainishwa na Jackline Ngalo, Mwanasheria wa Shirika la kutetea Wafanyakazi wa majumbani la Wote Sawa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi wa Majumbani yaliyofanyika jijini Mwanza yakiwa yameandaliwa na Wote Sawa, ambapo tangazo hilo linataka Mfanyakazi wa nyumbani apewe stahiki zake kama Wafanyakazi wengine wa ofisi mbalimbali ikiwemo likizo, mapumziko, kuwekewa fedha kwenye mifuko ya hifadhi za jamii, kupewa NIDA n.k.
Angela amesema “Kwa zaidi ya miaka 10 sasa Shirika la Wote Sawa linashirikiana na Serikali na Wadau wengine katika kuimarisha ulinzi wa Watoto, Wanawake na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi, katika kipindi hicho Wote Sawa imefikia Wafanyakazi wa majumbani elfu 10, Wananchi laki 3 katika kuwapa elimu na wamehudumia Manusura takribani 1500."
Kwa upande wao Wafanyakazi wa majumbani kupitia Wawakilishi wao wamepaza sauti wakielezea changamoto mbalimbali zinazowakabili, huku Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela, Wakili Mariam Msengi, ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda kwenye maadhimisho hayo akatoa maagizo ya RC Mtanda ya kuwataka Maafisa wa NIDA Mkoa na Wakuu wa Wilaya wote wa Mwanza kuwasaidia Wafanyakazi wa majumbani kupata vitambulisho vya NIDA.
