Na Gianna Amani
China ni nchi kubwa kiuchumi na yenye idadi ya watu wengi kuliko nchi zote duniani, na ni muumini mkubwa wa teknolojia katika shughuli zake mbalimbali. Miongoni mwa mambo ya kuvutia ni namna jinsi China inavyotumia teknolojia katika shughuli zake za bandari.
Bandari ya Qingdao iliyopo katika mkoa wa Shandong, ni miongoni mwa bandari nne kubwa duniani ikihudumia makontena zaidi ya milioni 5.3 kwa mwaka. Uwezo wa bandari hiyo kutoa huduma kwa idadi kubwa namna hiyo ya makontena, unatokana na matumizi ya teknolojia, kwani miaka kadhaa iliyopita kabla ya kuanza kutumia teknolojia za kisasa, bandari hiyo ilikuwa ikihudumia makontena 2.8 milioni.
Kwa sasa bandari hiyo ambayo huhudumia mizigo ya makontena pekee, imeachana na utegemezi wa watu zaidi katika utendaji wake, na sasa inategemea sayansi zaidi. Bandari hiyo sasa inatumia magari yasiyo na dereva kuchukua makontena yanaposhushwa kutoka kwenye meli na kuyapeleka sehemu ya maegesho, magari hayo hutumia umeme.
Licha ya kuwa magari hayo yanatumia umeme, hayahitaji kwenda kuchajiwa badala yake huchajiwa wakati yakiendelea na kazi zake. Lakini mbali na magari hayo, mitambo mingine ambayo hutumika kushusha na kupakia makontena, haiendeshwi na mwongozaji wa hapo hapo, bali waongozaji hutumia kompyuta wakiwa kwenye chumba maalumu hivyo kuongeza ufanisi.
Kwa mujibu wa viongozi wa bandari hiyo, kutokana na matumizi ya sayansi na teknolojia shughuli ambayo hapo awali ilikuwa inafanywa na watu 10, sasa inaweza kufanywa na watu watatu tu.