Licha ya kusema alipewa fedha kupindua serikali, Kasanga Tumbo (ni mara chache tulikuwa tunasikia jina lake la kwanza, Christopher, ingawa nalo lilijulikana) alikuwa na uhusiano na viongozi wa maasi ya jeshi, Colito Barracks, 1964. Victor Mkello pia alikuwa na uhusiano huo. Kuna mengi bado yamefichwa lakini Kasanga Tumbo na Mkello walikuwa wanatafuta njia ya kutumia maasi hayo kumuondoa Nyerere madarakani na kuunda serikali yao. Kulikuwa na viongozi wengine katika shirika la wafanyakazi na nje ya shirika hilo waliotegemea kuwa viongozi katika serikali ya Kasanga Tumbo na Victor Mkello viongozi hao wawili wangefanikiwa kumuondoa Nyerere. Inasemekana hata Nyerere aliamini kulikuwa na uhusiano kati ya waasi na viongozi hao wa wafanyakazi. Walikuwa siyo viongozi wa kuaminika.
Kwahiyo tofauti kati ya Nyerere na Kasanga Tumbo haikuwa ni ya mfumo wa vyama tu: tuwe na chama kimoja au vyama vingi vya siasa.
Jaribuni kumshawishi Mzee Lusinde atuambie yaliyotokea wakati ule wa maasi. Anajua mengi. Wengine waliojua nini kilitokea - Kawawa, Kambona na Bomani - wameisha tuondoka. Lakini kuna wengine ambao bado ni hai. Kuna mambo mengi pia ambayo Sarakikya anayajua kwa undani. Mwingine ni Mzee Kahama.
Kuhusu Kasanga Tumbo na vitisho vyake kwamba alipewa fedha Uingereza kumpindua Nyerere, pamoja na uhusiano wake na waasi wa jeshi na kujaribu kutumia maasi hayo kuunda serikali yake pamoja na Victor Mkello na viongozi wengine, amshukuru Nyerere hakuwa kama viongozi wengine. Katika nchi zingine za Kiafrika na hata nje ya bara letu, ungekuwa ndiyo mwisho wake wakati ule. Hata kaburi lake msigejua liko wapi.
Ni muhimu tujue historia yetu. Lakini mara nyingi maswali ya aina hii yanapoulizwa, kuna wale ambao wanajaribu kupindua ukweli au kutumia historia hiyo kumshambulia na kumlaumu Nyerere bila kuangalia upande mwingine kwa nini aliamua alivyoamua kuhusu mambo mbali mbali pamoja na yale yanayohusu usalama na umoja wa taifa letu. Alikuwa na mapungufu yake. Alifanya makosa kama binadamu wengine. But he shouldn't be blamed for everything that has gone wrong in our country since independence. Apportion guilt accordingly.