Fuso,
Naomba nami nikueleze machache kuhusu Christopher Kassanga Tumbo.
Mtaa wa Kanoni Isevya, Tabora mwanzo wa mtaa kwa mkono wa kushoto kama unaelekea Kachoma, kuna nyumba ya babu yangu Salum Abdallah maarufu kwa jina la Baba Popo.
Huyu Popo ni mwanae wa kwanza ambae kwangu mimi ni baba yangu mkubwa.
Jina lake hasa ni Humud lakini hili halikushika alijulikana kwa jina la Popo hadi mwisho wa maisha yake.
Jina lake kamili lilitakiwa liwe Mwekapopo jina la babu yake aliyeingia Tanganyika kutoka Belgian Congo kama askari katika jeshi la Wajerumani miaka ya mwisho 1880 lakini kwa ufupisho akawa wanamwita Popo.
Hapo mwanzo wa mtaa mkono wa kushoto ndipo ilipokuwa nyumba ya babu yangu Salum Abdallah Mwekapopo Samitungo Muyukwa.
Yote haya majina ya Kimanyema.
Nyumba ya babu yangu ilikuwa maarufu kwa kuwa katika miaka ile ya 1950 wakati harakati za kudai uhuru zimepamba moto yeye alikuwa mstari wa mbele dhidi ya Waingereza kwanza akiwa katika TAA, TANU na TRAU.
Mwisho wa mtaa wa Kanoni kabla hujafika Kachoma ilikuwapo nyumba nyingine ya babu yangu na mkabala wa nyumba hii ilikuwapo nyumba ya Christopher Kassanga Tumbo na zote mbili ni nyumba kwa wakati ule zlizokuwa nzuri mtaa mzima.
hii Kachoma ni sehemu maarufu kwa kuwa kulikuwa na kilabu cha pombe za kienyeji.
Mwaka wa 1955 mara tu baada ya kuundwa kwa TANU babu yangu na Kassanga Tumbo waliasisi chama cha wafanyakazi wa reli Tanganyika, kikijulikana kama Tanganyika Railway African Union (TRAU) babu yangu akiwa Rais na Kassanga Tumbo Katibu.
Wakati wa likizo mwaka wa 1964 nikiwa darasa la nne nililifika Tabora kumtembelea babu yangu lakini hakuwapo nyumbani na kwa akili za kitoto hili halikunishughulisha na baada ya likizo kwisha nikarudi Dar es Salaam bila ya kumuona.
Lakini kilichotokea kwa babu yangu kutokuwa nyumbani ni kuwa alikuwa amewekwa kizuizini jela ya Uyui kufuatia maasi ya wanajeshi tarehe 20 Januari,1964 na baada ya Jeshi la Kiingereza kumaliza maasi yale, serikali iliwakamata viongozi wote wa vyama vya wafanyakazi na kuwaweka kizuizini.
Kassanga Tumbo alipata taarifa za msako wa viongozi wa vyama vya wafanyakazi mapema na akawahi kutoroka akaenda Mombasa lakini alikamatwa baadae na akarejeshwa Tanzania na kuwekwa kizuizini.
Babu yangu pia alitoweka akawa haonekani mjini na makachero wakawa wanamsaka bila mafaniko hadi alipojitokeza mwenyewe kituo cha polisi na hapo ndipo alipokamatwa.
TRAU wakati wa uhai wake TANU ilipokuwa inapigania uhuru wa Tanganyika chama hiki kilikuwa na nguvu kubwa kwani viongozi hawa wawili waliunganisha nguvu ya TRAU na TANU kupambana na Waingereza na hili lilitoa uwanja mpana sana kwa TRAU kufanya siasa za mapambano.
Mwaka wa 1960 TRAU ilifanya mgomo uliodumu siku 82 mgomo huu ulivunja rekodi ya mgomo wa Kenya chini ya kiongozi Makhan Singh wa siku 62 ambao kabla ya huu mgomo wa TRAU ndiyo uliochukua muda mrefu zaidi kumalizika.
Inasemekana ilikuwa mgomo huu ndiyo uliomtia Mwalimu Nyerere hofu kwani kwa miezi mitatu wafanyakazi wa reli waligoma na kufanya treni, meli na mabasi yasimame.
Ikamdhihirikia Nyerere kuwa hawa ndiyo viongozi wa wafanyakazi ambao atakuja kukabiliananao katika Tanganyika huru.
Hii ndiyo ikawa sababu ya yeye kuwakamata viongozi wa vyama huru vya wafanyakazi baada ya maasi na kuwaweka kizuizini na kuunda NUTA chama kipya cha wafanyakazi na kukiweka chini ya TANU.
Wakati Kassanga Tumbo anaondoka kwenda Uingereza kuchukua nafasi yake kama Balozi alikwenda kumuaga babu yangu na alimwambia kuwa Nyerere kaamua kumpeleka Uingereza kuwa balozi ili apunguze nguvu ya TRAU.
Yapo mengi sana ambayo Kassanga Tumbo na babu yangu walifanya pamoja na kushauriana.
Katika picha kulia ni Christopher Kassanga Tumbo na pembeni yake aliyevaa mgolole ni babu yangu Salum Abdallah.
Unaweza kumsoma zaidi Salum Abdallah hapo chini:
Uncle Jei Jei: Tatizo Nyerere si muislam kwa dini wala mmanyema kwa kabila. Na kibaya zaidi, baba wa mwandishi huyu, a...
mohamedsaidsalum.blogspot.com
SIKU BABU YANGU SALUM ABDALLAH ALIPOMKABILI FREDRICK MCHAURU KATIKA MGOMO WA WAFANYAKAZI WA TANGANYIKA RAILWAYS TABORA 1947 Frederick ...
mohamedsaidsalum.blogspot.com