SoC01 Huyu ndiye Kiongozi tunayemtaka Watanzania

SoC01 Huyu ndiye Kiongozi tunayemtaka Watanzania

Stories of Change - 2021 Competition

DustBin

JF-Expert Member
Joined
Jun 3, 2021
Posts
609
Reaction score
604
Duniani ni sehemu mzuri sana kuishi kama sisi wenyewe tutaifanya dunia kuwa salama kwa ajili ya maisha yetu wenyewe. Hata hivyo hatuwezi kuishi kiholela, isipokuwa inatulazimu wawepo baadhi yetu watakao simamia mambo yetu na kutuwakilisha katika baadhi ya mambo. Watu hao ni viongozi na watawala wetu. Miongoni mwa mambo yanayo pelekea kuwa na maisha ya raha duniani ni kuwa na kiongozi mwenye sifa timilifu. Sisi watanzania kama wana dunia tuna kiu na hamu kubwa ya kupata viongozi watakao tufanya tuhisi duniani ni sehemu sahihi na salama kwetu kuweza kuishi.

Zifuatazo ni miongoni mwa sifa anazotakiwa kuwa nazo kiongozi tuanemtaka, ili tuishi maisha ya fanaka;-

  1. Mchamungu mwenye kumuogopa Mungu
    Kiongozi kuwa mchamungu ndio msingi wa sifa zingine zote. Uchamungu ndio asili ya kila kitu, hivyo inahitajika kiongozi wetu awe anamuogopa Mungu katika maisha yake ya kila siku. Asiwe kiongozi muasi, mwenye kuogelea kwenye bahari ya dhambi bali awe ni mwenye kuchunga mambo yote yenye kumkasirisha Mungu na ajiepushe na ajiweke mbali na mambo hayo.
    Kawaida uchamungu wa mtu huwa moyoni mwake, lakini matendo yake hudhihirisha kile kilichomo katika moyo. Kama vile ambavyo sponji ikitoswa kwenye maziwa ikikamuliwa hutoa maziwa, na ikizamishwa kwenye maji ikikamuliwa hutoa maji ndivyo mfano wa uchamungu kwenye matendo ya mwanadamu. Hussein A. Mwinyi ni mfano mzuri katika sifa hii.

  2. Mwenye elimu na kipawa cha akili
    Kiongozi apambike kwa elimu ya kutosha aliyoipata kwa mwendelezo wa kusoma katika mtiririko mzuri. Isiwe elimu ya kubambanya na kuungaunga kiasi watu wasijue elimu yake ameipatia wapi. Sambamba na hilo awe mwenye kipaji cha akili ya ziada. Kiongozi mwenye kipawa cha akili na akawa na elimu ya kutosha kwa viwango vizuri vya ufaulu tunategema atakua anafanya maamuzi sahihi na atakua ni mwenye kufahamu na kuzingatia miiko na taratibu za uongozi bora, na kubwa zaidi atakua ni mwenye kuamini asiyeyumbishwa na walafi wa mali za uma. Mfano mzuri katika sifa hii Tundu A. Lisu.

  3. Mkweli katika kauli zake na matendo yake
    Ukweli unamuweka mtu huru. Kiongozi akiwa mkweli kwa anaowaongoza inamfanya awe na uwezo wa kutumainiwa na anajiondosha kwenye tuhuma na kupunguza idadi ya watu kuhoji. Tunahitaji kiongozi atakaesema kweli, nyeupe aseme nyeupe na nyeusi aseme nyeusi. Asiwe na ndimi mbili kiasi jana alisema hiki na kesho anakuja kusema kingine akaleta mkanganyiko kwa anaowaongoza. Unafiki kwa kiongozi sio sifa nzuri.
    Zaidi ya hapo tunahitaji kiongozi aliye muwazi asiwe msiri na situfiche mambo yanayotuhusu sisi anaetuongoza. Profesa Asad anaweza kuwa mfano wa kuigwa katika ukweli na uwazi.

  4. Mwenye kujiweza kiuchumi
    Kwa hali tuliyofikia Tanzania leo tunahitaji kiongozi aliyejitosheleza kiuchumi. Kama ni utajiri awe nao tangia hapo na uongozi usiwe njia ya yeye kutafuta utajiri. Matatizo mengi tunayokumbana nayo ni kutokana na viongozi wengi wanaotuongoza kutaka kujitajirisha kupitia nyadhifa zao na ndio maana rushwa, unyonyaji na ubadhilifu haviishi. Kiongozi mwenye nguvu ya kiuchumi anakua na uwezo wa kuwawajibisha wa chini yake hata kama wanajiweza kimali na hali. Donald Trump ndie mtu sahihi wa kupigiwa mfano kwa hili.

  5. Jasiri asiyeogopa
    Ujasiri ni mtu kufanya jambo sahihi ambalo kwa wengine linaonekanwa kutowezekana kufanywa na yeye kutokana na vikwazo fulani. Nje ya mamlaka aliyonayo, binafsi kiongozi anatakiwa awe jasiri katika kufanya maamuzi magumu. Katu asiogope vitisho na blabla za wapiga vigelegele hasa anapopanga kufanya jambo husika. Tunaitaji kiongozi kama Joseph P. Magufuli katika ujasiri, kwani yeye ni kiongozi wa kupigiwa mfano.

  6. Mpole, mwenye huruma na msikivu
    Kiongozi bora awe msikivu awasikilize anaowaongoza na kuzingatia rai na maoni yao. Hata anapopitisha jambo lake awe mpole na awahurumie sana anaowaongoza. Kuwa jasiri haimaanishi usiwe na huruma, au usiwe msikivu, la hasha! Ujasiri ukiambatana na upole na usikivu humfanya kiongozi kuwa na huruma kwa anaowaongoza. Tujifunze kwa Samia. S. Hassani katika hili yeye ni mfano mzuri wa kuigwa.

  7. Asiwe mwenye chuki na vifundo katika moyo wake
    Kila mtu anao maadui zake hilo haliepukiki, hata uwe vipi lazima watakuwepo watakaokupinga. Kama walipingwa na kuchukiwa manabii wewe usichukiwe nani? Hata hivyo kiongozi anatakiwa awe na maono au mawazo chanya juu ya mahasimu na maadui zake. Daima asiwe na mafundo moyoni mwake dhidi ya wale wasiompenda au kumkwamisha katika utendaji wake, bali ayabebe hayo kama ni changamoto tu ndogondogo katika uongozi wake. Jakaya M. Kikwete anafaa kupigiwa mfano kwa sifa hii.


HITIMISHO

Kiongozi mwenye kuwa na sifa hizi moja kwa moja huwa ni kiongozi mwenye kufuata misingi ya utawala bora, ni kiongozi mwenye kuchunga haki za anaowaongoza, mwenye kuwatekelezea anaowaongozwa matakwa yao kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa kikatiba.

Hivyo kwa sisi watanzania tunahitaji kiongozi mwenye kukusanya sifa hizi zote na zingine za ziada ili nchi yetu iweze kufika tunapotamani kufikia. Ingawa kuna baadhi wanaweza wakasema ni muhali mtu mmoja akawa na sifa hizo zote, lakini inawezekana kumpata mtu huyo kwani hakuna kisichowezekana chini ya jua.


DustBin
 
Upvote 0
Back
Top Bottom