Waziri Karamagi aunga mkono TANESCO kupandisha umeme
Na Joseph Lugendo
WAZIRI wa Nishati na Madini Bw. Nazir Karamagi ameunga mkono mapendekezo ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupandisha bei ya huduma zake kwakuwa shirika hilo linatakiwa kujiendesha kibiashara.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari muda mfupi baada ya kufungua Warsha ya Wadau wa Mafuta ya Petroli iliyohusu majukumu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dar es Salaam jana, Bw. Karamagi alisema ongezeko la bei limetokana na kuondolewa kwa ruzuku ya Serikali iliyokuwepo kabla ya mapendekezo hayo.
"Si busara kuendelea kutumia fedha za bajeti kutoa ruzuku kuendeshea TANESCO," alisema Waziri Karamagi na kuongeza kwamba wahisani wataishagaa Tanzania ikiwa fedha wanazotoa kupitia mfuko wa bajeti zitatumika kutoa ruzuku kwenye shirika ambalo linazalisha.
Alitaka jamii ielewe kwamba hakuna shinikizo lolote kutoka kwa wahisani kutaka kuondolewa kwa ruzuku hiyo na kuongeza kwamba ni vyema shirika hilo likajiendesha kibiashara.
Hata hivyo, Bw. Karamagi alisema Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) wanayo mamlaka ya kupunguza bei inayopendekezwa kwa kuangalia upotevu wa mapato ulio ndani ya TANESCO kwa kuagiza shirika hilo kufidia sehemu itakayo punguzwa kwa kuziba pengo la upotevu wa mapato litakalobainika.
Kuhusu malalamiko ya wananchi yanayoashiria kupinga ongezeko hilo, Bw. Karamagi alisema wananchi wanaopata huduma ya nishati nchini ni asilimia 10 tu na kwamba wanaopinga ongezeko hilo ni asilimia 8 wanaoishi mjini na ambao wanauwezo ukiwemo wa kusema na kusikika.
"Tunapozungumza ongezeko la bei lazima tulinganishe na wengine ndio tufahamu hali halisi," alisema Bw. Karamagi na kuongeza kuwa hakuna mtu anayependa kuongezewa bei na kwamba wengi wangefurahi kama ingekuwa bure.
Alifafanua kwamba Serikali haihusiki kwenye upangaji wa bei na kwamba ikiwa ongezeko la asilimia 40 ya bei litakubaliwa na EWURA, bado bei hizo hazitazidi zilizopo katika nchi za Afrika Mashariki.
Akielezea hali ya mahitaji ya huduma hizo kwa wateja wapya wa vijijini Bw. Karamagi, alisema Serikali itaendelea kutoa ruzuku vijijini kupitia chombo kilichopo cha Wakala wa Umeme Vijijini.
Kuhusu taarifa za kujiuzulu kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Dkt. Idris Rashid, Waziri Karamagi, alisema shirika hilo lina Bodi ya Wakurugenzi ambayo imepeleka ripoti ofisini kwake wakati anakwenda kufungua warsha hiyo na kuwataka kusubiri mpaka atakapopitia ripoti ya Bodi hiyo.
Aliitaka jamii kuelewa kwamba Dkt. Rashid hakufukuzwa ila atakuwa amejiuzulu mwenyewe jambo ambalo ni hiyari yake kama ilivyo kwa mtu yeyote kuacha kazi anapoona hayupo tayari kuendelea nayo.
Source: Majira
Kwa maelezo haya Dr Idris Rashid amejiuzulu au hajajiuzulu?