CCM TAYARI IMESHASHINDA IGUNGA!
Jana jioni katika pitapita zangu za kupata moja baridi na moja moto nilishuhudia vichekesho kwenye baa moja ya hapa Tandika.
Watu watatu waliojiita vijana wa CCM ASILIA waliingia kwenye baa na wakawanunulia bia wateja wote waliokuwepo kwenye baa. Tulikuwa kama watu 5 kwenye baa kwa wakati ule. Walipoulizwa wanasherehekea nini, mmoja wao alijibu kwa sauti kali tena ya juu sana " tunasherehekea
ushindi wa Igunga". Mlevi mmoja akasimama na akawauliza kwa taratibu kuwa... "mbona uchaguzi bado?". Kijana wa CCM akajibu kwamba... "ushindi kwa CCM ni tayari na iliyobakia ilikuwa ni matokeo tu". Kwa kweli wote waliokuwepo kwenye ile baa waliacha kugida chupa zao na wakataka kujua ushindi huo umejulikanwa vipi wakati uchaguzi ni bado.
Akaendelea kijana wa CCM kuwa..." Matokeo ya Jumaapili yatakuwa ni kushinda au kushindwa kwa CCM. Matokeo yoyote yale ni ushindi kwetu sisi wana-CCM na ndio maana tunasema mapema kuwa CCM tayari imeshashinda Igunga". Alipoulizwa kijana ajieleze vizuri vipi kushindwa kutakuwa ni ushindi kwa CCM, kijana alisema... "Kukosa mbunge mmoja haina maana serikali ya CCM itaanguka. Tukishinda ndio furaha yetu,
lakini tukishindwa tutakuwa wa mwanzo kukubali matokeo. Nia yetu ni kuonesha kwamba sisi tunayapokea matokeo yoyote yale ya wananchi kwa mikono miwili, kwani tumebobea kwenye demokrasia".
Akaendelea kijana kuwa..." tukishindwa itakuwa ni vizuri zaidi kwetu sisi CCM, kwani tutaweza kuuonesha Ulimwengu kuwa matokeao ya 2010 hayakuchakuliwa na kuwa sisi tunakubali kushindwa na kushinda".
" Hawa watu bado wanaendelea kumuona Rais wetu kuwa ni illegitimate japokuwa wanasema ni legal. Sasa kama wakishinda wao na tukayakubali matokeo hio itakuwa kama kifuta machozi kwao na wataanza kujua kuwa sisi ni wapenzi wa kweli wa demokrasia na kuwa matokeo ya 2010 hayakuchakuliwa hata kidogo" alimalizia kijana. Kwavile watu walikuwa wenye kiu, hapakuulizwa masuala zaidi baada ya hapo na kila mtu akajimalizia bia zake 2 alizonunuliwa na akajiondokea zake.
Kwa kweli nilidhania kuwa mmoja wa wale vijana labda alikuwa ni Dr. HK, lakini ninahakika kuwa hakuwa yeye, kwani yeye bado yupo huko Igunga kwa sasa na pia nimeelezwa kuwa Dokta sio mtu wa baa.