Mchuano wa vyama waanza Igunga
WANASIASA 26 wamejitokeza kuwania kuteuliwa na vyama vyao kuwa wagombea wa ubunge katika Jimbo la Igunga mkoani Tabora katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu.
Jimbo la Igunga limeachwa wazi na aliyekuwa mbunge wake, Rostam Aziz ambaye alijiuzulu nafasi hiyo sambamba na nyadhifa zake zote ndani ya CCM Julai 14, mwaka huu.
Mpaka sasa ni vyama vya CCM, Chadema na CUF tu vilivyoonesha nia ya kuwania kuwania jimbo hilo huku vingine mbali na kutotangaza kutoa fomu, lakini pia vikikosa kuonesha hata bendera kama inshara ya kuwemo katika kinyang'anyiro hicho.
NCCR-Mageuzi imetangaza kutowania jimbo hilo na kutaka upinzani usimamishe mgombea mmoja. Jumamosi CCM ilifunga pazia la uchukuaji fomu hizo huku kukiwa na wagombea 13 wakati Chadema ikiwa na wagombea 12 huku ikitarajia kufunga pazia ya uchukuaji fomu hizo Jumanne.
Kwa upande wa CUF, Naibu Katibu Mkuu wake, Julius Mtatiro Jumapili alitangaza uamuzi wa chama hicho kumsimamisha Leopard Mahona (30) kuwa mgombea rasmi wa ubunge Igunga.
Akizungumza na 'Habarileo', Katibu wa CCM wa Wilaya ya Igunga, Neema Adamu alisema Agosti 18, mwaka huu Kamati ya CCM Mkoa itapitisha jina la mgombea wao.
Neema alisema katika uteuzi wa mgombea wa CCM, kura za maoni zitapigwa na wanachama wa matawi ya chama katika jimbo hilo.
Wanachama waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kupitia CCM ni Amina Ally Said, Ngassa Nicolaus, Shams Feruzi, Adama Brauni na Shell David na Dk. Dalaly Peter Kafumu ambaye ni Kamishna wa Madini nchini na aligombea mwaka jana na kushindwa na Rostam Aziz.
Wengine ni Makoba Mchenya, Joseph Omary, Self Hamis Gulamaly, Hamis Shaabani, Nathan Mboje, Hamadi Safari na Paul Ndohele.
Naye Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Chadema, Waitara Mwikabwe alitaja wanachama waliochukua fomu za Chadema kuwa ni Kajua Sebastiani na Marco Amos.
Wengine ni Kahema John, Buzinza Magego, Dickson Samsoni, Anwari Luhumbi, Erasto Tumbo, Joseph Mwandu, Juma Katigula, Frank Matto, Joseph Mapalala na Juma Chaha.
Baada ya kufunga pazia la kuchukua fomu hizo Jumanne saa 10 jioni, Mwikabwe alisema kamati teule ya chama hicho itafanya kazi kupitia majina hayo na kuteua mgombea atakayepeperusha bendera yao.
Mtatiro kwa upande wake alimsifu mgombea wa chama hicho kuwa mbali na kuwa mwenyeji wa Igunga, ana uwezo wa kujenga hoja na utawala na kwamba kwa sasa CUF inafanya kazi ya kuimarisha mtandao wake katika jimbo hilo.
"Harakati zinazoendelea kuimarisha mtandao wa CUF wa kuibuka na washindi, Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF ilikutana mjini Zanzibar ambapo pamoja na mambo mengine ilimpitisha rasmi Mahona.
"Mahona alipata kura zaidi ya nusu ya kura za Rostam na ndiye aliyepigana mpaka mwisho na kushinda vishawishi," alisema Mtatiro.
Alisema katika jimbo hilo CUF imeingia na operesheni chagua Mahona ambayo ni ya ushindi yenye lengo la kuhakikisha inashinda kwa kutumia uzoefu wake na mtandao.
Mtatiro alisema chama hicho kilituma vikosi mkakati ili kuweka sawa mazingira ya ushindi na kwa tathmini ya awali, anaamini chama chao kitapata mchuano mkali kutoka CCM.
Alisema tayari wana mkakati mzito wa kukabiliana na CCM kuhakikisha mgombea wao anapata ushindi na kuahidi kufanya kampeni za kistaarabu za kutangaza sera kwa wapiga kura kama Sheria ya Uchaguzi inavyotaka.
Kuhusu gharama zitakazotumika katika uchaguzi huo, alisema kwa mujibu wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi, Igunga ni miongoni mwa majimbo ambayo yanapaswa kutumia fedha zisizozidi Sh milioni 80.
Hivi karibuni, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa alipiga marufuku vyama ambavyo vilikuwa vimeanza kufanya kampeni mapema kabla ya kupata ridhaa hiyo ya kuhalalisha kampeni hizo.