CCM imezindua ilani yake ya uchaguzi wa 2015 - 2020.Katika ilani hiyo imeanisha kuwa vipaumbele ni Kupambana na umaskini,kupambana na rushwa,Ajira kwa vijana,Ulinzi na Usalama.Aidha CCM ina ahidi upya kuborsha miundombinu,kukuza uchumi,kuboresha viwanda,nishati,kilimo sanaa na michezo. Kabla ya kuamini na kuikubali ILANI hii ya CCM naomba tuchambue kwa ufupi ahadi hizo kwa miaka 54 ya Uhuru na Utawala wa TANU - CCM.
1. Kupambana na umaskini - CCM imeshindwa kabisa kupambana na umaskini kwa miaka yote 54.Umaskini umefikia hatua ya kutisha kiasi kwamba hata mlo mmoja umekuwa ni shida vijijini na mijini.Mgombea wa UKAWA naeleweka kidogo kwa kuwa amekuwa akisema kila wakati kwamba anauchukia umaskini na atapambana nao kwa nguvu zake zote.Unaweza vipi kukiamini chama kilichouwepo madarakani kwa miaka 54 na kikashindwa kabisa kuuondoa umaskini huo?MKUKUTA na MKURABITA imebaki kuwa katika makabrasha tu.Wachache ndio wanaonufaika na rasilimali za nchi.
2. Ajira kwa vijana - Hali ya ajira kwa vijana wa Tanzania ni janga ambalo linakaribia kuleta madhara. Mifano ni mingi.Vijana maelfu kwa mamia hawana ajira za kuaminika na wamekuwa wakihaha kujipatia ridhiki zao ili hali watoto wa vigogo wakichukua ajira muhimu za nchi.Kwa kijana maskini asiye na wa kumshika mkono hawezi kupata ajira kamwe.Uhamiaji walitangaza ajira kama 70 walijitokeza vijana zaidi ya 10,000 kuomba ajira ambazo pia walipatiwa watoto wa vigogo japo vyombo vya habari viliingila kati.Mh. Lowassa aliwahi kusema mara kwa mara kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana ni bomu linalosubiri kulipuka.Yeye yupo tayari kutatua kwa dhati tatizo la ajira kwa vjana wa Kitanzania wakauaga umaskini kwa rasilimali za nchi yetu.
3. Ulinzi na usalama - Hali ya usalama wa nchi ni mzuri.Hali ya usalama wa wananchi ipo matatani. Wananchi wa kanda ya Ziwa wanauawa kwa kukatwa makoromeo na serikali imekaa kimya hakuna hata tamko. Albino wanauawa na wengine wanakatwa viungo vyao.Jeshi la Polisi limekuwa likipambana naraia wasiokuwa na silaha kwa nguvu kubwa. Viongozi wa vyama upinzani na waandishi wa habari wamekuwa wakishambuliwa na idara nyeti za ulinzi na usalama.Matumizi ya mabavu kwa majeshi yetu yameondoa dhana nzima ya ulinzi na usalama kwa wananchi wa Tanzania ndani ya taifa lao. Wageni kutoka nchi jirani wamekuwa wakiingia Tanzania na kufanya shughuli zao huku wakihatarisha usalama wan chi na wanaohusika wakiaminika kupokea chochote.
4. Rushwa Hali ya rushwa ( Matumizi mabaya ya mali/Ofisi za umma kwa manufaa binafsi) ni tete nay a kutisha. Magali na vyombo vya usafiri vya Taifa vimekuwa vikitumika na Viongozi wa CCM nje ya utaratibu.Watumishi wa umma wamekuwa wakifanya kazi za chama ama zao binafsi na hivyo kuisababishia Nchi hasara kubwa katika muda ama Ofisi za Serikali.Hongo katika CCM imekuwa ya kupitiliza nay a kutisha.Viongozi wengi waliobwaga manyanga wanalalamikia hongo na rushwa katika kuwapitisha Viongozi katika uchaguzi. CCM itawezaje kutatua taizo la rushwa nchini ilihali imeshindwa kutatua ndani ya chama chake? Wala rushwa wengi na wakubwa wapo CCM.Mikataba ya kiulaghai imesainiwa na Viongozi wa Serikali chini ya CCM.Viongozi waandamizi wanatetea upuuzi huo.Hii ni hatari kubwa.
5. Ujenzi wa Miundombinu Pamoja na jitihada zinazoelezwa barabara nyingi zimejengwa chini ya kiwango kwa gharama kubwa.Paul Makonda amekaririwa akilalamika ujenzi duni katika Wilaya yake tu ndani ya Dar es salaam. Kwingine kukoje? Mkoa kama wa Morogoro bado haujaunganishwa na Ruvuma kwa barabara hata ya vumbi ukiacha ile ya wafugaji wa Kisukuma. Kwa chama kilichokaa mdarakani kwa miaka 54 haitoshi.Kinahitaji PUMZIKO.
6. Kukuza uchumi Uchumi wan chi umeporomoka kwa kasi ya ajabu. Bei ya mazao ya biashara nje imeshuka sana. Fedha za kigeni zimepanda na Shilingi imeshika kwa kasi ya ajabu. Shughuli za Kiuchumi kama Kilimo kimedidimia kutokana na kukosa pembejeo.Wawekezaji wa ndani na nje hawana habari kuwekeza katika kilimo kwa kuwa maeneo yanayolipa kwa haraka kama madini na gesi yapo nje nje. Bidhaa za ndani hazina soko kabisa na sasa tunatumia njiti za meno,sabuni,viberiti,nyembe,mishumaa,madodoki,soksi,chupi,leso,sidiria,njiti za masikioni nk kutoka nje.Viwanda vyetu havina thamani na vingine vimefungwa kabisa.Lowassa ameahidi kufufua viwanda kama General Tyre na vingine vingi.
7. Nishati Ni janga la Taifa kama majanga mengine. Mkoa unaopata umeme muda wote ni Kagera tu kwa kuwa unachukua nishaiti hii kutoka Uganda.Vyanzo vya kuzalisha umeme wa kutosha tunavyo shida ni uzembe na rushwa za Viongozi wetu.Vyanzo vinavyotajwa sasa vya gesi tayari vimetekwa na wawekezaji na wananchi hawataambulia lolote.Vijana wanaotegemea umeme kwa ajili ya saloon,uchomeleaji,usindikaji wa bidhaa,viwanda vidogo na vikubwa ni kero.
8. Kilimo Ukosefu wa pembejeo na matumizi ya jembe la mkono ambalo liltakiwa kuwa Makumbusho ya Taifa ni shida. Mkulima anahangaika mwaka mzima anachopata hakikidhi hata kwa miezi mitatu. Mkulima anaconda,mifugo inakonda na mfugaji anaconda pia. Masoko imekuwa ni kero nyingine. Viongozi wapo radhi kuleta mchele wa Thailand na kuuzwa kwa bei ya chini huku mchele wa Tanzania ukikosa soko. Sukari ya Tanzania inakosa soko nay a nje inauzwa kwa bei poa huku wafanyabiashara wakikwepa kodi.
9. Sanaa na michezo Kama kuna mahali serikali ya CCM imeshindwa kuendana na wakati ni katika Nyanja hii.Imeshindwa kuweka misingi bora na imeishia kuwekeza katika ushindi wa kubahatisha wa Timu za Taifa.Ni lazima uwekezaji uanzie chini na kwa usimamizi bora. Sanaa za maonesho zimeingiliwa.Tunu za Taifa hazijulikani.Wasanii na wanamichezo wameshaulika. Wanaokumbukwa ni wakina Diamond na Mrisho Mpoto lakini sio wakina Jangala na Pembe.Wengine wameishia kufa vifo vya aibu kutokana na kukosekana kwa misingi na sheria zakuwalinda. Kilichopo ni kuwapa kwa mkono huu na kuwanyanganya kwa mkono ule.
HITIMISHO
CCM haina jambo jipya la kutudanganya Watanzania kuwa tukiweke tena madarakani. Wakati umefika CCM ipumzike ili ijitafakari na kujipanga kwa wakati mwingine. Viongozi wamepoteza dira na chama kimepoteza mwelekeo. Hawazungumzi lugha moja tena na walio wengi wamekwama kwenye tope kubwa na hawawezi kujikwamua. Wanahitaji MABADILIKO ya UHAKIKA.Na UKAWA ndio mwisho wa MABADILIKO.