Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Mwalimu JK Nyerere na Bw. Patwas kualia kwake unapoitazama picha. Kulia mwenye koti na kofia Mzee Rashid Makoko Babu na wa pili yake ni mwanae Mamboleo Makoko na kushoto mwenye koti na kofia mzee Makata Mwinyimtwana.
Patwa alikuwa Muislam wa madhehebu ya Shia. Patwa alikuwa amehamia Tanganyika kutoka Zanzibar mwaka 1918 baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Kwanza. Pale Tanga Patwa alianzisha kiwanda cha soda na akatajirika. Wakati huo wa zama za ukoloni wakati Waasia wenzake walikuwa wakiwabagua Waafrika, Patwa alikuwa akikaa na Waafrika wa rika lake akinywa nao kahawa. Halikadhalika watoto wake wakawa wanacheza kandanda na vijana wenzao wa Kiafrika katika vilabu vya Tanga. Hili lilikuwa jambo geni na lisilokuwa la kawaida kutoka kwa familia ya Kiasia wakati wa ukoloni. Patwa alisaidia harakati za kudai uhuru kwa hali na mali, na akaifanyia kampeni TANU miongoni mwa jamii yake mwenyewe ya Kiasia. Wakati wa harakati Nyerere alikuwa akifanyiana maskhara na Patwa akimwambia, ‘’Mzee Patwa baada ya kupata uhuru nadhani tukuteuwe uwe balozi wetu India.’’ Lakini Patwa hakuiona Tanganyika huru, alifariki kabla ya uhuru kupatikana.
Baada ya kufungua tawi la TANU mjini Tanga, uongozi wa chama ulimwalika Julius Nyerere, Bibi Titi Mohamed, John Rupia na Mbutta Milando kufanya ziara Tanga. Nyerere alifikia nyumbani kwa Hamisi Heri. Ujumbe huu kutoka makao makuu ya TANU ulipata makaribisho makubwa yaliyoandaliwa na vyama vya lelemama ambavyo kwa kawaida vilikuwa vingi sana katika pwani ya Afrika ya Mashariki kutoka Mombasa nchini Kenya hadi Mikindani, Tanganyika. Kiongozi wa akina mama hawa mjini Tanga aliyesaidia kuieneza TANU alikuwa Bibi Mwanamwema bint Sultan, ndugu wa mbali wa mwenyekiti wa TANU Tanga, Hamisi Heri.
Matokeo ya ziara ya Nyerere Tanga ilikuwa ni kumrudisha Mwalimu Kihere katika siasa. Baada ya kushindwa kupata nafasi yoyote katika chama, Mwalimu Kihere alipoteza shauku ya siasa. Nyerere alipokuja Tanga kuifanyia kampeni TANU ndipo Mwalimu Kihere alikaribishwa kujiunga na chama. Mwalimu Kihere alifahamiana na Nyerere mwaka 1946 walipokutana Dar es Salaam katika mkutano wa mwaka wa African Association. Nyerere alipozuru Tanga Mwalimu Kihere alitaka kufanya dhifa nyumbani kwake kwa heshima yake. Uongozi wa TANU, hususan Hamisi Heri na Mzee Makoko walikataa kumruhusu Nyerere kuhudhuria dhifa hiyo kwa sababu Mwalimu Kihere alikuwa hajaonesha kuiunga mkono TANU. Nyerere akitambua utu uzima wa Mwalimu Kihere, uzoefu na sifa yake ya uongozi katika African Association, alishauri uongozi wa TANU Tanga usiache fursa ile ipite bure. Nyerere alitoa hoja kuwa, ilikuwa muhimu kukubali mwaliko wa Mwalimu Kihere na kutumia fursa hiyo kumuomba arudi kwenye harakati kwa kuwa TANU ingefaidika kutokana na uzoefu wake alioupata katika African Association. Kwa ajili ya nasaa hiyo TANU ilikubali mwaliko wa Mwalimu Kihere na Nyerere alihudhuria dhifa ile nyumbani kwa Mwalimu Kihere pamoja na wanachama wengine.
Mwalimu Kihere
Mwalimu Kihere alikuwa mwanasiasa wa msimamo wa wastani, alikuwa mbali na msimamo mkali dhidi ya serikali. Kwa ajili hii Mwalimu Kihere alielewana vizuri na utawala wa kikoloni. Hii ilikuwa kinyume kabisa na wazalendo wengine kama Mzee Makoko Rashid ambaye kwa miaka mingi alijulikana kwa chuki yake dhidi ya Waingereza. Inasadikiwa kwamba watu wawili wataingia katika historia kwa chuki zao mahsusi dhidi ya Waingereza, mtu wa kwanza ni Abdillah Schneider Plantan na wa pili ni Mzee Makoko Rashid. Wote wawili walifungwa gerezani kwa sababu ya msimamo wao dhidi ya serikali ya kikoloni. PC na DC wake wote wawili walikukubali mwaliko wa Mwalimu Kihere. Mwalimu Kihere alimtambulisha Nyerere kwa wageni mashuhuri na alimuomba azungumze maneno machache. Nyerere kwa kipaji chake cha ufasaha wa kuzungumza alitoa hotuba kuhusu lengo la TANU na kanuni za kidemokrasia kama zilivyoelezwa na Umoja wa Mataifa. P.C. alisimama baada ya Nyerere kuzungumza na akatoa hotuba kwa niaba ya serikali. P.C. alimsifu Nyerere kuwa ni mwanasiasa mzuri kinyume na vile alivyosikia kabla ya kukutana naye. Hapo hapo alitoa ruhusa kwa Nyerere na TANU kufanya mikutano ya hadhara katika wilaya zote za jimbo hilo. Lakini uhusiano huu haukudumu, serkali iliyapiga marufuku matawi kadhaa ya TANU Tanga mara tu baada ya kuundwa kwa UTP.
Siku iliyofuata mabingwa wa hotuba wa TANU, Julius Nyerere na Bibi Titi Mohamed walihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Tangamano. Hii ilikuwa hatua kubwa sana kwa TANU, na kwa harakati dhidi ya ukoloni pale Tanga. Ilikuwa muda mrefu umepita tangu zile siku za zile siasa za wasomi katika Discussion Group, kikundi cha majadiliano; na ile mizozo baina yao na ule uongozi Waarabu katika TAA. Baada ya hapo, Mwalimu Kihere alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TANU Tanga badala ya Hamisi Heri na Amos Kissenge alichaguliwa katibu. Abdallah Rashid Sembe mmoja wa wanachama waasisi wa mwanzo kabisa wa TANU alichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU akiwakilisha Jimbo la Tanga.
Ilikuwa chini ya hali ya hewa ya kisiasa kama hii ndipo TANU iliingia kwenye uchaguzi wake wa kwanza katika Tanganyika, chaguzi wa Kura tatu wa mwaka wa 1958 Tanga ambako United Tanganyika Party (UTP) ilikuwa imara, TANU iliwachagua John Keto, B. Krishna na R. N. Donaldson kama wagombea wake. John Keto akiwa miongoni mwa walimu wa St. Mary’s School, Minaki na alikuwa amefanya kazi kubwa katika siku za mwanzo kufungua matawi ya TANU huko Kisarawe. TANU iliamua kumteua Keto kusimama Tanga ambako ndiyo kulikuwa kwao. Katika uchaguzi huu serikali iliacha uandikishaji wa wapiga kura kwa vyama vyenyewe. Mzee Makoko Rashid, mwanasiasa wa makamo mwenye msimamo thabiti wa chama na kijana Mmaka Omari walikuwa maofisa waandikishaji wa wapiga kura katika wa TANU mjini Tanga. Makoko na Mmaka walikamatwa na kushitakiwa kwa kosa la kuwaandikisha watu ambao hawakutimiza masharti yaliyoelezwa na ilani ya uchaguzi. Katika ghera yao kwa TANU kushinda ule uchaguzi muhimu, Mzee Makoko alimsajili Mwafrika yoyote aliyetaka kuipigia kura TANU bila kujali sifa zake. Bhoke Munanka alikamatwa vilevile kule Mwanza kwa kosa hilo hilo. Hakukuwa na ushahidi wa kutosha dhidi ya Mmaka Omari kwa hiyo aliachiwa huru mara tu baada ya kukamatwa kwake. Mzee Makoko Rashid alipatikana na hatia na alihukumiwa kufungwa jela. Adhabu ya kifungo ilidhoofisha sana afya yake na mara baada ya kufunguliwa kutoka gereza baya sana la Maweni Mzee Makoko alifariki.
Iweje leo hawa mashujaa hakuna kumbukumbu zao Tanga ukitoa Makoko Road. Hivi ule Mtaa wa Maua pale katika ya mji una akisi kitu gani? Dessa una sauti CCM wakumbushe na wazindue kuhusu historia hii kama hawaijui mimi nitakuja kwa nauli yangu kuja kutoa mhadhara In Shaa Allah.
Mkutano wa Tabora ulitishia kuigawa TANU katika makundi hasimu yaliyokuwa yakivutana, kama isingekuwa kwa ule mkakati uliopangwa kule Mnyanjani, kijiji kidogo nje ya mji wa Tanga. Waliopanga mkakati huo - Nyerere mwenyewe, Amos Kisenge, Hamisi Heri, mwenyekiti wa TANU Tanga, Mwalim Kihere mwanasiasa mkongwe wa African Association, Sheikh Abdallah Rashid Sembe, Ng’anzi Mohamed, Mustafa Shauri na Abdallah Makata - Hawa ndiyo waliinusuru TANU isinase katika mtego uliotegwa na wakoloni ambao ungeifanya TANU igawike katika mapande mawili na kila moja dhaifu kuweza peke yake kuikabili serikali ya kikoloni.