Innocent Killer (The Revenge)

STORY: INNOCENT KILLER (THE REVENGE)
STORY WRITER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP : 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
SEHEMU YA 40

SONGA NAYO............
Vyombo vya habari vilikuwa viko busy sana kuongelea jambo moja hata mtaani watu walikuwa wamejazana kila sehemu wakiwa wanaongelea jambo moja ambalo liliishtua nchi majira hayo ya asubuhi, kilichokuwa kimeleta taharuki yote hiyo ni makaratasi ambayo yalikuwa yamesambazwa na kubandikwa kila sehemu ndani ya jiji la Dar ndicho kitu ambacho kilizua hiyo taharuki kubwa sana ndani ya hili jiji, yalibandikwa kuanzia kwenye nguzo za umeme, maofisi mbali mbali, kwenye mabango ya barabarani, kwenye vituo vya mabasi, treni, airport, viwandani, mpaka kwenye sehemu za biashara na masokoni. Maofisa wa polisi walisambazwa kila sehemu ili kuhakikisha karatasi hizo zinabanduliwa na kuondolewa kwa haraka sana lakini waliacha mara moja baada ya kupokea maagizo kutoka kwa IGP kwamba waache mara moja hicho walichokuwa wanakifanya kwa sababu walikuwa wanaelekea kulichafua jeshi la polisi.

“Mkuu hivi unahisi kuwazuia kuyatoa makaratasi hayo ni maamuzi sahihi sana” UTAPEWA alikuwa yupo karibu sana na IGP siku hiyo kwa sababu ndiye mtu ambaye aliwahi ofisini kwa bosi wake Kwenda kutoa hizo taarifa ambazo zilikuwa zinaonekana kuanza kuongelewa sana kila sehemu.

“Huo ndio uamuzi bora zaidi ambao utatuweka sisi kwenye mikono salama lasivyo tutajichafua sana na jeshi la polisi tutaonekana hatuna maana yoyote ile”
“Kivipi mkuu sijakuelewa”
“Angalia kilicho andikwa kwenye hayo makaratasi kisha pima hali ya wananchi kwenye vichwa vyao kwa sasa, kilicho andikwa ni kitu ambacho wao wanataka kifanyiwe kazi sasa ukianza kuyatoa utaamanisha nini? watajua kwamba huenda kuna mambo tunayaficha ndiyo maana hatutaki kuwaunga mkono watu ambao wamejitokeza kupambana na hiyo hali ambayo ilikuwa ianendelea kwenye nchi yetu. Ukiachana na hilo hizo habari zipo kila sehemu mpaka kwenye vyombo vikubwa vya habari kuanzia mtandaoni, kwenye runinga mpaka kwenye simu unahisi hapa ukizitoa utakuwa umefanya nini zaidi ya kupoteza muda” jibu la IGP lilimfanya kijana huyu ambaye siku ya kwanza wakiwa wameenda kuangalia sehemu ambayo jaji mkuu aliuawa walizinguana sana na ASP Bakari Zalimo ambaye alikuwa mkubwa wake kwa cheo naye ndiye alikuwa msaidizi wake lakini hawakuwa wakiiva sana kwa sababu Utapewa alikuwa anapenda sana kuchukulia mambo mazito kiwepesi mno.

“Nimekuelewa mkuu, kwahiyo kinatakiwa kifanyike nini?”
“Asp atakupa maelezo yote nini cha kufanya, yuko wapi kwanza?” alikunja sura baada ya mtu huyo kutajwa hapo
“Bado hajafika”
“Mpigie simu haraka sana mwambie namhitaji ofisini sasa hivi”
“Sawa mkuu” aliinyanyua simu yake wakati anataka kupiga Asp Bakari Zalimo alitokea kwenye hiyo sehemu na kutoa heshima kwa IGP hivyo hivyo Utapewa naye alitoa salamu kwa Asp ambaye hata hakuhangaika kumjibu chochote kile

“Nifuate ofisini”IGP alitamka akiwa anaanza kuondoka na Asp huyo alianza kumfuata, aligeuka kumwangalia Utapewa alikuwa anamwangalia jicho baya sana
“Ipo siku utaingia kwenye kumi na nane zangu tu” Utapewa alitamka mwenyewe kwa hasira sana akiwa anatoka hiyo sehemu na Kwenda kwenye ofisi yake kusubiri maagizo ambayo angekuja kupewa.

“Umeona kinacho endelea?”
“Mimi ndiye niliye ifanya hiyo kazi” maneno yake yalimfanya IGP ageuke na kumwangalia sana kijana wake huyo
“Ulikutana naye mara ya mwisho lini na wapi?
“Jana usiku, alinifuata Keko kwenye lile eneo langu”
“Ilikuaje?”
“Alikuja lile eneo nilishangaa sana imekuaje mpaka akajua nipo pale baadae akaja kunambia kwamba simu yangu ndiyo iliyo nifanya nijulikane, ila kilicho nishangaza anaonekana kwamba ananijua zaidi ya pale mpaka nilibaki namshangaa sana, nakumbuka kauli yake ya mwisho aliniambia kwamba nichapishe hizo karatasi kisha nitafute vijana wengi sana wazisambaze sehemu zote za jiji la Dar huku akiwa ameniachia milioni 50 za kitanzania kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo. Nilijiuliza sana huyu mtu ni nani mpaka ananiagiza mimi kazi hiyo ila sikutaka kumuuliza kwa sababu nilikuwa nina uhakika huenda ni wewe umemtuma kufuatia kauli ya mheshimiwa raisi ya mchana wa jana alivyosema kwamba atatoa majibu baada ya miezi sita hivyo bila shaka najua ni wewe ulimtuma ile kazi” Asp Bakari wasiwasi wake haukuwa mkubwa sana kwa sababu alihisi huenda mtu huyo ndiye ambaye alikuwa amemtuma Jason kumpa zile karatasi akabandike.

“Ulisoma kilicho andikwa ndani yake?”
“Hapana, maana nilinunua tu mavazi meusi na mask nikatafuta boda boda ambaye nimezunguka naye kutafuta vijana wenye njaa kali wapo wengi sana nikawa nawapa hiyo kazi na ujira wao nimeimaliza hiyo kazi saa kumi ya usiku nikaenda kulala hivyo sikupata hata nafasi ya kusoma kilicho andikwa nilipiga tu kopi nyingi sana”
“Kwanini hukusoma?”
“Nilijua ni kazi ya kipolisi hivyo sikuwa na shaka nayo” mzee huyo baada ya kuisikia hiyo kauli ya kijana wake, alichukua rimoti kwenye meza yake na kuwasha runinga kubwa ambayo ilikuwa mbele ya macho yao hapo ndipo Asp alijilaumu kuchukulia poa hilo jambo, kila chombo cha habari kilikuwa kinazungumzia kuhusu hiyo barua ikiwa imeambatanishwa pembeni na ilikuwa inasomeka hivi.


KUTOKA KWA RAIA MWEMA
“Kwenu watanzania wote, nawasalimieni kwa jina la nchi yangu pendwa ambayo kila mtu nina uhakika anaijua vizuri sana kwa sababu ni nchi ya kipekee sana ila kwenye hii nchi wametokea watu wachache sana ambao wameamua kujimilikisha hii nchi na kuigeuza kuwa ya kwao, wanafanya kila wanalo litaka wao na muda wanao uhitaji wao bila kujua kwamba hii nchi ina misingi yake na sheria zake”
“Kufuatia kilicho tokea mauaji ya mheshimiwa wangu raisi wa nchi ya Tanzania, mauaji ya kikatili ya jaji mkuu Markvelous Japhary na familia yake yote mkewe mjamzito na mwanae ambaye amemuacha mdogo wake akiwa mkiwa pamoja na tukio la kutekwa kwa mwanasheria ambaye ni kipenzi cha wengi Yasinta kobe basi NATANGAZA HADHARANI KWAMBA NATOA MUDA WA WAHUSIKA WA HILI JAMBO KUJITOKEZA HADHARANI, NAWAPA MIEZI SITA INAWATOSHA SANA INATAKIWA WAWE WAMEJITOKEZA MBELE YA VYOMBO VYA HABARI NA KUJA KUKIRI MAKOSA YAO PAMOJA NA KUOMBA MSAMAHA KWA JAMII NA WATANZANIA WOTE IKIWEMO FAMILIA AMBAZO WAMEZILETEA MATATIZO MAKUBWA YA KUWAONDOA NDUGU ZAO, kama watajitokeza na watanzania wakawasamehe kwa moyo wote basi nami nitawasamehe na wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria ya nchi ya Tanzania ila kama wakikaidi badi siku ya kwanza baada ya miezi sita kupita kuanzia leo nitaanza kuwapa adhabu mimi mwenyewe mmoja mmoja kati ya hao watu na kwa huo muda sitakuwa na muwa mwingine tena wa nyongeza kuwasamehe”.

“MWANASHERIA Yasinta Kobe NITAMRUDISHA KWAKE SIKU YA JUMATANO SAA SABA KAMILI MCHANA IKIWA NI SIKU MBILI TU KUANZIA HII LEO”.
“Ahsante naipenda sana nchi yangu Tanzania”.

Huo ndio ujumbe ambao ulikuwa umeandikwa kwenye hizo karatasi Asp alijiona yeye ni moja ya watu wazembe sana kuwahi kutokea yaani alikuwa anasambaza yeye mwenyewe na bado hakujua kitu kilichokuwa kimeandikwa humo ndani
“Mimi sina mamlaka ya kumtuma huyo mtu eneo lolote lile wala sina hiyo nguvu ya kumpangia cha kufanya, anafanya anacho jisikia yeye mwenyewe labda raisi pekee ndiye mtu ambaye anaweza akaongea naye vizuri ila sisi wengine anaongea na sisi kikawaida sana na tunaweza kumshauri tu na sio kuanza kumpa amri” hayo maneno yalimshtua Asp kutoka kwenye mwazo mazito ambayo yalikuwa kwenye kichwa chake.

“Mkuu unajua bado sikuelewi unacho kisema hapa naona kama utakuwa umechanganyikiwa sio bure, kumbuka siku ile kule Mbagala ulinipa kazi ya kusafisha ile miili kwa kusema kwamba huyo ndiye aliyekuwa ameua na hakuna sheria yoyote ambayo ilitumika kumkamata wala kuuweka wazi huo ujinga aliokuwa ameufanya, leo tena mimi nimefanya kazi nikijua ni amri yako wewe kumbe ni yule kijana kwa akili zake ndiye aliyekuja kwangu na kunituma kama mtoto wake nitamtafuta na nitamfanya kitu kibaya sana” maneno yake yalimfanya IGP amimine maji kwenye kikombe na kumpatia ili apunguze presha kwanza maana aliona kijana huyo anaropoka vitu ambavyo hata havijui.

“Alivyokuja kwako jana hakuna kauli yoyote yenye utata ambayo alikuachia” Asp aliacha kunywa hayo maji baada ya kuona mkubwa wake amekuwa siriasi sana, alijaribu kukumbuka kwa umakini sana

“Yes,aliniambia kama nikibandika hizi karatasi tutakutana baada ya miezi sita lakini kama nisipo bandika basi leo tungekutana kwangu” alijibu akiwa ana uhakika kwamba kumbukumbu zake hazikumdanganya kabisa.
“Sasa kwanini hayo maswali hukumuuliza yeye unaanza kulalamika hapa?”
“Kwa sababu nilijua huenda ni amri yako wewe”
“Ulishindwa kunipigia simu ili kupata uhakika kama ni mimi? Kwahiyo akija mtu hapo akakwambia fanya mauaji bosi wako kanituma utafanya na baadae uanze kunilaumu mimi? Hivyo ndivyo nilivyo kufundisha kufanya kazi?” maneno hayo yalimgusa ni kweli alifanya uzembe mkubwa sana kuruhusu hicho kitu kitokee, alikaa kimya kwa sababu aliambiwa ukweli
“Unataka kumjua yule ni nani?” IGP aliongea kwa sauti nzito ambayo ilianza kumtisha hata Asp Bakari Zalimo
“Yule ni mkurugenzi wa usalama wa taifa?”
“Whaaaaaaat?”
“Huyo ndiye anaye hakikisha usalama wa hili taifa” Asp alikaa chini yaani kiufupi alichoka sana, yule alikuwa ni kama kijana mwenzake, mara ya kwanza alihisi IGP anampendelea kwa sababu alikuwa ni mdogo wa jaji mkuu lakini haikuwa kweli kilichokuwa kinafanya mpaka wamheshimu sana kilikuwa ni cheo chake kikubwa sana ambacho kilikuwa kwenye vifua vya watu wachache sana

“Mkuu yule bwana mdogo ndiye mkurugenzi wa usalama wa taifa hili?”
“Ndiye huyo huyo, mpaka akaja kwako na kukupa kazi jua ameamua kukuamini sana tena sana kwa sababu huwa hajitokezi kirahisi sana namna hiyo kwa mtu yeyote yule na kama siku ukitokea ukauvunja huo uaminifu wako kwake basi ndiyo itakuwa habari yako ya mwisho kuendelea kuwa hai kwenye uso wa hii dunia” Asp alinyanyuka kwa kujilazimisha na Kwenda kukaa kwenye kiti, alikuwa na maswali mengi sana mpaka alihisi kama kichwa chake kinamuuma sana, bosi wake alilijua hilo IGP alisogea mpaka kwenye kabati akatoa vidonge na maji na kumpatia kijana wake huyo ili atulize kichwa chake maana alikuwa anaambiwa mambo ya kikubwa mno.

“Kwanini umeniweka wazi jambo ambalo linaonekana kuwa la hatari na siri kubwa snaa namna hii?”
“Yeye ndiye aliyetaka mimi nikwambie wewe ukweli”
“Alitakaje kuniambia ukweli na vipi kama nitatoboa siri hii kwa watu?”
“Utakuwa umejifupishia maisha yako wewe mwenywe, nimekupa hizi taarifa kwa sababu wewe ni kijana wangu ambaye nakujua na nakuamini sana, kuna mambo mengi sana ambayo yanaendelea kwenye nchi hii lakini wewe hapo hauwezi kuyaelewa mpaka siku ambayo baadhi ya watu wataamua kuyaweka hadharani. Yule ni mwanadamu kama wewe kimwonekano tu ila kuna muda hata mimi huwa namuogopa sana japo mimi ndiye pekee mtu ambaye anamsikiliza sana ukimtoa raisi ila havumiliki ipo siku utamuona kwenye macho yako ndipo utakuja kunielewa kwamba yule ni nani”

“Nahisi kama nimechanganyikiwa maana nilikuwa namchukulia poa sana yule, sikuwahi kufikiria kabisa kwamba anaweza kuwa mtu wa hatari kama unavyosema wewe, naweza kujua tafadhali hata historia ya maisha yake japo kwa ufupi na kwanini mtu huyo ni wa siri sana na anaishi nje ya nchi halafu muda huo huo ndiye mkurugenzi wa usalama wa taifa? Na ni kwanini hizi taarifa huwa zinafichwa sana namna hii?” Asp aliuliza swali ambalo lilimfanya IGP asikitike sana.

“Nenda kamwambie Utapewa kwamba aende mtaani akahakikishe usalama wa raia kwa sababu huo ujumbe unaweza ukafanya watu wakaanza kuandamana mitaani huko mwisho wa siku ikaanza kuleta taharuki kubwa ambayo inaweza kutufanya tukawa sehemu mbaya, hizo taarifa ambazo wewe unazihitaji hata mimi sizijui kama una shida ya kuzijua sana basi subiri akirudi huko aliko ukamuulize mwenyewe au kama akiwa na kazi nawewe basi atakutafuta yeye ila kama akirudi huko nchi itakuwa kwenye hali ya kutisha sana namjua vizuri yule kichaa, nakupa likizo ya wiki moja kapumzike na familia yako" Asp alishangazwa sana na maamuzi ya bosi wake hakumjibu swali lake na kingine alimpa likizo ya ghafla sana basi hakuwa na namna alitoka humo ndani kinyonge sana akiwa amejishika kiunoni haamini alichokuwa anaambiwa na kukishuhudia kwa macho yake.

Alitoka mpaka nje ambako alimpa msaidizi wake huyo majukumu yote na kumwambia alitakiwa kusimama kwenye nafasi yake kwani wiki nzima asingeweza kuonekana ndani ya hilo eneo, aliondoka na kupanda piki piki yake ambayo ndiyo alikuja nayo siku hiyo akiwa na mawazo mengi sana, hakuwa anauelewa ulimwengu vizuri alikuwa kila akipita njiani anawaangalia sana watu hakutaka kuendelea kuwaamini wanadamu tena kwenye maisha yake unaweza ukamuona mtu wa kawaida sana kwenye macho yako ila nyuma yake ana mambo mengi sana ya kutisha na huo ndio ulimwengu ambao alikuwa amefunguliwa kwenye macho yake.

Sehemu ya 40 inafika mwisho sina la ziada tena tukutane sehemu inayo fuata.

Wasalaam

Bux the storyteller.
 
STORY: INNOCENT KILLER (THE REVENGE)
STORY WRITER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP : 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
SEHEMU YA 41

SONGA NAYO............
THE FIFTEEN GREATEST WALLS
Hii ni sehemu ambayo ilikuwa na kuta maarufu sana 15, haikuwa ulaya wala haikuwa marekani wala bara lingine lolote bali ni ndani ya nchi ya Tanzania, kilomita 10 kutoka ilipo Kibaha Maili moja ndipo zilipokuwa zinapatikana hizo kuta 15 ambazo jina hilo lilitambulika kwa watu wachache sana, juu ya kuta za kuingilia ndani ya hizo kuta 15 paliandikwa THE 15 FLOUR’S PRODUCERS.

Watu wengi kama sio wote ndani ya Kibaha walikuwa wanajua kwamba ndani ya hilo eneo kilichokuwa kinazalishwa ulikuwa ni unga wa chakula na hata kama ungemuuliza raia yeyote yule ambaye alikuwa anatokea ndani ya hilo eneo basi angekujibu hivyo kwa kuwa na uhakika wa asilimia zaidi ya miamoja. Ni moja kati ya viwanda (kama ilivyo julikana kwa watu) ambacho kilikuwa ni msaada mkubwa sana kwa jamii hususani kwa wale watu ambao walikuwa hawana uwezo wa kumudu milo yao wengi wao walipata msaada mkubwa sana kutoka ndani ya hicho kiwanda.

Kila siku zilikuwa zinatoka tani za unga za kutosha ndani ya kiwanda hicho ambazo zilisaidia sana kuweza kukuza uchumi wa nchi kwani walikuwa wanauza sana na hata kutoa sana msaada kwa wananchi wa Kibaha lakini pamoja na maeneo mengine mengi sana ya Tanzania.

lakini ilikuwa ukiingia ndani kabisa ya kiwanda kiwanda hicho kama kilivyokuwa kinasemekana kwa ndani sana ndiko ulikuwa umeandikwa ule uhalisia wa hilo eneo THE 15 GREATEST WALLS ikiwa na maana kwamba kuta kuu 15, kilicho saidia sana kuweza kulinda hiyo siri ilikuwa ni ufanyaji wa kazi wa eneo hilo hakuna mtu wala gari kutoka kwenye kampuni zingine ambazo ziliruhusiwa kuingia ndani ya kiwanda hicho kila kitu walikuwa wanakamilisha kwa kuzitumia gari zao wenyewe hivyo kuwafanya kufanya mambo yao kwa usiri mkubwa sana.

Ndani ya hizo kuta kulikuwa na jela moja kubwa sana na ya kutisha mno, jela hiyo haikuwa kwa ajili ya watu ambao walikuwa wanaiba kuku au kufumaniwa na wake za watu, jela hiyo ilikuwa ipo maalumu kwa ajili ya kuwahifadhi watu ambao walikuwa na matukio ya kutishia usalama wa nchi, kulikuwa na magaidi wa kutosha ambao walikuwa wamekamatwa kutoka kwenye makundi mbali mbali ambayo yalijaribu kuivamia nchi ya Tanzania, kama vile Al shabaab, M23, Boko haramu na mengine mengi lakini pia huko walikuwa wanahifadhiwa wale wanaume ambao walikuwa wakifanya kazi za mauaji huwa wanaitwa professional killers pamoja na ubakaji huko ndiko kulikuwa makazi yao. Mwanaume ambaye angepelekwa huko akiwa mnyonge basi ni wazi angeenda kuwa mke wa watu hivyo walikuwa wanakutana wazee wa kazi watupu na wale ambao walikuwa wametenda makosa ambayo hakukuwa na namna zaidi ya kusubiri kuuawa tu na kunyongwa nao pia walihifadhiwa ndani ya hilo eneo.

Kuta hizo ziliitwa THE GREATEST 15 WALLS kwa sababu zilijengwa kuta jumla 15 mpaka kufika ndani kabisa ya hiyo jela, huko ndani kabisa ndiko ambako kulikuwa na makazi ya bwana jela pamoja na maofisa ambao walikuwa na vyeo vikubwa, kuwafikia mahali ambapo walikuwepo ilihitajika kuzivuka kuta zote 15 ndipo ungefanikiwa kuongea na bwana jela, ni eneo ambalo lilikuwa na ulinzi mkali sana hakuna hata sisimizi ambaye angekatiza bila kuonekana kwamba amepita ndani ya hilo eneo.

Jela hiyo haikuwa imejengwa na serikali ya nchi ya Tanzania ilikuwa imejengwa na serikali ya nchi ya marekani na wao ndio ambao walikuwa wanaiongoza hiyo jela, lengo la kuijenga ndani ya nchi ya Tanzania ni baada ya serikali ya Tanzania kuomba msaada wa kusaidiwa kuweza kupata gereza ambalo lingetumika kuwahifadhia watu hatari kama hao kwani ni mara kadhaa serikali imewahi kujaribu kuwafunga baadhi ya watu kama hao wakaishia kutoroshwa na wenzao huku wakisababisha vifo kwa maaskari wengi sana na kuleta hasara kubwa ya kubomoa miundo mbinu ambayo iliiingiza serikali kwenye gharama kubwa kupita kiasi. Kwa msaada ambao serikali iliomba kutimiziwa serikali ya nchi ya Marekani ilikubali lakini kwa kutoa masharti mawili

Hilo jengo litajengwa ila kwa siri sana hakuna mtanzania ambaye atatakiwa kulijua zaidi ya viongozi wa juu zaidi wa serikali ambao watakuwa na umuhimu wa kulijua jengo hilo.

Jengo hilo litasimamiwa na serikali ya nchi ya Marekani japo wataingia ubia wa kushirikiana kwenye kutokomeza suala la uhalifu kiasi kwamba kama atatakiwa kuhifadhiwa huko basi serikali zote mbili zitakuwa zinaruhusiwa kufanya hilo jambo kwa mawasiliano ya karibu ila usimamizi wote na namna ya kuendesha jela hiyo serikali ya Marekani ndiyo itashughulikia kwa kila kitu.

Hali hiyo ilipelekea sehemu hiyo kuwa na wamarekani wengi sana kama wafanyakazi ndani ya hiyo jela na watanzania walikuwa ni wachache sana ambao walikuwa wanaajiriwa humo ndani kwa nafasi maalumu tu ambazo watu hao wangetaka iwe hivyo, hivyo hata kiwanda kilijulikana kuwa kama cha wamarekani na hata biashara ya unga wao ndio waliokuwa wanaisimamia na wananchi walijua watu hao wanalipia kodi serikalini lakini haikuwa hivyo lengo halikuwa kiwanda lengo lilikuwa ni kuweza kujenga gereza hilo la siri ambalo lilifanikishwa kwa asilimia miamoja na mpango ukaenda kama ulivyokuwa umepangwa na humo ndani walikuwa wamehifadhiwa watu wa shoka kweli japo hakuna mwananchi ambaye alikuwa na hizo taarifa, je ni kweli hakukuwa na sababu nyingine ya kuanzia gereza hilo zaidi tu ya hiyo?

Ndani ya moja ya vyumba vya jela hiyo ambacho kilikuwa na kila kitu ndani yake, ungekiona hicho chumba ungekataa mtu anapo kwambia kwamba hiyo ilikuwa ni jela, alionekana mwanaume mmoja ambaye alikuwa na weusi wa kimarekani ambao ulikolea sana kuonyesha kwamba muda mrefu aliutumia huko, alikuwa amevaa suruali moja ambayo ilikuwa inavutika kwenye mwili wake, alikuwa ameinama chini kwa saa zima akiwa anapiga pushapu kwa kasi ya ajabu sana huku akiwa kifua wazi. kwenye mgongo wake alikuwa na tatoo ambayo ilikuwa na picha ya mwanaume mmoja ambaye ameacha historia kubwa sana kwenye ulimwengu kila siku anaimbwa na kuogopwa sana mpaka leo, jina lake huyo mwanaume ambaye alikuwa kwenye mwili wake alikuwa akiitwa Pedro Alonso Lopez, alipata kuzaliwa miaka ya 1948 ambaye kuna watu walimpatia jina la utani kama The monster of the Andes. Historia yake inadai kwamba ni Mkolombia kwa kuzaliwa, kitu kilichompa sana umaarufu mwanaume huyu ni uuaji wa mfululizo waweza kumuita serial killer kwa kesi ya mauaji ya sio chini ya watu 300 ambao aliwahi kuwaua huko Colombia, Peru na Equador.

Maisha yake yalikuwa ya utata mkubwa sana kwa sababu tangu akiwa mtoto alikuwa ni mbakaji mkubwa sana na wahanga wakubwa sana kwake walikuwa ni wanawake mabinti pamoja na wasichana wadogo ambao alikuwa akiwabaka na kuwaua, kwa mara ya mwisho mwanaume huyu alionekana mwaka 2002 lakini mpaka sasa kimebaki ni kitendawili kikubwa sana duniani hakuna mtu ambaye anajua kwamba huyu jamaa yuko wapi ni kama alipotea kwenye uso wa ulimwengu.

Huyo Pedro Lopez ndiye mwanaume ambaye tatoo yake ilikaa kwenye mgongo wa huyo mwanaume ambaye alikuwa ndani ya chumba hicho akiwa anapiga pushup kwa saa zima bila kupumzika halafu juu yake akiwa ameandika “my role model” akiwa na maana kwamba huyo mtu ndiye ambaye alikuwa ni mfano wake wa kuuiga kwenye maisha yake, kichwa chake kilikuwa kinang’aa sana kwa upara na kilionekana vyema baada ya yeye kusimama, mwili ulikuwa umepasuka sana kwa mazoezi makali kiasi kwamba unaweza ukahisi kwamba kuna mtu alikuwa anaugawa mafungu mafungu, baada ya kusimama alisogea ukutani akaanza kupiga na ngumi zake ukutani kwa hasira sana, kuna vitu vilikuwa vinajirudia kwenye kichwa chake vilikuwa vinamchanganya, kuna picha zilikuwa zinakuja na kutoweka zilimfanya aanze kupiga sana makelele kwa nguvu akawa anazidisha kupiga ukuta huo ambao alipiga ngumi moja mpaka sehemu hiyo ikabonyea kidogo. Mkono wake mmoja ulikuwa unavuja damu lakini hata hakujali, alielekea sehemu ya bafuni ambako kulikuwa na bomba la maji mbele ya kioo kikubwa alijitazama sana kwenye hicho kioo, akiwa hapo alihisi kuna mtu ameingia ndani ya chumba chake.

“Mnasemaje” aliongea kwa sauti ambayo ilikuwa imeshiba sana ikiwa inaonekana kabisa kwamba alikuwa amethiriwa na ile lafudhi ya kimarekani, alitamka hivyo baada ya kutoka na kuwakuta moja ya wanaume ambao walikuwa wamevaa magwanda ya kimarekani ambayo yalikuwa yana nyota kwenye mabega yao

“Mkuu amekuja kukuona”
“Sawa mwambie nakuja sasa hivi” alitafuta t-shirt ya jeshi haraka sana na kuiweka kwenye mwili wake akiwa anaonekana kwamba alikuwa anamheshimu sana huyo mtu ambaye alikuwa amefika hapo aliyekuwa ametambulishwa kama mkuu wake, alitembea haraka haraka sana kuwahi hiyo sehemu, alipandisha juu kama ghorofani kisha akapanda lifti mpaka floo ya tatu, alitoka na kunyoosha moja kwa moja kwenye mlango ambao nje yake ulikuwa na watu watano nje wanaulinda, alikaguliwa hapo na kuruhusiwa kuweza kuingia moja kwa moja ndani.

“Mkuu” alitamka huku akiwa anatoa salamu ya heshima kwa mtu ambaye alikuwa amempa mgongo na kuangalia upande wa pili

“Unaendeleaje” ilikuwa ni sauti ya mtu huyo akiwa bado hajageuka kabisa
“Mimi niko vizuri kabisa mkuu” baada ya kutamka hivyo mtu huyo ambaye alikuwa hapo ndani aligeuka akiwa anaangaliana na huyo mwanaume ambaye bila shaka alikuwa mdogo wake kicheo cha kazi. Kitu cha ajabu sana na cha kushangaza mwanaume ambaye alikuwa amefika humo ndani alikuwa ni mtu ambaye watu wengi sana walikuwa wanamfahamu ndani ya jiji la Dar na sio hapo tu bali Tanzania nzima kwa sababu alikuwa ni mtu maarufu sana kutokana na huduma ambayo yeye alikuwa akiitoa ndani ya nchi ya Tanzania, John Mwituka mchungaji wa kanisa la WITH GOD YES WE CAN ndiye mtu ambaye alikuwa amefika humo ndani huku wao wakimuita kama bosi wao na ndiye ambaye alikuwa kiongozi ndani ya hilo eneo la hilo gereza au waweza kukiita kiwanda cha unga kama wengi nje walivyokuwa wanakijua, huyu ndiye mtu ambaye Monalisa alikuwa anamuita baba na alikuwa amekuja ndani ya nchi ya Tanzani sehemu ya kufikia ilionekana ni kwa huyo huyo mtu ambaye alikuwa ni mchungani maarufu sana na Monalisa alikuwa ni CIA agent je kulikuwa kuna uhusiano gani kati ya hawa watu?

“Tangu ufanye hilo tukio hatujaonana kabisa lakini kwa bahati iliyokuwa, na mbaya zaidi hilo tukio hukulifanya wewe kuna mtu mwingine ambaye ndiye alikuwa mhusika mkuu wa hilo jambo” hiyo kauli ya John Mwituka haikumshtua sana mwanaume huyo ni kama alikuwa ana taarifa nayo na alikuwa anaijua moja kwa moja bila hata shaka kabisa.

“Ndiyo naelewa hilo mkuu maana wakati narusha risasi yangu haikumpata kwa sababu kulikuwa na mtu ambaye aliwahi na alionekana alikuwa karibu zaidi yangu maana wakati risasi yangu inakaribia kumpata alikuwa tayari amepigwa na mtu mwingine hivyo risasi yangu ilienda kugota kwenye kioo cha gari” alijibu akiwa amesimama kikakamavu sana.

“Na hicho ndicho kilicho nileta hapa, hilo sio mhimu kivile sana ila kitu ambacho kimenishangaza mimi ni kivipi mtu mwingine alijua kama wewe utakuwa pale?” hilo swali lilimshtua sana mwanaume huyo
“Sijakuelewa bosi mtu mwingine nani huyo?”
“Kila siku huwa nakusihi sana uwe unahakikisha unaingia kwenye mitandao mara moja moja, wakati wewe unalitenda lile tukio kuna mtu ambaye alikuwa anakurekodi moja kwa moja”
“Whaaaat?”
“Yes, ndiyo hivyo”
“Inawezekanaje?”
“Sasa hilo ndilo jambo la mhimu ambalo mimi na wewe nataka tulizungumze hapa muda huu na ndiyo sababu ambayo imenitoa kwenye majukumu yangu mengine na kunileta hapa kwa sababu kazi yako ilifanywa kizembe sana kitu ambacho kinaweza kutuchafulia sana jina kama hili jambo likifika mbali ila mwenye hiyo video mmoja yupo kwenye mkono wangu ni mwanasheria sasa sijui kama ni yeye tu au walikuwa wapo wengi wenye hii video” alikuwa anayatamka maneno yake kwa mpangilio sahihi sana kuonyesha kwamba hilo jambo alikuwa na uhakika nalo moja kwa moja.

Huyu ndiye John Mwituka, watanzania walimjua kama mchungaji mwenye nguvu kubwa sana, sasa yeye na huyo mtu ambaye anaonekana wazi ni muuaji wa hatari sana walikuwa na uhusiano gani? Kwanini yupo hapo? Yeye ni nani mpaka anaishi kwa kujificha ficha sana namna hii? Na Tanzania walikuwa wamefuata kitu gani hasa mpaka wanaonekana kabisa kuwa makini sana namna hii kiasi cha kupelekea hata kifo cha raisi wa nchi?....41 natia nukta panapo majaaliwa tukutane ndani ya sehemu ambazo zinafuata.

Wasalaam

Bux the storyteller.
 
STORY: INNOCENT KILLER (THE REVENGE)
STORY WRITER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP : 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
SEHEMU YA 42

SONGA NAYO............
Baada ya Monalisa kuondoka sehemu ambayo yeye alitoka akiwa ana maswali mengi sana kwa sababu mara kwanza alijua ni nyumbani kwa professor Michael lakini baada ya kufika hapo alikutana na mzee ambaye alimwambia kwamba yeye alikuwa anaitwa Dr Morgan, professor Michael mwenyewe alibaki ndani ametulia akipata kahawa safi baada ya kutoka kwenye mashine ambayo ilimfanya ile sura yake ya kuchonga iweze kutoka na kumrudisha kwenye uhalisia wake, akiwa hapo kijana wake alikuja akiwa amevaa suti safi sana.
“Huajamuumiza sana yule binti?”
“Hapana bosi nimemgusa kidogo naona bado mifupa yake ni milaini mno kama ningempiga pigo baya ningemuua nadhani, ni imara sana ila hatakiwi kukutana na mikono kama hii”
“Ni bora sidhani kama kiongozi wako angekuelewa kama ungemuua maana huwa simuelewi kama anampenda yule mwanamke au hampendi kama ambavyo huwa anasisitiza kwamba ni mambo ya kazi ndiyo yamemfanya awe naye karibu sana” Dr Michael aliongea akiwa anasimama na kujinyoosha na kuiweka vizuri miwani yake.

“Namjua yule huenda angenifanya kitu kibaya sana ndiyo maana nilichukua tahadhari mapema”
“Yule hatakiwi kukupiga na ule mkono wake wa kulia kwa sababu kuna mawili hiyo sehemu ambayo atakupiga huenda inaweza kuoza au ukafa kama akiamua kutumia uwezo wake wote, ana nguvu za ajabu ambazo hata mimi huwa namshangaa lakini yote haya aliyataka kaka yake japo nina amani sana maana hata nikifa leo najua kabisa nitakuwa nimeiacha nchi kwa mtu salama japo tumepata pigo kubwa sana la kumpoteza mheshimiwa raisi pamoja na jaji mkuu” kwa maelezo yake namna yalivyokuwa moja kwa moja professor Michael alionekana kuwa ni mtu kutoka ndani ya nchi ya Tanzania.

“Kwahiyo kuna haja ya kurudi nyumbani kwa dharura?”
“Hapana hatuwezi kurudi kienyeji sana namna hii, mimi siku ya kuondoka itatakiwa niigize kifo”
“Mkuu hivi unajua hatari ya hicho unacho kisema?”
“Hiyo ndiyo njia pekee ya kuondoka salama ndani ya nchi hii bila kushtukiwa na mtu yeyote yule na hili tukio litafanyika miezi mitatu ijayo kuanzia sasa hivyo anza kujiandaa maana kila mtu huwa anajua wewe ni mwanangu kabisa wa kumzaa. Nikifa kwa hiyo miezi mitatu basi baada ya miezi mingine mitatu hata mwenzako naye atatakiwa kufa japo yule kuna hatari kubwa ya kufa moja kwa moja maana anatakiwa kufanyiwa tukio ambalo mpaka madaktari watathibitisha kwamba amekufa kweli na atakaguliwa sana kwa sababu ni moja ya maafisa wakubwa sana ndani ya CIA”

“Bosi Hapana, unataka kusema atauawa kweli? Sasa ina umuhimu gani wa yeye kufanyiwa yote hayo na kama akifa moja kwa moja itakuwaje?” kijana huyo alionekana kupingana na hayo mawazo kumhusu huyo mwenzake ambaye walisema moja kwa moja kwamba ni CIA

“Unajijua kwamba wewe ni nani?”
“Ndiyo bosi”
“Unaweza ukanieleza japo kwa uchache?”
“Sisi ni wale wauaji wa mfululizo tulio tiwa sumu, tunaishi kama wafu ambao hatuna maisha kwenye mikono yetu, kwetu maisha ni bahati nasibu ya kupata na kukosa kwa sekunde yoyote na muda wowote ule ndiyo maana serikali yetu tunaibeba kwenye migongo yetu”
“Sasa umenielewa?” kauli ya mtu ambaye alikuwa ni kiongozi wake ilikuwa sahihi japo yeye hakuwa na raha kwa mpango wa huyo kiongozi wake ambao alikuja nao mezani.

“Lakini bosi kwani hakuna namna nyingine ya kuweza kufanya hilo jambo zaidi ya hilo?”
“Je kama angekuwa ni kiongozi wako ndo yupo hapa ungeweza kumbishia namna hiyo?”
“Hapana”

“Sasa yeye ndiye aliye amua kwamba iwe hivi na mimi siwezi kumpinga wala kumzuia kwa sasa maamuzi yenu yote yeye ndiye mwenye kauli ya mwisho kwahiyo sina namna ambayo naweza kukusaidia juu ya hilo”

“Bosi bado unaweza ukawa na namna nyingine ya kumshawishi hili jambo ni la hatatri sana,yule anakusikiliza sana wewe kuliko binadamu yeyote yule kwanini usitumie hiyo nafasi kuweza kumbadili mawazo tukae upya mezani ili huo mpango tuuweke kwenye namna nyingine kuliko hayo maigizo ya kufa mtu atakufa kweli”

“Kwahiyo unaogopa kufa?”
“Hapana sijamaanisha hivyo”
“Sasa shida nini?”
“Kumbuka kwenye ile TOXIC he is the only X surviving, huyo ndiye ambaye kwenye kichwa chake kuna taarifa nyeti sana ambazo tunazihitaji, yule ndiye ambaye hata kiongozi anamsubiri kwa hamu sana ili akatupatie taarifa zote ambazo amezikusanya kwa miaka yote hii sasa akiwekwa kwenye huo mstari kutakuwa hakuna maana yoyote ile tutaanza na moja tena wakati kwa sasa ni jambo ambalo tunaenda kuanza kulitenda kwa muda mfupi tu ujao” aliongea kwa uchungu na kwa maelezo yake huyu alionekana kuwa miongoni mwa wale wa tano ambao walikuwa wanaunda kundi la “Five poisoned serial killers au THE TOXIC” na huyo ambaye walikuwa wakimzungumzia kwamba njia ya yeye kutoka salama ilikuwa ni kujulikana kama amekufa na madaktari watampima kabisa kwahivyo njia ambayo ingetumika kumtoa ndani ya taifa hilo kubwa ilikuwa na asilimia 90 za kuondoka na uhai wake lakini 10 pekee ndo ilikuwa uhakika wa yeye kuendelea kuwa hai

Huyo ndiye mbaye alikuwa mmiliki wa herufi X kwenye hiyo TOXIC na ndiye ambaye alikuwa hajawahi kujulikana kwamba ni wapi yupo, anaishije, anafanya shughuli gani na kwa maelezo ya IGP alidai kwamba unaweza ukaja kuzipata taarifa za wanne kwenye hilo kundi ila huyo X ilikuwa ni haiwezekani kuzipata taarifa zake hata kama ungekuwa nani, huyo ndio ulikuwa moyo wa hilo kundi hatari sana la hao vijana watano na ndiye ambaye alikuwa anategemewa zaidi siku akizifikisha taarifa ambazo kundi lao limezisubiri kwa miaka mingi kidogo sasa kama ikitokea amekufa hali itakuwaje maana yake walikuwa wanaenda kuanza na moja tena.

“Najua una elimu kubwa sana tena sana na mafunzo makali na kila kitu unacho kuhusu haya mambo lakini leo ngoja nikukumbushie jembo ambalo huenda umeanza kulisahau kwenye kichwa chako, najua mnapendana sana na huwa hampo tayari kumpoteza mwenzenu hata mmoja ila duniani hakuna kazi ngumu kama kujitolea maisha yako kumlinda mtu ambaye hata hajitambui na hajui chochote kwamba maisha yako unayaweka kwenye mstari wa kifo kwa sababu ya kumpigania yeye. Leo wananchi wa Tanzania wanalala na kuamka na Kwenda kubishana kwenye vilinge vyao wengine wakiitukana na kuidhalilisha serikali kwa sababu wanaishi kwa amani ila kuna mtu kama wewe hapo ambaye hata kulala tu masaa zaidi ya Matano hujawahi muda wote macho yako yapo juu muda mwingine inakulazimu kutumia mpaka vidonge ili uifanye kazi kwa ufanisi kwa ajili ya taifa lako halafu kuna mjinga mmoja yupo kilingeni kwa sababu kashiba ugali wa mama yake anaanza kukutukana na hayo ndiyo maisha yako wewe mpaka siku unakufa.”

“Kazi ya kulilinda taifa sio rahisi kama unavyohisi kwa sasa kwa sababu ya mapenzi kwa huyo ndugu yenu, kiongozi wenu kutoa hiyo ruhusa siyo kwamba yeye anapenda kwamba itokee kuna mmoja kati yenu amepotea hapana inawezekana yeye ndiye anaye umia zaidi kuliko hata ninyi japo hawezi kuonyesha udhaifu mbele yenu maana uongozi ni sawa na kuwa kiongozi wa familia hata kama unajua kwamba hali imeshindikana kabisa hautakiwi kuonyesha kukata tamaa mbele ya familia yako kwa sababu matumanini yao yapo kwenye kicheko na tabasamu lako sasa kama kiongozi wa familia umejikatia tamaa vipi wana familia wengine watakuwaje?”

“Kumuingiza tu ndani ya CIA zilitumika roho za watu ambao kwa lugha rahisi naweza kusema kwamba walitolewa kafara japo sio kichawi namaanisha kuna watu wengi sana walikufa ili aipate ile nafasi kule, yule kule hajaenda wala hayupo kucheza, yupo pale kama double agent, nchi ya marekani wanamtambua kama jajusi wao yule na sisi Tanzania tunamtambua kama jasusi wetu, wale namna yao ya maisha ni tofauti na nyie majasusi wa Tanzania, wao wanalindwa na kuchunguzwa isivyo kawaida na kama wakikuhisi kwamba unawasaliti basi moja kwa moja wanakuua, sasa je upo tayari hayo mashaka yako yamuue mwenzako kuliko kujaribu namna sahihi ya kuweza kumsaidia ili hata kama akifa basi afe akiwa anapambania nafasi ya kuwa hai tena?” utu uzima dawa hawakukosea, professor Michael alimchambulia kijana wake huyo namna ambavyo ilikuwa ni lazima kijana huyo aonekane kwamba ameuawa ili aweze kurudishwa Tanzania na kujaribu bahati ya kuona kama vile atakuwa salama au vipi atakufa wakiwa kwenye hilo jaribio, kijana huyo alihema kwa nguvu sana

“Mpango ni upi?”
“Hii nchi huwa kuna namna nyingi sana za kupata ajira au kuajiriwa ila mpaka uipate hiyo ajira inategemeana na ajira yenyewe, kwa mfano mimi kama mhadhiri wa chuo kikubwa kama kile haikuwa rahisi kukaa pale, huku ualimu ni moja ya kazi nyeti kuliko kazi yoyote ile kwenye nchi hii kwa sababu wanajua kwamba ndiyo inashika maisha ya baadae ya nchi hivyo huwa ni ngumu sana kuweza kuajiriwa kama wewe sio raia wa nchi ya Marekani hivyo kama unataka kuajiriwa na sio raia wa huku basi unahitajika kuwa na akili isivyokuwa kawaida hapo ndipo utapata nafasi kama njia ambayo niliitumia mimi hapa”
“Kumbuka kule nyumbani mimi mpaka sasa ni watu wachache sana ambao wanajua kwamba mimi nipo hai wengi huwa wanajua kwamba mimi nilipotea kwenye mazingira ya kutatanisha sana na kulingana na nafasi ambayo mimi nilikuwa nayo wengine wakamaliza kwamba nilishakufa, baada ya kuja huku niliyaanza maisha mapya sasa maisha ambayo niliyaanza mimi hapa ni maisha ambayo ni kama ya mkataba wa maisha kwa sababu nilisaini kwamba nitafundisha mpaka siku ya mwisho kabisa ya maisha yangu na kama ningeukataa huo mkataba basi siku ile hata kazi yenyewe nisingepewa kabisa kwa maana hiyo sikuwa na namna ningeweza kufanya zaidi ya kuukubali mkataba kama ulivyokuwa unaeleza”

“Sasa kwenye huo mkataba ambao nilisaini ni kwamba nitarudi ndani ya nchi ya Tanzania siku nikifa maana yake mwili wangu ndio utakao rudishwa kule nyumbani hivyo hakuna namna ambayo ninaweza kutoka ndani ya nchi hii nikiwa hai na hata kama nitafanikiwa basi nitatafutwa vibaya sana na sitaweza kuishi nchi yoyote ile duniani maana nikionyesha sura yangu tu lazima watanikamata na nadhani nchi hii unaijua vizuri ilivyo pale wanapo amua kukubananisha kwenye kumi na nane zao. Sasa njia pekee ya mimi kuweza kurudi ndani ya nchi ya Tanzania ni kufeki kifo ili nipelekwe kule kama maiti halafu baada ya hapo nikifika kule itatakiwa nibadilike kabisa niwe mtu mpya ili nisije kuhisiwa maana nikikamatwa basi mpango wetu wa miaka mingi yote hii utakuwa kama vile tulienda mtoni na kikapu na kutegemea kwamba tutayafikisha maji nyumbani yakiwa yamejaa kwenye hicho kikapu hivyo lazima niigize kifo japo ni hatari sana” mzee huyo alitulia kwanza baada ya kumpa kijana wake maelezo ya muda mrefu kuhusu namna ya yeye kuweza kutoka ndani ya nchi ya Marekani akiwa salama bila kushtukiwa japo ilikuwa ni hatari kubwa sana.

“Na kuhusu ndugu yako na hatari yake ya asilimia 90 za kufa yeye mpango wake ni tofauti kabisa na mimi na ndiyo maana tumeuweka miezi mitatu mbele baada ya mimi kurudi Tanzania kuna sababu kubwa sana ya kufanya hivi na mpango uko hivi…….”

Sijui kuna nini ambacho wamekipanga mpaka wanahatarisha asilimia 90 za maisha ya mwenzao namna hii inaonekana kuna mambo mazito sana mpaka watu wanaigiza kufa ili waweze kufanikiwa kutoka wakiwa salama, huenda hakuna tunacho kijua bado mpaka sasa kwenye simulizi hii kuhusu heka heka za hawa watu pamoja na bosi wao au mkurugenzi wa usalama wa taifa Jason ambaye anaishi kwenye mgongo wa kijana mmoja mstaarabu na legelege sana ila wanao mjua wanaonekana kumuogopa isivyo kawaida.

42 nafika tamati tukutane sehemu ijayo.

Wasalaam

Bux the storyteller.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
STORY: INNOCENT KILLER (THE REVENGE)
STORY WRITER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP : 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
SEHEMU YA 43

SONGA NAYO............
“Mwenzako yeye atakufa kwa siku 3, sababu ambayo imefanya nikwambie kwamba yule akiigiza kifo kuna uhakika wa asilimia 90 za yeye kufa moja kwa moja ni kwa sababu mwili wake hautakuwa unafanya kazi kabisa kwa hizo siku na daktari akimpima atajua ni kweli amekufa maana hawezi kusafirishwa bila madaktari wao wakubwa kuthibitisha hilo. Siku moja kabla ya siku ya tukio ambayo sisi tumeipanga ni siku ambayo yeye na wenzake watatumwa kuifanya kazi moja kubwa sana ya kiserikali ndani ya Marekani huko Hauston na yeye ndiye ambaye wanamtegemea sana hivyo hiyo itakuwa nafasi ya kipekee sisi kumpatia hicho kitu ambacho kwa asilimia miamoja kitafanya aonekane amekufa”
“Kuna dawa ambayo atachomwa kwenye mwili wake itaanza kufanya kazi kwenye moyo ambapo moyo utasimama kabisa na kuacha kufanya kazi yaani kiufupi ni kwamba moyo wake utafeli, baada ya moyo kushindwa kufanya kazi hapo ndipo ambapo viungo vingine ndani ya mwili wake navyo havitakuwa na uwezo wowote ule wa kuweza kuifanya kazi na mwisho wa siku ataonekana amekufa kwa sababu ya moyo kufeli kutokana na presha, huwa hawaishii hapo tu wale watu ni wadadisi sana lazima watataka kujua mtu imara kama yule anakufaje kwa presha? Hivyo kuna tukio ambalo tumepanga kulitengeneza kupitia chip zilizopo kwenye kichwa chake tutatengeneza tukio la kutisha sana ambalo hata CIA watakapo jaribu kulichunguza kwenye kichwa chake itaonekana kama hilo tukio ndilo ambalo lilimpa sana presha mpaka akapata mshtuko huo wa kufa ghafla”

“Unaweza ukajiuliza sana kwamba inawezekanaje tukamchoma sindano ya sumu ya kuusimamisha mwili wake kuweza kufanya kazi na wasijue? Hapo ndipo ulipo mtego mkali sana na tulilijua hilo mapema mno hivyo kitu ambacho kitafanyika wakati anachomwa hiyo sindano ambayo ndani yake itakuwa na dawa yenye sumu pia atachomwa dawa nyingine ambayo itaonekana kama ilitaka kumponyesha lakini itafeli na dawa hiyo kazi yake kubwa ni kutoa dalili zote za kuonyesha kwamba mtu huyo alikuwa amechomwa sindano au kuingiziwa dawa au sumu yoyote ndani ya mwili wake ndani ya hizo siku hivyo hata kama watampima vipi hakuna mtu hata mmoja ambaye atakuwa na huo uwezo wa kujua kama kuna dawa tumeiiingiza ndani yake”

“Marekani wameenda mbali sana kwenye mambo ya teknolojia na mambo ya intelijensia hicho ndicho kitu ambacho kilitufanya tupige mahesabu makali sana kwenye kila nukta, nampa pongezi sana Jason licha ya kuwa kijana mdogo lakini akili yake ilifanya kazi kama umeme kwenye hili jambo na ndiyo ile siku ambayo mimi niliamua kumuachia kiti changu baada ya kuona kwamba alikuwa ana uwezo mkubwa sana kwenye kichwa chake kuliko binadamu wengi hususani kwenye suala la ubunifu yakinifu na namna sahihi ya kuchambua taarifa na mambo makubwa sana. X mwili wake utakuwa haufanyi kazi kwa siku 3 ambayo ni masaa 72, ndani ya nchi ya Marekani atakaa kwa masaa 37 ikiwa masaa 15 yatatumika kuuchunguza mwili wake, masaa 15 yatatumika kuuaga mwili wake na kumpa heshima zote za kijeshi na masaa 7 ambayo yatabaki utafanyika utaratibu kwa kuusafirisha mwili wake kuupeleka airport kwa ajili ya kuusafirisha hivyo kutakuwa kumebakiwa na masaa 35 ili kuyakamilisha hayo 72. Kutoka Marekani mpaka Tanzania ni masaa 15 na dakika 51 mpaka kufika tunaweza kusema ni masaa 16 jumla pamoja na heka heka za airport hapo yanabaki masaa 19.”

“Ndani ya hayo masaa 19 yatatumika masaa 7 ya serikali ya marekani kumkabidhi kwenye mikono ya serikali ya Tanzania ambapo yanabaki ya kuhesabu 12, harakati za Kwenda kuuhifadhi mwili na walinzi kuanza kupungua mpaka hali kutulia ni masaa 7 yanakuwa yamebaki masaa 5 pekee na oparesheni ya kumrudisha kwenye hali yake inahitaji masaa 5 maana yake tunakuwa hatuna hata dakika moja ya ziada” professor Michael alipumzika kidogo baada ya kutoa hayo maelezo ambayo ndani yake yalikuwa na mahesabu makali sana kisha akaendelea

“Mpaka hapo umeiona hiyo hatari ya kwanza na ikizidi hata sekunde moja tu yaani hata ikiwa ni masaa 72 na sekunde moja basi tunampoteza na kunakuwa hakuna namna tena ya kumrudisha kuwa hai, na siyo hilo tu lakini pia hatari nyingine ni kwamba hiyo dawa ya kuweza kumrudisha ni 50/50 inaweza ifanye kazi au isifanye kazi ndiyo maana nakwambia kwamba yule ana asilimia 10 tu za kuwa hai ila 90 atakufa hivyo tunatakiwa kuzidisha sana maombi hili jambo tulimalize salama na hii itaitwa THE 72 HOURS OPERATION” alihitimisha maelezo yake akiwa anamwangalia kijana wake huyo ambaye alibaki amechoka sana hakuwa na nguvu za kusimama tena alienda kukaa kwenye kiti ili angalau apate balansi kidogo, aliinama na kuyafikicha macho yake mambo yalikuwa yanazidi kuwa magumu sana kila dakika moja ambavyo ilikuwa inaenda.

“Sikuwahi kudhania kwamba mambo yangekuja kuwa magumu sana kwetu namna hii, nilihisi kwa uwezo ambao sisi tunao basi kila kitu kwetu kingekuwa chepesi tu nadhani nilijidanganya sana” aliongea kinyonge akiwa anamimina maji ya baridi kwenye bilauri ambalo lilikuwa mezani na kuyabugia mdomoni kushushia ili kidogo mwili upoe maana alikuwa anahisi joto sana kwa hizo namba ambazo alikuwa amechambuliwa aliona mlima ambao walitakiwa kuupanda haukuwa na vilele virahisi sana kama namna yeye alivyokuwa ameamua kuvichukulia.

“Kuna muda mambo huwa ni kama ule mchezo wa mpira, kuna wachezaji kama uliwahi kuwaona Xavi, Iniesta, Ronaldinho, Zidane, JJ Okocha, Neymar hao watakuaminisha kwamba mpira ni moja ya vitu rahisi sana kuvifanya huenda hata wewe hapo nikikuuliza hicho kitu unaweza ukawa na jibu hilo hilo kwa kuamini kwamba ni rahisi sana kuucheza huo mchezo lakini tukikupeleka wewe ndipo utaamini kwamba mpira ni moja ya michezo migumu zaidi kuwahi kutokea, hiyo ni sawa na mtazamo wa maisha pia leo hii unavyo sikia matajiri wakubwa wanatajwa kwa mawazo ya kawaida unaweza ukahisi kwamba ni rahisi sana kufikia pale walipo ila ukianza hizo harakati za Kwenda pale walipo ndipo utagundua kwamba haijawahi kuwa kawaida. Sikushangai sana kwa kusema kwamba ulikuwa unachukulia haya mambo kwa wepesi sana kama ulivyo sema mwenyewe ila nikuhakikishie kama ulikuwa unahisi umemaliza basi hata mchezo wenyewe haujaingia kabisa kuucheza huko mbele kuna hatari kubwa sana ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha ya watu, kutoa roho za watu pamoja na kusalitiwa sana, kusingiziwa sana lakini kikubwa tu usijisahau wewe ni nani na unataka kufanya nini kwa muda ambao bado utakuwa unaendelea kuwa hai hapa duniani hivyo vitu vitakupa wakati mzuri sana kwenye haya maisha na hata siku ambayo utakuwa unakufa utakuwa hauna majuto makubwa sana kama mimi hapa hakuna kipya tena hapa duniani hivyo kwa sasa nasubiri tu siku yangu ya kufa ifike ili nikapumzike huko kwa MUNGU japo sijui kama mimi ni wake au siyo wake” maelezo marefu yalikuwa ni kwa ajili ya kumhakikishia kijana wake kwamba kama alikuwa anahisi huo mchezo upo dakika za 80 ili kumalizika ila kichwani kwake atatakiwa kujua kwamba bado hata kuanza walikuwa hawajaanza kabisa, alichoka sana.

“Hivi kwanini mlimchagua yeye ndiye aende kule CIA na sio mtu mwingine?” aliuliza swali ambalo lilimfanya mzee huyo atabasamu sana na kugeukia upande wa pili sehemu ambayo kulikuwa na picha moja ndogo sana kwenye ukuta
“Yeye ndiye huyo kwenye hiyo picha ambayo unaiona hapo juu ya huo ukuta, nimemlea kama mwanangu wa kumzaa kabisa baada ya kumuokota mtaani akiwa hana msaada wowote wala mtu yeyote yule wa kumpa malezi, nilimpenda sana kuliko hata nilivyo jipenda mimi mwenyewe baada ya familia yangu yote kuuawa hivyo huyo ndiye aliyekuwa amebaki kuwa familia yangu ya pekee, inaniuma sana baadae amekuja kuwa mtoto ambaye mimi mwenyewe ndiye niliye mtelekeza huwa muda mwingine natoa mpaka machozi maana kama ningemuacha aishi maisha ya kawaida mpaka sasa angekuwa na maisha ya kawaida tu mtaani na familia yake huenda hata angekuwa mkulima au mfanya biashara mashuhuri sana ndani ya jiji la Dar ila kwa bahati mbaya sana nilimuingiza kwenye hii dunia ambayo inakuchagulia yenyewe muda wa kufa na wala sio kwa mapenzi ya Mungu kwa sababu hata wewe mwili wako unakuwa unanuka sana damu za watu ambao unakuwa umewaua” alipumzika na kutoa kitambaa kwenye mfuko wake professor Michael akajifuta machozi kwenye macho yake na hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kabisa kwenye maisha yake yeye kutoa machozi hadharani hata huyo kijana wake alimshangaa sana hakuwahi kabisa kumuona kwenye hiyo hali hata siku moja, alirudisha kitambaa chake mfukoni kisha akaendelea tena.

“Hapo ulipo unatakiwa umshukuru sana MUNGU licha ya kwamba unaishi maisha haya ya kujificha ficha mpaka siku yako ya mwisho utakayo kufa basi una ahueni unajua kila kinacho endelea kwenye huu ulimwengu, unaelewa kwamba Tanzania ndiyo nyumbani kwenu, unajua familia yako ilipo japo wao wanajua kwamba ulishakufa hivyo mara moja moja hata kwa kuibia unaweza kuwaona ndugu zako, hapo ulipo hata kama uliwahi kuwa na mchumba wako basi utamkumbuka na huenda siku moja mkawa wote tena lakini yule mwenzako hana ufahamu wowote ule kuhusu maisha yake ya nyuma, hajui chochote na wala hakumbuki chochote yeye anaishi wakati uliopo na ujao wala hana wakati uliopita kuhusu Tanzania kwenye kichwa chake” mzee huyo alitoa kitambaa tena akiwa anajifuta machozi ambayo kwa sasa yalikuwa yanatoka kwa wingi sana alikuwa anaongea mambo ambayo yalikuwa yanamkumbusha mbali sana.

“MUNGU naomba unisamehe sana kuyaharibu maisha ya huyu mtoto sijui kama kuna kitu gani nitaweza kulipia mpaka wewe na yeye mkanisamehe ila naomba nisamehe sana kwa sababu nilifanya haya ili kuyalinda mamilioni ya maisha ya watu wangu wa Tanzania ambao hawajui hili wala lile ambalo linatokea kwenye nchi yao” aliongea kwa sauti kubwa sana akiwa anaenda kuitoa picha hiyo ukutani na kuiweka kwenye mikono yake, alitoa ishara na kijana wake alielewa professor huyo alichokuwa anakihitaji, aliletewa sigara ya bei kubwa sana, aliiweka kwenye mdomo wake na kuanza kuivuta kwa hisia sana huku akiwa anasogelea dirishani na kuangalia mazingira mazuri ambayo yalikuwa yamelizunguka hilo eneo.
“Mkuu sijakuelewa unavyosema yeye ni kama mnyama na una maana ipi kusema kwamba hana kumbukumbu ya kitu chochote kwenye maisha yake na hii inakuwaje kwamba itafikia hatua kwamba hata sisi anaweza akaja kutusahau?” maneno ya kijana huyo wa kundi la TOXIC yalimfanya mzee huyo akohoe kidogo ili kumjibu swali lake.

“Yule hawezi kuwasahau nyie, hata kama angeamka kutoka usingizini basi kitu cha kwanza ambacho huwa kinakuja kichwani kwake ni sura 9 tu kisha huwa zinafuata zingine na taarifa zingine kati ya hizo sura 9 tano ni za kwenu nyie na hata huko aliko na yeye pia anajua kwamba Jason ni kiongozi wake na anamheshimu na kumuogopa sana kwa sababu kuna siku aliwahi kujaribu kupigana naye Jason alitaka kumuua hiy……” alitaka kuendelea kijana wake alimkatisha

“Unataka kuniambia X aliwahi kupigana na kiongozi?”
“Ndiyo”
“Kivipi? Kwamba hakujua au?”
“Alikuwa anajua tu nadhani lengo lake alitaka kujaribu kuzipima nguvu zake kubwa sana ambazo anazo alihisi anaweza kutamba nazo kwa Jason pia hivyo alitaka kujipima kama atammudu kiongozi wake”
“Kipi kilitokea siku hiyo?”
“Alivunjwa mbavu zake na kama tungechelewa kumtibia angekufa”
“Hii unanisimulia ni tamthiliya au ni kweli”
“Siku mkikutana tena angalia mbavu yake ya kulia kuna ubavu mmoja haupo ulitolewa kwa sababu hiyo hiyo ndiyo maana nimekwambia usije ukaruhusu Jason akakupiga na mkono wake wa kulia nakuapia utakufa kama sio hiyo sehemu kuharibika vibaya na kuhitajika kutolewa mwilini siyo mwanadamu yule”
“Mhhhh bosi unanitisha sana”
“Hiyo siyo kukutisha nakwambia ukweli hata siku moja usije ukataka kuleta ujuaji mbele ya Jason unaweza ukanichezea hata mimi nitakuonea huruma ila sio yule japo nyie nyote wanne anawapenda sana na hakuna mfano yupo tayari hata kuutoa moyo wake pale inapo bidi ili kumtibia mmoja wenu”

“Tumebahatika kupata kiongozi bora sana, sasa bosi ilikuwaje X unasema kwa Tanzania ana watu 9 kichwani mwake ambao anawakumbuka na kuwajua wakati hata ndugu zake tu hawawezi kuwa wachache hivyo na watu hao wengine ni akina nani ambao anawakumbuka”

“Ukitoa nyie watano mtu mwingine ni mimi hapa wa 6, IGP wa 7, Markvelous Japhary wa 8 na mheshimiwa raisi ambaye ameuawa alikuwa wa 9. Hao ndio watu pekee ambao hata akikutana nao leo hawezi kuwadhuru ila huko kwingine kama akipewa nafasi ya kuua basi huwa anaua hata bila kuuliza”
“Unamaanisha hata akiletewa ndugu yake hapa anaweza kumuua?”
“Ndugu zake kwake yeye ni sisi watu 9 tu basi”

“Mhhhh mbona haya mambo sijawahi kuyajua kabla?”
“Unahisi yeye anajua kuhusu wewe?”
“Sijui”
“Kati yenu ambaye ana taarifa zenu zote ni Jason tu basi ila nyie wengine mnajuana kwamba ni ndugu kwenye kazi tu basi ila hakuna ambaye ana taarifa za mwenzake”

“Hii ni hatari kuliko hata nilivyokuwa ninafikiria naona mambo yatazidi kubadilika kila sekunde moja inavyo hesabu”

“Unataka kujua kwanini anawakumbuka watu 9 tu kwenye akili yake?”
“Ndiyo mkuu” alijibu akiwa ana shauku sana ya kuweza kulijua hilo jambo maana haikuwa ikimuingia akilini kabisa kuambiwa kwamba mtu ambaye alikuwa mtu mzima kabisa awe anawakumbuka watu 9 tu kwenye maisha yake kutoka ndani ya nchi ya Tanzania, Professor Michael alivuta moshi mwingi na kuupuliza nje kisha akaizima sigara hiyo na kuliweka koo lake sawa alihitaji kumfunulia uhalisia wa X ambaye ni kijana asiye julikana kabisa ndani ya kundi la hatari la FIVE POISONED SERIAL KILLERS.

Haya mambo ni ya kweli anacho kiongea huyu mzee kwamba mtu awe anawakumbuka watu 9 tu kutoka ndani ya taifa alilo zaliwa?..43 naweka nukta tunafika mwisho.

Wasalaam

Bux the storyteller.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
STORY: INNOCENT KILLER (THE REVENGE)
STORY WRITER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP : 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
SEHEMU YA 44

SONGA NAYO............
“Nitakupa upande nusu wa maisha yake huko kunako bakia siku ukikutana naye muulize yeye mwenyewe aweze kukuelezea, nitakwambia yale ambayo ni ya mhimu kumhusu yeye na kwanini yeye ndiye kiunganishi kwenye hiyo TOXIC akiwa anaiwakilisha herufi ya X na utajua kwanini kwamba bila yeye kazi inaweza kuanza na moja”
“Kama nilivyosema ni kwamba nimemlea mimi mwenyewe kwa mkono wangu, nimemkuza mwenyewe kwa mkono wangu, nimemsomesha mwenyewe kwa mikono yangu na baadae nikaja kumtengeneza kuwa kiumbe cha namna hii kwa mikono yangu mwenyewe hata huko aliko ni mimi mwenyewe nilimpeleka kwa mikono yangu pia. Huyo mtu nimesema kwamba anawakumbuka watu 9 tu pekee kwa sababu tulimtoa kumbukumbu ya maisha yake yote ya nyuma na kumuwekea kumbukumbu ambazo tulikuwa tunazitaka sisi wenyewe na ndiyo sababu hawezi kukumbuka chochote mpaka siku atakapo rudishwa kwenye hali yake ya kawaida napo itamchukua miezi 6 mpaka mwaka mzima ndipo aweze kurejesha kumbukumbu zote na kwa wakati wote huo atakuwa anapitia kipindi cha maumivu makali sana kwenye kichwa chake ambayo yatamfanya atamani hata kufa”
“Sasa swali ambalo ulitakiwa kujiuliza ni kwamba kwanini tulimtoa hizo kumbukumbu zake na kumuwekea ambazo sisi tulihitaji kuziweka?, jibu lake ni kwamba wakati unaandaliwa huu mpango kwa mara ya kwanza ilipangwa nyie kila mtu apelekwe kwenye nchi yake na wala msijuaje kabisa na ndicho kilicho fanyika kwa mara ya kwanza hamkuwahi kujuana kabisa mpaka ilipokuja kutokea ulazima wa nyie kuwa pamoja tukaamua kuwaweka pamoja na hapo tulipata wakati mgumu sana kumpata kiongozi wa kundi lenu ambaye kila mmoja kati yenu anaweza kumheshimu, kumtii, kumuogopa pamoja na kuwa tayari kujitoa kwa lolote kwa ajili yake, ulifanyika mchujo mkali sana ambao kati yenu hakuna hata mmoja ambaye aliwahi kuujua kwani mlikuwa mnapewa mitihani mizito sana bila nyie kuelewa na hapo ndipo tulimpata Jason”

“yule ana nguvu ya uongozi ndani yake, ana mamlaka, ni mtu mwenye hekima sana ila akibadilika hata mnyama anasubiri mbele yake sina imani hata kama simba mwenywe anaweza akawa na ujasiri wa kusimama mbele yake kwa dakika zaidi ya tano, na kingine ambacho kilimpa pointi kubwa sana yeye kuwa kiongozi ni uwezo wake wa kimapigano na namna ya kuyatenda mambo, alikuwa anafanya vitu ambavyo hata sisi wenyewe tulikuwa hatuwezi kuvifanya na tangu hapo tukamtangaza kuwa yeye ndiye kiongozi na bosi wenu mpya nadhani baada ya muda kwa uwezo wake hata nyie mlianza kumtii sana”
“Ule mpango wa kuwarudisha na kuwaweka pamoja baada ya kumpata kiongozi wenu sasa mezani zilichangwa karata za mtu wa kumpata ili kuweza kumuingiza ndani ya CIA, hapa tulipata shida kubwa sana tena sana kwani vigezo vya mtu kuweza kuingizwa kule huwa inachimbuliwa historia ya maisha yake kuanzia siku aliyo zaliwa mpaka siku ambayo yupo kwenye mikono ya hao watu na wanataka kumfanya kuwa mmoja wao. Kuna baadhi ya sifa ambazo lazima mtu uwe nazo ili angalau upate hiyo nafasi ya kuingizwa huko, kwanza uwe na akili sana tena sana hiyo ilimpitisha kwa asilimia 100 kwa sababu kati yenu wote yule ndiye mtu ambaye alizaliwa na akili kupitiliza kwa baadhi ya sisi tunao mjua kwa kina huwa tunamuita the living alien kwa kupima uwezo wake hata kwa kutumia mashine. Baada ya kupita kwenye hilo tuliangalia kitu cha pili uwezo na uvumilivu kwenye mwili wake huo alikuwa nao, tulimuangalia namna ya uchambuaji wake wa taarifa, siri je anaweza kukaa na kitu hata kama atateswa vipi, yes alikuwa ana huo uwezo mkubwa baadae tukahitimisha na namna ya ufanyaji wa upelelezi tukakuta huyu anafaa kwenye kila sehemu hivyo jina lake moja kwa moja likawa limepita huko”
“Jason ndiye ambaye alitakiwa kuwekwa hapa ila kilichokuja kumkwamisha yeye tuliangalia kwamba huyu kaka yake ni jaji mkuu kuna siku taarifa zake zitakuja kuwa wazi sana hiki kitu kinaweza kuleta madhara makubwa sana na huenda kila kitu kitakuja kuwa hadharani mwisho wa siku tukaharibu kila kitu kitu ambacho kitapelekea hata uhusiano wetu na nchi ya marekani kuweza kufa tukaamua kumchukua huyo ambaye ninyi mnamjua kama X ila jina lake la kuzaliwa anaitwa Sospeters Lukas na sasa kilichokuwa kimebaki hapo ni kwamba je tutafanikiwa vipi kumuingiza huko?”

“Hilo swali lilituchukua muda mrefu kidogo kuweza kulichunguza kwa umakini kwani kama tungeharibu hata nukta moja tu basi mpango mzima ulikuwa unaingia maji na unga unakuwa hauna kazi, uamuzi wa kwanza ilikuwa ni kuzifuta kumbukumbu zake zote za nyuma ili asiwe na uwezo wa kukumbuka alikotoka ni wapi, yeye ni nani, ndugu zake ni akina nani na maisha aliyowahi kuyaishi nyuma asikumbuke chochote kile maana kwa maelezo yake licha ya kumuokota mtaani ila familia alikuwa nayo japo wanajua amekufa kwa muda mrefu sana ba…..”

“Bosi samahani sana kulikua na haja gani ya kuweza kumpotezeshea kumbukumbu wakati mlikuwa na uwezo wa kufanya hicho kitu akiwa ana utimamu wake?” kijana huyo alimuuliza kiongozi wake hiyo sehemu maana ka mtazamo wake aliona kama ni kitu ambacho hakikuwa sawa kabisa ni kama viongozi wake walikurupuka sana kufanya maamuzi hayo.

“Kwenye maisha yako unatakiwa kujua kwamba udhaifu mkubwa wa binadamu yeyote yule huwa ni kumbu kumbu, kumbukumbu zinaweza kukufanya ukafanikiwa sana, zinaweza kukufanya ukarudi nyuma sana, lakini zinaweza kukuleta mpaka magonjwa ya akili sana. kila jambo ambalo unaliona mtu anateseka nalo au anafurahia nalo ujue kwamba nyuma yake kuna historia nzito sana juu ya jambo hilo hapa nitakuwekea mifano kadhaa ili unielewe”
“Mfano kwa kwanza nayaweka mapenzi, mapenzi kama yalivyo huwa sio tatizo sana na sio kitu ambacho kinamuuma sana mtu pindi anapokuwa ameachwa au ametendwa vibaya sana tofauti na matarajio yake yalivyokuwa tangu mwanzo ila kitu ambacho huwa kinamfanya mpaka mtu anaumia sana huwa ni yale mazoea, na maisha ambayo waliyaishi kabla hapo ndipo linakuja suala zima la kumbukumbu za mtu maana yake bila kumbukumbu huwezi ukayakumbuka hayo mazoea wala ule wakati ambao mlikuwa kwenye furaha kubwa hivyo kwa wakati huo wewe hata kama mtu akikuacha utaona sawa tu tofauti na huyo ambaye kumbukumbu zote amezihifadhi kwenye kichwa chake”

“Mfano wa pili ni kwa wale wanaume wapiga punyeto, lile tendo ni baya sana kwa afya ya mwanaume hususani kwenye uzazi pale mtu anapo lifanya linakuwa sugu sana, hilo tatizo huwa haliji tu kutoka sehemu isiyo julikana huwa ni kumbukumbu za marejeo wa hayo matukio ambayo mwisho wa siku huwa yanakaa kwenye kichwa yaani akili yanahifadhiwa huko hivyo huwa inafanya mtu kila akikumbuka anakuwa na ashiki kubwa ya kurudia tena na hupelekea mpaka saikolojia ya mtu kuathirika pakubwa sana na mkichelewa kulitibu linaweza kupelekea hadi mwanaume kutokuwa na uwezo kabisa wa kuzalisha”

“Mfano wa tatu ni maisha, kwenye maisha mtu ambaye amepitia mambo mazuri sana basi hata baadaye yake huwa ni njema na nzuri kuliko mtu yeyote yule kwani kwenye kichwa chake yanakuwa yametawala mambo yaliyokuwa bora tu ila ni tofauti na yule mtu ambaye kwenye maisha yake ana historia za kutisha na maisha magumu sana au aliwahi kukumbwa na matatizo makubwa sana kama kutengwa, kunyanyaswa au kutumikishwa kingono basi hizo kumbukumbu huwa zinapelekea mpaka akili yake inaathirika moja kwa moja na kuwa ya hovyo sana kiasi kwamba kuna muda huwa inashusha mpaka ufanisi wa mtu kama kwenye kazi na sehemu zingine ambazo mtu anatakiwa kupambana kwa sababu ya kuileta baadae bora kwake”

“Mifano ni mingi sana ila nimekupa hayo machache sana ili unielewa baadae usiwe na maswali mengi, kwahiyo lengo la kumfuta kumbukumbu zake ni kwamba tulihitaji eneo ambalo tunampeleka akafanye kazi kwa asilimia angalau 90 mpaka 100, nyuma ya pazia ni kwamba kwenye moyo wake ana kisasi Kizito sana kwa ndugu zake kwa sababu walimtupa maana yake kama angekuwa na kumbukumbu zake basi angeishi kwa kuteseka sana na huenda ingeharibu kazi kwa sababu hizo kumbukumbu kuna mashine ukiwekwa zinaweza kuonekana vizuri tu na wataalamu wa usalama hususani kwa nchi kubwa kama Marekani maana yake ni kwamba kama angekutwa na hiyo hali basi moja kwa moja mpango ungefeli kwani wangeupata uhalisia wa maisha yake ya nyuma kwa wepesi sana unahisi ingekuwaje? Mpaka hapo jibu unalolipata ni kwamba mpaka leo angekuwa alishauawa kwa sababu ukijulikana kwamba wewe ni mamluki haupewi hata nafasi ya kujielezea uneteswa ili utapike siri zote kisha unauliwa na maisha mengine yanaendelea” alipumzika mzee huyo ambaye alikuwa amemuweka chini kijana huyo akiwa anagusa gusa kuhusu stori ambazo zilijificha nyuma ya pazia kwenye hilo jambo ambalo walikuwa wanalifanya.

“Kilifanyika nini mpaka akafanikiwa kuingia kule?” aliuliza kijana huyo akiwa bado na shauku ya kuweza kumaliziwa taarifa zote ambazo moja kwa moja zingempa muongozo wa kupata baadhi ya taarifa za mhimu kuhusu hilo jambo

“CIA wanataka watu wenye uwezo mkubwa sana kiakili sasa kwa sababu yeye alikuwa ana uwezo mkubwa sana wa kiakili haikutupa shida kuhusu hilo, baada ya kumaliza kufuta kumbukumbu zake ndipo tuliingiza picha na taarifa za hao watu tisa ili asije akawasahau kwenye maisha yake kisha tukamjazia taarifa nyingi sana kwenye kichwa chake za CIA ili atakapo amka awe ana taarifa nyingi sana kuhusu CIA na baadhi ya mipango yao mikubwa ambayo walikuwa wamepanga Kwenda kuifanya kwa hapo baadae na hapo ndipo ambapo kete yetu ya kwanza ilikuwa inaenda kuanzia maana bila hivyo hakuna kitu ambacho tungefanikisha kukifanya”

“Mkuu sijakuelewa hapo umemaanisha nini kusema kwamba ndiyo ilikuwa kete yenu ya kwanza kuanza kuisukuma?”

“Yes hiyo ndiyo ilikuwa kete yetu ya kwanza hatukumpatia taarifa za CIA tu tulimpatia za usalama wa nchi nyingi sana zingine ambazo majasusi wetu walihangaika sana wengine wakipoteza mpaka maisha ili kuzipigania hizo zote ilikuwa tu ni kwa ajili ya kumuingiza ndani ya shirika hilo wanalo dai kwamba ndilo namba moja kwa usalama zaidi ndani ya dunia na huo ndio ulikuwa mwanzo wa mchezo wa kumtoa kafara yule mtoto na kumtoa rasmi kwenye mkono wangu na kumpeleka kwenye mkono wa mtu mwingine ambaye hatukuwa na imani sana kwamba anaweza akawa hai huko atakako kuwa” aliongea kwa msisitizo mkubwa sana mzee huyo kwenye kulielezea jambo hilo la namna alivyoweza kumpoteza kijana wake kwenye mkono wake baada ya kumtoa kumbukumbu zake zote kwenye kichwa chake.

Mbona hii historia ya X inatisha sana, walifanyaje mpaka kufanikisha kumuingiza ndani ya hilo shirika bila kushtukiwa na hatima yake ilikuja kuwaje mpaka kumtoa huko inatakiwa afe? Huyo X ni nani hasa na ana taarifa gani za mhimu sana namna hiyo?..44 naweka nukta tukutane sehemu inayokuja ili tuufunue ukurasa mpya wa maisha ya X baada ya kutoka kwenye mikono ya professor Michael.

Wasalaam

Bux the storyteller.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
STORY: INNOCENT KILLER (THE REVENGE)
STORY WRITER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP : 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
SEHEMU YA 45

SONGA NAYO............

Makelele yalikuwa ni mengi sana ndani ya jiji la Dar es salaam kuhusiana na lile jambo ambalo lilikuwa limekutwa kwenye makaratasi ambayo yalikuwa yamesambazwa mtaani watu wengi waliunga mkono sana hizo hoja kwamba kwa watu waliokuwa wamehusika na hilo jambo basi hawakupaswa kabisa kuchekewa na kama kuna mtu atatokea kama ilivyo elekezwa kuwapa adhabu watu hao basi wananchi wangempa sapoti ya moja kwa moja mtu huyo kama angehitaji msaada wao lakini haikuwa hivyo tu kuna wananchi wengine walikuwa wapo kinyume kabisa na jambo hilo kwao waliamini kwamba hiyo ilikuwa ni michezo ya serikali kuweza kulizima hilo jambo ili wananchi wachukuliwe kama wajinga na waamini vitu ambavyo walikuwa na uhakika navyo kwamba vilikuwa ni vya uongo.

Watu ambao walikuwa wanapingana na hilo jambo walidai kwamba ili waweze kuamini kwamba hicho kitu kilikuwa ni cha kweli basi watathibitisha pale ambapo mwanasheria Yasinta Kobe atarudishwa mtaani baada ya siku mbili kama ilivyokuwa imeandikwa, kama mtu huyo atafanikisha jambo hilo basi wataweza kuanza kumuamini kwamba aliyo yaongea ni kweli na watahitaji aeleze kwamba alimtoa wapi mwanasheria huyo isije kuwa ni yeye amemteka halafu anajifanya kumuokoa, siku zilikuwa ni mbili tu ambazo zilitolewa kwamba mwanasheria huyo anatakiwa kupatikana.

Mambo yote hayo ambayo yalikuwa yanaendelea Nayrah ama waweza kumuita Nurryat Hashim na familia yake walikuwa wanaona tukio hilo moja kwa moja kwenye moja ya jengo la kifahari sana ambalo walipelekwa huko Kigamboni, maisha yalikuwa yanaenda kwa kasi kubwa sana kwa upande wao na hivyo wakaamua kuuamini muda kwamba ungewapa kila kitu, alikuwa anajiandaa siku hiyo kwa sababu ndiyo siku ambayo alitakiwa Kwenda kuanza rasmi kazi ndani ya hospitali ya taifa ya Mhimbili hivyo wakati huo walikuwa sebuleni na familia wakipata kifungua kinywa kilichokuwa kimeandaliwa na mama yake mzazi. Kitu ambacho kilimfanya Nayrah ashindwe kuendelea kupata hiyo chai ya asubuhi na baada ya kuona ule muda ambao ulikuwa umetolewa kwa ajili ya mtu huyo kulipa hayo mambo kwa wale wahusika ambao hawatakuwa wamejitokeza ndani ya miezi sita, akili yake pia ilimtuma kwamba hata Jason aliahidi kurudi ndani ya muda wa miezi sita, alijikuta hata hamu ya kula imemuisha kabisa akili yake ilikuwa inataka kuanza kuunganisha hayo matukio lakini moyo uligoma kabisa kwani alikuwa haamini kama yule mtu ambaye mpaka muda huo alikuwa ameamua kumkabidhi moyo wake alikuwa ni mtu ambaye alikuwa ana uwezo wa kufanya tukio lolote la namna hiyo, alitoka nje haraka sana akiwaacha wote wakiwa wanamshangaa tu.

Alifika nje na kumfuata mwanaume mmoja ambaye alikuwa amekaa kwenye bustani mmoja hivi chini ya mti akiwa kwenye nguo nyepesi za mazoezi, alionekana kwamba ni muda mfupi tu alitoka kufanya mazioezi na hivyo alikuwa anapumzika kidogo mbele yake pakiwa na maji ya moto kabisa ambayo yalitoka kuchemshwa, alishtuka kidogo baada ya kumuona mwanamke huyo akiwa anakuja kama anahofu sana kwenye moyo wake.

“Karibu madam” alimkaribisha kwa heshima akiwa anamuonyesha sehemu ya kukaa, Nayrah hakujibu kwanza alikuwa bado anayashangaa yale maji ya moto na kumshangaa kijana huyo ambaye umri wake ulikuwa wa kawaida sana, hali hilo ilimfanya kijana huyo atabasamu kidogo

“Unashangaa kwamba ni kwanini nakunywa maji ya moto namna hiyo?” hakujibu bali aliitikia kwa kichwa tu kukubali.
“Mwili wangu hautakiwi kuingiza ndani vitu vya baridi japo ninaweza kukaa sehemu yenye barafu kwa siku mbili nikiwa bado nipo hai kwa sababu ndani mwili wangu una uwezo mkubwa sana wa kuhifadhi joto lakini pia huwa sinywi maji ya baridi kwa sababu yana athari kubwa sana kwangu utakuja kujua hapo mbele, okay naona kama umekuja na wasiwasi sana nadhani utakuwa una maswali unaruhusiwa kuuliza madam” alimjibu mwanamke huyo akinyanyua kikombe na kunywa maji hayo ambayo yalikuwa ya moto mpaka yanafuka moshi, Nayrah alisisimka sana kwa hicho kitendo.

“Kwani nyie ni akina nani?”
“Kwanini unauliza hivyo?”
“Kwa sababu nilisikia unamuita bosi na cha ajabu nikamuona mpaka IGP sasa yule Jason anahusika nini na IGP mbona kama mnanichanganya, ghafla tu naambiwa nikaanze kazi kirahisi tu ambayo nimeihangaikia kwa mwaka mzima nikiwa nateseka, mmekuja huku na kutuhifadhi kwenye hii nyumba mpya na ya gharama kubwa sana, mama yangu mmesema anaanza matibabu kwa gharama yoyote ile na hata baba yangu pia kitu ambacho sicho cha kawaida kwenye haya maisha ya mwanadamu mtu kupoteza muda wake, pesa zake na watu wake kwa sababu ya kukutetea wewe ambaye hata hakujui sana hivyo nataka kujua japo kidogo tafadhali maana mpaka sasa sielewi” Nayrah alikuwa anauliza kwa mashaka sana bado alikuwa ana wasiwasi maana alihisi kwamba hakuwa akijua hata ABC ya hao watu na walionekana kumheshimu sana.

“Kwanza naomba nikusahihishe kidogo ndipo uulize maswali yako maana umeongea mambo mengi sana mpaka nashindwa nianze na lipi. Hii nyumba sio kwamba umekuja kuhifadhiwa hapana hii nyumba ni ya kwako na ni mali yako halali kuanzia sasa ilibaki tu kwamba tukupeleke kazini baadae uje ukabidhiwe nyaraka zo…..” alitaka kuendelea kuongea lakini Nayrah alicheka sana baada ya kuona kama kijana huyo alikuwa anamdhihaki

“Hahahah hahaha hahah nadhani utakuwa umelewa mapema sana mimi hapa wapi na wapi na hizi nyumba?” jibu lake lilimsikitisha sana huyo kijana ambaye aliishia kusikitika tu.

“Hii nyumba ni mali yako wewe na unaweza kutufukuza hata sisi hapa kama ukitaka, unawaona wale (akiwa anawaonyesha wanaume wanne ambao walikuwa wamekaa maeneo tofauti tofauti wakiwa kwenye suti za bei sana wakidumisha ulinzi) wale wanahakikisha wanakufa wao kwanza, kisha mimi ndipo ufuate wewe jibu rahisi ni kwamba hakuna mkono wa mtu ambaye alizaliwa na mwanamke unaweza kukugusa wewe bila ridhaa yako kama wale wako hai na mimi hapa hivyo haya yote unayo yaona hapa ni kwa ajili yako”

“Hapana hapana hapana hii haiwezekani, why me? Kuna nini mpaka unambie mimi napaswa kutendewa yote hayo? Unanichanganya aaaaghr” Nayrah alijishika kichwa akiwa anaongea kwa sauti hayo mambo yalikuwa kama vile anasimuliwa tamthiliya ambayo angeamka akakuta imeisha cha ajabu yeye ndiye alikuwa mhusika mkuu kwenye hiyo tahmthiliya na haikuwa na dalili kabisa ya kuisha.

“Haya maswali mengi utatakiwa kumuuliza bosi mwenyewe kwa sababu kama kuna kosa likifanyika ukapatwa na kitu kibaya basi ataniua” maelezo ya huyo kijana yalimfanya Nayrah atoe macho kama vile fundi simu kapoteza nati ya simu ya watu ambayo ni ya bei ghali sana
“Whaaaaaat?”
“Unatakiwa kuwa salama kwa masaa 24 ya mwaka mzima”
“Bosi wako ni IGP au nani?”
“Hapana”
“Ni nani sasa”

“Jason”
“How”
“Mhhh wewe unataka kujua nini kwani kumhusu yeye?”
“Yeye ni nani hasa mbona kama mwanzo nilimuona kwamba ni mtu wa kawaida sana”
“Yule ndiye wewe ulimuona wa kawaida?”
“Ndiyo”
“Okay haya maswali basi siku ukimuona tena unatakiwa kumuuliza yeye mwenyewe”

“Familia yake iko wapi?” swali la Nayrah lilimfanya kijana huyo ainamishe kichwa chake chini, aliingiza mkono kwenye mfuko wake akaitoa simu, aliikagua kwa dakika moja tu na kumpatia Nayrah, mbele ya kioo cha simu ilikuwa inaonekana picha ya watu wanne, jaji mkuu wa nchi ya Tanzania, mkewe na jaji mkuu, mtoto wake wa kike huku pembeni akiwa amesimama Jason akiwa kwenye suti iliyokuwa imempendeza sana akiwa mwingi wa tabasamu kwenye uso wake, Nayrah ni kama alishikwa na kigugumizi

“What is this? (Hiki ni nini?)”
“Hiyo ndiyo familia yake”
“Una maanisha nini kusema hivyo? huyu ninaye muona hapa ni jaji mkuu sasa unasemaje ni familia yake?” Nayrah alikuwa kama vile anaona mtu huyo anamchanganya, kijana huyo aliichukua simu kutoka kwenye mikono yake akaiweka tena mfukoni na kutamka.

“Jason ni mdogo wa damu kabisa wa kuzaliwa wa jaji mkuu ambaye ameuliwa hapo juzi, hivyo hao wote ambao walikufa na huo msiba wa kitaifa ulikuwa unamhusu sana yeye, kwao walikuwa wapo wawili tu pekee hivyo kwa sasa amebaki yeye mwenyewe akiwa hana ndugu wa damu hata mmoja zaidi tu ya sisi hapa ndugu zake wanne ambao jumla yetu tupo watano” maelezo yake yalionyesha moja kwa moja naye ni memba wa kundi la Five poisoned serial killers, sasa walikuwa wanakamilika wote, mmoja tulimuona maeneo ya chuo cha NIT akiwa kama mlinzi wa pale kisha baadae akatoweka baada ya wanajeshi waliotumwa na mkuu wa majeshi kuuawa, wa pili alikuwa ni mlinzi wa professor Michael nchini marekani, watatu alikuwa ni X ambaye kwa taarifa alidaiwa kuwa ndani ya CIA, wanne alikuwa ni huyu ambaye alipewa kazi ya kumlinda bibie na wa tano alikuwa ni kiongozi wao mwenyewe ambaye ndiye Jason hivyo hawa watu walikuwa wametawanyika namna hii ila walidaiwa kuwa watu wa hatari kuliko isivyo kawaida kwenye maisha yao. Nayrah kwa maelezo aliyokuwa amepewa hapo alijishika kwenye eneo lake la moyo, alitamani kupiga kelele za kilio lakini sauti yake ni kama ilimsaliti kabisa haikutoka, alitamani dunia ijue namna alivyokuwa anajiskia lakini hapo walikuwa wawili tu pekee wamekaa, machozi yalianza kumshuka taratibu kwenye uso wake hakuwa akiamini kile alichokuwa anaambiwa.

“Kwanini hakuniambia, kwanini akaamua kunificha na kujifanya yeye ni mtu wa furaha sana kumbe alikuw ameipoteza familia yake yote? Bora angeniambia mimi niwepo wakati kama huu ambao yeye anahitaji mtu wa kuwa naye karibu kumpa furaha, atakuwa kwenye hali gani huko aliko please naomba uniletee Jason wangu hapa, nakuomba tafadhali nataka kumuona mbele yangu” aliongea kwa uchungu sana akiwa analia, alijisikia vibaya sana hiyo hali ilimfanya hata kijana huyo ajisikie vibaya sana kwani aliona kama binti atateseka sana kuingia kwenye dunia ya kumpenda mtu kama huyo, alisogea na kumkumbatia Nayrah hakumnyamazisha kulia ila alimpa bega lake alie mpaka pale hasira na dukuduku litakapo toka shingoni kwake ndipo waweze kuongea, hiyo ndiyo huwa dawa ya kilio unapo jisikia kulia usijizuie lia sana tena sana ila hakikisha pale utakapo nyamaza kulia basi hautalia tena kwa sababu ile ile ambayo ilikufanya ukalia mwanzo. Alilia kwa dakika kumi mpaka pale ambapo alianza kulia kwa kwikwi, mwanaume alimpatia kitambaa na kumkabidhi ili ajifute kisha kama alikuwa ana chochote cha kumwambia basi amjibu.

“Sitaki jambo lolote lile ila nataka kwanza unihakikishie kama huko aliko yupo salama, nataka uniambie kuna uhusiano gani wa yeye kusema kwamba nitamuona baada ya miezi sita, na kauli ya mhehsimiwa raisi kwamba baada ya miezi sita wahusika watakuwa wamepatikana lakini pia kwenye hizo karatasi ambazo zimesambaa sana mtaani ambazo nazo zinaelezea hiyo hiyo miezi sita naomba uniambie hayo tu sitakuuliza tena chochote kuhusu yeye” mwanamke huyo aliongea huku akiwa anajifuta machozi ambayo yalikuwa yanaishia usoni kwake.

“Yule yupo salama masaa 24 hakuna kitu ambacho kinaweza kumkuta popote pale atakapokuwa, kuhusu miezi sita hata mimi sijui ina maana gani maana hajaniambia ila nahisi kwamba anahitaji muda wa kukaa mwenyewe kutokana na haya matatizo ambayo yamemtokea yeye inampa ugumu sana kujichanganya na watu hivyo kuwa na subra msubirie yeye mwenyewe atarudi” alijibu kwa kifupi sana hakuhitaji kuanza kuchimbua taarifa nyingi sana kuhusu maisha yao halisi.

“Na IGP anahusikaje na haya na kwanini wewe ndiye amekuamini sana kukuweka karibu namimi?”
“Anajua kwamba hakuna ukucha wa mtu unaweza kukatiza mbele yako ninapokuwepo mimi, naomba nisiongee sana kuhusu IGP kwa maana sijui chochote nadhani utakapo onana naye itakuwa ni vyema sana ukimuuliza mwenyewe, ni muda wa kwenda hospitali madam ukaripoti naomba ujiandae namimi nikajiandae tuweze kuelekea huko” aliongea akinyanyuka na kumuacha Nayrah akiwa amekaa chini akizama kwenye mawazo mazito sana kuna mambo hayakuwa rahisi sana kuyachukulia kawaida kama ambavyo kijana huyo aliionekana kuyachukulia, mambo yalikuwa mazito alihisi kichwa kinamuuama sana.

Tupo taratibu sana na INNOCENT KILLER, wale watano nadhani kwa sasa umewajua wote huenda unasubiri kuona kwamba huyo mlinzi wa Nayrah yupoje uhalisia wake na anaiwakilisha herufi gani kwenye ile TOXIC na kazi yake ni ipi, twende taratibu tu utanielewa vyema, 45 nafika tamati tukutane sehemu zinazo fuata.

Wasalaam

Bux the storyteller.

Sent from my SM-A107F using JamiiForums mobile app
 
Sana, tupe vitu jomba
Ebwana hii story ni ya kimataifa na kama umeitunga wewe mwenyewe kwa akili zako basi wewe ni nyoko wa kimataifa katika utunzi, ukimpata mtu kama Jason Statham akakaa mbele ya kamera ikachezwa....[emoji119][emoji119][emoji119][emoji119]ebwanaeee[emoji119][emoji119] ni noma


Sent from my SM-A037F using JamiiForums mobile app
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…