Innocent Killer (The Revenge)

Innocent Killer (The Revenge)

STORY: INNOCENT KILLER (THE REVENGE)
STORY WRITER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP : 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
SEHEMU YA 20

SONGA NAYO............
Jason baada ya kufika nje ya Ikulu, kulikuwa na gari moja ya bei ghali sana yenye namba za Ikulu ilikuwa ikimsubiri yeye ili impeleke mahali ambapo alitakiwa Kwenda kupumzika usiku wa siku hiyo, aliingia humo ndani ambamo kulikuwa na dereva mmoja tu ila hakuwa tu dereva alikuwa ni komando ambaye alipewa kazi ya kuhakikisha anamfikisha mwanaume huyo salama sehemu yoyote ambayo angetakiwa Kwenda kwa muda wowote ule.

“Nadhani umeambiwa sehemu ambayo unatakiwa kunipeleka” aliongea Jason kwa sauti yake nzito sana
“Ndiyo mheshimiwa” mwanaume huyo aliyekuwa naye kwenye suti nzito nyeusi alijibu huku akiwa anaiwasha gari hiyo na kuanza kuondoka lakini aliombwa kusimamisha gari hiyo baada ya Jason kuona simu yake inaita na namba ilikuwa ni ngeni, aliiangalia kwa sekunde thelathini baada ya kuona inaendelea kuita tu aliamua kuipokea.

“Hello” sauti ya mtume ilisikika upande wa pili, sauti isiyokuwa na hatia yoyote ndani ya ulimwengu, ni sauti laini sana ambayo iliweza kumsulubu Samson akasahau kwamba kuna siri hakutakiwa kuzitoa, ni lafudhi ambayo haikuwa ikiumiza masikio pale mtu yeyote anapo pata bahati ya kuisikia, Jason alitulia baada ya kuisikia sauti hiyo ya kike ambayo ilikuwa na utulivu mkubwa sana ndani yake.

“Naongea na nani?” mwanaume alitamka baada ya kuwaza sana lakini hakuweza kuitambua sauti hiyo

“Nayrah” hili jina lilimfanya aumize ubongo wake haraka haraka ili aweze kuona kama anaweza kukumbuka mahali alipokutana na mwanamke mwenye jina kama hilo, ndipo ubongo ulipo msafirisha mpaka maeneo ya Mbagala wakati ameenda kuonana na ASP Bakari Zalimo alitabasamu kwa mbali.

“Ooooh nambie Nayrah”

“Samahani naweza kukuona?”
“Muda huu?”
“Ndiyo”

“Ok nipe nusu saa nakuja nitakuwa pale uwanjani nilipo kukuta siku ile ndani ya huo muda”
“Sawa” alishusha pumzi ndefu sana kisha kaangalia saa yake

“Kuna sehemu ambayo tunaweza kupata nguo za kawaida kwa muda huu?” alimshtua dereva huyo kwa sauti hiyo nzito.

“Ndiyo kiongozi kuna maduka yatakuwa wazi bado mapema sana saivi Kariakoo hapo hata njiani zinapatikana”

“Basi naomba tupite huko ukanichukulie nguo za kawaida kisha wewe utaniacha hiyo sehemu baada ya kunipa hizo nguo”

“Lakini mheshimiwa ameniambia nihakikishe ulinzi wako na kuhakikisha unafika salama sasa nitamweleza nini akiniuliza”

“Mwambie mimi ndiye niliyekupa maagizo uniache mwenyewe sihitaji kuwa na mtu yeyote yule kwa huu muda”

“Sawa kiongozi” Basi safari ilianza kuelekea Kariakoo ambapo gari yao ilikuwa ipo taratibu sana ili wahakikishe wanafanikiwa kuzipata nguo hizo kama Jason alivyokuwa ameagiza, kabla hata ya kufika kuna duka moja njiani waliona kwa ndani kuna suruali jeans za wanaume, tshirt na Laba, Jason aliomba gari isimamishwe hapo pangewafaa kuweza kumaliza hilo tatizo. Alitoa pesa mfukoni lakini mwanaume huyo alitikisa kichwa kukataa hiyo bili angemalizana nayo mwenyewe, basi alipewa vipimo na aina ya nguo za Kwenda kubeba kisha akatoka kwenye hiyo gari, ndani ya dakika 10 za kuhesabu alikuwa amesha maliza manunuzi, alirudi akiwa na mfuko uliokuwa umejaa.

Jason alibadilisha nguo humo humo ndani ya gari, mwilini alibakia na jeans, laba nyeupe na prova ambayo ilikuwa imeufiti mwili wake vyema na kumfanya kuonekana kama miongoni mwa vijana wa kisasa, nguo hizo kiasi chake zilisaidia kuuficha mwili wake ambao ulikuwa umejikata sana kwa mazoezi makali mno ila kwa kumuangalia ungehisi kwamba ni kijana mlegevu ambaye alikuwa anapenda kunyanyua tu vyuma vya kawaida kwa sababu mwili wake haukuwa umeumuka sana ulikuwa mwili wa kawaida ila ambao kila nyama ilikuwa imapangwa vyema sana mahali pake.

“Hiyo suti unaweza ukaitumia mwenyewe na kama haikufai basi waweza mpa hata rafiki yako, safari yako inaishia hapa niseme tu nashukuru mno kwa wema wako nina imani haitakuwa mwisho wa sisi kukutana ipo siku tunaweza kuja kukutana tena, uwe na usiku mwema” Jason aliongea kumpa mtu huyo maelekezo huku akiwa anaiweka vyema kofia yake kichwani na alikuwa amesha anza kuondoka ndani ya hilo eneo.

“Sawa kiongozi kuwa makini” baada ya kuisikia sauti hiyo alitabasamu kwa mbali huku akimnyooshea mwanaume huyo mkono wa kwaheri bila kugeuka, alitembea kwa dakika tano kuna tax aliiona ikiwa inapita aliipa mkono nayo ikaitikia na kusimama, akamuelekeza dereva tax huyo sehemu ambayo alitakiwa kuwepo na muda ambao ulitakiwa kutumika mpaka kuweza kufika ndani ya hilo eneo.

Dakika ishirini na tano ziliwatosha kufika Mbagala karibu kabisa na eneo ambalo Jason alikuwa amekusudia kufika japo zilibaki kama hatua hamsini ili aweze kutokekezea kwenye uwanja wa eneo ambalo ndipo alipanga kumkuta mrembo huyo, alilipa pesa yake na kuangalia muda ambao ulikuwa umesoma dakika 50 tangu aondoke ndani ya Ikulu maana yake kwa muda ambao alikuwa amemuahidi mrembo huyo alikuwa amevusha dakika 20, alijisonya mwenyewe kwa hasira kwa sababu alikuwa anachukia sana kwenda nje na muda ambao yeye mwenyewe alikuwa akijiwekea. Akiwa anaangaza huku na huku na kuanza kutembea kwenye njia ya chocho ambayo aliona itakuwa ni mkato wa kutokezea kwenye hiyo sehemu yenye uwanja mkubwa kirahisi alihisi kama nyuma yake kulikuwa na mtu, ni kweli baada ya kugeuka aliona kuna vijana sita ambao walikuwa na mapanga kwenye mikono yao haikumpa shaka kwamba hao walikuwa ni vibaka ambao huwa wanatumia mabavu kuweza kujichumia pesa alisikitika sana na kuanza kuondoka hapo.

“Acha dharau kabla hatujakupunguza kipande cha mkono wako mbwa wewe yaani unatuona na unajifanya kama vile hakuna kitu hautujui vizuri sio?” kuna sauti moja ya uvundo ambao ndani yake ilionekana kulikuwa na ugoro ulitoka kuliwa sio muda sana ilisikia masikioni kwa mwanaume ikamfanya kusimama, lilikuwa ni kosa kubwa sana kibaka kama huyo kumuita yeye mbwa na kuamrishwa mtu ambaye hata raisi wa nchi anaongea naye kistaarabu na kumuomba pale anapo mhitaji afanye jambo fulani, aligeuka akiwa ana hasira sana nadhani hata huyo kibaka kama angejua kwamba mwanaume huyo hiyo siku alitoka kumzika kaka yake wa damu basi asingethubutu kumuongelesha mtu wa namna hiyo.

“Kati yenu hapo ni nani ambaye amepata hicho kiburi cha kuniita mimi mbwa?” aliuliza kwa hasira huku akiwa anarudi walipo vijana hao ambao nao walikuwa wanamfuata, walidhani kwamba wamempata mwanaume mshamba ambaye walikuwa wanaenda kubeba kila alichokuwa nacho kwenye mwili wake, kabla hajafanya chochote simu yake ilianza kuita, aliitoa mfukoni na kuiangalia namba iliyokuwa inapiga ni ile ile ya Nayra, aliirudisha simu hiyo kwenye mfuko wake, simu ilikuwa ya gharama sana japo ilikuwa ni usiku wanaume hao walizidi kupata tamaa. Aliyekuwa mbele yao alijibu kwa kujigamba huku akiwa anasogea kwa kumkimbilia Jason alipokuwa akiwa ameunyanyua upanga wake mkononi.

“Ni mimi hapa ms***** wewe unasemaje?” alijibu kwa jeuri akiwa anaushusha upanga huo kwenye bega la Jason alihitaji kuutengenisha mkono huo kwa sababu waliona kama anawaletea jeuri watoto wa mjini, mkono wake alihisi huenda ni mfupi kwa sababu hakujua mwanaume huyo alimfikia saa ngapi, mkono wake ulidakwa kwenye kifundo chake ulivutwa na kuvunjwa kwa kutumia mkono mmoja tu, alipiga makelele sana upanga ulimponyoka mkononi lakini haukudondoka chini ulidakwa na Jason aliuzungusha na kumpiga kijana huyo na ubapa wa upanga kwenye shingo yake, hakutamka neno lolote lile alibaki ameganda kama ulikuwa mti hapo mwanaume akamsukumia pembeni na kulitupa panga hilo chini.

“Nisije nikawakuta kwenye haya maeneo tena wapuuzi nyie hamjui hata namna ya kuyatumia haya mapanga yenu halafu mnawakazia sauti watu na kuwapora, mbebeni mwenzenu ataamka keshokutwa na akiamka apelekwe hospitali maana mkimchelewesha atakufa, nitakaye mkuta tena sitakuwa na msamaha mwingine nitamuua” aliongea kwa hasira na kuwafanya vijana hao watano ambao walishuhudia hilo tukio la kutisha waanze kutetemeka, walimbeba mwenzao na kukimbia sana huku wakipiga kelele za kuyatete maisha yao, aliitoa simu yake mfukoni na kuipiga kwa mwanamke huyo ambaye alimuomba samahani kwa kuchelewa na kuhitaji amueleze ni wapi alipokuwa kwa wakati huo.

Nayrah baada ya kumuona mwanaume huyo alimkimbilia na kumkumbatia, kwake alikuwa anamuona mwanaume bora sana, mkarimu na mwenye moyo wa huruma sana ila kama angejua namna huyo binadamu anavyo ogopwa basi huenda hata kuwa na namba yake tu angejutia kwenye maisha yake.

“Kwanini umeniita na usiku saivi?” mwanaume huyo aliuliza wakiwa wamekaa kwenye tairi kubwa wakiwa wanaangalia namna watu walivyokuwa wanapishana mtaani hapo.

“Nimekuitia hapa kwa mambo matatu, jambo la kwanza nataka niseme kwamba asante sana kwa msaada wako wa siku ile kwa sababu sio rahisi sana mtu ambaye hakujui kabisa kukupa msaada kama ule sina cha kukulipa ila nina imani MUNGU atanilipia hilo, jambo la pili ni siku ile baada ya kunipa ule msaada zile pesa ilibidi nimfikishie na mama yangu ambaye aliniuliza nimepata wapi pesa zote kama zile ilibidi nimwelekeze kilicho tokea lakini hakuweza kabisa kuniamini mimi hivyo akawa anaomba kwamba anahitaji akuone ili ahakikishe awe na amani maana anakuwa kwenye wakati mgumu sana kutumia pesa ambazo hata hajui zinatoka wapi na malipo yake ni nini. lakini jambo la tatu nataka nikuombe msamaha sana kwa kile nilicho kifanya pale mbele yako siku ile kwa kujirahisisha kwamba najiuza na pia nahitaji kukupatia historia ya kweli kabisa ya maisha yangu” Nayrah aliongea kwa sauti yake ya kistaarabu sana ambayo ilimfanya aonekane kama ni mwanamke bora sana kwenye macho ya kila mwanaume ambaye angekuwa anamtazama kwa wakati huo.

Siku hiyo Nayrah alikuwa ni tofauti kidogo, alikuwa amevaa nguo za heshima sana huku kichwa chake kikiwa kimefunikwa na mtandio safi sana, Jason alikuwa makini sana kumsikiliza mwanamke huyo.

“Huogopi kukutana usiku kama huu na mwanaume ambaye hata humjui kwa sababu tu alikusaidia vipi kama anahitaji kukufanyia kitu kibaya? Huoni kama itakuwa ni tatizo kubwa sana kwako?” Jason alimuuliza Nayrah swali ambalo lilimfanya ainame chini kwa aibu, kwa namna walivyokuwa wanaongea ungehisi kwamba ni watu ambao walikuwa wamejuana kwa muda mrefu sana na hata kwa mtu ambaye angewaona angehisi watu hao walikuwa ni wapenzi wa muda mrefu sana bila kujua kwamba siku hiyo ilikuwa ni mara ya pili kukutana kwenye maisha yao.

“Kama ungekuwa na lengo baya namimi basi siku ile ile ambayo nilijirahisisha kwako ungeitumia kunifanya kile ambacho ungeona inafaa kwa upande wako lakini ulionyesha kwamba wewe ni mwanadamu wa tofauti sana ndiyo maana nikakuamini sana tangu siku ile” aliongea kistaarabu sana mwanaumke huyo kitu ambacho kilikuwa kinampeleka mbali sana Jason na kujikuta anatabasamu sana.

“Usiwaamini sana wanadamu kwenye maisha yako hata mimi usije ukaniamini tena kuanzia sasa, sina muda mrefu sana wa kukaa hapa ila mambo ya mhimu ni mawili tu hilo la asante unapaswa kumshukuru MUNGU na sio mimi, jambo la kwanza nahitaji unipe hiyo historia yako wewe na pia nitajitahidi sana niweze kwenda kuwaona wazazi wako kabla sijaondoka jappo sitakaa sana huko” Mwanaume huyo alijibu kwa sauti kavu sana kitu ambacho kilimfurahisha sana mrembo huyo kwa sababu alitamani sana kuaminika sana kwa wazazi wake hususani mama yake ambaye alikuwa akijielewa ukiachana na baba yake ambaye alikuwa ana ugonjwa wa ukichaa lakini pia alihitaji mama yake aweze kumuona mwanaume huyo ambaye kwake alikuwa kama shujaa kwake.

Je mwanamke huyu historia yake ina mambo gani ambayo yamejificha? Kwanini anahitaji mwanaume huyu aweze kuifahamu? Jason ni maamuzi gani aliyachukua?

Sehemu ya 20 inafika tamati panapo majaaliwa tukutane tena wakati ujao.

Wasalaam

Bux the storyteller.
 
STORY: INNOCENT KILLER (THE REVENGE)
STORY WRITER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP : 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
SEHEMU YA 21

SONGA NAYO............
“Nayrah sio jina langu la kuzaliwa ila hili nimejipa mimi mwenyewe na ndilo ambalo huwa nalitumia mtaani na watu wengi wananijia kwa jina hilo hawalijui kabisa jina langu halisi la kuzaliwa. Mimi kwa jina la kuzaliwa naitwa Nurryat Hashim, ni mzaliwa wa nyanda za juu kusini huko katika ardhi ya walima korosho, nilizaliwa kwenye moja ya familia ambazo zilikuwa na maisha bora sana tena sana, kwetu kulikuwa na kila kitu hakuna kitu ningeomba kwa wazazi wangu nikakikosa hiyo ilinifanya niamini ulimwengu ni miongoni mwa sehemu bora zaidi ambazo yanapatikana maisha bora katika historia ya uumbwaji huenda nilikuwa sahihi sana kwa wakati ule ila kiuhalisia sidhani kama kuna usahihi wowote ule ambao niliuona baadae.

Mimi ni mzaliwa wa kwanza (kifungua mimba) katika uzao wa watoto watatu na mimi ndiye mwanamke pekee kwenye idadi ya hao watoto, mimi ni miongoni mwa watoto ambao wamesoma shule bora sana na za gharama mno utotoni mpaka nilipofikia katika elimu ya sekondari ndiyo hapo mambo yalipo anza kubadilika sana. Baba yangu alikuwa ni mtu tajiri sana kwa sababu kwa historia yake ambayo nilipewa na mama yangu ni kwamba baba yangu enzi za ujana wake alikuwa miongoni mwa vijana ambao walijikita sana kwenye utafutaji wa mali, hakuwa akipata muda wa kufanya starehe wala kuwekeza kwenye mambo ya dunia hivyo hiyo ilimpelekea kuwa mtu ambaye mafanikio yalikaa naye upande mmoja.

Mzee Hashim alikuwa ni muwekezaji mkubwa sana kwenye kilimo hususani kwenye biashara ya korosho, alikuwa anamiliki mashamba ambayo ulikuwa huwezi kuyatembelea kwa miguu ukamaliza ilihitajika usafiri ambao ilikuwa ni kama mtu unafunga safari ya kutoka mkoa mmoja Kwenda mkoa mwingine kwa sababu ilikuwa mkitembelea mashamba hayo basi mngemaliza siku nzima kuyaona tu nilikuwa hata sijui idadi yake ni mangapi, na MUNGU alikuwa upande wake alibahatika kuoa mwanamke mzuri sana ambaye ndiye mama yangu mzazi, licha ya uzuri wa mwanamke huyo lakini alikuwa ni miongoni mwa wanawake bora sana ambaye kwa kiasi kikubwa mno amechangia baba yangu kuwa miongoni mwa watu ambao waliishi kwenye utajiri katika historia ya maisha yao.

Nikiwa mdogo nilikuwa nikiona watu kadhaa wakiwa wanakuja nyumbani kwetu kuhitaji msaada wa baba yangu na wengi wao alikuwa akinitambulisha kama ndugu zetu japo hatukuwa na mazoea ya kukaa muda mrefu pamoja hivyo wengi mimi nilikuwa siwajui, ilikuwa nikiwaona tu najua basi hawa ni shida zimewaleta na shida zao kama zikiisha najua sitawaona tena na ndiyo yalikuwa maisha ya kila siku pale ilifika sehemu mimi nilizoea tu kuwaona japo walikuwa kila wakija nyumbani basi wanahitaji ni msaada na baba yangu hakuwa na makuu alikuwa akiwasaidia sana kama kuwalipia watoto wao ada, pesa za mahitaji pamoja na matumizi yao wenyewe lakini hakuishia hapo tu kuna wengine aliwafungulia mpaka biashara za kufanya, haikumaanisha kwamba walikuwa wakiishi vizuri sana na hao ndugu zake hapana wala hawakuwahi kuhusika hata kidogo kwenye kuutafuta utajiri wake lakini yeye alifanya hivyo kwa sababu alijua hata iweje wale bado ni ndugu zake tu na yeye kufanikiwa haimaanishi aanze kuwakimbia au kuwakataa ingemfanya yeye mwenyewe aanze kuujutia utajiri wake.

Usiku mmoja tukiwa tupo mezani tunakula chakula cha usiku na wakati huo nilikuwa nipo katika masomo yangu ya sekondari ila wadogo zangu hawakuwa wakisoma maana walikuwa ni wadogo na walipishana kwa miaka miwili tu hivyo wao walikuwa muda mwingi wapo na mama, siku ile baba alirudi na mgeni ambaye alitutambulisha kama ni mtoto wa baba yake mkubwa yeye mama alikuwa akimjua vizuri mwanaume huyo. Kwa mwonekano alikuwa ni mdogo kwa baba, baba alimuomba mama kwamba mtu huyo alikuja hapo kukaa kwa muda fulani na baada ya huo muda basi angeondoka na maisha mengine yakaanza baada ya hapo.

Hatukujua dhamira ya yule mtu kuja kuishi maeneo ya pale nyumbani na tusingeweza kumfukuza kwa sababu alikuwa ni ndugu tena wa damu kabisa upande wa baba yangu hata jamii ingetufikiria vibaya sana, nadhani kama tungeelewa ni kipi mtu huyo alikuwa akihitaji basi tusingethubutu hata kuwa naye karibu. Ni jioni moja ambayo ndo ulikuwa mwanzo wa haya maisha ambayo ninayaishi mpaka hii leo ninavyo zungumza nawewe, nilirudi shule nikakuta nyumbani pamepoa sana basi sikuwa na namna baada ya kushuka tu ndani ya gari nikaingia ndani moja kwa moja nilitahamaki kumuona baba akiwa na bukta tu yupo kifua wazi akiwa anazunguka nyumba nzima kama mtu ambaye alikuwa amechanganyikiwa, nilishtuka na kuogopa sana kwa sababu baba yangu alikuwa ni mtu ambaye alikuwa anajiheshimu mno hakuwahi kufanya hivyo mbele ya sisi watoto wake hivyo nilielewa kwamba kulikuwa kuna tatizo kubwa sana.

Mama yangu sikumuona kabisa hapo sebuleni hivyo sikumuuliza yeyote baba wala mfanyakazi wa ndani nikakimbilia chumbani ambako nilishangaa nakutana na jopo la madkatari sasa nikajiuliza ni nani anaumwa mpaka madaktari waje nyumbani kwa sababu wakati naondoka kila mtu alikuwa mzima wa afya kabisa, nilikuwa na wasi wasi sana ikanilazimu kusogea pembeni mwa kile kitanda lahaula! Mtu aliyekuwa amezungukwa na wale madaktari alikuwa ni mama yangu mzazi akiwa hata hawezi kupumua mwenyewe anategemea msaada wa machine, sikuelewa kilicho endelea pale ambacho nakumbuka kwa wakati ule nilipiga kelele moja tu “mama” kisha nikazimia.

Nilizinduka baadaye sana nikiwa hospitali, nilikuwa nikipiga kelele sana kwamba nahitaji kumuona mama yangu lakini hakuna aliye nijibu na kilicho endelea kunitia shaka sana ni baada ya kuto muona mtu yeyote yule ambaye nilikuwa namfahamu, ili kupunguza usumbufu walinichoma sindano ya usingizi hapo hapo nikalala. Nilizinduka kesho yake asubuhi kitu ambacho sikukiamini ni kwamba pembeni yangu alikuwa amekaa mama yangu akiwa ameketi kwa kushika tama huku akiwa ananitazama kwa huruma sana, nilijikuta ninafurahi huku nikiwa nayamwaga machozi nampenda sana mama yangu ile hali ambayo nilimkuta nayo ilinikatisha hata mimi tamaa ya kuendelea kuishi. Hali yangu ilikuwa imetengamaa kiasi mama alinisogelea pale kitandani na kunikumbatia na hapo ndipo nilipata nafasi nzuri ya kulia, nililia sana siku ile na mama alikuwa haongei chochote zaidi ya kunipiga piga mgongoni kama ilivyo kawaida kwa mama kumbembeleza mtoto wake pale ambapo anahitaji pumziko la amani, nililia sana ila hata kama ungeniuliza kwamba kwanini ninalia vile basi sikuwa na jibu wala sababu ya msingi ila nilijikuta tu ninahitaji kulia sana.

Kwa siku ile sikuwahi kujua kwamba ni nini kilitokea mpaka baadae sana ambapo nilikuja kugundua kwamba siku ile mama yangu alipewa sumu japo ilikuwa ni kwa kiwango kidogo na ndiyo ilimfanya yeye kuwa kwenye ile hali kwa wakati ule narudi nyumbani, sasa sababu ya yeye kupewa ile sumu ndiyo ilitufanya tukawa tunaishi kwenye haya maisha ambayo unaona nayaishi leo na familia yangu” Binti Nurryat ambaye sisi tunamjua kama Nayrah alipumzika kidogo baada ya kusimulia kwa takribani nusu saa historia ya maisha yake huku akiwa anashusha machozi kisha akaendelea tena maana mwanaume hakujibu chochote alikuwa yupo makini sana kumsikiliza mwanamke huyo.

“Siku ile baada ya kutoka hospitali na kufika nyumbani tulimkuta mfanyakazi wetu tu na watoto na mlinzi, baba hakuwepo pale tulivyo jaribu kumuulizia mfanyakazi wetu alitujibu kwamba aliondoka tangu jana yake na hakurudi tena hapo nyumbani nilimuona mama yangu akinyong’onyea sana lakini alijitahidi sana kujikaza mbele yangu na mbele ya watoto ambao walikuwa wanalia kwa sababu ilikuwa ni siku ya pili hawajamuona hivyo walivyo muona walikuwa na shauku kubwa sana na mama yao, baada ya muda mama alienda chumbani kwao na kuufunga mlango, alikaa huko kwa muda mrefu sana na baada ya kutoka uso wake ulikuwa umevimba sana bila shaka nilielewa alikuwa analia japo sikujua ni sababu ipi ambayo ilimfanya mama alie na ndiyo kwa mara ya kwanza nilimuona mama yangu akiwa kwenye hali hiyo tangu nizaliwe sikuwahi kumuona akilia kwa sababu waliishi kwa upendo sana na baba hakuwahi kumpiga hata kibao kimoja hivyo hiyo ilimfanya mama kuwa miongoni mwa wanawake waliokuwa wakiishi kwa furaha sana.

Siku ilienda bila amani nyumbani na kesho yake hata shule sikwenda kabisa wakati ule nilikuwa form four lakini nilishangaa hata mama haniulizi chochote kile, kesho yake majira ya jioni baba alirudi akiwa kama mtu aliye changanyikiwa sana wakati huo tulikuwa tupo mezani kula chakula cha jioni, baada ya kufika alipitiliza moja kwa moja chumbani na mama ikabidi amfuate huko huko ambapo walikaa nusu saa nzima tukiwa hatuelewi ni kipi kilikuwa kinaendelea huko, tukiwa kwenye huo mshangao na chakula tumesha maliza kula, nakumbuka wadogo zangu walikuwa wanaangalia katuni sebuleni wakiwa kwenye masofa, walikuwa kwenye furaha sana bila kujua kile ambacho kilikuwa kinaendelea.

Tulisikia mlango wa nje ukigongwa kwa nguvu sana, mlinzi aliufungua na ndipo tuliposhuhudia kundi la watu wengi sana wakiwa wanaingia hapo ndani bila hata hodi, walikuwa watu wasio pungua kumi nakumbuka, wanaume wanne walikuwa kwenye suti na watano walikuwa na nguo za polisi ambao hata bila shaka baadae nilikuwa kugundua kwamba walikuwa ni maaskari lakini mmoja wao alivaa suti ya tofauti na wenzake na alikuwa na begi mkononi akiwa na miwani pia, kwa elimu niliyokuwa nayo nilijua moja kwa moja mwanaume huyo atakuwa ni mwanasheria, kitu kilicho nishangaza ni baada ya kumuona mwanaume yule ambaye siku kadhaa hapo nyuma alikuwa amekuja pale nyumbani kama ndugu yake na baba na aliomba kuweza kukaa hapo nyumbani mpaka pale ambapo mambo yake yangekuwa sawa naye alikuwa kwenye suti tena ndiye aliye onekana kuwaongoza watu hao mpaka kufika hapo na ujio wake haukuwa wa kirafiki kwa mwonekano wake tu.

“Baba yenu na mama yenu wako wapi” ilikuwa ni sauti kali ya mmoja wa maaskari wale ambao walikuwepo mle ndani, alinitia hofu sana ikanilazimu kuwajibu.

“Wapo chumbani” nilijibu huku nikiwa na wasiwasi sana
“Kawaite haraka sana” aliniamuru kwa nguvu hivyo nilipita kwenye korido moja na Kwenda mpaka kwenye chumba cha wazazi wangu, niliwagongea na aliye fungua pale alikuwa ni mama yangu ambaye nilimpa taarifa iliyo onekana kumshtua sana, alisema anakuja kisha akafunga mlango na kuingia tena chumbani. Ile ndiyo siku ya kwanza ambayo nilimuona baba yangu akiwa kwenye hali ya kutisha kama ile, alitoka kule chumbani akiwa na silaha mkononi ambayo bila shaka ilikuwa ni bastola, alikuwa mwenye hasira sana alitamka maneno machache ambayo yaliwafanya mpaka wale askari watoe silaha zao na kumuweka chini ya ulinzi.

“Tokeni nyumbani kwangu mbwa wakubwa nyie, hivi mnadhani hizi mali niliziokota sio sitaki kuwaona nyumbani kwangu tokeni” alikuwa kwenye hasira lakini nilimhurumia sana baba yangu, alikuwa anaongea huku akilia na mwili wote ulilowa jasho, sikuwahi kumuona kwenye ile hali hivyo nilijua mambo yalikuwa yameheribika sana, licha ya kuongea hayo maneno lakini hakuna alicho fanikiwa wale maaskari walikuwa na silaha mikononi hivyo walimuweka chini ya ulinzi na kumtia nguvuni, mama yangu alikuwa anatokwa na machozi akiwa ameketi kwenye kochi moja alinisihi niwapeleke wadogo zangu chumbani, wakati natoka hapo nilisikia moja ya kauli mbaya zaidi kuwahi kuzisikia kwenye maisha yangu kwa wakati ule na ilitoka kwa yule yule ndugu yake baba ambaye alikuja hapo nyumbani kuomba msaada siku kadhaa nyumba”

“Na hivyo vijini vinaenda wapi hebu vitoeni huko haraka kabla havija aanza kuichafua nyumba yangu siyo muda nahitaji kulala mimi” aliongea kwa kujiamini na kwa jeuri kubwa sana kitu ambacho kiliniuma lakini pia kilinishangaza sana yaani nyumbani kwetu ndo anatutukana tena kutuhitaji tuondoke ama kweli dunia kwangu kwa siku ile ilikuwa imepinduka sana hata hivyo sikusimama niliwapeleka wadogo zangu chumbani kisha nikarudi nikakaa pembeni mwa ukuta ila nilikuwa nasikia kila kilichokuwa kinaendelea pale. wale maaskari kiukweli walimpiga sana baba yangu, nadhani ni kwa sababu ya ile bastola ambayo aliwatisha nayo ungedhani ni mtu ambaye alikuwa ameua watu lakini kiuhalisia hakuwa na hatia yoyote ile hata mama alipo jaribu Kwenda kumtetea alipigwa vibaya sana ikamlazimu kukaa kimya huku akiwa anayashusha machozi yake taratibu.

“Ndugu yangu Hashim hawa hapa nadhani unawajua kwamba ni ndugu zako na huyo mwingine anasema uliamua kumchukua na kuanza kumtesa hapa hapa ulipokuwa ukiishi tena kwenye kitu ambacho yeye ndiye mwenye uhalali wake, kwa ushahidi kabisa ambao umethibitishwa mbele ya mahakama ni kwamba hizi mali wewe hauhusiki nazo kabisa na wala hautakiwi kuwa karibu na kila mali ambayo ulikuwa ukijihusisha nazo tangu hapo zamani kidogo. Ushahidi unaonyesha kwamba uliwadhulumu ndugu zako hizi mali kwa miaka mingi sana wamejaribu kukuomba basi ufanye hata kuwagawia kidogo wafanye nao biashara kubadilisha maisha yao lakini haukufanya hivyo zaidi ulianza na kuwatumikisha kabisa kwa mali ulizo wapora wewe mwenyewe. Wenyewe wamesema hawana ubaya nawewe kwa sababu wangeamua kwa ulicho wafanyia wangekufunga jela maisha yako yote ila kwa sababu wewe ni ndugu wanataka kuanzia muda huu uondoke hapa na mali zao uwaachie kwa amani tu kwani kitu ulicho kifanya ni kinyume na sheria ya nchi yetu” hiyo ni kauli kutoka kwa yule mwanasheria ambaye toka mwanzo nilimhisi hivyo, nadhani siyo baba tu ambaye aliumizwa na hilo jambo na mama bali mimi nilishtuka sana kusikia hiyo kauli kutoka kwa huyo mwanasheria na kiufupi ni kwamba nilichanganyikiwa sana huenda ndiyo sababu kubwa huwa naichukia sana sheria pamoja na mamlaka kama polisi duniani.

Kipi kilijiri kwenye hii familia? ilikuwaje mali za baba yake aonekane kama aliwapora ndugu zake je ni kweli? Nini hatima yake mpaka kufikia kuishi ndani ya Mbagala?

Sehemu ya 21 niseme sina la nyongeza tukutane tena wakati ujao

Wasalaam

Bux the storyteller.
 
STORY: INNOCENT KILLER (THE REVENGE)
STORY WRITER: BUX THE STORYTELLER
WHATSAPP : 0621567672
EMAIL: thomasibabuya@gmail.com
AGE: 18+
SEHEMU YA 22

SONGA NAYO............
“Ebu tazama namna ulimwengu ulivyokuwa umekosa huruma, angalia namna wanadamu walivyokuwa na roho za ajabu, kuna wakati hii dunia hata shetani mwenyewe nina uhakika anaiogopa, kuna watu wana roho za kutisha sana hata shetani mwenyewe anajifunza kwao. Nilimuonea huruma sana yule mzee, kupitia baba yangu nilipata somo kubwa sana kwamba wanaume wengi mno kuna mambo mazito sana ambayo huwa wanayapitia ila huwa wanaamua kuyafukia vifuani mwao hata sisi wanawake tupige kelele vipi huwa wanaigiza kuwa na tabasamu zito sana usoni lakini kiuhalisia wengi wanapitia wakati mgumu sana kwenye maisha yao. Nilijua huenda namimi nitakuwa muhanga wa kile kitu ila nilimhurumia zaidi baba yangu, chozi lilinitirirka kwenye mashavu yangu nilipo mshuhudia baba yangu akilia kama mtoto mdogo pale chini kwa kugala gala na kumuomba ndugu yake asimfanyie hivyo amemtoa mbali sana.

“Mdogo wangu kipi umetaka kwangu nikakunyima? Ulipata kila ulicho kitaka, ulipata kila pesa ambayo uliiomba na kumbuka mimi nawewe undugu ni kwa baba zetu lakini nimekutunza kama tumezaliwa pamoja kwanini ufikie hatua ya kunifanyia ukatili mkubwa sana namna hii, hauwaonei hata huruma wadogo zako wataenda kuishi maisha gani kwenye dunia hii ambayo imejaa dhuluma kila mahali? Kwanini unanifanyia hivi mdogo wangu” aliongea kwa uchungu sana baba yangu akiwa anamwambia yule ndugu yake ambaye alikuja nyumbani kwa kisingizio cha kuomba msaada lakini ni kama zilikuwa kelele za chura tu ambazo hazikuwa na uwezo wa kumzuia tembo kuweza kunywa maji, maneno yake yalipokelewa kwa kicheko kikali sana kutoka kwa wote waliokuwa pale kasoro mwanasheria na wale maaskari, aliwageukia ndugu wengine ambao bila shaka nao walikuwa ndugu zake ambao walikuwa wanakamilisha idadi ya wale watu wanne kwa ujumla.

“Jamani naombeni mmshauri mdogo wenu kwanini ananifanyia ukatili mkubwa sana namna hii nitaenda wapi kwenye ulimwengu wa kikatili kama huu?” aliongea baba yangu huku akiwa anatembelea magoti kwa wale ndugu ambao wote waliishia kumdhalilisha tu na kumcheka, kile kitu kiliniuma sana nilijuta kuzaliwa wa kike kwa sababu kama ningezaliwa mwanaume basi wale wote nadhani mpaka leo ningewatafuta na kuwaua. Baada ya pale ilitolewa amri tutolewe mle ndani muda huo huo hakuna aliyeweza kujali kitu nilicho kifanya nilikimbilia kwenye chumba changu na kutoa kadi zangu za benki nikaziweka kifuani kwangu mama na baba walikuwa pale pale sebuleni, nilishtuka baada ya kusikia wadogo wangu wakiwa wanalia bila shaka nilijua kwamba walikuwa wanatolewa humo ndani.

Zilitumika dakika kumi tu tulitupwa nje ya ile nyumba ya kifahari sana ambapo kiuhalisia palikuwa ni nyumbani kwetu ila kuanzia muda huo pale na sisi hapakuwa kwetu wala hatukuwa na uhalali wowote wa kupaita nyumbani, wadogo zangu walikuwa wakilia sana, mama alikuwa amejiinamia akiwa anamwaga machozi, baba alikuwa anatembea tembea kwenye lile geti kwa nje akiwa anatukana, alianza kucheka cheka mwenyewe pale huku akiwa anachana chana nguo zake mwenyewe na ile ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya baba kuwa kwenye utimamu wake alipata ugonjwa wa akili kuanzia pale pale nadhani ni kwa sababu ya mali zake nyingi ambazo zilichukuliwa kiwepesi sana tena na ndugu zake ambao yeye mwenyewe alijitolea kuwasaidia kwa lolote lile.

Mimi sikujizingatia sana pale watu ambao kwangu nilikuwa nawaonea sana huruma alikuwa ni mama yangu na wadogo zangu ilibidi mimi ndiye niwe jasiri pale wa kuanza kuwabembeleza. Tulikaa pale kwa masaa mawili mpaka tulipokuja kufukuzwa na wale maaskari kwa sababu baba alikuwa anaendelea kupiga makelele huku akiwa anaendelea kucheka sana, dunia haikuwa fair kwa upande wetu na nadhani siku ile hata MUNGU alituacha kwa muda kwa sababu nilikuwa naona maluwe luwe tu. Baada ya pale tuliondoka Kwenda mahali tusipo pajua nilihangaika na kutafuta chumba maeneo ya mbali kidogo na pale nilipata vyumba viwili ambapo kimoja ilikuwa ni kwa ajili yangu na wadogo zangu na kimoja kwa ajili ya mama yangu. Niseme tu namshukuru sana MUNGU kuweza kunipa mama kama yule, ni shujaa wangu anapambana sana, licha ya baba kuwa kwenye ile hali lakini alisimama imara sana hakuwahi kuuonyesha udhaifu mbele yake ila akiwa mwenyewe alikuwa mtu mwenye mawazo makali sana.

Mama kwenye akaunti yale alikuwa amebakiwa na pesa kiasi na mimi kwenye akaunti yangu ambayo baba alikuwa ananiwekea pesa kulikuwa na pesa kiasi, kwa sababu wakati ule ilikuwa imebakia wiki chache sana tufanye mtihani wa taifa wa form four basi mama alinisihi nipambane nimalize kabisa kwa sababu mimi ndiye naweza kuja kuwa msaada wa pekee kwenye familia yangu, licha ya maneno machafu na kejeli ambazo nilizipata kutoka shuleni kwa baba yangu kuonekana alikuwa ni tajiri kumbe tapeli na mtu ambaye alitaka kudhulumu haki za watu lakini bado nilipambana na kumaliza na pale ndipo tulipo amua Kwenda mbali na Mtwara na kuja kuishi sehemu ambayo hakuna mtu ambaye angeweza kuja kutuona tena kwenye haya maisha na hapo ndipo safari ya kuja kuishi ndani ya jiji la Dar es salaam ilipo zaliwa.

Wakati huo nilikuwa nimemaliza masomo yangu ya form four ndipo tulipo hamia kwenye hili jiji, tulikuwa na maisha magumu sana ukilinganisha na maisha ya raha ambayo tuliyazoea kuishi, sasa tulikuwa tukiishi kwa mahesabu makali mno, pesa ambayo ilikuwa imebakia ndiyo ambayo tulibahatika kununua nyumba ya vyumba vinne hapa mbagala mimi na mama yangu lakini akiba iliyo bakia ilitakiwa mimi niende kwenye shule ambayo ilikuwa na ubora wa kawaida kwa sababu mama yangu aliwekeza imani kubwa sana kwenye elimu kwamba ingeweza kunifanya nikaja kuwa msaada mkubwa sana kwenye haya maisha na yeye wakati mimi naendelea na shule basi angekuwa anafanya biashara ndogo ndogo mtaani ambayo ingetusaidia kupata chakula, yule Kwangu ni mama bora sana na kumbuka mpaka wakati huo baba yangu alikuwa amekuwa mgonjwa wa akili jumla hivyo yeye akawa kama anatutegemea sisi kwa kila kitu ilikuwa inaniuma sana kumuona baba yangu kwenye hali kama ile kwa sababu ya tamaa ya watu wachache.

Matokeo yalitoka na nilikuwa nimepata alama za juu sana kwa sababu nilisoma shule za gharama mno, hivyo mama yangu hakuhitaji nipate elimu ndogo tena tulitafuta shule ambayo ilikuwa nzuri kwa sababu kuna akiba kidogo ilibakia kwenye zile pesa za mama na za kwenye akaunti zangu, tulilipa ada ya miaka yote miwili kwa kufanya makubaliano na mmiliki wa ile shule kwamba nisije nikasumbuliwa mpaka namaliza na nilikuwa natoka nyumbani kila siku ya MUNGU kwa sababu ilitakiwa nimsaidie mama yangu baadhi ya majukumu hivyo ilitafutwa shule ambayo haikuwa nje ya Dar es salaam ili kuwe na urahisi wa mimi kufanya vyote kwa pamoja. Kwa wakati huo nilikuwa nikiwachukia sana wanaume wote kwa sababu nilihisi wote ndio wale wale kama walioweza kututapeli mali zetu na kutuacha kwenye umaskini mkubwa sana, licha ya kusumbuliwa na vijana wengi sana hakuna ambaye alifanikiwa kuweza kunipata kwa wakati ule.

Mimi sijawahi kumjua mwanaume kwenye maisha yangu, hakuna mwanaume hata mmoja ambaye amefanikiwa kuuona hata mwili wangu ukiwa bila nguo, hakuna mwanaume hata mmoja ambaye aliwahi kupata nafasi ya kuushika mwili wangu hata kunikumbatia tu wewe ndiye mtu wa kwanza kabisa kuugusa huu mwili kwa kuupa kumbatio, mimi siyo malaya wala sijiuzi na naomba unisamehe sana kama ulinifikiria hivyo (aliongea akiwa anatoa machozi), mimi ni mwanamke ambaye nimelelewa kwenye maadili bora sana licha ya kupitia changamoto nyingi sana kwenye maisha yangu na mimi ni mwanamke ambaye sijawahi kupenda hata siku moja kwenye maisha yangu nahisi ni kwa sababu niliathirika kimawazo na yale mambo ambayo yalitukuta kwa hiyo miaka hivyo huwa naiwazia sana familia yangu kuliko kitu chochote kile.

Nilisoma kwa shida sana ndani ya ile miaka miwili, kuna muda ilikuwa inakosekana hata pesa ya nauli kwa sababu pia nyumbani tulitakiwa kula ila nilipambana sana mpaka nikafanikiwa kulikamilisha hilo na nilifaulu vizuri sana kitu ambacho kiliendelea kumpa matuamini mama yangu ila kadri muda ulivyokuwa unazidi Kwenda nilikuwa namuona mama yangu afya yake inadhorota sana huku baba naye akiwa ndiyo kabisa amekuwa kichaa na hakuwa na uwezo wa kujipa hata msaada yeye mwenyewe, hicho kitu kilinitesa sana ndipo siku moja tulienda hospitali na mama ambapo niligundua tatizo ambalo mama alikuwa amekiri kwamba alikuwa nalo kwa muda mrefu sana tangu tupate hayo matatizo na aliamua kunificha ili nisije kuwa na udhaifu kwenye kupambana kwangu na ndiyo siku ambayo alinisimulia kipi kilifanyika mpaka tukaweza kuchukuliwa kila kilichokuwa chetu na yule ndugu yake baba, mama yangu alikuwa na matatizo ya moyo.

Yule mtu hakuja nyumbani kwa bahati mbaya, naweza kusema kwamba alikuwa ametumwa na familia yao yote kufika pale, lengo lake la kuja pale ulikuwa ni mpango wa kupata hati za nyumba, mashamba, kadi za magari yote ya abiria, ya kutembelea ambayo alikuwa anayamiliki baba pamoja na pesa taslimu ambazo zilikuwa zipo Bank, hatukujua chochote na kwa maelezo ya mama ni kwamba mwanaume huyo alikuwa ametegesha vinasa sauti kila sehemu ndani ya nyumba yetu na alikuwa makini sana kufuatilia kila hatua ya ile nyumba pamoja na maisha kwa ujumla yalivyokuwa yanaendelea mle ndani ndiyo maana alifanikiwa kuukamilisha mpango wake kirahisi. Kwa sababu alikuwa kama mwana familia hiyo ilitufanya tusimpeleleze sana na isingekuwa vizuri mtu anaishi nyumbani kwako halafu uanze kumpeleleza kwa sababu tu unajua kwamba hakuna ubaya unaweza kufanyika ila kupitia hilo limenipa funzo sitakuja kumuamini mgeni yeyote ambaye atakuja iwe ni nyumbani kwetu au hata kwangu nitakapo pata bahati ya kuolewa.

Hiyo ilimpa nafasi kubwa sana ya yeye kufanya kile ambacho alikusudia kukifanya, kupitia vinasa sauti na mawasiliano ambavyo alivitegesha kila sehemu ya nyumba vilimsaidia yeye kuweza kujua kila kitu kuhusu mali za baba kwa sababu baba alikuwa akimuamini sana mama na ndiye mtu ambaye alimfanya mpaka akawa na utajiri wote huo mkubwa hivyo wakiwa chumbani walikuwa wakishauriana mambo mengi sana kuhusu biashara na maisha ya ujumla lakini baba alikuwa akimuweka wazi mama kila kitu kuhusu pesa zake, sehemu za kuhifadhi hati za nyumba zake zote, magari, hati za mashamba na viwanja lakini pia hata namba za siri za akaunti za benki ambazo kwa mahesabu ya mama ni kwamba kwenye akaunti ya baba ya biashara ilikuwa na pesa za kitanzania bilioni miamoja na hapo ndipo nilipo elewa kwamba ni kwanini baba alipata ugonjwa wa akili kwa kupoteza mali zake nyuma yake pia kulikuwa na pesa nyingi sana. Baada ya kujua kila kitu ndipo alipotegea siku ambayo baba aliondoka akawa amemuwekea mama sumu kwenye supu ya nyama ya kuku ambayo mama aliipenda sana na kuna muda ilikuwa inaandaliwa kwa ajili yake tu hivyo mwanaume yule baada ya kuhakikisha mfanyakazi ameiandaa alifanya kila anachokiweza na kufanikiwa kuweka sumu na ndiyo ile siku ambayo nilimkuta baba yangu kachanganyikiwa nyumbani kukiwa na madaktari wakiwa chumbani wanamtibia mama.

Alivyofanikisha kumuwekea mama sumu ndio muda ambao alibeba hati zote na kadi za magari yote kwa sababu kule chumbani kulikuwa na droo za chuma za siri sana ambazo kufungua kwake hata kama ungekuwa na chuma usingeweza na walikuwa wanafungua watu wawili tu baba na mama pamoja namimi hapa na kwa sababu alikuwa anajua kila kitu hiyo ilimrahisishia yeye kufungua, alibeba kila kitu hakuacha chochote maana yake mpaka wakati huo yeye ndiye alikuwa mmiliki halali wa mali zote za baba yangu, wakati mama na mimi tunarudi nyumbani tuliambiwa baba hayupo ameondoka kumbe alikuwa kufuatilia jambo hilo kwa sababu alikuwa ameelewa kila kilichokuwa kimefanyika hivyo aliwafuata watu wake ambao wanaweza kumsaidia haraka kama atafanikisha jambo hilo lakini ni kama huko alikokuwa ameenda mambo yalienda tofauti na ndo ule ule usiku ambao yeye alirudi akiwa amechanganyikiwa wakati tunakula mama akamfuata chumbani, haukupita muda mrefu nao wakawa wanaingia na ndipo hapo tulipo fukuzwa rasmi, mama alikuwa akijua kila kitu toka mwanzo ila hakuhitaji kutupa hofu sisi hivyo naye alivumilia kama hajui chochote mpaka siku hiyo ndipo alikuwa ananipa hiyo simulizi ya hayo maisha kiukweli nilihisi kama wamenitonesha kidonda tena nilianza kulia upya na kuhisi huenda mimi sikuwa mwanadamu mwenye bahati kuzaliwa duniani kama ilivyo kwa wanadamu wengine niliumia sana.

Tulirudi nyumbani na ilitakiwa mimi nianze kusoma chuo ambacho kiuhalisia sikuwa na mpango nacho tena kwa sababu nilikuwa nimesoma shule za gharama sana hivyo nilikuwa na uhakika kwamba hata mkopo siwezi kupata na sikuwa na pesa kabisa ya kujilipia na kwa wakati huo hata nyumbani pesa ilikuwa imeisha, mama yangu alikuwa akitegemea genge ambalo alishindwa kuliendesha baada ya kujua kwamba ana hilo tatizo la presha ya moyo muda wowote ilikuwa inampanda na kushuka kutokana na mawazo hivyo jukumu la kumlea yeye, baba, na wadogo zangu ulibaki kuwa mtihani kwangu hiyo ndiyo sababu iliyo nifanya kabisa niyafute mawazo ya Kwenda kusoma chuo kwenye maisha yangu na niliamini kabisa kwamba sitakuja kuendelea tena na masomo basi hilo nililifuta kichwani mwangu sasa nikawa napambana kulifufua genge la mama yangu ambalo lilitegemewa kuendeshea maisha ya pale nyumbani na bahati iliyokuwa nzuri nyumba tulinunua hivyo hatukuwa na hesabu za kulipa kodi kwani kama tusingefanya hivyo mapema nadhani tungekuwa hatuna sehemu ya kulala mpaka sasa” aliongea kwa uchungu sana akiwa anamwanga machozi ya kutosha, aliunyanyua uso wake na kumwangalia Jason kwa huruma sana, mwanaume alimfuta machozi yake na kumbusu eneo la paji la uso kidogo akatabasamu na sasa alihitaji kumweleza alifanyaje fanyaje mpaka akaja kuwa msomi mkubwa tu wa udaktari ambaye hakuwa na kazi yoyote mtaani huko zaidi ya kuvaa vijora tu.

Tuna mengi sana ya kujifunza humu ndani, mapenzi, maisha, maumivu, furaha, siri bila kusahau lengo kuu kabisa la hadithi usisahau ni hadithi ya kijasusi inayo mhusu muuaji ambaye hata hatia na namna anavyo fanya kisasi chake hivyo tegemea matukio ya kijasusi ya kutisha sana humu ndani utaenda kuwajua namna binadamu wanavyo uishi ulimwengu wa wababe na ulimwengu unao tisha sana lakini utapata love story moja kali sana wataalamu wanaitwa LOVE CUBE (mapenzi ya mwanaume mmoja kuwa na wanawake watatu jumla yao wanakuwa wanne) namna wanawake watatu walivyo mpenda sana mwanaume mmoja ambapo kila mwanamke huenda alihisi mwanaume huyo ndiye hatima yake bila kumjua vizuri huyo mwanaume mwenyewe.

22 inafika mwisho panapo majaaliwa tukutane tena wakati unao kuja.

Wasalaam

Bux the storyteller.
 
Huu mzigo kwa sasa upo mpaka mwisho (MUUAJI ASIYE NA HATIA (KISASI). Ina kurasa za kawaida 135. Lakini kwa wale ambao wanahitaji softcopy ina page za pdf 1490 kwa yenye font size 18, lakini ina page 1840 kwa pdf yenye fontsize 20.

Bei yake ni shilingi 5000 tu mpaka mwisho kwa sasa.

Unaweza ukalipia kupitia namba
0621567672
0745982347

Jina FEBIANI BABUYA.

Jipatie ya kwako ili uifanye wikiendi yako kuwa fupi na uburudike kwa kusoma andiko bora sana.

Wasalaam.
Screenshot_20230513-161307_WPS%20Office.jpg
 
Back
Top Bottom